Tarehe 15 Aprili, 2019
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Kumi – Tarehe 15 Aprili, 2019 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. MOSSY LUKUVI – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA):- Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka wa fedha 2019/2020. NAIBU SPIKA: Ahsante, Katibu. NDG. MOSSY LUKUVI – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, maswali, tutaanza na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum, sasa aulize swali lake. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Na. 78 Malipo Stahiki Kwa Walimu Waliopanda Daraja MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Serikali imekuwa ikiwapandisha madaraja walimu lakini haitoi malipo stahiki kwa madaraja hayo mapya kwa kipindi kirefu tangu walipopandishwa madaraja yao:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao mara wanapopandishwa madaraja? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilisitisha kupandisha walimu na watumishi wengine madaraja katika mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017 kutokana na uhakiki wa watumishi uliohusisha uhalali wa vyeti, elimu na ngazi za mishahara.
[Show full text]