Hotuba Ya Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi Na Mawasiliano Mheshimiwa Prof
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
HOTUBA YA WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO MHESHIMIWA PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019 A. UTANGULIZI 1. Mheshimiwa Spika, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuweka mezani Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2018/2019. 2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuijalia nchi yetu amani na utulivu na kutuwezesha kushiriki katika Mkutano huu wa 11 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 3. Mheshimiwa Spika, kipekee nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri unaoonesha nia ya dhati ya kuipeleka nchi yetu kwenye hatua kubwa zaidi ya maendeleo. Uzalendo uliotukuka na uthabiti wake katika kulinda rasilimali za taifa letu una manufaa 1 makubwa kwa nchi yetu sasa na kwa vizazi vijavyo. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda na kumpa nguvu na afya njema ili aweze kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Dkt. Ally Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar; Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiongoza vema nchi yetu kwa hekima na busara. 4. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa pole kwako binafsi, Bunge lako tukufu, familia ya marehemu na wananchi wa Jimbo la Songea mjini kwa kuondokewa na Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama. Kifo cha Mbunge huyu kimeleta majonzi makubwa kwa Bunge na Taifa kwa ujumla. Marehemu atakumbukwa kwa michango yake katika maendeleo ya nchi hii. Mungu amweke mahali pema peponi, Amina. 5. Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati natoa pongezi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu hususan Mwenyekiti Mheshimiwa Moshi Seleman Kakoso (Mb.) pamoja na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma (Mb.) kwa kuchaguliwa kuiongoza Kamati hii. Aidha, nawapongeza Wajumbe wapya waliojiunga na Kamati hii na Wajumbe wa zamani kwa kuchaguliwa kuendelea kuwepo kwenye Kamati hii. Wizara inathamini ushirikiano na ushauri wenu mnaotoa katika kuboresha utendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. 2 6. Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia waheshimiwa Wabunge walioaminiwa na kuchaguliwa na wananchi katika chaguzi ndogo zilizofanyika katika mwaka wa fedha 2017/2018. Wabunge hao ni Mheshimiwa Maulid Abdallah Mtulia, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni; Mheshimiwa Dkt. Godwin Aloyce Ole Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha; Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini; Mheshimiwa Justin Joseph Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini na Mheshimiwa Dkt. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita, Mbunge wa Jimbo la Longido. Ushindi walioupata unaonesha imani waliyonayo Wananchi kwao, kwa Serikali yao na Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Rukia Ahmed Kassim (Mb.); Mheshimiwa Shamsia Aziz Mtamba (Mb.); Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye (Mb.); Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amir (Mb.); Mheshimiwa Sonia Juma Magogo (Mb.); Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi (Mb.) na Mheshimiwa Nuru Awadh Bafadhili (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 7. Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa, Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kwa hotuba zao. Hotuba hizo zimefafanua vizuri utekelezaji wa mipango na mikakati ya Serikali yenye lengo la kuimarisha na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii nchini. 3 B. MAJUKUMU YA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO 8. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inajumuisha sekta kuu tatu ambazo ni Sekta ya Ujenzi, Sekta ya Uchukuzi na Sekta ya Mawasiliano. 9. Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Sekta ya Ujenzi ni kusimamia utekelezaji wa Sera ya Ujenzi (2003) pamoja na Sera ya Taifa ya Usalama Barabarani (2009); ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, madaraja na vivuko; ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege; ujenzi na ukarabati wa nyumba na majengo ya Serikali; usimamizi wa masuala ya ufundi na umeme; usimamizi wa shughuli za ukandarasi, uhandisi, ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi; usimamizi wa maabara na vifaa vya ujenzi; usimamizi wa masuala ya usalama na mazingira katika Sekta; uboreshaji utendaji na uendelezaji wa watumishi wa Sekta na usimamizi wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Sekta. 10. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uchukuzi ina majukumu ya kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchukuzi ya mwaka 2003; ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya reli na bandari; usafiri na usafirishaji kwa njia ya anga, reli na bandari; utoaji wa leseni za usafirishaji; usalama katika usafirishaji; usimamizi wa huduma za hali ya hewa; kuendeleza rasilimali watu na kusimamia Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyo chini ya Sekta ya Uchukuzi. 4 11. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Mawasiliano, majukumu yake ni pamoja na kusimamia Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003; na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya mwaka 2016 na utekelezaji wake. Aidha, Sekta ya Mawasiliano ina dhamana ya kuhakikisha kuwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano inachangia katika maendeleo ya nchi yetu, pamoja na usimamizi wa majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Mawasiliano. C. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018 12. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021), Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015, Malengo Endelevu ya Maendeleo, Ahadi na Maagizo ya Viongozi Wakuu wa Serikali na Sera nyinginezo za Kisekta, Kitaifa na Kimataifa. 13. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo sasa naomba nitoe taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na Mpango na Bajeti ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa kila sekta. 5 C.1 UTENDAJI WA SEKTA ZILIZO CHINI YA WIZARA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2017/2018 C.1.1 SEKTA YA UJENZI Bajeti ya Matumizi ya Kawaida 14. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Sekta ya Ujenzi ilitengewa kiasi cha Shilingi 36,032,513,782.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi 33,977,384,800.00 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Sekta ya Ujenzi na Taasisi zake na Shilingi 2,055,128,982.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Hadi Machi, 2018 Shilingi 22,904,459,689.20 zilikuwa zimetolewa na HAZINA. Kati ya fedha hizo, Shilingi 21,080,142,689.20 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Wizara na Taasisi na Shilingi 1,824,317,000.00 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Bajeti ya Miradi ya Maendeleo 15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Sekta ya Ujenzi ilitengewa Shilingi 2,411,026,062,496.20 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, fedha za ndani ni Shilingi 1,865,443,630,496.20 na Shilingi 545,582,432,000.00 zilikuwa ni fedha za nje. Fedha za ndani zinajumuisha Shilingi 642,284,000,000.00 za Mfuko wa Barabara. 6 Hadi Machi, 2018 fedha zilizotolewa ni Shilingi 1,673,417,096,716.54. Kati ya fedha hizo, Shilingi 1,435,534,514,202.54 ni fedha za ndani na Shilingi 237,882,582,514.00 ni fedha za nje. Fedha za ndani zilizotolewa zinajumuisha Shilingi 424,702,386,374.00 za Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja. Kwa ujumla, kiasi kilichotolewa hadi Machi, 2018 ni sawa na asilimia 69 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018. UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO Miradi ya Barabara na Madaraja 16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Sekta ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilipanga kutekeleza kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara kuu na za mikoa. Kwa upande wa barabara kuu, miradi ya barabara iliyokamilika hadi Machi, 2018 ni pamoja na barabara ya Mayamaya – Mela – Bonga (km 188.15), Tabora – Puge – Nzega (km 113.90), Tabora – Nyahua (km 85) na Kaliua – Kazilambwa (km 58.9). Miradi mingine iliyokamilika katika kipindi hiki ni barabara ya Sumbawanga – Kanazi (km 75), Kanazi – Kizi – Kibaoni (km 76.6), Kyaka – Bugene (km 59.1), Magole – Turiani (km 45.2), Uyovu - Bwanga (km 45), KIA – Mererani (km 26), Usagara – Kisesa (Mwanza Bypass – km 17) na Mwigumbi – Maswa (km 50.30) pamoja na madaraja ya Kilombero na Kavuu. Aidha, Wizara ilikamilisha 7 ukarabati wa jumla ya kilometa 77 za barabara kuu kwa kiwango cha lami. 17. Mheshimiwa Spika, miradi ya barabara kuu iliyoendelea kutekelezwa na kukarabatiwa kwa kiwango cha lami ni pamoja na barabara za Sumbawanga – Matai – Kasanga Port (km 112), Kidahwe – Kasulu (km 63), Kakonko – Nyakanazi (km 50), Mafinga – Igawa (km 137.9), barabara ya mchepuo wa Arusha (km 42.4), Makutano – Natta (km 50), Maswa – Bariadi (km 49.7), Bwanga – Biharamulo (km 67), Bulamba – Kisorya (km 51), Ushirombo – Lusahunga (km 110), Tabora – Koga – Mpanda (km 370), Nyahua – Chaya (km 85.4), Mbinga – Mbamba Bay (km 66), Itoni – Ludewa – Manda sehemu ya Lusitu – Mawengi (km 50), Mpemba – Isongole (km 50.3), Njombe – Ndulamo – Makete (km 109), Mtwara – Newala – Masasi (Mtwara – Mnivata – km 50), Mto wa Mbu Loliondo (Waso) – Sale (km 49), Urambo – Kaliua (km 28), Mpanda – Vikonge (km 35), Sanya Juu – Elerai (km 32.2) na Chunya – Makongolosi (km 43).