Tarehe 27 Aprili, 2021
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Kumi na Saba – Tarehe 27 Aprili, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nawaomba tukae. Tunaendelea na Kikao chetu cha Kumi na Saba leo lakini ndani ya Mkutano wetu wa Tatu, Katibu. NDG. RAMADHAN ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na: NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2021/2022. NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa mwaka wa fedha 2021/2022. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MHE. JOSEPH K. MHAGAMA - K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) kwa mwaka wa fedha 2020/2021 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022. MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA - K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022. SPIKA: Ahsante sana. Katibu. NDG. RAMADHAN ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Tunaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini. Na. 139 Barabara ya Rau Madukani – Mamboleo - Shimbwe Juu - Moshi Vijijini MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara yenye kilometa 13 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) kuanzia Rau Madukani – Mamboleo – Shimbwe Juu katika Jimbo la Moshi Vijijini? SPIKA: Majibu ya swali hilo, Mheshimiwa Naibu Waziri, David Silinde, tafadhali. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:- Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza ahadi zilizotolewa na Waheshimiwa Marais walizozitoa katika Awamu zote. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 na 2019/ 2020 Serikali imeendelea kujenga kipande cha barabara chenye urefu wa mita 288 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 190 kwa barabara ya Rau Madukani – Mamboleo - Shimbwe Juu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, barabara hi iilifanyiwa matengenezo ya muda maalum yenye urefu wa kilometa 9 kwa kiwango cha changarawe ambayo iligharimu shilingi milioni 148.85. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 barabara hii imetengewa bajeti ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilometa 2. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi na matengenezo ya barabara nchini ikiwemo Moshi Vijijini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. SPIKA: Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, swali la nyongeza. MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Mheshimiwa Spika, kutokana na jiografia ya Mkoa wa Kilimanjaro, niseme ukweli kwamba changamoto yetu kubwa 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) kule Kilimanjaro ni barabara hasa Jimbo langu la Moshi Vijijini na wakati wa mvua kama huu kuna mafuriko makubwa sana. Naomba nimuulize Naibu Waziri ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya TPC – Mabogini – Kahe yenye urefu wa kilometa 11.4 na kumalizia zile za Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School - Kiboriloni - Sudini – Kidia? Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ilishasema ingeanza upembuzi yakinifu wa barabara ya Uru – Mamboleo - Materuni yenye kilometa 10.2, ni lini Serikali itafanya zoezi hilo. Ahsante. (Makofi) SPIKA: Sasa Profesa, kwenye swali lako la msingi lilihusu hii barabara ya kilometa 13 kwenye nyongeza umeuliza barabara zingine kabisa, hii wala hujaigusa maana yake umeridhika na swali. Kwa hiyo, Naibu Waziri, jibu lile la pili. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kama ulivyoniongoza, umeniomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kuhusu ni lini upembuzi yakinifu utaanza katika barabara ya Uru – Mamboleo – Materuni yenye urefu wa kilometa 10.2. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais makini kabisa Mama Samia Hassan Suluhu, tumesikiliza maombi ya Mheshimiwa Mbunge. Kwa sababu ameomba tu upembuzi yakinifu na nafahamu mpaka muda huu TARURA wananisikiliza ni agizo langu kwao kwamba sasa watenge fedha waanze upembuzi yakinifu kwa ajili ya barabara hiyo ili iweze kujengwa. (Makofi) Mheshimiwa Spika, pia hizo barabara nyingine zote ambazo ameziainisha, Serikali imesikia tutaziweka katika Mpango kuhakikisha zinakamilika kwa wakati. Ahsante sana. (Makofi) 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) SPIKA: Bado tuko TAMISEMI, swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau. Na. 140 Kero ya Mafuriko Jimbo la Kawe MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la mafuriko katika maeneo ya Mbweni Teta, Bunju Basihaya, Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni katika Jimbo la Kawe? SPIKA: Majibu ya swali hilo, Mheshimiwa David Silinde, tafadhali. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: - Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya mafuriko katika maeneo ya Mbweni Teta, Bunju Basihaya, Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni katika Jimbo la kawe. Serikali kupitia Mradi wa kuboresha Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam (DMDP) imetenga shilingi bilioni 8.4 kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa maji ya mvua wenye urefu wa kilomita 8.89 katika Kata ya Mbweni. Awamu ya pili ya mradi huu itajumuisha mifereji ya maji ya mvua katika maeneo ya Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji ya maji ya mvua ili kuondoa kero ya mafuriko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam ikiwemo Jimbo la Kawe. 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) SPIKA: Swali la nyongeza, nimekuona Mheshimiwa Felista. MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwa sababu mpaka sasa kuna kaya kumi ambazo maji yameingia ndani na hawana pa kuishi katika Mtaa wa Ununio, Serikali ina mkakati gani wa dharura kabla ya kutekeleza mradi huu alioutaja ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata mahali pa kuishi na sehemu zile nilizoainisha zinapata majibu mapema? (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilio hiki ni cha nchi nzima kwa maana matatizo haya yamekuwa yanajirudia kila eneo la nchi; ni lini basi Serikali itaweka mikakati madhubuti ya kujenga mifereji imara ili basi maeneo haya maji yaweze kuelekezwa kwenda kwenye maziwa, mito hata bahari ili kuepuka adha ya magonjwa ya milipuko pia na adha kwa wananchi? Ahsante. (Makofi) SPIKA: Majibu ya swali hilo, Naibu Waziri-TAMISEMI, Mheshimiwa David Silinde, tafadhali. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza alikuwa anaomba kujua upi ni mkakati wa dharura katika eneo la Ununio ambao Serikali imeuweka kuhakikisha tunatatua tatizo hilo la mafuriko. Nimuambie tu kabisa kwamba Serikali iko kazini na baada ya janga hili inafanya tathmini ya mwisho kuhakikisha kwamba tunasaidia maeneo hayo hususan maeneo ya Ununio katika Kata hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha. 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza ni lini Serikali itaweka mikakati madhubuti kuhakikisha kwamba tunaondoa majanga haya hususan kwa kujenga mifereji. Nimhakikishie kabisa kwamba sasa hivi moja ya mkakati mkubwa ambao Serikali unao katika kila barabara tunayoijenga tunaambatanisha na ujenzi wa miundombinu hususan mifereji. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu ya mikakati ambayo ipo na tutaendelea kufanya hivyo. Kwa kadri fedha zitakavyopatikana tutajenga mifereji mikubwa pamoja na midogo kuhakikisha janga la mafuriko nchi nzima katika maeneo yote ambayo tunayasimamia hayapatwi na hii adha ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha. Ahsante sana. SPIKA: Bado tuko Wizara hii hii, tunaendelea na swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu. Na. 141 Ahadi ya Barabara ya Kilometa Tatu Katika Mji wa Kakonko MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:- Mwaka 2015 wakati wa Kampeni, Mhe. Rais aliahidi kujenga barabara ya kilometa tatu katika Mji wa Kakonko ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya. Je, kwa nini