Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Tatu – Tarehe 8 Mei, 2014 (Mkutano Ulianza Saa tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Job J. Ndugai) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati ifuatayo iliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA, UTAWALA BORA NA MAHUSIANO NA UTARATIBU: Randama za Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Mahusiano na Uratibu kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MASWALI NA MAJIBU Na. 20 Kuhamisha Soko la Mwika MHE. DKT. AUGUTINE L. MREMA aliuliza:- Soko la Mwika liko barabarani na kuna hatari ya wananchi kugongwa na magari:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta eneo kubwa na kuhamisha soko hilo ili kukwepa athari hizi? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- 1 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Augustino Lyatonga Mrema Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Soko la Mwika liko katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi karibu na barabara. Soko hili lina ukubwa wa ekari 2.5 na idadi ya wafanyabiashara wanaotumia soko hili ni kati ya 1,000 hadi 1,500. Kimsingi kuna ongezeko kubwa la wafanyabiashara kufuatia mahitaji ya walaji ambao wanajumuisha wananchi wa Kata ya Mwika Kaskazini na Mwika Kusini. Kwa kutambua changamoto ya soko hili kuwa karibu na barabara, Halmashauri inaandaa mpango wa kuboresha soko hilo ili liwe la kisasa na kuondoa athari za ajali katika eneo hilo. Mpango uliopo wa Halmashauri ni kukopa katika Bodi ya Mikopo katika Serikali za Mitaa, yaani the Local Government Loans Board ili kutekeleza mpango huo. Kwa sasa Halmashauri iko katika hatua ya upembuzi yakinifu wa eneo hilo ili kujua gharama zitakazohitajika kukamilisha kazi hiyo. Wakati mpango wa muda mrefu wa kuboresha soko hilo unaendelea, Halmashauri imewasilisha maombi kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro kwa barua ya tarehe 17 Januari, 2014 ili iweze kuruhusu ziwekwe alama na tahadhari kwa maana ya kuonyesha maeneo ya kuvukia katika eneo hilo. Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuona umuhimu wa kuchukua tahadhari na kuona haja ya kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao katika soko hilo. Aidha, napenda kutoa rai kwa wananchi kuzingatia Sheria za Barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima. Vilevile wafanyabiashara wote wanakumbushwa kutumia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya biashara na kuacha kuweka bidhaa barabarani kwa ajili ya usalama wao na mali zao. MHE. DKT. AUGUSTINE L. MREMA: Kwa kuwa, wewe Naibu Waziri wa TAMISEMI na umefanya kazi nzuri kwenye Jimbo langu hasa ulivyonisaidia ile barabara ya Uchira, Kisomachi, Kwalaria, kuna Shilingi milioni 300 zilitaka kuibiwa ukazizuia, sasa naomba nikuulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni kuhusu ushuru unaotozwa kwa wafanyabiashara pale Mwika Sokoni. Tumeona kwamba biashara wanayofanya, wanafanya barabarani. Mwanzoni walivyokuwa wanapakia maparachichi na nini, tani moja ya Fuso ilikuwa inatozwa Sh. 20,000/= wakapandisha kuwa Sh. 40,000/=. Fuso diff mbili wakapandisha kutoka Sh. 20,000/= mpaka Sh. 60,000/= wakafanya wale wafanyabiashara wanahangaika, hawajui wafanye nini. Hilo la kwanza. Sijui ni nini msimamo wa Serikali kuhusu huo ushuru. 2 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) La pili, ni wale wafanyabiashara wadogo wandogo akina mama wetu ambao walinichagua mimi na Mheshimiwa Rais; mtu ana ndizi kwenye malboro anatembea nazo tena hapo barabarani; karanga, nini anatozwa Sh. 300/=. Naomba niambiwe msimamo wa Serikali hii, itasaidiaje wale wananchi wa pale Sokoni Mwika waweze kufanya biashara kwa amani na kwa starehe? Jibu! NAIBU SPIKA: Majibu ya swali hilo, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Mwanri. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Kwanza, namshukuru kwa shukrani zake lakini la pili kuhusu ushuru ambao Mheshimiwa Lyatonga Mrema anauzungumzia, hii siyo mara yake ya kwanza kuzungumzia hapa. Mara nyingi sana amekuwa akijitokeza hapa wakati wa Bajeti na kipindi hiki sasa tunamwona amerudi tena. Tatizo hili lilikuwepo na tukazungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, anaitwa Mponzi, tukamwambia kumekuwa na haya malalamiko. Nami ninavyokumbuka, ushuru huu ulishuka kutoka Sh. 40,000/= kwa Fuso ukaenda kwenye Sh. 20,000/=. Ulibadilika huu. Sasa umeshuka, umerudi hapa. Mheshimiwa Mbunge utatusaidia kufuatilia kujua kwamba inaendelea hivyo au haiendelei hivyo. La pili, hili swali la pili analoliuliza linalohusu kitu kinachoitwa Kodi Ushuru Wenye Kero, walikuwa wanaitwa Nuisance Taxes. Hili nataka niliseme hapa kwasababu nimemsikia Waziri wa Nchi akizungumzia kuhusu Halmashauri na mkakati wa kuongeza mapato ya Halmashauri. Wakati alipokuwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Bazil Mramba, ushuru huu uliondolewa kwasababu ulionekana unakuwa kero. Kwanza gharama ya kwenda kutoza. Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alinituma Kigoma kurudi kule mara ya pili kwenda ku-demonstrate. Naomba ni-demonstrate. Wanaozungumzwa hapa ni wale wanaobeba samaki kwenye ki-table au kwenye ungo, kwenye tray, wanasema haya samaki! Haya samaki tena! Haya samaki! Wateja wanasema, samaki! Anakwenda anauza. Maana watatoka watu hapa watakwenda na magunia wamekaa pale wanasema tuwaambie ushuru walipe. Wale wanaouza vitumbua; haya vitumbua! Haya vitumbua! Vitumbuaaa! Ameshikilia hivi, hakai mahali pamoja; anatembea kwenye soko hivi, anatoka nje, anakwenda ndani. Ushuru huo umepigwa marufuku na Serikali! (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mwananchi anayezungumzwa hapa ni mwananchi ambaye anakwenda kujikimu. Mwananchi huyu ukiangalia hata anapokwenda sokoni, haendi kwa kupanda pikipiki wala kwa kutumia bajaji, anakwenda kwa mguu. Akifika kule sokoni vitu anavyonunua; ananunua 3 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) utumbo wa taulo, utumbo mweupe, sabuni ya kuoga na kufua ni hiyo hiyo ya kufulia. Huyu mama akitoka pale anachukua mafuta ya taa kwa chupa ile ya Kilimanjaro nusu. Hawa wananchi ndiyo ambao Serikali imesema wasitozwe ushuru wa aina yoyote. Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge mwende mkatusaidie kwenye hilo jambo. Mheshimiwa Lyatonga Mrema nakushukuru kwa kulileta hili jambo hapa. Lakini wale akina mama wanaokwenda na Fuso pale na mikungu ya ndizi inayotoka Vunjo, inakwenda Arusha na Tanga, wale wanalipa ushuru kwasababu wanafanya business. NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Tunaendelea na swali linalofuata, Mheshimiwa Kakoso. Na. 21 Tatizo Sugu la Maji Mpanda Vijijini MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Kuna tatizo sugu la maji katika Jimbo la Mpanda Vijijini. Je, Serikali imejipanga vipi kumaliza tatizo hilo hasa katika vijiji vya Kamsanga, Bugwe, Sibwesa, Mpemba, Mwese na Bujombe? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mpanda inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 179,136 ambapo kati yao wakazi 85,985 sawa na asilimia 48, wanapata huduma ya maji safi na salama. Hivyo bado iko changamoto ya upatikanaji wa huduma hii kwa wakazi wa Wilaya hii. Ili kutatua tatizo la maji katika vijiji, hivyo Serikali inatekeleza mradi wa maji wa kisima kifupi kimoja katika Kijiji cha Kamsanga na tayari upimaji wa eneo la kuchimba kisima kirefu umefanyika na kitachimbwa kabla ya mwezi Juni, 2014. Vilevile katika Kijiji cha Bujombe katika bajeti ya mwaka 2013/2014 kimetengewa Shilingi milioni 8.0 kwa ajili ya kisima kifupi kimoja. 4 Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Mwese Serikali kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki katika mwaka 2013/2014 imepanga kutumia Shilingi milioni 65, kwa ajili ya ujenzi wa maji mserereko utakaohudumia wananchi wengi zaidi kukiwa na vituo vya kuchotea maji vitano. Aidha, kijiji hiki pamoja na Kijiji cha Mpembe vimeingizwa katika Mpango wa Kuleta Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambapo miradi ya maji yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.4 inatarajiwa kujengwa ifikapo 2015/2016. Kijiji cha Sibwesa kina visima vifupi viwili, na mwaka huu wa fedha 2013/2014 Serikali imetenga Shilingi milioni 53 kwa ajili ya uchimbaji wa kisima na ujenzi wa lambo kwa matumizi ya mifugo kwa eneo hilo. Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imepokea kiasi cha Shilingi milioni 742.6 kwa mwaka wa fedha 2013/2014, fedha hizi zikiwa ni kuendelea kutekeleza miradi yote ya maji kama ilivyotajwa hapo awali. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufuatilia kwa karibu ili kiasi cha fedha kilichobaki kiweze kupatikana kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imetenga jumla ya Shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 15 Wilayani humo miradi hii itakapokamilika inatarajiwa kuhudumia wananchi wapatao 28,886. Mheshimiwa Naibu Spika, utekeleazaji wa miradi ya maji katika vijiji vingine vikiwemo Kabage na Bugwe kufanyika kwa awamu kwa kuzingatia upatikanaji wa rasilimali fedha. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kakoso, swali la nyongeza. MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado kuna changamoto kubwa sana