MKUTANO WA KUMI NA SITA Kikao Cha Thelathini
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ________________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA KUMI NA SITA Kikao cha Thelathini - Tarehe 21 Julai, 2004 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Pius Msekwa) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MHE. ARCADO D. NTAGAZWA): Taarifa ya Mwaka na Hesabu za Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira kwa Mwaka Ulioishia Tarehe 30 Juni, 2003 (The Annual Report and Accounts of the National Environment Management Council (NEMC) for the year ended 30th June, 2003). WAZIRI WA SHERIA NA MAMBO YA KATIBA: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba kwa Mwaka wa Fedha 2004/2005. MHE. GEORGE M. LUBELEJE - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA: Taarifa ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala Kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba kwa Mwaka wa fedha Uliopita, Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2004/2005. 1 MASWALI NA MAJIBU Na. 286 Matumizi ya Jina la Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere MHE. ELIACHIM J. SIMPASA aliuliza:- Kwa kuwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere alifanya mambo mengi na makubwa na mema ndani na nje ya nchi kama vile kuwaunganisha Watanzania kujiona wamoja, kuweka misingi ya maendeleo kama shughuli za uchumi, elimu, afya, miundombinu lakini zaidi alikuwa Kiongozi Mashuhuri wa karne katika harakati za Ukombozi wa Afrika, kupinga unyanyasaji, ubaguzi, ukandamizaji wa aina yoyote popote duniani na hivyo kujijengea umaarufu ndani na nje ya Taifa letu:- (a) Je, isingekuwa jambo la busara na la hekima kuhakikisha kuwa Jina hilo (Nyerere) linatajwa kila siku ndani na nje ya nchi kwa kuvipa jina lake vitu kama Dar es Salaam International Airport ikaitwa Nyerere International Airport (NIA) na University of Dar es Salaam kuitwa Nyerere University? (b) Je, kuna utaratibu gani unaotumika katika uchongaji na uchoraji wa Sanamu ya Mwalimu Nyerere ili zionyeshe sura yake kamili kuliko ilivyo sasa? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJEMENTI YA UTUMISHI WA UMMA alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Eliachim Simpasa, Mbunge wa Mbozi Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi wakati nikijibu Swali Na. 259 la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Wawi kuwa, kutunza kumbukumbu za nchi hususan za Waasisi wa Taifa ni jambo la msingi. Aidha, kwa sasa Serikali inaandaa utaratibu wa Sheria utakaojenga mazingira ya kuwa na utamaduni wa kudumu wa kuthamini, kutunza na kudhibiti kumbukumbu za Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa ili kuhakikisha kuwa hazina waliyonayo viongozi wetu hawa haipotei na inakuwepo kwa ajili ya vizazi vijavyo. Mapendekezo ya Mheshimiwa Eliachim Simpasa, ni mazuri na Serikali imeyapokea na itayawasilisha kwa wadau mbalimbali likiwemo Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kupitia Muswada na kutunga Sheria. (Makofi) Mheshimiwa Spika, moja ya mambo ambayo Muswada utazingatia ni matumizi ya Jina la Baba wa Taifa. Muswada huu utaweka utaratibu wa matumizi sahihi ya majina ya Waasisi wa Taifa letu kwa kuhakikisha kwamba, majina yao hayatumiki kibiashara, hayadhalilishwi na hadhi yao haipotei. (Makofi) 2 (b) Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Serikali bado haijawa na utaratibu wa ithibati unaoongoza uchoraji wa picha au uchongaji wa sanamu, hivyo kupelekea watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuchora na kuchonga sanamu za Mwalimu Nyerere zisizoonyesha sura yake kamili. Utaratibu wa kuchora picha au kuchonga sanamu unatokana na fikra, uelewa na ujuzi katika fani ya sanaa. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa Sheria, italifanyia kazi jambo hili ili pawepo na ithibati ya uchoraji picha na uchongaji sanamu zinazoonyesha sura sahihi za viongozi wetu kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sahihi kwa Taifa letu na vizazi vijavyo. MHE. ELIACHIM J. SIMPASA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwa majibu yake mazuri lakini niulize maswali mawili madogo. (a) Katika haya aliyotuahidi na najua utaratibu wa Serikali inaweza kuchukua muda sana, je, anatuhakikishia kwamba inaweza kuchukua muda mfupi iwezekanavyo sheria hiyo kuletwa na utaratibu uweze kuwekwa kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sahihi za Mwalimu na Viongozi wengine? (b) Kwa kuwa sasa kuna sanamu nimeziona mahali fulani na wenzetu wameziona ambazo kwa kweli hazifanani na hata picha kwenye noti ya Sh.1,000/= mimi sijui kama na yenyewe iko sawasawa, je, sasa kama ni sanamu mbaya mbaya ambazo tumeziona zinaweza kubomolewa ili tusahihishe makosa? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJEMENTI YA UTUMISHI WA UMMA: Mheshimiwa Spika, naamini haitachukua muda mrefu kwa sababu process ya kutayarisha Muswada ilishaanza. Nina imani pengine kabla ya mwaka huu wa 2204 kwisha au mapema mwaka 2005, sheria hii itapitishwa. Mheshimiwa Spika, kuhusu sanamu, muda mfupi baada ya kifo cha Baba wa Taifa wataalam mbalimbali walialikwa kukagua sanamu ya Baba wa Taifa iliyotengenezwa na Mtaalam kutoka Urusi. Wataalam walioalikwa walitoka Baraza la Sanaa Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Wizara ya Mambo ya Nje. Wataalam hao walifikia uamuzi kuwa sanamu haikuwa sahihi na sura ya Baba wa Taifa haikuwa sahihi. Hata hivyo, kulikuwa na sanamu iliyochongwa kule Tanga. Sanamu hiyo vile vile haikuwa sahihi na ilivunjwa na ikachongwa upya. Kwa hiyo, Serikali inapenda kuona kwamba, sura za viongozi wetu zinachongwa au zinachorwa kwa usahihi. Na. 287 Ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea za Chumvichumvi MHE. PAUL P. KIMITI (k.n.y. MHE. DR. LAWRENCE M. GAMA) aliuliza:- 3 Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu imejenga heshima kubwa kwa Makampuni na Mashirika ya Kitaifa/Kimataifa kuwekeza katika Taifa letu. Je, kumekuwa na ugumu gani katika kuyashawishi Mashirika/Makampuni hayo ili yakubali kujenga kiwanda cha kisasa cha mbolea nchini kwetu? NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dr. Lawrence Gama, Mbunge wa Songea Vijijini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali ya Awamu ya Tatu imejenga heshima kubwa kwa makampuni na Mashirika ya Kitaifa kuwekeza katika Taifa letu kwa ujumla. Kama inavyojulikana, ushawishi huu upo katika kuweka mazingira mazuri ya kiuchumi ili wanaofikiria kuwekeza waone urahisi wa kufanya hivyo. Katika kipindi kilichopita, hakuna mwekezaji makini aliyejitokeza aidha kufufua kiwanda cha zamani cha mbolea Tanga au kujenga kiwanda kipya mahali pengine. Serikali inaendelea kuhamasisha makampuni ambayo yamekuwa yakifanya biashara ya mbolea ili yaweze kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea nchini hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu inazo malighafi za mbolea ikiwemo gesi asili ya Songo Songo na machimbo ya madini ya phosphate. Malighafi hizo zinaweza kutumika kutengeneza mbolea ambazo zinaweza kufaa sana kwa udongo wa nchi yetu na nchi jirani. Mheshimiwa Spika, suala la kuwekeza au kutowekeza litachukua sura kamili pale mwekezaji atakapojua faida ya kuwekeza katika mradi husika na baada ya kufanya upembuzi yakinifu na upembuzi huo kukubalika katika Mabenki yanayokopesha kwa vile wawekezaji wengi hutumia fedha za Mabenki kuanzisha miradi kama hiyo. MHE. PAUL P. KIMITI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, Waziri atakubaliana nami kwamba, moja ya matatizo ambayo Makampuni mengi na wawekezaji wengi wanayapata ni masharti magumu wanayopewa ili kuingia katika Mikataba hii? Kiwanda cha Mbolea cha Tanga ambacho kimekuwepo kwa siku nyingi kingekuwa ni mfano mzuri wa kumpa mtu yeyote hata kwa mpango wa dola moja, kwa nini tusitumie nafasi hiyo ili angalau tukampata mwekezaji ambaye alionekana angeweza kupatikana ili kiwanda hiki kwa kushirikiana na Kiwanda cha Minjingu, kiendelee kutoa mbolea kwa ajili ya matumizi ya nchi yetu? NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba, hata ingebidi kukitoa Kiwanda cha Tanga bure tungekitoa lakini tumejitahidi kama tulivyojitahidi na Kiwanda cha Southern Paper Mill zaidi ya miaka 15, hatukupata mwekezaji yeyote aliyejitokeza wala aliyetamani kuzalisha kwa kutumia 4 mitambo iliyokuwepo. PSRC ikaona matangi yanaharibika, mitambo inazidi kuoza, wakakiuza kiwanda hicho kwa Kampuni ya Gulf Bulk Petroleum Tanzania Limited. Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina wazo la kutafatuta mwekezaji makini haswa kama nilivyosema katika swali la msingi kwamba tunayo gesi ya Songosongo na pia tunayo phosphate ya Minjingu ambayo tunaweza kuitumia kama malighafi ya kuanzisha Kiwanda hicho. MHE. MUSA A. LUPATU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mwekezaji aliyenunua Kiwanda cha Mbolea Tanga amenunua eneo kubwa sana la zaidi ya heka 60 na heka hizi ziko mjini na kwa kuwa yeye kazi yake ni kuuza mafuta, je, Serikali haioni kwamba ingekuwa jambo la busara kama eneo hili lingegawiwa akachukua eneo tu ambalo linatosheleza kazi ambayo angehitaji kufanya? (Makofi) WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, aliyenunua Kiwanda cha zamani cha Mbolea cha Tanga amenunua non- core assets. Ukinunua non- core assets, mali ambayo siyo ya msingi, huna masharti ya kukiendeleza kiwanda kile. Ananunua eneo lile kwa madhumuni ya kufanya shughuli nyingine ndio maana huyu bwana anaendesha shughuli ya mafuta. Lakini kama alinunua eneo kubwa heka 60 ambazo yeye hazitumii, utaratibu upo wa kuwezesha sehemu moja ya eneo lile likatengwa kwa ajili