1450872983-17Machi20
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA KUMI NA TISA Kikao cha Kwanza - Tarehe 17 Machi, 2015 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) WIMBO WA TAIFA (Hapa Wabunge Waliimba Wimbo wa Taifa) D U A Spika (Mhe. Anna S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu, hatua inayofuata! TAARIFA YA SPIKA SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, toka tuondoke kipindi kilichopita na tulipoanza shughuli za Kamati, tulipata msiba mkubwa. Ndugu yetu Mheshimiwa John Damiano Komba, alifariki tarehe 28 Februari, 2015 na tukamzika tarehe 3 Machi, 2015, nyumbani kwao Lituhi Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma. Mheshimiwa John Komba, kama mlivyoelezwa wakati wa msiba, alikuwa kazini mpaka wakati umauti unampata. Ilikuwa siku hiyo wanajiandaa kwenda Nchi ya Ethiopia kwa shughuli za Kamati kama ilivyo kawaida na katika maandalizi hayo ndiyo jioni yake aliondoka duniani. Kwa hiyo, kilikuwa kifo cha ghafla sana. Kwa sababu hiyo, Waheshimiwa Wabunge, nawaombeni msimame, tuomboleze kwa muda wa dakika moja. (Hapa Wabunge walisimama kwa dakika moja kumkumbuka aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Marehemu Mheshimiwa Capt. John Damiano Komba aliyefariki dunia tarehe 28 Februari, 2015) SPIKA: Mwenyezi Mungu, aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi; amen. Ahsante, tukae. Taarifa ya pili, Waheshimiwa Wabunge, kama mlivyosikia kwenye Vyombo vya Habari, Waziri Mkuu hivi sasa yupo Japani na badala yake amemteua Mheshimiwa John Samuel Sitta, Waziri wa Uchukuzi, aweze kushika nafasi ya kuongoza shughuli za Serikali hapa Bungeni kwa kipindi hiki ambacho hatakuwepo. Sasa tunakukabidhi. (Makofi) Katibu, hatua inayofuata! 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunaanza na maswali ya Ofisi ya Waziri Mkuu na atakayeuliza swali letu la kwanza ni Mheshimiwa Josephine Genzabuke.
[Show full text]