Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Thelathini na Tatu – Tarehe 31 Julai, 2006 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Job J. Ndugai) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI: Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kwa Mwaka wa Fedha 2006/2007. MHE. DR. HAJI MWITA HAJI - (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA HUDUMA ZA JAMII): Maoni ya Kamati ya Huduma za Jamii Kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa Mwaka wa Fedha Uliopita, Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2006/2007. MHE. DR. ALI TARAB ALI - MSEMAJI WA MKUU WA KAMBI YA UPINZANI: Maoni ya Kambi ya Upinzani Kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa Mwaka wa Fedha Uliopita, Pamoja na Maoni Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2006/2007. MASWALI NA MAJIBU Na. 307 Wilaya ya Geita Kuwa Mkoa MHE. ERNEST G. MABINA aliuliza:- 1 Kwa kuwa moja ya vigezo vya kupata Mkoa ni pamoja na idadi ya watu na kwa kuwa Wilaya ya Geita ina watu zaidi ya laki saba na Sengerema ina watu zaidi ya laki tano kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002. (a) Je, ni lini Serikali itatoa kibali cha kuanzisha Mkoa wa Geita ambao utachanganywa na Sengerema na kuwa na idadi ya watu milioni moja na laki mbili? (b) Kama Geita na Sengerema zitachanganywa na bado Mkoa usitoshe. Je, kwa nini Wilaya za Chato na Bukombe nazo zisiongezwe? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, MAAFA NA KAMPENI DHIDI YA UKIMWI) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Ernest Gakeya Mabina, Mbunge wa Geita, lenye sehemu (a) na (b) naomba kutoa maelezo yafuatayo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala unatekelezwa chini ya Sheria Na. 7 ya Mamlaka za Wilaya, Sheria Na. 8 ya Mamlaka za Mji zote za mwaka 1982 na sheria na taratibu za uanzishaji wa Mikoa na Wilaya Na. 12 ya mwaka 1994. Pamoja na sheria hizi vipo vigezo vingine vinavyopaswa kuzingatiwa kabla ya kuanzisha Mkoa. Vigezo hivi ni pamoja na vifuatavyo:- (i) Maombi kupitia kwenye Vikao halali vya Mkoa kabla ya kuleta Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (ii) Eneo linalohusika lazima liwe na ukubwa usiopungua kilometa za mraba elfu kumi (10,000). (iii) Eneo linalohusika lazima liwe na idadi ya watu wasiopungua laki tano (500,000). (iv) Eneo linalohusika lazima liwe na jiografia ambayo inafanya utoaji wa huduma kwa wananchi kuwa mgumu. (v) Rasilimali, fedha, watu na miundombinu. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Geita, ina eneo la km za mraba 6,775 na jumla ya wakazi 7879 kulingana na sensa ya mwaka 2002. Pia ina Tarafa saba (7), Kata 33, Vijiji 187 na vitongoji 826. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:- 2 (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Geita, inakosa baadhi ya vigezo nilivyotaja hapo juu, ili kuweza kuwa Mkoa kamili kwa mfano maombi kupitia katika vikao vya Mkoa na kuwasilishwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, pia eneo lake ni dogo na pia haina jiografia inayozuia utoaji wa huduma kwa wananchi kirahisi. Kwa sababu hiyo, Serikali kwa sasa haina mpango wa kuanzisha Mkoa mpya wa Geita. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Geita ni miongoni mwa Wilaya, ambazo zimeshafanyiwa tathmini na kuonekana kuwa zinastahili kugawanywa. Hivyo basi kwa sasa ofisi yangu inaangalia zaidi uwezekano wa kuigawa Wilaya hii kuwa Wilaya mbili, endapo itakidhi vigezo muhimu vitakavyoruhusu kuigawa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa zaidi ofisi yangu imepata habari kuwa tarehe 5 na 6 Julai, 2006 Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Geita, lilikuwa na kikao na tayari wameridhia kuigawa Wilaya hii kuwa Wilaya mbili. Endapo Mkoa utaridhia na kutoa baraka zake Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa, kwa kuangalia uwezo wa Serikali itaiweka Wilaya hii katika mpango wa kuigawa. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hapo juu, kwa sasa Serikali inaangalia zaidi uwezekano wa kuigawa Wilaya ya Geita na haina mpango wa kuziongezea Wilaya za Sengerema, Chato na Bukombe ili iweze kuifanya ikidhi vigezo vya kuwa Mkoa kamili. MHE. ERNEST G. MABINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vigezo vyote alivyovitaja Mheshimiwa Naibu Waziri na kulingana na swali langu nilikuwa nimezungumzia kwamba Wilaya zote nne zijumuishwe tuwe na Mkoa kamili kufuatana na jiografia ilivyo katika utoaji wa huduma ambao umesababisha Wilaya hizi ziwe na matatizo sana hasa ukizingatia kwamba kutoka Geita kwenda Mwanza ni mbali au kutoka Chato kwenda Bukoba ni mbali na kutoka Bukombe kwenda Shinyanga ni mbali. Je, Serikali haiwezi ikarudisha moyo wake angalau ikazifikiria hizi Wilaya zikajitegemea zikawa hata Mkoa mmoja? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, MAAFA NA KAMPENI DHIDI YA UKIMWI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha kusema katika jibu la swali la msingi, Serikali kwa sasa hivi haina mpango wa kuunda Mkoa wa Geita na kama nilivyokwisha kusema Wilaya ya Geita, ina miundombinu inayoruhusu kuhudumiwa kutoka Mkoa wa Mwanza pale ilivyo na pia ieleweke wazi kwamba ni gharama sana kuunda Mkoa, ambayo gharama ya chini kabisa ni bilioni 6. Hivyo kwa sasa Serikali haina uwezo. MHE. JAMES P. MUSALIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Mwanza ni mkubwa sana una watu zaidi ya milioni 3 una Wilaya 8. Majimbo ya uchaguzi 13 na kwa kuwa ulistahili kugawanywa kabla hata ule wa Arusha. Je, sasa kwa ukweli huu sasa iko tayari kuugawa Mkoa huo ili Geita na zile Wilaya zingine zifanywe Mkoa kama ilivyofanya Arusha? (Makofi) 3 MWENYEKITI: Nafikiri Serikali ilishajibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, MAAFA NA KAMPENI DHIDI YA UKIMWI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani swali hili linajirudia. Hivyo basi bado Serikali haina mpango wa kuugawa Mkoa wa Mwanza na itaendelea kuhudumiwa jinsi ilivyo. Na. 308 Kiu ya Maendeleo Mtwara MHE. DUNSTAN DANIEL MKAPA aliuliza:- Kwa kuwa, Mkoa wa Mtwara uko nyuma sana kimaendeleo katika sekta zote ikiwa ni pamoja na Elimu, Afya, Miundombinu na huduma nyingine za jamii na kwa kuwa, hali hiyo imetokana na sababu kuwa, Mkoa huo ulikuwa ni uwanja wa mapambano wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika hivyo wakati Mikoa mingine inafanya shughuli za maendeleo, Mkoa wa Mtwara haukuweza kufanya hivyo:- (a) Je, Serikali haioni kuwa kuna haja kubwa ya kuupa upendeleo mkubwa Mkoa huo ili uweze kufanana na Mikoa mingine? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kusukuma maendeleo ya haraka katika Mkoa huo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, MAAFA NA KAMPENI DHIDI YA UKIMWI) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Daniel Mkapa, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa Mikoa iliyokuwa katika ukanda wa vita vya ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Hii ni sababu mojawapo iliyofanya Mkoa huu kuwa nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na baadhi ya Mikoa. Kwa kutambua hilo, Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali imekuwa ikiendesha shughuli za maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi na kuleta ustawi wa jamii, kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara. Mheshimwia Mwenyekiti, napenda kumwarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, kuwa Serikali imeona kuwa kuna haja ya kuwa na upendeleo maalum kwa Mikoa yote ya pembezoni ukiwemo Mkoa wa Mtwara. Ili kusisitiza suala hili Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amekwishatoa msimamo wa Serikali ya Awamu ya Nne wa kutoa kipaumbele kwa Mikoa nane (8) ya pembezoni katika kugawa rasilimali. 4 (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua za Serikali nilizozitaja, pia Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweza kuimarisha huduma za jamii katika sekta mbalimbali kwa mfano:- (i) Mheshimiwa Spika, kupitia ufadhili wa wahisani wa miradi au mipango kama District Health Improvement Programme (DHIP), Tanzanian German Programme to Support Health, (GPSH) na Support to the public Health system, Serikali imeweza kuboresha huduma kwa kukarabati zahanati 66, vituo vya afya 3 na kujenga nyumba za watumishi 35 katika zahanati na vituo vya afya vya Mkoa wa Mtwara. Aidha mpango wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa, umeanza kutekelezwa ambapo hatua za awali za ujenzi zimekwishaanza. (ii) Mheshimiwa Spika, katika sekta ya elimu, uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari kupitia mpango wa MMEM na MMES unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa katika Mkoa huu. Aidha sasa hivi Serikali, ina mpango wa kukifanya Chuo cha Ualimu cha Mtwara kuwa Chuo Kikuu Kishiriki na tayari eneo la ujenzi wa chuo hicho limekwishapatikana. (iii) Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya mpango wa ukanda wa maendeleo Mtwara, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Msumbiji inajenga Daraja la Umoja (Unity Bridge) katika Mto Ruvuma eneo la Mtambaa Swala. Aidha, Serikali imekuwa na mipango ifuatayo: x Ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam hadi Mingoyo. x Mradi wa Nishati wa Mtwara ambao upo katika awamu ya pili ya utandazaji wa mabomba na utoboaji visima 4 vya ziada. Kukamilisha kwa mradi huu kutafanya Mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa na umeme wa uhakiki na hivyo kuvutia wawezekaji. x Kuimarishwa kwa Export Processing zone (EZP) katika Bandari ya Mtwara kutachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Mkoa huu. Ili kufanikisha mpango huu, eneo la eneo la Bandari ya Mtwara, limepanuliwa toka hekta 80 hadi hekta 2,626. Bandari imechimbwa na mchanga uliokuwa katika njia ya kupitia meli kuondolewa, ili kuziwezesha meli kuingia na kutoka kwa urahisi na pia minara ya taa za kuongoza meli imejengwa. x Mkoa huu kama Mikoa mingine unatekeleza mipango mbalimbali ya Kitaifa kama TASAF. Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizi zinazofanywa na Serikali, maendeleo ya Mkoa wa Mtwara yataletwa na wananchi wenyewe wa Mtwara. Hivyo basi Serikali inatoa wito kwa wananchi wa Mkoa huu kuwa na umoja, ushirikiano, katika kazi za maendeleo na kufanya kazi kwa bidii ili kukuza uchumi wa Mkoa wa Taifa kwa ujumla.