Tarehe 10 Juni, 2016
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Arobaini – Tarehe 10 Juni, 2016 (Bunge lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA, Tukae, Katibu. (Hapa Waheshimiwa Wabunge wa Kambi ya Upinzani Walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge na kubakia Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. David D. Silinde) NDG. JOSHUA CHAMWELA – KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/2017 – 2020/2021 (The National Five Year Development Plan, 2016/2017 -2020/2021). MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BAJETI: Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/2017, Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/2016 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) MHE. DAVID D. SILINDE – NAIBU MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/17; pamoja na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. NAIBU SPIKA: Katibu. NDG. JOSHUA CHAMWELA: Maswali MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Tutaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Na. 334 Wabunge wa Viti Maalum Kushiriki katika Kamati za Fedha na Mipango za Halmashauri MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:- Kamati za Fedha za Mipango za Halmashauri za Wilaya ni Kamati muhimu sana kwa Wabunge wote kushiriki bila kujali ni wa Viti Maalum au wa Jimbo kwa sababu zinashughulika na masuala ya fedha, bajeti na mipango ya miradi ya maendeleo; na kwa muda mrefu sasa Wabunge wa Viti Maalum wamekuwa wakiomba kuondolewa kwa sheria kandamizi na ya kibaguzi ya kuwazuia kushiriki katika Kamati hizo:- (a) Je, Serikali iko tayari kusikiliza kilio cha Wabunge wa Viti Maalum ili kuwaruhusu kushiriki kwenye Kamati hizo? (b) Je, Serikali iko tayari kufuta sheria hiyo kandamizi na yenye ubaguzi ambayo haina tija na hasa ikizingatiwa kuwa ilitungwa mwaka 1998 wakati ambao Ubunge wa Viti Maalum bado haujaanza? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. 2 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Halmashauri wametajwa katika kifungu cha 75(6) cha Sheria, Sura 287 ya Mamlaka za Serikali za Wilaya na kifungu cha 47(4) cha Sheria Sura 288 ya Mamlaka za Miji. Kwa mujibu wa sheria hizo mbili, Wajumbe wa Kamati hawatazidi theluthi moja (1/3) ya Madiwani wote isipokuwa Kamati ya Fedha na Mipango ambayo Wajumbe wake ni wale wanaoingia kwa nyadhifa zao. Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango umefafanuliwa katika Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa kila Halmashauri ambapo Wajumbe wake ni Mwenyekiti au Meya wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Naibu Meya wa Halmashauri, Mbunge au Wabunge wa Majimbo wanaowakilisha majimbo katika eneo la Halmashauri, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri na Wajumbe wengine wasiozidi wawili watakaopendekezwa na Mwenyekiti/Meya kisha kupigiwa kura na Baraza la Halmashauri mmoja kati yao awe mwanaume au mwanamke. Hivyo, ili Wabunge wa Viti Maalum waweze kushiriki kwenye Kamati za Fedha tutahitaji kubadili sheria kwanza ili pendekezo hilo liweze kutekelezeka. (b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika sehemu (a) ya jibu hili, Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango wataendelea kuwa ni wale waliotajwa katika Sheria na Kanuni za Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi hapo sheria itakapofanyiwa marekebisho kwa kushirikisha wadau mbalimbali. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Martha Umbulla swali la nyongeza. MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zote za Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini zinapita kwenye Halmashauri za Wilaya na katika vikao vya Halmashauri za Wilaya hasa Kamati hiyo ya Fedha na Mipango Wabunge wa Viti Maalum hawashiriki na ndiyo watu wenye dhamana na maendeleo ya wanawake. 3 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Kwa kuwa sheria hiyo iliyotungwa ambayo inawakataza Wabunge wa Viti Maalum kuingia kwenye Kamati hizo ilitungwa zamani sana kabla hata utaratibu wa Ubunge wa Viti Maalum haujaanza bali kulikuwa na Wabunge wa Majimbo na Wabunge wa Kuteuliwa na Rais; na kwa kuwa mwaka jana kwenye Bunge la Kumi, Mheshimiwa Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri alipokuwa anajibu swali hapa Bungeni, alitueleza kwamba sheria hiyo ni kandamizi na tunahitaji kuileta hapa Bungeni ili tuirekebishe Wabunge wa Viti Maalum washiriki. Je, Serikali italeta lini hiyo sheria ili Wabunge wa Viti Maalum waweze kushiriki katika Kamati hii muhimu? Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri zetu za Wilaya hasa kwa Mkoa wetu wa Manyara zinatenga asilimia kumi za fedha kwa ajili ya miradi ya wanawake. Utaratibu na mfumo wa utoaji wa fedha hizo kwa ajili ya miradi ya wanawake hauko vizuri na kuna upotevu mkubwa sana wa fedha hizo za Serikali. Je, ni kwa nini Madiwani wa Viti Maalum wakisaidiana na Wabunge wao wasisimamie kikamilifu utoaji na urejeshaji wa fedha hizo ili ziweze kuwafikia walengwa? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kila kitu kipo kwa mujibu wa sheria na kanuni zake. Katika jibu langu la msingi katika eneo la pili nikasema mchakato unaweza ukaendeshwa kwa kuwashirikisha wadau. Hili la kuwashirikisha wadau kama nilivyosema lina umuhimu mkubwa sana. Katika maeneo mengine kwa mfano nikichukua Jimbo langu mimi la Kisarawe, Mbunge wangu wa Viti Maalum anaingia katika Kamati ya Fedha na sehemu zingine wanaingia katika Kamati hii, ina maana hivi sasa katika zile nafasi mbili Mwenyekiti anaweza akateua Mbunge wa Viti Maalum kuweza kuingia pale. Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kusimamia fedha ni wajibu wa Madiwani na Wabunge wahusika katika eneo hilo. Kwa upana wa jambo hili, ndiyo maana nimesema wadau lazima washirikishwe. Kuna baadhi ya Majimbo, mfano Jimbo la Ilala, lina Wabunge wa Majimbo watatu, lina Madiwani wa Viti Maalum wasiopungua watano, kwa hiyo ukiangalia hapo, ndiyo maana nasema lazima wadau washirikishwe kuona jambo hilo linakaajekaaje na kuangalia ni jinsi gani tutafanya Kamati ya Fedha iweze kufanya vizuri. Kwa mfano, kwa hali ya sasa hivi ukisema Jimbo la Ilala Wabunge wote wa Viti 4 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Maalum waingie katika Kamati ya Fedha mtapata sura hapo, ndiyo maana nasema lazima sheria hiyo tuitazame kwa upana na wadau washiriki kila mmoja katika eneo lake kuangalia jinsi gani tutafanya, hilo ni jambo la msingi lakini kwa sasa hivi sheria inasimama hivyo. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu asilimia tano ya akina mama na siyo ya akina mama peke yake, ni ya vijana na akina mama. Jambo hili nililisema katika vikao mbalimbali kwamba jukumu la Kamati ya Fedha ni kuhakikisha kwamba fedha zinazokusanywa kutoka own source ziweze kuyafikia yale makundi ya akina mama na vijana. Kwa bahati mbaya hata katika kaguzi mbalimbali zilizopita hili ni miongoni mwa eneo lenye changamoto kubwa na ndiyo maana tumetoa maelekezo kuhusu suala hili. Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema agenda ya kuhakikisha akina mama na vijana wanapata fedha hii ni yetu sote. Ndiyo maana bajeti ya mwaka huu criteria tuliyotumia kuhakikisha Halmashauri zote zinatengewa bajeti ni kuhakikisha kwamba wanatenga asilimia tano ya vijana na akina mama na walemavu watakuwa katika mchakato huo. Kwa hiyo, hili ni agizo la jumla kwamba kwa vile bajeti tumeipitisha basi kila Halmashauri ihakikishe inasimamia asilimia tano za akina mama na tano za vijana ziweze kuwafikia walengwa. (Makofi) NAIBU SPIKA: Tuendelee Waheshimiwa na swali linalofuata. Na. 335 Uwekaji wa Mipaka Upya - Makambako MHE. DEO K. SANGA aliuliza:- Kutoka Kijiji cha Mutelewele kwenda Makambako ni kilometa tano wakati kwenda Halmashauri ya Wanging‘ombe ni kilometa 65; kutoka Kata ya Soja kuja Makambako Mjini ni kilometa 25 na kwenda Halmashauri yao ya Wanging‘ombe ni kilometa 88 na kutoka Kijiji cha Nyigo kuja Makambako ni kilometa 8 wakati kwenda Halmashauri ya Mufindi ni kilometa 88 na huduma zote zikiwemo matibabu wanazipata Makambako; kutoka Kijiji cha Igongolo ni umbali wa kilometa 6 kwenda Makambako wakati kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni kilometa 54. (a) Je, Serikali itakuwa tayari kugawa mipaka upya ili wananchi wapate huduma karibu na Halmashauri yao ili iendane na kauli mbiu ya kusogeza huduma karibu na wananchi? (b) Je, ni lini sasa Serikali itapima upya mipaka hiyo? 5 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, Vijiji vya Mutewele na Saja viko katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging‘ombe na Kijiji cha Nyigo kiko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa vijiji hivyo kijiografia viko karibu na Halmashauri ya Mji wa Makambako kwa maana ya huduma. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia njema ya Mheshimiwa Mbunge ya kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi vipo vigezo na taratibu zinazozingatiwa katika kusajili au kubadili mipaka ya vijiji.