Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Arobaini na Sita – Tarehe 13Agosti, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) DUA Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2011/2012. HOJA ZA SERIKALI Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Wizara ya Nishati na Madini (Majadiliano yanaendelea) MICHANGO KWA MAANDISHI MHE. KISYERI W. CHAMBIRI: Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni zaidi ya miaka kumi, umeme umepita katika maeneo ya Maweni, Majengo, Mukuyuni A, Mukuyuni B, Ari Halaa, Singu, Signo. Umeme huo ni wa msongo wa KV 33. Hakuna juhudi zozote zimefanywa kuwapatia wananchi umeme katika maeneo hayo. Nataka kufahamu lini wananchi wa maeneo hayo watapatiwa umeme? Mheshimiwa Spika, pili, katika bajeti ya TANESCO ya mwaka huu, fedha zimetengwa kupeleka umeme mtaa wa Muruki, Babati Mjini. Meneja wa Mkoa amekataa kupeleka umeme Muruki kwa kisingizio kuwa hakuna njia. Halmashauri ya Mji wameandika barua TANESCO na kuthibitisha njia ipo. Lini wananchi wa Muruki watapata umeme? Mheshimiwa Spika, tatu, ingawa tayari wameleta nguzo kwa ajili ya umeme Mamagha, Banga, Himiti, Haraa, hoja sasa ni muda mrefu sana, lini umeme utawekwa katika maeneo hayo? Mheshimiwa Spika, nne, muda mrefu sasa tumeomba umeme upelekwe Vijiji vya Imbilili, Mtuka, Malangi na Kiongozi. Lini maeneo hayo yatawekwa katika mpango na kupelekewa umeme? Mheshimiwa Spika, pamoja na hoja hizo hapo juu, nimeomba Meneja wa Mkoa atayarishe makisio ya maeneo hayo kupata umeme.
[Show full text]