Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE __________________ MKUTANO WA TANO Kikao cha Nne – Tarehe 11 Novemba, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe.George B. Simbachawene) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 41 Serikali Kuwatengea Maeneo Wafanyabiashara Ndogondogo MHE. JOSEPHINE T. CHAGULLA aliuliza:- Biashara ndogondogo kama Wamachinga na Mama lishe, huwawezesha wananchi kujiajiri na kujipatia vipato ili kukabiliana na ugumu wa maisha:- Je, kwa nini Serikali isiwajengee wafanyabiashara hao wadogowadogo maeneo ya kufanyia biashara ili kuondoa kero na usumbufu wanaoupata? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Thabitha Chagulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ndogondogo ni biashara zinazoendeshwa katika mfumo wa wa sekta isiyo rasmi (Informal Sector) zikiwa na mitaji midogo. Serikali inatambua kuwepo kwa wafanyabiashara ndogondogo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kwa maana ya Vijijini na Mijini. Kundi hili la Watanzania linachangia katika ukuaji wa ajira za kujiajiri, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo likiwemo Jiji la Dar-es-Salaam ambapo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, maeneo yaliyotengwa ni Mchikichini, Mtaa wa Kilwa, Kibasila, Kigogo Sambusa, Mtaa wa Lumumba, Soko la Kisutu, Ilala na Buguruni, masoko mapya ya Kitunda, Tabata, Segerea na Ukonga. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, maeneo ya TAZARA, Tandika, Mbagala Rangi Tatu, Soko la Temeke Stereo na masoko mengine na Manispaa ya Kinondoni maeneo ya Kapera, Babati, Manzese, Msufini, Mikocheni, Sinza I na II, Mabibo, Mburahati, Urafiki, Tegeta, Makumbusho na Kawe.
[Show full text]