20 Juni, 2013
20 JUNI, 2013 BUNGE LA TANZANIA _____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Hamsini na Tatu – Tarehe 20 Juni, 2013 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua KIAPO CHA UTII Mbunge afuataye alikula Kiapo cha Utii na Kukaa katika nafasi yake Bungeni:- Mhe. Yussuf Salim Hussein. MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kufuatana na Kanuni yetu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani hayupo, kwa hiyo, nitaenda moja kwa moja kumwita anayefuatia, Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah! MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia leo hii kusimama hapa. Mheshimiwa Waziri Mkuu, rushwa na ufisadi vinaliangamiza Taifa letu. Hivi karibuni tulimsikia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisikitishwa sana na jinsi rushwa ilivyokithiri katika Chaguzi za Chama chake. Tarehe 16 tumemsikia Spika akikemea na kusikitishwa na rushwa. Siyo hao tu, tumemsikia Jaji Kiongozi wa 1 20 JUNI, 2013 Mahakama Kuu ya Tanzania, akisikitishwa pia na suala la rushwa. Mihimili yote mitatu inalalamika kuhusu rushwa ilivyokithiri. Je, Serikali ina mikakati gani madhubuti ya kuweza kudhibiti au kuondoa rushwa hii? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah, swali lake zuri sana kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwanza, niseme kwamba, Viongozi hawa wanaposema siyo kwamba wanalalamika, ni namna ya kuwatahadharisha Watanzania, muda wote wakae wanajua kwamba rushwa siyo jambo zuri, ni jambo la hovyo. Huo ndiyo ujumbe ambao wote wanajaribu kutupa. Hata Bungeni, mnapokuwa mna jambo, juzi nili- attend ule Mkutano wa APNAC, yale siyo malalamiko ni namna ya kuwaambia Wananchi na Watanzania juu ya uovu wa jambo hili.
[Show full text]