Tarehe 9 Mei, 2019
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA _________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Ishirini na Nne – Tarehe 9 Mei, 2019 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tukae. Katibu. NDG. JOSHUA CHAMWELA – KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2019/2020. MHE. ASHA MSHIMBA JECHA (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU): Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MHE. QAMBALO W. QULWI – NAIBU MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Kuhusu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano juu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020. NAIBU SPIKA: Ahsante. Waheshimiwa tunaendelea. Katibu. NDG. JOSHUA CHAMWELA – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Maswali, tutaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi sasa aulize swali lake. Na. 196 Serikali Kuzipatia Waganga Zahanati za Jimbo la Manyoni Magharibi MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:- Wananchi wa Manyoni Magharibi kwa kushirikiana na Serikali kupitia miradi mbalimbali ikiwemo TASAF wamejenga zahanati katika Vijiji vya Gurungu, Sanjaranda, Kitopeni, Ipande, Doroto, Itagata, Kalangali, Makale, Mwamagembe na Kintanula, lakini mpaka sasa zahanati hizi hazina Waganga:- Je, ni lini Serikali itazipatia zahanati hizo Waganga, ili wananchi wapate huduma kufuatana na sera yake? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, majibu.
[Show full text]