MKUTANO WA WA KUMI NA TANO Kikao Cha Ishirini – Tarehe 3 Mei
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA _________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA WA KUMI NA TANO Kikao cha Ishirini – Tarehe 3 Mei, 2019 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Mkutano wetu wa Kumi na Tano na leo ni Kikao cha Ishirini. Katibu. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: Maswali. SPIKA: Katibu njoo kwanza kabla hatujaanza maswali. Katibu tena. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: TAARIFA YA SPIKA SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kama ambavyo tayari mnafahamu, ndugu yetu Dkt. Reginald Abraham Mengi alifariki huko Dubai usiku wa kuamkia jana tarehe 2 Mei, 2019. Dkt. Mengi alikuwa ni Mtanzania ambaye kwa bidii, juhudi na maarifa aliweza kukua kiuchumi kutoka maisha duni ya kijijini hadi kufikia kuwa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa hapa kwetu Tanzania, Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Katika kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa, sisi Bunge tunaungana na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, familia ya Marehemu na Watanzania wote tukimshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa wote na tukimshukuru Mheshimiwa Mengi kwa mchango wake mkubwa usiopimika kwetu Watanzania. Tutamkumbuka daima kwa jinsi ambavyo alisaidia sana hifadhi ya mazingira hasa maeneo yanayozunguka mlima Kilimanjaro kwa kupanda miti mingi sana kwa mamilioni bila kuchoka. Alikuwa ni mmiliki wa vyombo mbalimbali vya habari zikiwemo televisheni, redio na magazeti kadhaa, alikuwa mmiliki wa viwanda kadhaa hasa kwenye sekta ya manufacturing. Pia, Dkt. Mengi alikuwa ni kiongozi wa Umma akiwa ni Mwenyekiti wa Bodi mbalimbali ikiwemo IPP Limited na mengine mengi ya binafsi na ya Umma kama kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mazingira, Mwenyekiti wa NBAA, Kamishna wa TACAIDS, Mwenyekiti wa CTI na nyadhifa nyingine nyingi. Pia Dkt. Mengi katika maisha yake alipata tuzo nyingi za Kitaifa na Kimataifa. Dkt. Mengi alijulikana kwa utoaji wake mkubwa wa misaada ya kijamii (philanthropist), alitoa sana katika ujenzi wa misikiti, ujenzi wa makanisa; alitoa sana kwa masikini na wasiojiweza, wanyonge na walemavu. Alisaidia sana katika maeneo ya tiba ya wagonjwa mbalimbali wakiwemo wagonjwa wa moyo. Ni hivi majuzi tu ambapo Dkt. Mengi alichangia shilingi milioni 50 kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutuunga mkono kwenye mradi uliobuniwa na Wabunge Wanawake (TWPG) wa kujenga vyoo vya mfano kwa mtoto wa kike katika majimbo yote Tanzania. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe, Amina. 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Katibu. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Maswali tunaanza na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi. Na. 158 Barabara Inayounganisha Umba na Mtae MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Mafuriko yaliyotokea Mlalo mwaka 1993 yalisababisha uharibifu mkubwa kwa barabara inayounganisha Tarafa za Umba na Mtae:- Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kukarabati barabara hiyo muhimu? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, barabara inayounganisha Tarafa za Umba na Mtae yenye urefu wa kilometa 12.7 inajulikana kama barabara ya Mtae – Mtii – Mnazi. TARURA Wilaya ya Lushoto imekamilisha usanifu na tathmini ya kuifanyia matengenezo makubwa, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kinahitajika. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia matengenezo hayo kwa kuwa inatambua umuhimu wa barabara hii. 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) SPIKA: Mheshimiwa Shangazi, nimekuona. MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu hayo, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (a) Kwa kuwa barabara hii ya Mtii – Mtae – Mnazi, kilometa 12.7 pamoja na Kwekanda – Hekcho – Rugulu hadi Mkomazi kilometa 17.5, zote hizi tumeziweka katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2019/2020 na bajeti tayari tumeshapitisha. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi wa Mlalo? (b) Kwa kuwa, barabara hizi siyo tu kwamba zinaunganisha Tarafa za Umba – Mlalo na Mtae, lakini pia zinaunganisha wilaya jirani za Korogwe na Same: Je, Serikali haioni kwamba kwa kutofanya wepesi wa kurekebisha barabara hizi inakuwa ni kikwazo kwa fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Mlalo? SPIKA: Majibu ya maswali hayo, Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kipekee kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Shangazi, amekuwa akipigia kelele sana kuhusu barabara hii ya kwenda Mtae na mara nyingi sana amefika ofisini kwetu. Naomba nimpongeze katika hilo. Mheshimiwa Spika, katika swali lake anaulizia kwamba tayari bajeti imeshapitishwa, nini tamko la Serikali kuhusiana na ujenzi wa barabara hiyo? Bajeti ambayo imepitishwa kwa ajili ya Wilaya ya Lushoto ni jumla ya shilingi bilioni 1.8. Kama katika bajeti yao na barabara hii ipo, ni vizuri wakahakikisha kwamba barabara hii ni muhimu ikaanza kutengenezwa mapema. Mheshimiwa Spika, kwa vile bajeti inahusu shilingi bilioni 2.5 ambayo siyo rahisi, Bajeti ambayo imepitishwa ni 1.4 na wao wanahitaji shilingi bilioni 2.5; na kilometa katika 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Wilaya ya Lushoto ni jumla ya 935. Naomba Meneja wa TARURA ahakikishe katika vipaumbele vya barabara za kutengenezwa iwe pamoja na barabara hii. Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anaulizia je, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza barabara ya kuunganisha kwenda Lushoto na wilaya nyingine kwa maana ya fursa ya kiuchumi? Ni ukweli usiopingika kwamba maeneo ambayo barabara haipitiki tunakuwa tunawanyima wananchi fursa ya kiuchumi. Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika pia kwamba bajeti yetu haiwezi ikakidhi kwa mara moja maeneo yote. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira na yeye mwenyewe ni shuhuda, tangu tumeanzisha chombo cha TARURA kazi inayofanyika ni nzuri na hakika na barabara hii itawekwa kipaumbele ili iweze kutengenezwa. (Makofi) SPIKA: Nilikuona Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Barabara, Mheshimiwa Kakoso. MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Ikola – Kasangantongwe imeharibika sana na mvua zilizonyesha na kusababisha wananchi kushindwa kutumia barabara hiyo na kuanza kutumia njia ya majini ambayo siyo salama. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha kuijenga barabara hiyo ya Kasangantongwe? SPIKA: Majibu Mheshimiwa Naibu Waziri, Josephat S. Kandege, Mbunge wa Kalambo, tafadhali. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) Mheshimiwa Spika, nimepata fursa ya kutembelea Jimbo la Mheshimiwa Kakoso na katika maeneo ambayo barabara zinajengwa unaona thamani ya pesa ni pamoja na Jimboni kwake. Yeye mwenyewe anakiri kwamba barabara hii ambayo anaitaja 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) imeharibika kutokana na mvua ambazo zinanyesha na ni ukweli usiopingika kwamba katika maeneo ambayo mvua ni za uhakika ni pamoja na Jimboni kwake. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumwagiza Meneja wa TARURA ili akaangalie uharibifu wa hiyo barabara namna aone namna ambavyo anaweza angalau akafanya maboresho katika maeneo korofi sana ili barabara hii iweze kuendelea kupitika na wananchi waendelee kufaidi matunda ya CCM. SPIKA: Tunahamia swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum. Na. 159 Barabara ya Segerea – Sheli – Kipawa MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:- Je, ni lini barabara ya Segerea – Sheli kwenda Kipawa kupitia Seminari itaanza kutengenezwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, barabara ya Segerea – Sheli – Kipawa kupitia seminari yenye urefu wa kilometa 2.93 inasimamiwa na TARURA Manispaa ya Ilala, imesajiliwa kwa jina la Majumba Sita, Sitakishari. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, barabara hiyo imechongwa kwa grader ili kuiwezesha kupitika. Hata hivyo, barabara hii inakatisha katika mto Msimbazi ambapo hakuna daraja. Daraja linalohitajika kujengwa ni kubwa na usanifu wake ulishafanyika. 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo inatokana na mto kutanuka, hivyo inahitajika kufanyiwa study ya kina na mapitio ya usanifu wa awali ili kupata mahitaji halisi ya ujenzi wa daraja kutokana na changamoto hiyo. Mara baada ya kukamilika kwa mapitio ya usanifu na tathmini ya gharama Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kujenga daraja na kuifanyia matengenezo makubwa barabara hii. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia TARURA imeitengea barabara hii jumla ya shilingi milioni 43 kwa ajili ya matengenezo ya maeneo korofi. SPIKA: Mheshimiwa Anatropia swali la nyongeza. MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa ni zaidi ya miaka 15 wananchi wa Segerea kupitia hiyo barabara ya Majumba Sita, Sitakishari wamekuwa wanapitia hiyo adha ya kukosa daraja, lakini ni kiungo kikubwa cha Gereza la Segerea, Seminari na sekondari mbalimbali: Je, Serikali haioni ni wakati sahihi wa kutengeneza hilo daraja ili kuondokana na hiyo adha? Mheshimiwa Spika, swali la