MKUTANO WA TATU Kikao Cha Thelathini
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Thelathini na Tano - Tarehe 2 Juni, 2016 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua (Hapa Waheshimiwa Wabunge wa Kambi ya Upinzani Walitoka Nje) NAIBU SPIKA: Tukae, Katibu. MBUNGE FULANI: Hamna posho ninyi. NAIBU SPIKA: Katibu. NDG. NEEMA MSANGI – KATIBU MEZANI: Maswali. MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum swali lake litaulizwa na Mheshimiwa Ally Keissy. Na. 284 Unyanyasaji Unaofanywa na Mgambo/Askari Kwa Wafanyabiashara Wadogo Wadogo MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) aliuliza:- Kumekuwa na hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na mgambo na askari polisi wanapotekeleza maagizo ya Serikali dhidi ya 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) wafanyabiashara wadogo wadogo hususan mama lishe, bodaboda pamoja na machinga. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, mgambo wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria ya polisi wasaidizi ya mwaka 1969 kwa kuzingatia sheria hiyo, Halmashauri zimeruhusiwa kuajiri askari ngambo kwa ajili ya kusaidia usimamizi wa Sheria Ndogondogo za Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya. Mheshimiwa Naibu Spika, askari mgambo anayefanya kazi katika Halmashauri anawajibika kuzingatia sheria za nchi pamoja na sheria ndogo ndogo zilizotungwa na Halmashauri.
[Show full text]