8 FEBRUARI, 2019.Pmd
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA KUMI NA NNE Kikao cha Kumi – Tarehe 8 Februari, 2019 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Mussa A. Zungu) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tukae. NDG. JOSHUA CHAMWELA – KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Hati ya Uhamishaji Fedha Na. 1 kwa Nusu ya Kwanza ya Mwaka 2018/2019 (Statement of Re-allocation Warrant No. 1 between Votes for the First Half of 2018/2019). Hati ya Uhamiaji Fedha Na. 2 kwa Nusu ya Kwanza ya Mwaka 2018/2019 (Statement of Re-allocation Warrant No. 2 between Votes for the First Half of 2018/2019). Muhtasari wa Tamko la Sera ya Fedha, Mapitio ya Nusu Mwaka 2018/2019 (The Monetary Policy Statement, The Mid- year Review for the Year 2018/2019). 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018. MHE. ZAINAB A. KATIMBA - K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO (MHE. ANDREW J. CHENGE): Taarifa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018. MWENYEKITI: Ahsante. Katibu. NDG. JOSHUA CHAMWELA – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Tunaanza na maswali Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Leah Jeremiah, Komanya. Na. 109 Mkakati wa EQUIP wa Kuinua Elimu kwa Watoto wa Kike NHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Moja ya mkakati wa EQUIP – Tanzania ni kuinua ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa kike ili waweze kuhitimu Shule ya Msingi na kuendelea na Sekondari, lakini mtoto wa kike ana vikwazo vinavyoweza kukatiza ndoto hii:- (a) Je, mpango huu umejikita vipi katika kutokomeza mimba na ndoto za utotoni, udhalilishaji kingono, ukeketaji na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto? 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) (b) Je, ni upi usaidizi wa mpango wa wanafunzi walio katika hatari zaidi kwa makundi kama vile waliotelekezwa, walio katika umasikini wa kupindukia, yatima na walionusurika kutokana na unyanyasaji? MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, udhalilishaji kongono na ukeketaji, Serikali kupitia programu ya EQIP Tanzania imeanzisha clubs za wanafunzi ziitwazo Jiamini Uwezo Unao (JUU) kwenye Shule za Msingi 4,476. Malengo ya clubs hizo ni kuwajengea wanafunzi hasa wa kike uwezo wa kujiamini, kujieleza na kujitambua. Kupitia clubs hizo, wanafunzi wanajifunza masuala mbalimbali ikiwemo hedhi salama na athari za kupata mimba katika umri mdogo. Aidha, ili kuboresha mazingira ya watoto wa kike, mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kwa kupitia programu hii ilitoa ruzuku ya jumla ya shilingi bilioni 2.46 kwenye shule 4,476 ambazo kila shule ilipewa shilingi 550,000/=. Kupitia ruzuku hiyo, elimu ilitolewa kwa wanafunzi wa kike na wazazi kupitia ushirikiano wa Wazazi na Waalimu (UWAWA), kuhusu namna ya kutengeneza taulo salama za kike. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali kupitia programu ya EQUIP Tanzania imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii wakiwemo wanafunzi, wazazi na Walimu kupiga vita vitendo vya ukatili kwa watoto na kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia kwa makundi maalum wakiwemo watoto wa kike. 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia programu ya EQUIP Tanzania, Serikali imeongeza fursa ya kujifunza kwa watoto wa kike sawa na wa kiume na kuwakinga na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto. Jumla ya shilingi bilioni 6.8 zimetumika kuwajengea uwezo Walimu 50,446 kuhusu mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo matumizi ya mbinu zinazojali jinsia na ujenzi wa mazingira rafiki na salama ya kujifunzia. Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huo umeboresha mbinu rafiki na zinazozingatia jinsia katika ufundishaji na ujifunzaji kutoka asilimia 54 mwaka 2014 hadi aslimia 65 mwaka 2016 katika shule zilizo katika Mikoa iliyotekeleza programu hiyo ya EQUIP Tanzania. Tathimini inaonesha kuwa wasichana waliopata wastani wa juu katika kumudu stadi za kusoma na kuandika, walifikia asilimia 26.7 ikilinganishwa na wavulana asilimia 18 katika kipindi hicho. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi) MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Leah. MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa fedha za mafunzo zimekuwa zikibaki kila mwaka kutokana na wawezeshaji kutoka Vyuo vikuu Vya Tanzania; fedha hizo zimekuwa zikibaki kwa sababu wakati wa kutekeleza, wawezeshaji kutoka Vyuo Vikuu wamekuwa na programu nyingine katika vyuo vyao. Je, Serikali haioni ipo haja ya kutengeneza TOT wa Mkoa ili hata kama mradi utakapokwisha wanafunzi waendelee kupewa mafunzo? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya mimba katika Mkoa wa Simiyu bado ni kubwa. Kwa mwaka 2017 wanafunzi 37 wa Shule za Msingi walipata ujauzito; 2018 wanafunzi 38; halikadhalika katika Sekondari kwa mwaka 2017 wanafunzi 159 walipata ujauzito; na mwaka 2018 wanafunzi 153. 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchungu huo mkubwa wananchi waliamua kuanzisha ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Mwanjoro: Je, Serikali ipo tayari kuunga nguvu za wananchi waliofikisha jengo usawa wa boma? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru? (Makofi) MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Waziri, majibu kwa kifupi sana. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Leah Komanya kwa kuendelea kutaka watoto wa kike wapate elimu nzuri na juhudi hizi za kuunga mkono Serikali ambazo imeziweka. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anasema kuna fedha zinabaki kwenye programu hii. Ni kweli katika mazingira mbalimbali fedha inaweza kubaki, lakini maelekezo ya Serikali ni kwamba fedha ikibaki, wahusika wanapewa taarifa kwenye Wizara na inapangiwa majukumu mengi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo Mheshimiwa Mbunge aliyotoa ni mazuri, tuyapokee; kuandaa TOT ili programu itakapoisha wawezeshwe watu wa eneo husika kwani itapunguza gharama, wenyewe kwa wenyewe watafundishana kwa lugha zao za nyumbani, hii kazi itaenda vizuri. Kwa hiyo, tunapokea wazo hili, tunalifanyia kazi. Ni wazo jema sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, anazungumza habari ya mimba na kuunga mkono juhudi za kujenga mabweni. Utakumbuka tangu juzi mpaka jana kumekuwa na mjadala katika Bunge hili Tukufu la kumalizia maboma ya madarasa lakini pia na mabweni na Vituo vya Afya. 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba kazi hii inatekelezwa na Serikali inaunga mkono juhudi za wananchi, tunafanya mpango, tukipata fedha tutaweka nguvu katika maeneo hayo. Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo imepewa miradi mingi ya kuwezesha watoto wa kike wasome, kujenga madarasa, matundu ya vyoo na mabweni. Jambo hili tunalifanyia kazi. Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika programu ijayo, fedha ikipatikana tutatoka hapa kuunga mkono nguvu za wananchi katika kumalizia mabweni ambayo wananchi wamechangia wenyewe. MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini. MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimba za watoto mashuleni ni jambo la aibu kweli kweli; nasi kama wazazi lazima tulichukulie very serious. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tulivyoanza programu ya kujenga madarasa ya Shule za Kata, tukajenga mabweni, ni kwa nini Serikali isiagize Halmashauri kwa makusudi kabisa kwamba ni lazima katika Halmashauri bajeti itengwe ili mabweni yajengwe, lisiwe ni suala la hiari? Kwa sababu hawa watoto wanapata mimba kutokana na bodaboda, kutokana na njaa, watoto wamechoka kwa sababu ya umbali wa shule; kwa nini Serikali isiamue kabisa kwamba mwaka huu wa fedha kila Halmashauri ihakikishe angalau wamejenga mabweni mawili au matatu? (Makofi) MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu kwa kifupi. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli kwamba jambo la kujenga mabweni na hasa ya watoto wa kike ni jambo ambalo haliepukiki, ni jambo la lazima na naomba pia tulizingatie. Ndiyo maana kwenye miradi mbalimbali ya Serikali, kwa 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) mfano mradi wa EP4R tumeshajenga mabweni 533 katika shule zote za Sekondari katika maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu hoja ni kwamba tutenge fedha kwenye bajeti hii, Mheshimiwa Mbunge ni Mbunge; na Waheshimiwa Wabunge wote nawaomba sana, wakati huu ndiyo tunaandaa bajeti zetu za Halmashauri. Kila Halmashauri ina maelekezo mahususi ya Serikali, asilimia 40 au 60 kulingana na mapato ya Halmashauri inaenda kwenye shughuli za maendeleo na hasa miundombinu ikiwepo mabweni. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwenye bajeti ambazo zinaandaliwa sasa, hiki kipengele tumetoa maelekezo, Serikali ngazi ya juu ya Taifa tunapanga fedha, Halmashauri zitenge fedha. Wakuu wa Mikoa wameelekezwa, tunapozungumza maboma ni pamoja na madarasa na mabweni