MKUTANO WA TATU Kikao Cha Saba – Tarehe 14 Aprili, 2011
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Saba – Tarehe 14 Aprili, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, leo ni Siku ya Alhamisi, kama kawaida yetu, siku hii dakika thelathini za kwanza tunakuwa na maswali kwa Waziri Mkuu. Anayeanza ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani. MHE. FREEMAN A. MBOWE (KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI): Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la kwanza kwa Waziri Mkuu. Kwa kuwa Katiba ni Roho ya Taifa; na kwa kuwa kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya mabadiliko au kuandikwa upya kwa Katiba ya Nchi, jambo ambalo Serikali imeridhia kupitia kwa Rais; na kwa sababu Serikali ilileta Muswada katika utaratibu wa haraka, Muswada wa Constitution Review:- Je, baada ya Serikali kuona reaction ya wadau mbalimbali wakiwemo wanazuoni, Vyama vya Siasa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau wengine mbalimbali, ambao wanafikiri kwamba, mchakato huu pengine unakwenda kwenye kasi ambayo badala ya kujenga inaweza ikatia nyufa katika mahusiano yetu; ni kwa nini Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu wasitoe tamko rasmi la Serikali la kukubaliana na utashi wa wadau ili kuusogeza Muswada huu mbele Wananchi wapate fursa ya kutosha ili kuweka mahusiano mema ambayo tunategemea katika Taifa letu? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimjibu Mheshimiwa Mbowe, ambaye ndiye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, swali lake kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali imewasilisha Muswada hapa Bungeni na tuliwasilisha kwa Hati ya Dharura, kwa dhamira njema kabisa kwa kuwa tuliamini kabisa kwamba, watu wana hamu na shauku kubwa ya kutaka kufikia hatua ya 1 pili ya mchakato, kwa maana ya Katiba yenyewe baada ya kuwa Tume ya Katiba imeundwa.
[Show full text]