1458137638-Hs-4-4-20
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA NNE KIKAO CHA NNE – TAREHE 14 JUNI, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 37 Ardhi Iliyotolewa Kujenga Shule ya Msingi Kiraracha MHE. AUGUSTINO L. MREMA aliuliza:- Mzee Pauli Sananga Lekule wa Kijiji cha Kiraracha, Kata ya Marangu, Wilaya ya Moshi Vijijini, alitoa ardhi yake ikatumika kujenga shule ya msingi Kiraracha, Marangu miaka 10 iliyopita akiahidiwa na Serikali kupewa eneo jingine kama fidia lakini mpaka sasa hajapewa eneo jingine kama fidia jambo lililomfanya aione Serikali haikumtendea haki. Je, ni lini Serikali itamlipa haki yake kutokana na makubaliano hayo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Lyatonga Mrema, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa Ndugu Pauli Sananga Lekule wa Kijiji cha Kiraracha, Kata ya Marangu Magharibi, alitoa ardhi yake kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Kiraracha, Kata ya Marangu Magharibi kwa ahadi ya kufidiwa eneo lililoko Njia panda. Aidha eneo ambalo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ilitarajia kumfudia Ndugu Lekule lipo katika mgogoro na kesi bado inaendelea Mahakama Kuu. 1 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo lililopimwa viwanja na kutarajia mlalamikaji lipo katika mgogoro wa kisheria kati ya Halmashauri na wananchi, Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa kesi na mara shauri litakapomalizika Mahakamani mhusika atapewa eneo lake. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali kuhakikisha shauri hili haliendelei kuchukua muda mrefu, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi imeunda timu kwa ajili ya kufuatilia na kuharakisha shauri hili ili ikiwezekana limalizike nje ya Mahakama ili Ndugu Lekule Sananga aweze kupata haki yake mapema.
[Show full text]