Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _____________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ MKUTANO WA TANO Kikao cha Nane – Tarehe 17 Novemba, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati ifuatayo iliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, URATIBU NA BUNGE): Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2010. MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunaanza maswali kwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa Kanuni yetu ya 38(2), leo Waziri Mkuu hayupo, kwa hiyo, tunaendelea na maswali ya kawaida. Na. 99 Kukosekana kwa Huduma ya Maji Safi na Salama Tarime MHE. NYAMBARI C. M. NYANGWINE aliuliza:- Tangu enzi za Uhuru hadi sasa Wilaya ya Tarime haijawahi kupata maji safi na salama kwa matumizi ya Wananchi:- (a) Je, Serikali haioni kuwa haiwatendei haki Wananchi wa Tarime kwa kutowapatia huduma ya maji safi na salama? (b) Je, Serikali ina mkakati gani katika kutatua tatizo hilo haraka iwezekanavyo? (c) Je, Serikali inasema nini juu ya ahadi zilizowahi kutolewa za kutatua tatizo la maji Wilaya ya Tarime? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, NInaomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyambari Chacha Mariba Nyangwine, Mbunge wa Tarime, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Wilaya ya Tarime ni asilimia 30 kwa maeneo ya Vijijini na asilimia 52 katika maeneo ya Mijini hadi kufikia mwaka 2010.
[Show full text]