Tarehe 12 Aprili, 2019
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Tisa – Tarehe 12 Aprili, 2019 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Andrew J. Chenge) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. NEEMA MSANGI - KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Swali letu la kwanza asubuhi ya leo linaelekezwa kwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na linaulizwa na Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto. Na. 68 Kukarabati Shule za Msingi na Sekondari - Lushoto MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Serikali imekuwa na utaratibu wa kukarabati shule zake za msingi na sekondari nchini:- Je, ni lini Serikali itazifanyia ukarabati Shule za Msingi Kwemashai, Bandi, Milungui, Kilole na Shule za Sekondari za Ntambwe, Ngulwi - Mazashai na Mdando? 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MWENYEKITI: Ahsante. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Waitara. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2018/2019, Serikali kupitia Program ya Lipa Kulingana na Matokeo (EPforR) imepeleka jumla ya shilingi milioni 467 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, matundu sita ya vyoo na madarasa mawili katika Shule ya Msingi Shukilai (Shule ya Elimu Maalum) na ujenzi wa mabweni mawili Shule ya Sekondari Magamba, ujenzi wa bweni moja na madarasa mawili Shule ya Sekondari Umba. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa Fedha 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 2,392 ya madarasa nchi nzima ambapo kati ya fedha hizo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imepewa kiasi cha Sh.512,500,000 kwa ajili ya kukamilisha maboma 46 ya madarasa shule za sekondari.
[Show full text]