HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA WAKATI AKIFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA MAJADILIANO YA MAKANDARASI ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MTAKATIFU GASPAR – DODOMA, TAREHE 17 JULAI 2008.

Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa (Mb.), Waziri wa Miundombinu;

Mheshimiwa , (Mb.), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu;

Ndugu , Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi;

Wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi;

Wenyeviti wa Bodi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Miundombinu;

Mhandisi Boniface Muhegi, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi;

Ndugu Makandarasi mliopo hapa;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

Natoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu kwa kuninialika kufungua Mkutano wa Mwaka wa Majadiliano ya Makandarasi na kuweza kuzungumza nanyi pamoja na Washiriki wengine kwa ujumla.

Nimefarijika kusikia kwamba Mkutano huu wa Majadiliano unashirikisha Wamiliki na Wakurugenzi wa Makampuni ya Ukandarasi, Viongozi Wakuu na Wadau wa Sekta ya Ujenzi. Lengo likiwa ni kutathmini Utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano uliofanyika mwaka uliopita. Vilevile, ni mategemeo yangu kwamba, mtatumia fursa hii kujiwekea Mikakati na Malengo ya namna ya kukabili changamoto mbalimbali za kisekta pamoja na kuondoa matatizo yanayoikabili Sekta ya Ukandarasi.

Ndugu Mwenyekiti, baada ya kupata mwaliko, nilifurahi na kukubali kuhudhuria kwa sababu kuu mbili:

Kwanza, Makandarasi ni Wafanyabiashara wenye umuhimu wa pekee kwa maendeleo ya Taifa. Miundombinu ya aina zote ikiwemo ujenzi wa Barabara, Makazi ya Watu, Nyumba za Ibada, Majengo ya Mikutano, Majumba ya Starehe, Viwanda, Mitambo, njia za kupeleka Umeme, Mahospitali, Shule, Migodi ya Madini na Malambo ya Maji, yote haya ni matokeo ya kazi za Makandarasi. Vilevile, kiasi kikubwa cha Bajeti ya Serikali hutumika kwenye Sekta hii ambayo hutoa ajira na kuwanufaisha Watanzania wengi kwa namna mbalimbali. Wapo Wahandisi, Wapasua Mbao, Mama Lishe kwa ajili ya Mafundi, Mafundi Uashi, Waponda Kokoto Wadogo Wadogo, Waendesha Mikokoteni na wengi wengineo ambao hunufaika na shughuli za Wakandarasi.

Pili, hivi sasa dunia inaendeshwa na Mfumo wa Utandawazi ambao unatawaliwa zaidi na mbinu za hali ya juu za Sayansi, Teknolojia na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Makandarasi wetu hawawezi kuiepuka hali hiyo, hivyo nao wanatakiwa kuongeza kasi ya ubunifu ili wasiachwe nyuma.

Ndugu Mwenyekiti, Mada ya mwaka huu inahusu “Uendeshaji Bora wa Makampuni ya Ukandarasi”. Serikali ni Mdau na mtumiaji mkubwa wa Makandarasi na mwenye dhamana ya kuwaendeleza Makandarasi Wazalendo. Kwa maana hiyo, azma ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na ni kuendelea kuwaondolea Wananchi kero za Umaskini, Ujinga na Maradhi kwa kadri ya uwezo uliopo. Nia ya Serikali ni kuona miundombinu kama barabara, usambazaji wa maji, nishati, shule na huduma za afya inaimarishwa na kuendelezwa. Nia hii nzuri ya Serikali inadhihirika kwenye Bajeti ya Mwaka huu 2008/2009 ambapo fedha nyingi imetengwa kwa ajili ya miundombinu. Jumla ya Shilingi bilioni 593.2 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ya Barabara na Shilingi bilioni 41.2 kwa ajili ya miradi ya Viwanja vya Ndege na Reli. Pamoja na fedha hizo, Mfuko wa Barabara umeweza kuongeza fedha za matengenezo kutoka Shilingi bilioni 85.7 mwaka 2006/2007 hadi bilioni 218.5 mwaka 2008/2009. Kiasi hiki cha fedha ni kingi sana iwapo kitasimamiwa na kutumika vizuri. Wanaopewa dhamana ya kusimamia miradi hiyo lazima kazi zao zionyeshe thamani ya fedha hiyo (value for money).

Ndugu Mwenyekiti, ongezeko kubwa la Bajeti ya Serikali katika Sekta ya Ujenzi ni ishara kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2008/2009 kutakuwa na ongezeko kubwa la kazi za ujenzi. Hivyo basi, ni jukumu la Bodi kuhakikisha inasimamia vizuri shughuli za Makandarasi. Wale wote ambao wanashindwa kufanya kazi zao kwa kuzingatia muda na ubora wadhibitiwe ili fedha za Serikali ziweze kutumika kama zilivyopangwa. Lengo ni kupata miundombinu bora na salama kwa maendeleo ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

Pamoja na juhudi hizo, bado baadhi ya Makandarasi wamekuwa wakifanya kazi ambazo hazizingatii muda na ubora. Wote tunasikia na kuona ucheleweshwaji wa miradi ambayo mara nyingi husababisha gharama za ujenzi na kibaya zaidi, kuharibika kwa miundombinu iliyokamilika katika kipindi cha muda mfupi. Hivyo basi, tunayo changamoto mbele yetu ya kuhakikisha kwamba, ongezeko la fedha kwa ajili ya miundombinu linakwenda sambamba na ubora wa kazi na uzingatiaji wa muda wa kukamilisha miradi ya ujenzi kwa muda unaotakiwa. Hivyo ni wakati mzuri wa kuangalia upya muundo na uendeshaji wa Makampuni yenu ya Ukandarasi ili kukabiliana na changamoto ya ongezeko la bajeti ya ujenzi.

Ndugu Mwenyekiti, matatizo ya kazi za ujenzi ambazo zinafanywa kwa viwango duni mbali ya kusababisha hasara kubwa kwa Serikali na usumbufu kwa Wananchi kwa ujumla, husababisha pia maafa. Hivi karibuni, tumeshuhudia kuanguka kwa jengo la ghorofa kumi Jijini Dar es Salaam. Maafa yaliyosababishwa na kuanguka kwa jengo hilo ikiwemo kupoteza maisha, kujeruhiwa kwa watu na uharibifu mkubwa wa mali, siyo kwamba inasikitisha tu, bali pia inatia doa taaluma nzima ya Uhandisi. Kama ambavyo mnafahamu, Serikali imeunda Tume ambayo inaendelea na uchunguzi wa kina wa suala hili ili kubaini sababu za kudondoka kwa jengo hilo. Vilevile, inaendelea na zoezi la kuwatambua wale wote waliohusika katika hatua mbalimbali za ujenzi ili hatua za kisheria zinazostahili zilichukuliwe kulingana na sababu zitakazobainika kwenye uchunguzi huo. Wakati tukisubiri matokeo ya Tume ya Uchunguzi, ni vyema basi nikachukua fursa hii kuwaagiza Makandarasi, Wahandisi Washauri, Wabunifu Majengo, Wakadiriaji Ujenzi na Wadau wengine wote katika Sekta ya Ujenzi, kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia viwango sahihi, Taratibu, Kanuni na Sheria za Ujenzi sambamba na kuhakikisha kila mmoja anatekeleza jukumu lake kwa umakini.

Pamoja na uhaba wa Wahandisi uliopo hapa Nchini, bado hatujafikia hatua ya kuwepo kwa viwango duni vya ujenzi kwa kiasi hicho. Ukweli ni kwamba, kuna mahali hatutimizi wajibu wetu inavyotakiwa. Tufike mahali tuseme hapana kwa viwango duni vya ujenzi. Tulinde heshima ya taaluma za Ukandarasi na Uhandisi. Tuweke maadili mbele na kukumbuka kwamba tukicheza na viwango, tunacheza zaidi na maisha ya Watu, mali ambazo watu wametafuta kwa tabu na muda mrefu na hata mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za fedha.

Nachukua fursa hii kuviagiza Vyombo na Taasisi zote zinazohusika na Usimamizi na Uratibu wa Sekta ya Ujenzi kuhakikisha kila Taasisi inasimamia Taratibu, Kanuni na Sheria za Ujenzi kwa ufanisi wa hali ya juu. Pale ambapo itabainika uwepo wa mapungufu katika Sheria, ni vyema mapendekezo juu ya mabadiliko ya Sheria husika yakaletwa Serikalini ili kuyafanyia kazi.

Ndugu Mwenyekiti, nafahamu hatua mbalimbali za dhati kabisa ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi katika kusimamia na kudhibiti mienendo na utendaji wa Makandarasi. Ni jambo la kutia moyo kusikia kwamba Bodi yako kama chombo cha Serikali imekuwa haisiti kuwafuta au kuwasimamisha Makandarasi kwa sababu ya ubabaishaji au kukiuka masharti ya usajili. Vilevile, Bodi hii imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali ya kujenga uwezo wa Makandarasi ili waweze kuongeza viwango vyao vya kutekeleza miradi mbalimbali.

Napongeza hatua hizo ambazo ni muhimu na zinazolenga kuimarisha Sekta ya Ujenzi. Napenda kuwapa moyo Makandarasi wote ambao wamekuwa wakizingatia maadili na miiko ya Ukandarasi. Endeleeni hivyo hivyo. Acheni kuazimishana majina. Fuateni Taratibu, Kanuni na Sheria zilizowekwa ili kuifanya Sekta hii iweze kuaminika na kuheshimika. Kwa kufanya hivyo, kutaondoa wasiwasi unaoanza kujitokeza kuhusu uwezo wa kufanya kazi zenye ubora na zenye kuaminika. Wakati Serikali inafanya jitihada kuwatumia Makandarasi Wazalendo katika kazi zake. Makadarasi nanyi mfanye jihada ya kuboresha viwango vya kazi zenu ili kuondoa hisia za kutoaminiana.

Ndugu Mwenyekiti, Dhamana kubwa ambayo Makandarasi wamepewa ni kuhakikisha miradi ya ujenzi inakidhi matakwa na azma ya Serikali na waendelezaji wengine. Kwa kuelewa dhamana iliyo mbele ya Makandarasi, hasa Wazalendo, wataweza kuwahudumia Watanzania na hasa wale wa Vijijini ambako Makandarasi wakubwa hawafiki. Fursa za kazi zilizoko Vijijini, ni njia mojawapo ya Makandarasi Wadogo kutoa huduma na kujiimarisha. Vile vile, kujiimarisha kutawafanya Makandarasi wa ndani waweze kushindana kwenye Soko huria Ndani na Nje ya Nchi yetu.

Zipo taarifa kwamba, asilimia 97 ya Makandarasi waliosajiliwa hapa Nchini ni Watanzania. Hata hivyo, pamoja na wingi wao wanagawana asilimia 40 tu ya kazi za ujenzi hapa Nchini. Ni kweli kwamba hali hii haipendezi na wala haina manufaa kwa Makandarasi wetu. Ufumbuzi wa tatizo hili, siyo kuendelea kulalamika au kutunga Sheria ya kuwanyima kazi wageni bali ni kutafuta njia za kushirikiana nao kutekeleza miradi kwa ubia au “subcontract”. Lazima tukubali kwamba, Nchi yetu haijapata Makandarasi Wakubwa wa kutosha wenye uwezo mkubwa kama walivyo wageni. Njia nyingine ni Makandarasi kujiunga kwa lengo la kukuza mtaji na kuongeza utaalam ili kushindana na Kampuni nyingine kubwa ambazo nazo zinaomba kazi hizo hizo. Msipoungana mtaendelea kuwa wadogo, ubora wa kazi na uharaka wa kukamilisha miradi utaondoka na matokeo yake mtashindwa kushindana. Ili Serikali iweze kuwasaidia Wazalendo, ni vyema wakaonyesha nao jitihada kwamba wanaweza kufanya kazi nzuri na kwa wakati. Tujitahidi kupiga hatua ili nasi tujivunie chetu.

Ndugu Mwenyekiti, najua zipo changamoto zinazowakabili Makandarasi hapa Nchini kama vile ukosefu wa mitambo, uhaba wa kazi za kutosha, ukosefu wa mitaji n.k. Ni jukumu la Bodi ya Makandarasi kwa kushirikiana na Wadau wengine kutoa mapendekezo ya namna Serikali itakavyoweza kusaidia suala la upatikanaji wa mitambo. Kuhusiana na uhaba wa kazi, Serikali itafanya kila linalowezekana ili Makandarasi ambao watajiunga na kushirikiana pamoja katika kufanya kazi wapewe kipaumbele. Dawa ya kuwaendeleza Makandarasi wetu ni kwa wao kuwa waadilifu, makini na wenye kujituma.

Nawataka Makandarasi Watanzania kutambua kwamba Sekta Binafsi ina kazi nyingi. Hii ni kutokana na matakwa ya Sheria, kwani kulingana na Sheria, kila Mtu au Taasisi anatakiwa kutumia Makandarasi iwapo anafanya kazi za gharama kubwa za ujenzi, kukarabati majengo, mitambo, malambo na vitu vingine. Wale wanaokiuka Sheria wachukuliwe hatua. Natambua kwamba Sheria ya Usajili wa Makandarasi ya mwaka 1997 inafanyiwa marekebisho ili kuiboresha taaluma ya ukandarasi nchini.

Ndugu Mwenyekiti, nafahamu kuwa katika kupunguza gharama, Serikali na baadhi ya Taasisi zimekuwa zikitumia nguvu za Wananchi katika kutekeleza miradi ya kuondoa kero za Wananchi. Ingawa utaratibu huu uliwekwa kwa nia njema, utekelezaji wake kwa baadhi ya maeneo umeonyesha kasoro za hapa na pale ambazo zimeathiri ubora wa kazi. Kwa mfano, kuna Shule na Zahanati ambazo zimejengwa kwa kutumia nguvu za Wananchi na Mafundi wa Vijijini peke yake na kuharibika baada ya miezi michache. Ni katika maeneo kama haya ambayo nasema, ili kulinda usalama wa Wananchi na kutumia fedha kidogo kwa manufaa ya Taifa, Makandarasi wapewe kazi hizo kwa masharti ya kutumia nguvu kazi na ikiwezekana mali ghafi kutoka eneo husika. Kama hatua hii inazingatia Sheria, inaongeza kazi kwa Makandarasi wetu na inaweka bayana uwajibikaji wa ubora basi ni jambo jema. Hii ni kwa sababu Mkandarasi huyo pamoja na kusimamiwa na aliyemwajiri, atawajibishwa na Bodi inayomwezesha kufanya biashara hiyo.

Ndugu Mwenyekiti, zipo tetesi kwamba, Makandarasi wengi wanaoshindwa ama kuchelewesha kumaliza kazi ndani ya muda uliopangwa pamoja na matatizo mengine ni wale ambao Zabuni zao hazikuzingatia gharama halisi za ukamilishaji wa kazi anazoomba. Mkandarasi kama huyu anataka kupata kazi huku akijua wazi kwamba hawezi kukamilisha, au akikamilisha haitakuwa na ubora unaotakiwa. Ni muhimu sana kwa Waajiri wa Makandarasi kuzingatia vigezo vyote muhimu kwa Mkandarasi na sio gharama tu. Vile vile, ni vyema kwa watoa kazi kuepuka kumpatia Mkandarasi mmoja kazi nyingi kwa wakati mmoja bila kuzingatia uwezo halisi wa Mkandarasi huyo katika kuendesha miradi mingi kwa wakati mmoja. Napenda kuchukua fursa hii kuziagiza Taasisi za Serikali zinazohusika na utoaji kazi za Miradi ya Ujenzi kwa Makandarasi kuhakikisha kwamba Mkandarasi anayepewa kazi ni yule ambaye amechujwa vya kutosha na kujiridhisha kuwa anakidhi matakwa ya mradi husika katika nyanja zote ikiwemo uhalisia wa bei na gharama za utekelezaji wa Mradi.

Ndugu Mwenyekiti, Ni dhahiri katika siku ya leo, yapo mambo mengi yanayoweza kuongelewa hapa. Hata hivyo, nisingependa kutumia muda wenu mwingi. Kwa sababu hiyo, napenda nihitimishe mchango wangu kwa kuipongeza tena Bodi yako na Wizara ya Miundombinu kwa kazi nzuri mnayoifanya. Ninategemea kwamba mtasimamia mipango yenu ya mafunzo, utafiti na Mfuko wa Msaada kwa Makandarasi kwa uangalifu na uadilifu ili sote pamoja na Wananchi wapate matunda yaliyokusudiwa. Napenda kuwahimiza muendelee na mipango yenu ya kuwaelimisha Wadau wa Sekta hii ili waweze kushirikiana nanyi kikamilifu katika kujenga Sekta iliyo bora na ambayo italeta manufaa kwa kila mtu. Jengeni utamaduni wa kushiriki katika kila ngazi ya uteuzi wa Makandarasi ikiwa ni pamoja na hatua za mwanzo kabisa za kuteua Makandarasi hao. Vile vile, usajili wa Makandarasi ufuate taratibu kuepuka kusajili Kampuni za “mfukoni” zisizo rasmi ambazo baadaye zitaleta madhara na kushusha heshima ya taaluma nzima ya Ukandarasi.

Ndugu Mwenyekiti, niipongeze Bodi yako kwa namna ya pekee kwa kuweza kushirikiana na Serikali vizuri na hivyo kuweza kujitegemea na kusimamia utekelezaji wa miradi, hasa ya barabara. Changamoto kubwa iliyo mbele yenu ni kuongeza bidii na hatimaye kuishauri Serikali njia bora zaidi ya kutekeleza Miradi hiyo kwa gharama iliyopangwa. Ni matumaini yangu kwamba Bodi itatumia Mkutano huu kuangalia mapungufu yaliyopo na hivyo kujipanga vizuri zaidi katika kukabiliana na majukumu yaliyo mbele yetu. Serikali itakuwa tayari kushirikiana nanyi katika kutekeleza mapendekezo mtakayoyatoa katika Mkutano huu. Tuendelee kuzingatia Sheria za Nchi, Kanuni na Taratibu za Sekta hii. Maadili mema ndiyo msingi wa maendeleo ya Sekta hii na Nchi yetu kwa ujumla. Mkizingatia hayo, sina shaka mtafanya vizuri katika kujiendeleza wenyewe na kuendeleza gurudumu la Maendeleo ya Nchi yetu.

Ndugu Mwenyekiti, washiriki wote, Mabibi na Mabwana, baada ya kusema hayo sasa natamka kwamba Mkutano wa Majadiliano wa Makandarasi wa mwaka 2008 umefunguliwa rasmi.

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.