Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA MBILI Kikao cha Ishirini na Mbili - Tarehe 11 Julai, 2003 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Pius Msekwa) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 210 Muundo wa Utumishi wa Watendaji wa Kata na Vijiji MHE. ANATORY K. CHOYA (k.n.y. MHE. MGANA I. MSINDAI) aliuliza:- Kwa kuwa Muundo wa Utumishi wa Watendaji wa Kata na Vijiji ulitengenezwa mwaka 1993 na kwamba sasa umepitwa na wakati na kuleta ugumu katika kupandisha vyeo na kuajiri upya Watendaji wa Kata na Vijiji:- (a) Je, Serikali inasema nini juu ya hali hiyo? (b) Kwa kuwa sasa hivi tunao watu wengi wasomi hata waliomaliza Vyuo Vikuu wanaoomba kazi hizo, je, Serikali itakuwa tayari kutoa muundo mpya sasa? (c) Je, Serikali itakuwa tayari kupitia miundo yote ambayo imepitwa na wakati ikiwemo muundo wa wapiga type, Makatibu Mahsusi na Waandishi Waendesha Ofisi uliotolewa tarehe 29 Agosti, 1991 na 1993? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgana Msindai, Mbunge wa Iramba Mashariki, swali lake lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, naomba kukubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa muundo wa utumishi wa Watendaji wa Kata na Vijiji umepitwa na wakati. Aidha, muundo huo umekuwa unakumbwa na mabadiliko mengi na hivyo kuleta ugumu katika 1 kupandisha vyeo na kuajiri upya Maafisa Watendaji Kata na Vijiji. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Ofisi yangu kwa kushirikiana na Idara Kuu ya Utumishi imekwishaandaa miundo mipya ya ajira za Maafisa hawa inayozingatia dosari zilizopo na mahitaji ya sasa ya wataalam. Miundo hii imekwishapitishwa na Baraza la Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa mwanzoni mwa mwaka huu wa 2003. (b) Mheshimiwa Spika, ni kweli katika soko kuna wasomi wa ngazi zote wanaoomba kazi za Uafisa Mtendaji wa Kijiji na Kata. Kama nilivyosema katika jibu la kwanza, kwa kuzingatia mahitaji halisi ya sasa, Ofisi yangu imekwishakamilisha kuandaa na kupitisha miundo mipya ya Maafisa Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa itakayowezesha kuwapata wasomi waliopo katika soko. Tunashauri Waheshimiwa Wabunge tusaidiane kuwahamasisha wasomi hawa walioko katika Majimbo yetu ili waweze kuomba nafasi hizo muda utakapowadia. (c) Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imekuwa daima ikiboresha miundo ya watumishi wake hali inaporuhusu. TUMITAA imekwishafanya mapitio ya miundo mbalimbali ya watumishi katika Serikali za Mitaa ipatayo 50 ambapo kada za watumishi waliotajwa na Mheshimiwa Mbunge pia imepitiwa. Hivi sasa imepelekwa kwa Mpiga Chapa na baada ya hapo itasambazwa na kuanza kutumika katika mwaka wa fedha wa 2003/2004. MHE. LUCAS L. SELELII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa kazi hii ya Utendaji wa Kata au Utendaji wa Kijiji inahitaji taaluma kama zilivyo kazi nyingine zenye taaluma. Lakini kwa bahati mbaya sana hakuna vyuo ambavyo vinafundisha kazi ya Watendaji wa Kijiji au wa Kata; na kwa kuwa sasa hivi Serikali imekwishaondoa kazi ya kukusanya kodi hivyo wanashiriki katika ulinzi wa amani na kuleta maendeleo; je, Wizara ipo tayari kutayarisha vyuo ili kuweza kuwatayarisha Watendaji wa Kata na Vijiji waweze kwenda sambamba na maendeleo na ulinzi wa amani kama sera inavyotakiwa? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, vyuo kwa ajili ya kuwasaidia Watendaji wa Kata na Vijiji kuweza kuboresha elimu yao tunavyo. Kipo Chuo cha Hombolo ambacho ni mahsusi kwa ajili ya shughuli za Serikali za Mitaa na kwa sasa kimekwishaanza kutumika katika mafunzo ya awali kwa ajili ya Watendaji wa Kata. Lakini vile vile kipo pia Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ambacho kipo chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji, ambacho nacho ni chuo kinachotoa mafunzo mazuri tu kwa ajili ya ngazi kama hizi wa Watendaji katika kuwawezesha kuweza kufanya kazi zao vizuri. Kwa hiyo, tutakachofanya ni kuendeleza hizi juhudi zilizopo hivi sasa na kama hapana budi tutatumia hata vyuo vingine vya maendeleo ya jamii vilivyoko katika Mikoa ili kuweza kuboresha hali hiyo. (Makofi) MHE. MARIAM SALUM MFAKI:Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. 2 Mheshimiwa Spika, kutokana na majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa niulize kwamba, sasa hivi Serikali imekubali kuwalipa Watendaji wa Kata na Vijiji; je, Serikali imeandaa muundo ambao utasaidia kuonyesha utaratibu wa upandishaji vyeo kwa wakati unaokuja? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimeeleza katika maelezo ya msingi hapa kwamba miundo kwa ajili ya Watendaji wa Kata na Vijiji tayari imekwishaandaliwa na imekwishakamilishwa, hivi sasa tumeshaipeleka kwa Mchapaji wa Serikali, nadhani ikiishatoka tutafanya jitihada pengine kuisambaza kwa Waheshimiwa Wabunge ili muweze kupata fursa vile vile ya kuona kilichowekwa katika miundo hiyo ni kitu gani. Na. 211 Huduma na Mishahara ya Walimu MHE. BENEDICTO M. MUTUNGIREHI (k.n.y. MHE. MUTTAMWEGA B. MGAYWA) aliuliza:- Kwa kuwa Walimu ni muhimu kama watumishi wengine katika jamii inayojua maana ya maendeleo:- (a) Je, ni kwa nini mishahara ya walimu imeendelea kuwa midogo, inacheleweshwa kulipwa na kila wakati walimu hulazimika kulipwa mishahara yao kwa kujipanga mstari kama watoto? (b) Je, ni kwa nini walimu hawapewi huduma ya usafiri wa mazishi wanapofiwa na ndugu zao wa karibu kama vile mume, mke na watoto kama ilivyo kwa watumishi wengine? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muttamwega Mgaywa, Mbunge wa Mwibara, swali lake lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa walimu ni muhimu kama watumishi wengine katika jamii yoyote ile inayojua maana ya maendeleo. Hivyo wote wanapaswa kushughulikiwa sawa na Serikali. Kuhusu tatizo la mishahara ya walimu kuwa midogo, ni suala linalowakabili watumishi wote wa Serikali na sio walimu peke yao. Mishahara ya walimu kama ilivyo mishahara ya watumishi wengine hupangwa na Serikali na hutangazwa kupitia Waraka wa Serikali wa mwaka husika. Karibu kila mwaka mishahara ya watumishi ikiwemo ya 3 walimu imekuwa ikiboreshwa kulingana na uwezo wa Serikali na itaendelea kuboreshwa kadri hali itakavyozidi kuwa nzuri. Mheshimiwa Spika, kuhusu ucheleweshaji wa malipo ya mishahara kwa walimu. Tamko la Mheshimiwa Rais la kulipa mishahara ya watumishi wote ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi kwa sehemu kubwa kabisa linazingatiwa na mamlaka za Halmashauri zetu hapa nchini. Walimu katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge tunapenda kumthibitishia kwamba wamekuwa wanalipwa mishahara yao kwa kuzingatia tamko hilo kila wakati. Mheshimiwa Spika, kuhusu walimu kujipanga katika mstari wakati wa kupokea mishahara, utaratibu huu ni wa kawaida na hutumika kwa watumishi wote wanaopokelea mishahara yao Maofisini ili kurahisisha ulipaji, kupunguza msongamano na fujo. Aidha, utaratibu huu hutumika pia sehemu nyingine kama vile maeneo ya huduma za afya, Mabenki na hata wakati wa kupiga kura. Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, yenyewe inao utaratibu mzuri zaidi kwani wametenga maeneo matatu kwa ajili ya kulipia mishahara. Maeneo hayo ni Kibara, Nyamuswa na Makao Makuu ya Halmashauri. Utaratibu huu umesaidia sana kupunguza msongamano katika eneo moja. (b) Mheshimiwa Spika, kulingana na Kanuni za Tume ya Utumishi wa Walimu, Kanuni Na. 72, mwalimu anapopata maafa yeye mwenyewe atahudumiwa kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Serikali. Huduma anazotakiwa kupewa kwa mujibu wa kanuni hizo ni jeneza, sanda, mashada na kusafirisha mwili wa marehemu nyumbani kwake. Mheshimiwa Spika, katika kutoa huduma hii, Halmashauri za Wilaya ambazo kieneo ni kubwa na bado zina miundombinu duni, huduma hizi hazitolewi kwa ufanisi kama zinavyotolewa katika Halmashauri za Miji. Iwapo mwalimu atafiwa mzazi, mwenzake au mtoto kwa utaratibu ulivyo sasa hapati huduma hizo au hastahili kupata huduma hizo ingawa mara nyingi Wahasibu wamekuwa wakitumia ubinadamu kutoa huduma mbalimbali. MHE. BENEDICTO M. MUTUNGIREHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa majibu yake mazuri. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa walimu katika utumishi wa Serikali ndio wengi; na kwa kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa mikopo kwa vikundi vya wakulima, vijana na wetu wengine; je, Serikali kuanzia sasa iko tayari kuweka programu ya kuwakopesha walimu kwa kuwa mishahara yao inapita kwenye payroll na inaweza kuwajua huko waliko kwa kupitia Benki ya NMB? (Makofi) Mheshimiwa Spika, pili, kama Serikali inaona kuwa wazo hili inaweza ikalichukua, iko tayari kuanzia sasa kulifanyia kazi ili ifikapo mwaka 2004/2005 iweze kuweka utaratibu, walimu waweze kukopa? (Makofi) 4 NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba walimu kama watumishi wengine wanastahili vile vile kupewa mikopo katika Halmashauri zao kulingana na uwezo wa Halmashauri. Mheshimiwa Spika, nami ninayo mifano ya baadhi ya Halmashauri ambao wamefanya juhudi za kukopesha baiskeli kwa walimu wao na wameendelea kuwakata bila tatizo lolote. Kwa hiyo, ni suala tu kwa kweli la kuendeleza pengine na kupanua elimu hii kwa Halmashauri zote ili waweze kila watakapoweza kutoa mikopo. Kwa hiyo, suala la utaratibu lipo, nadhani