HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA KATIKA IBADA YA KUWEKWA WAKFU NA KUMUWEKA KITINI REV. CANON JOHN ANDREW SIMALENGA KUWA ASKOFU WA SABA WA DAYOSISI YA SOUTH WEST YA KANISA LA ANGLIKANA TANZANIA ILIYOFANYIKA KATIKA KANISA KUU LA MTAKATIFU ANDREA, NJOMBE, TAREHE 6 JULAI 2008

Mhashamu Dkt. , Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania;

Mheshimiwa Hajjat Amina Mrisho Said, Mkuu wa Mkoa wa Iringa;

Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, Jaji Mkuu wa Tanzania;

Mheshimiwa Philemon Luhanjo, Katibu Mkuu Kiongozi;

Wahasham Baba Maaskofu;

Waheshimiwa Viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya Dini;

Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;

Waheshimiwa Wageni Waalikwa;

Ndugu Waumini wa Dayosisi;

Mabibi na Mabwana.

Bwana Asifiwe sana! Awali ya yotena kwa moyo wa unyenyekevu namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutulinda, kutupa afya njema na kutuwezesha kukusanyika hapa siku ya leo kushuhudia kazi yake njema. Vile vile, namshukuru sana kwa kutusafirisha salama kuja kushuhudia tendo hili katika siku hii aliyoipanga Yeye Mwenyewe ya Kuwekwa Wakfu na Kuwekwa Kitini Askofu John Andrew Simalenga kuwa Askofu wa Saba wa Dayosisi ya South West Tanganyika.

Pili, nakushukuru sana Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Dkt. Valentino Mokiwa, na Viongozi wenzako kwa kunialika niwe nanyi kwenye Ibada hii Takatifu.

Tatu, naungana na wote waliozungumza kabla yangu, pamoja nanyi nyote, katika kumpongeza Askofu mpya, pamoja na familia yake kwa heshima na wajibu mkubwa aliopewa wa kuiongoza Dayosisi hii.

Nne, nawapongezeni Wana-Dayosisi hii kwa kumpata Kiongozi wenu mpya, aliyepatikana kwa haki, amani na utulivu na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Kanisa lenu na Taratibu mlizojiwekea. Nawapongeza sana!

Baba Askofu na Ndugu Waumini, Sote tunakumbuka matatizo na majaribu mengi mliyoyapata katika kipindi cha miaka takriban kumi iliyopita tangu mwaka 1998 mlipofanya uchaguzi. Niwasifu kwa moyo wenu wa uvumilivu na busara kubwa Mungu aliyowapa katika kipindi hicho hadi leo tunaposhuhudia Dayosisi hii kupata Askofu wake. Ninaamini mlikaa kwa kufunga na kuomba na sasa mmepewa kwani hata maandiko yanasema “Ombeni nanyi Mtapewa …….. kwa maana kila aombaye hupokea” (Mathayo 7:7,8). Leo mnampokea Askofu mpya ikiwa ni matokeo ya maombi yenu! Matokeo haya yamezidisha upendo kati yenu na kuwajenga zaidi kiroho na katika kumtegemea Bwana.

Wajibu na Majukumu Baba Askofu Simalenga na Ndugu Waumini, Sinodi Maalum ya Uchaguzi wa Dayosisi ya South West Tanganyika imekuchagua wewe kuwa Kiongozi wa Dayosisi hii kwa asilimia 76.7. Hizi ni kura nyingi. Labda utajiuliza kwa nini wamekuchagua wewe na si mwingine? Maana kuwa Kiongozi wa Watu kiroho na kimwili ni mzigo mzito. Lakini nikikutazama ninaona bado una nguvu ya kubeba mzigo huu mzito wa kuwaongoza Waumini wa Dayosisi hii. Vile vile, Viongozi wenzako na Waumini kwa ujumla wanaonyesha nyuso za furaha zenye matumaini kwamba, unao uwezo mkubwa wa kuwaongoza na wana imani kubwa kwako. Nakuomba upokee mzigo huo kwa unyenyekevu, kwa matumaini na bila kusita, kwani ninaamini wenzako watakusaidia na kukuombea kwa Mwenyezi Mungu upate nguvu, busara na hekima zaidi ya kuwaongoza. Najiunga na wenzangu wa Dayosisi ya South West Tanganyika kukuombea kwa Mungu ili uendelee kupata afya njema na nguvu ili ukaseme yale yaliyoandikwa katika Kitabu cha Wafilipi 4:13 kwamba, “Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye Nguvu”. Bila shaka Mwenyezi Mungu ana kusudi lake nawe katika kipindi cha historia ya Kanisa na Dayosisi hii. Jitwishe mzigo huu kwa imani kwamba utaubeba bila kuchoka.

Baba Askofu Simalenga na Ndugu Waumini, Unakabidhiwa kazi hii wakati ambapo Dunia inapita katika kipindi kigumu cha Utandawazi; Sayansi na Teknolojia; na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kipindi hiki kina changamoto nyingi, majaribu, vishawishi na mabadiliko mengi ambayo mengi hayaendani kabisa na Maadili ya Jamiii tunamoishi. Kipindi hiki kimetawaliwa na imani potofu, maradhi, umaskini, ukahaba, imani za uchawi na ushirikina na mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii.

Nchi yetu nayo inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na mmomonyoko huo wa Maadili na changamoto hizo. Hata hivyo, sisi kama Nchi hatuwezi kukwepa kupita katika kipindi hiki ila inatubidi tusimamie kikamilifu Maadili mema katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla. Hapa Kanisa lina jukumu kubwa sana la kufundisha na kukujenga Maadili mema katika familia na jamii.

Dunia nzima na hasa Nchi maskini Tanzania ikiwemo, inakabiliwa na tatizo kubwa la Ugonjwa hatari wa UKIMWI. Naomba sote tuliokusanyika hapa na Watanzania wengine wote wanaonisikiliza waelewe kuwa Ugonjwa huu haujali umri, jinsia, uwezo, dini au mipaka ya Kijiji, Tarafa, Kata, Wilaya, Mikoa na hata Nchi na Nchi. Tatizo lingine linalotishia amani, utulivu na usalama wa Nchi yetu ni imani potofu za kishirikina na kichawi. Matatizo haya kwa asilimia kubwa yanasababishwa na ukosefu wa malezi mema na mmomonyoko mkubwa wa Maadili katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla. Vile vile, tunalo tatizo la ajira na elimu kwa watoto wetu. Hizi ni baadhi tu ya changamoto ambazo nitapenda kutumia nafasi hii kuzizungumzia japo kwa kifupi sana.

Ugonjwa wa UKIMWI Baba Askofu Simalenga na Ndugu Wana-Dayosisi, Nianze na changamoto ya ugonjwa hatari wa UKIMWI. Tatizo la UKIMWI limekuwa na athari kubwa za kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu na Dunia nzima kwa ujumla. UKIMWI umeendelea kuenea kwa kasi ukiathiri watu wa rika zote Vijana kwa Wazee.

Kufuatana na Takwimu za Utafiti wa Tanzania ‘HIV/AIDS Indicator Survey’ 2007/2008 uliokamilika hivi karibuni, kiwango cha maambukizi Kitaifa ni asilimia 5.8. Takwimu zinaonyesha kwamba, kiwango hiki kimepungua kwa asilimia 1.2 ikilinganishwa na kiwango cha wastani wa asilimia 7.0 mwaka 2003/2004. Hiki ni kiwango ambacho bado ni kikubwa kwa maisha ya binadamu. Lakini, jambo ambalo limenifanya niongelee changamoto hii na kuifanya ya kwanza ni kwamba, wakati takwimu za Kitaifa zinaonyesha kushuka kutoka asilimia 7.0 hadi asilimia 5.8, mchanganuo Kimkoa unaonyesha kwamba, iko Mikoa ambayo kasi ya maambukizi inazidi kuongezeka tena kwa kasi. Kwa mfano, Mkoa unaoongoza kwa maambukizi na ambayo yamepita wastani wa kiwango cha Taifa cha asilimia 5.8 kwa mujibu wa matokeo ya Viashiria ni Mkoa huu wa Iringa wenye asilimia 15.7. Mikoa mingine yenye viwango vikubwa vya maambukizi baada ya Iringa ni Dar-es-Salaam wenye asilimia 9.3, Mkoa jirani wa Mbeyaasilimia 9.2, Mara asilimia 7.7, Shinyanga asilimia 7.4, Pwani 6.7, Tabora 6.4 na Ruvuma 5.9.

Katika Mkoa wa Iringa ziko dalili kwamba, Wilaya ya Makete ambayo iko katika Dayosisi hii ndiyo imeathirika zaidi na ugonjwa huu. Inasadikiwa kuwa kati ya Watoto yatima zaidi ya milioni 2.5 Nchini, wengi wao wametokana na ugonjwa wa UKIMWI na wapo katika Mkoa wa Iringa. Takwimu tulizonazo zinaonyesha kuwa Mkoa wa Iringa una yatima takriban 50,000 na kati ya hao, 13,000 walikuwa ni kutoka Wilaya ya Makete, wakati Mufindi walikuwepo Yatima 14,000.

Nimeona ni muhimu kutaja Takwimu hizi, sio kwa kuwatisha Waumini wa Dayosisi hii na Wananchi wa Iringa, lakini ni kuonyesha jinsi tatizo lilivyo kubwa katika eneo hili na majirani zenu wa Mbeya na Ruvuma. Ni vizuri ikaeleweka kuwa UKIMWI hauna chanjo wala tiba. Dawa za kurefusha maisha siyo tiba ila zinakuongezea tu siku za kuishi. Tusipokuwa makini kukabiliana nao ni dhahiri utatumaliza. Mwandishi wa habari, Mwanasiasa, na Mtetea Haki Duniani, Profesa Norman Cousin aliwahi kusema: “Msiba sio kifo, bali ni kile kinachoruhusu kifo wakati tungali hai.” Ni kweli misiba mingi imetokea kutokana na vifo vingi vinavyosababishwa na ugonjwa hatari wa UKIMWI. Wengi wetu ni mashahidi. Lakini nakubaliana na Mwandishi huyu kwamba, suala sasa sio vifo vinavyotokea, bali kile kinachosababisha vifo hivyo ambavyo ndivyo vinakuwa misiba miongoni mwa jamii. Tupambane na UKIMWI ili usituletee misiba miongoni mwa familia na jamii. Nawaomba sana Viongozi wetu tuendelee kwa nguvu zote kuwaelimisha Waumini wetu kuhusu tatizo hili. Ni tatizo kubwa linalohitaji nguvu za pamoja kulikabili. Kanisa lina nafasi kubwa katika kukabiliana na Ugonjwa huu. Naomba niseme kuwa, njia kubwa za kuepukana na ugonjwa huu ni: i. kubadili tabia; ii. jamii kuhimizwa kuoana wanapofikia umri wa kuoana; iii. wanandoa kuwa waaminifu na kuheshimu ndoa zao; na iv. wale ambao hawana ndoa waache ngono kabisa.

Baba Askofu Simalenga na Ndugu Waumini, Binadamu ni kiumbe kilichojaa madhaifu ya namna mbalimbali na haya si ya leo. Yamekuwepo tangu enzi za Babu zetu na juhudi za kuwaasa Binadamu kujiepusha na vishawishi vya kutenda dhambi nazo zimekuwepo kila mara. Katika Kitabu cha Kwanza cha Wakorintho Sura ya Saba, Mstari wa Kwanza hadi wa Pili na Mstari wa Nane hadi wa Tisa (Wakorintho 7:1-2, 8-9) Mtume Paulo anatuasa kama ifuatavyo: “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri Mwanamume asimguse Mwanamke. Lakini, kwa sababu ya zinaa kila Mwanamume na awe na Mke wake mwenyewe, na kila Mwanamke na awe na Mume wake mwenyewe…….. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na Wajane, ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”. mwisho wa kunukuu.

Wakati mafundisho haya yalipotolewa maradhi ya UKIMWI hayakuwepo. Mafundisho haya yanahitajika zaidi hivi sasa kuliko hata enzi hizo za zamani. Tukiyafuata na kuishi kama Maandiko haya Matakatifu yanavyoelekeza tunaweza kabisa kwa sehemu kubwa tukaushinda ugonjwa huu hatari wa UKIMWI. Lakini kama nilivyosema awali, Binadamu ni dhaifu hivyo hatuna budi muda wote kukumbushana mambo haya. Serikali inaungana nanyi katika kuendelea kutoa mafundisho haya ya Mtume Paulo. Lakini kwa kuzingatia mazingira yaliyopo hivi sasa, tumelazimika vile vile kuwaasa Wananchi wale ambao wanashindwa kujizuia na hawajaoana, basi WAJIEPUSHE NA NGONO ZEMBE KWA KUTUMIA MBINU ZA SASA ZA KINGA. Naelewa sana kuwa Wahubiri wa Madhehebu ya Dini mbalimbali hawaungi mkono mahubiri ya Serikali ya MATUMIZI YA NGONO YANAYOZINGATIA KINGA. Sawa, lakini basi, ninawaomba msiwakataze Wananchi kutumia kinga hizo kwa wale wanaoshindwa kujizuia na hawajaoa wala kuolewa. Kwa kufanya hivi, tutalinusuru Taifa letu kuteketea. Vile vile, ninawahimiza Viongozi wote wa Madhehebu ya dini na hasa wale wanaotoka katika Mikoa ambayo maambukizi ya UKIMWI bado yako juu ya wastani wa kiwango cha Taifa wa Asilimia 5.8 kuwahimiza Waumini wenu na Wananchi kwa jumla kupima kwa hiari ili kujikinga afya zao kwani “TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA”

Tofauti zitokanazo na Chaguzi Baba Askofu Simalenga na Ndugu Wananchi, Uzoefu wa Chaguzi katika Vyama vya Siasa na Dola hasa pale unapotawaliwa na Mfumo au Itikadi ya Vyama vingi, mara nyingi huzaa migawanyiko, visasi na chuki. Kwa bahati nzuri Mfumo wa kupata Viongozi wa ngazi ya Askofu katika Dhehebu lenu la Kanisa la Anglikana ni kwa kupiga kura. Huu ni mfumo mzuri sana maana hauna upendeleo na ni wa kidemokrasia. Nasema hivyo kwa kuwa Mfumo huo ndiyo unaotumika kupata Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa wa ngazi mbalimbali hapa Nchini. Hata hivyo, tofauti iliyopo ni kuwa katika uchaguzi wa Kanisa, watu wote ni wenye imani moja na wanaomtegemea Mungu mmoja. Kwa kutumia njia hii, Mwenyezi Mungu humteua Kiongozi wa kuongoza Waumini wake. Naamini uteuzi wako huu una Baraka za Mungu na kwa hiyo haupaswi kuzaa tofauti kama zile tunazoziona katika Mifumo mingine Serikalini na kwenye Vyama vya Siasa.

Yaliyotokea mwaka 1998 na kusababisha kushindikana kupatikana kwa Uongozi hadi Mungu alipobariki uteuzi wako hivi leo, ni fundisho muhimu kwetu wote kuepuka ubinafsi, chuki, ukabila na hisia za ushirikina mambo ambayo mara nyingi hayapo kwenye Maadili ya Kanisa. Hivyo, wito wangu kwa Viongozi wa Makanisa yote ni kujifunza kuishi kwa utulivu, upendo, haki, amani, kumuamini Mungu na kufanya kazi kwa wito. Changamoto kubwa iliyo mbele yako ni kuleta mshikamano, umoja, upendo na utulivu miongoni mwa Waumini wa Dayosisi yako na Kanisa lote la Anglikana kwa jumla. Ninakupongeza sana na ninawapongeza Waumini wa Dayosisi ya Kusini Magharibi mwa Tanganyika kwa uvumilivu wao. Wahenga walisema “Mvumilivu hula Mbivu” na leo Dayosisi hii inashuhudia usemi huo ukitimizwa.

Baba Askofu na Ndugu Wana-Dayosisi Kabla sijafika mwisho, naomba nirejee maeneo ambayo kwa kweli yananigusa sana nikiyafikiria. Tunao yatima wengi ambao wanahitaji msaada. Vile vile, tunao waathirika wengi wa UKIMWI ambao tunaishi nao. Tuwasaidie tusiwanyanyapae. Ninawashukuru kwa kuwa ninyi mnavyo Vituo vya Watoto Yatima. Tuwatunze, tuwape moyo na tumaini la maisha ili waendelee kuishi kwa matumaini. Mganga mmoja wa akili kwa Jina Al Koran na ambaye ni maarufu sana Duniani, aliandika katika moja ya Sura za Kitabu chake ‘Bring out the Magic in Your Mind’ kuhusu “SIRI YA UTAJIRI” aliandika: “Utakapo kutumia pesa zako kumbuka kila wakati kuziombea zibarikiwe. Ziombee ili kila atakayezitumia abarikiwe, zibariki ili ziwalishe wasio na chakula, zibariki ili ziwavishe wasio na nguo, na zibariki ili zikirudi kwako zirudi mara milioni zaidi”. Sasa ndugu zangu, tunao wenzetu Wahitaji. Ni Yatima. Ni Waathirika. Ni Waumini wenzetu na ni Majirani zetu. Tunaishi nao. Tuwasaidie na tuwaombee ili kila tunachokitoa kwao kiturudie mara dufu.

Baba Askofu, Ndugu Wana-Dayosisi, Asubuhi ya leo tumesikia masomo mazuri. Nisingependa kuwachosha zaidi. Nirudie kuwakumbusha ule msemo wa watu wa kale unaosema “Nilililia sana kupata viatu mpaka nilipomuona mtu ambaye hakuwa na miguu.” Tusijisahau kwa kukuza matatizo yetu kwa kisingizio cha kukwepa kuwajali wenye shida. Kwa maana, kwa kufanya hivyo tunakosa Baraka ambazo tayari Mwenyezi Mungu ameshatuandalia. Ukitumia muda wako kwa kujitolea kuwasaidia wengine ambao wana mahitaji, ni njia nzuri ya kupata Baraka za Mwenyezi Mungu na kupata mafanikio zaidi.

Napenda kurudia kuwashukuru sana kwa kunikaribisha katika kushuhudia tuko hili muhimu na la kihistoria katika Dayosisi hii. Mwenyezi Mungu awabariki na zaidi ambariki Baba Askofu JOHN ANDREW SIMALENGA aliyewekwa Wakfu leo na kukabidhiwa Fimbo ili aweze kutimiza kazi aliyotumwa ya kuchunga kondoo zake.

Bwana awabariki sana!

Asanteni kwa kunisikiliza.