Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ BUNGE LA KUMI NA MOJA MKUTANO WA SABA Kikao cha Hamsini na Moja – Tarehe 20 Juni, 2017 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Najma Murtaza Giga) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. RAMADHAN ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Maswali Ofisi ya Rais - TAMISEMI, tunaanza na Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, sasa aulize swali lake. Na. 416 Mkakati wa Kuhakikisha Manispaa ya Mpanda Inakuwa Safi MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:- Pamoja na lengo la Serikali kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi na kuzuia magonjwa ya mlipuko, Manispaa ya Mpanda ina changamoto ya ukosefu wa vifaa kama magari ya taka. 1 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Manispaa ya Mpanda ina maroli mawili kati ya manne yanayohitajika kwa ajili ya kuzolea taka ngumu. Kutokana na changamoto hiyo, uongozi wa Manispaa umejiwekea mikakati ifuatayo:- (i) Manispaa ya Mpanda imebinafsisha (outsource) shughuli ya uzoaji na udhibiti wa taka kwa mzabuni anayelipwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, mMzabuni huyu ana magari mawili na hivyo kufanya jumla ya magari kuwa manne. (ii) Manispaa ya Mpanda imeanzisha mpango shirikishi jamii wenye jumla ya vikundi vya uzoaji na udhibiti wa taka ngumu katika mitaa 17, vimejengwa vizimba vitano kwa ajili ya kuhifadhia taka na vitakabidhiwa mikokoteni 17 tarehe 21/06/2017 siku ya uzinduzi. (iii) Kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi wananchi wote hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya makazi, biashara na maeneo mbalimbali ya kufanyia kazi. (iv) Kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi usafi wa kina hufanyika ambapo wananchi pamoja na viongozi mbalimbali hushiriki kufanya usafi katika maeneo yao. (v) Siku hiyo ya Ijumaa kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi 2 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) saa 3:30 asubuhi watumishi wa Manispaa hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya Ofisi ya Manispaa. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhamasisha usafi nchini ili kuepuka mlipuko wa magonjwa na kuongeza unadhifu wa miji yetu. MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Majibu ya Mheshimiwa Waziri nadhani hayana uhalisia na mazingira ya Manispaa ya Mpanda. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Machi, 2014 Halmashauri ya Mpanda ilitenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa gari la kukusanya taka, gari la kisasa na siyo haya malori mawili ambayo umeyasema. Kutokana na ubadhirifu ambao umefanyika kwenye Manispaa hii, Serikali inachukua hatua gani kwa huyu mzabuni aliyetumia fedha hizi na mpaka sasa hajarudisha na baadhi ya hao watendaji ambao wamekula pesa hii, wananchi wa Manispaa ya Mpanda hivi tunavyoongea wanashinda na takataka ndani, wanashindwa kuzitoa na Manispaa imeshindwa kukusanya hizi taka kwa wakati. Serikali inamchukulia hatua gani huyu Ndugu Kisira pamoja na watendaji waliokula pesa hizi katika Manispaa ya Mpanda? (Makofi) Swali la pili, imekuwa ni tabia ya Serikali kuendelea kuhamasisha wananchi kufanya usafi kwenye maeneo yao, lakini kitu kibaya zaidi ni kwamba wananchi hawa wanalazimishwa kufunga maduka, kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 1:00 asubuhi mpaka saa 4:00 aasubuhi na siyo Mkoa wa Katavi peke yake au Manispaa ya Mpanda peke yake ni nchi nzima, ikiwepo na maduka ya Dar es Salaam, Kigoma, Mbeya, Mwanza pamoja na Katavi. MWENYEKITI: Mheshimiwa uliza swali umeshaeleweka. MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tabia hii ya kuendelea kufunga maduka, je, Serikali 3 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) hamuoni kwamba mnapoteza uchumi wa wananchi wao kuendelea kufunga maduka na huku wakiendelea kufanya usafi? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Rhoda tutende haki, swali lako ulilouliza halafu una ajenda, inawezekana swali lako ungeli-frame vizuri lingepata majibu mazuri sana. Kwa sababu swali lako lilikuwa linajenga suala la ubadhirifu wa fedha zilizotengwa, ungelitengeneza vizuri halafu tungeweza kupata majibu mazuri sana katika hilo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimesema kwamba pale kuna magari ya taka mawili, kama kuna suala la ubadhilifu hiyo ni ajenda nyingine, tunachotakiwa kukifanya ni kwamba hatuvumilii ubadhirifu wa aina yoyote, na kama ubadhirifu huo upo, tutaenda kuufanyia kazi tutaenda kufuatilia nini kilichojiri katika Manispaa ya Mpanda kama fedha zilizitengwa lakini hazikutumika vizuri katika suala hilo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la ajenda kwamba siku ya Jumamosi wananchi wanafunga maduka, kumbukumbu yangu Waziri Mkuu hapa aliulizwa na Mheshimiwa Ulega, Mbunge wa Mkuranga katika suala ya siku ya Jumamosi utaratibu wa kufanya, lengo kubwa ilikuwa usafi ufanyike lakini usizuie shughuli za wananchi katika maeneo hayo. Mheshimiwa Mwenyekiti, agizo hili limeishatolewa kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya katika maeneo yao tunapofanya utaratibu wa usafi tuangalie modality nzuri usafi ufanyike, lakini kama kuna mambo mengine ambayo saa nyingine yanahusu shughuli mahsusi zinaweza kufanyika. Hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo naomba tufanye rejea ile vizuri tusitoe majibu mawili itakuwa ni sub-standard siyo vizuri. (Makofi) 4 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niichukue kwamba hoja yako ya usafi ni ajenda yetu ya Kitaifa, lazima kama Wabunge, lazima kama Viongozi tusimame pamoja katika jambo hili. (Makofi) MWENYEKITI: Mheshimiwa Lubeleje na baadaye Mheshimiwa Selasini. MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa magari ya kunyonya maji machafu na kuzoa taka siyo lazima tu iwe kwenye Manispaa au Majiji, hata Wilaya zetu tunahitaji magari ya kunyonya maji machafu na magari ya kuzoa taka. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka gari la kunyonya maji machafu pamoja na kuzoa taka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI naomba kujibu swali la Mzee wangu Lubeleje, mimi namuita greda la zamani makali yale yale kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mzee Lubeleje naomba tuiweke katika vipaumbele vyetu vya Halmashauri, naomba nikusihi Mheshimiwa Lubeleje katika mpango wenu wa Halmashauri hilo jambo mkiliainisha, na sisi katika kupitisha bajeti tutalipa kipaumbele. Ninajua kwamba kweli ni jambo la msingi kufanya usafi na kuwa na mitambo hii ya kuzolea taka na kunyonyea maji, kwa hiyo mkiweka katika kipaumbele, mchakato wa bajeti ujao kama Mpwapwa mtaweka kipaumbele basi sisi hatutasita kuhakikisha jambo hilo tunaliwekea kipaumbele hilo ili Mpwapwa mpate gari la kunyonyea maji taka. MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Takataka zinaweza zikasababisha uchumi mkubwa sana kwa wananchi wetu kwa sababu taka 5 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) zinaweza zikatengeneza matofali, zinaweza zikazalisha umeme, zinaweza zikatengeneza mbolea nzuri sana na sasa hivi kwa sababu maeneo ya kutupa taka yanaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali isifanye uamuzi wa makusudi, kabisa ikaleta hii teknolojia nchini, ikaanza na majiji yetu ili kuwafanya wananchi wakapata kipato kwa kukusanya takataka na kuzipeleka kwenye maeneo hayo ambayo yanaweza yakazi-process na kuzalisha vitu vingine kwa faida ya Taifa kwa ujumla? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Selasini jambo lako ni zuri sana, ndiyo maana katika ofisi yetu tuna mradi mmoja unaitwa Strategic City Project, katika miji mbalimbali tumetenga utaratibu wa kutengeneza haya madampo ya kisasa, ambapo ukienda Mbeya utayakuta, hapa Dodoma tunajenga na maeneo mbalimbali tunatengeneza madampo kama yale. Lengo letu kubwa ni kwamba taka zitakazozolewa baadaye ziingizwe katika system maalum kuweza ku-convert katika shughuli zingine. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sasa hivi tunakaribisha wawekezaji mbalimbali ambao katika njia moja au nyingine watasaidia ukusanyaji wa hizi taka kuweka katika malighafi nyingine, ikiwemo suala zima la utengenezaji wa mkaa. Kwa hiyo, ni hilo ni jambo zuri Serikali na wadau mbalimbali tushirikiane kwa mustakabali wa nchi yetu ambao mwisho wa siku taka hizi baada ya kuwa uchafu inaweza ikawa malighafi na zitasaidia kujenga uchumi katika nchi yetu. (Makofi) MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri, tunaendelea na Wizara ya Fedha na Mipango Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, sasa aulize swali lake. 6 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Na. 417 Risiti za EFD Kutodumu kwa Muda Mrefu MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:- Electronic Fiscal Device (EFD) risiti hazidumu kwa muda mrefu kwani zinafutika maandishi ndani ya muda mfupi. Je, TRA wataridhika na maelezo ya mlipakodi bila ushahidi wa risiti? NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti,