Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ___________________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Thelathini na Nne – Tarehe 27 Julai, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Sylvester Massele Mabumba) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha, 2011/2012. NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI: Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha, 2011/2012. MWENYEKITI WA KAMATI YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi kwa Mwaka 2010/2011 Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani juu ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MASWALI NA WAJIBU Na. 312 Kuimarisha Barabara ya Mpopera – Mkarongo – Kipatimu MHE. MURTAZA A. MANGUNGU aliuliza:- Kata ya Kandawale ni kisiwa ambapo mvua zinanyesha na hakuna daraja kwenye Mto Matandu la kuunganisha Njinjo na Kandawale. 1 Je, Serikali i na mpango gani wa kuimarisha barabara ya Wilaya ya Mpopera – Mkarongo – Kipatimu ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa iliomba fedha za ziada kwa ajili ya hiyo miaka sita iliyopita. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Murtaza Mangungu, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa barabara za Halmashauri zikiwemo barabara za Kata ya Kandawale. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Serikali kuanzia mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2010/2011 iliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 1.327 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 832 ili ziweze kupitika wakati wowote. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imeidhinishiwa shilingi milioni 436 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 284. Hali hii inaonesha kuwa fedha za matengenezo ya barabara katika Halmashauri ya wilaya ya Lindi zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka sawa na ongezeko la asilimia hamsini na tano (55%) ya Bajeti. Aidha, kwa mwaka 2011/2012 Halmashauri imetenga shilingi milioni 27 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo barabara ya Mkarongo – Kipatimu yenye urefu wa kilomita 12 kupitia TASAF. Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga fedha kupitia Mfuko wa Barabara ili kutengeneza barabara hii ili iweze kupitika wakati wote. (Makofi) MHE. MURTAZA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Majibu ya Mheshimiwa Waziri kwa imani yangu hayawiani na swali ambalo nimeuliza. Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa iliomba fedha maalum kupitia Mfuko wa Barabara, ili barabara hii iweze kutengenezwa. Wilaya ya Kilwa na Mheshimiwa Waziri mwenyewe anajua ukubwa wake ni almost karibu mkoa mzima wa Kilimanjaro. Shilingi bilioni 1.3 kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa ajili ya kutengeneza barabara zote za Wilaya ya Kilwa ni jambo ambalo halipo. (i) Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba Mheshimiwa Waziri anikubalie na aliambie Bunge hili na wananchi wa wilaya ya Kilwa, kama yuko tayari kwenda kutembelea eneo husika ili majibu yake au utekelezaji wa Serikali uwiane na matakwa halisi, siyo takwimu ambazo zinaletwa hapa na Wataalam ambazo siyo sahihi na si za kweli. Hilo la kwanza. (ii)Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa wananchi wanasumbuka sana kuzunguka umbali mrefu mno, lakini bado tuna tatizo la daraja katika barabara hiyo, kipande cha kati ya Njinjo na Kandawale, mto Matandu. Je, Waziri yupo tayari kufuatana na mimi tukaangalie eneo hilo ili aone uhalisia na atutengee fedha ili daraja lijengwe? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (TAMISEMI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Murtaza Mangungu, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wala sipati taabu kuelewa kitu anachozungumzia Mheshimiwa Murtaza Mangungu. Hii shida wanayopata pale hajaeleza zaidi, hapo kwenye hilo daraja analolisema amewahi kufa mtu. Kwa hiyo, siyo jambo ambalo mimi ninalichukua kwa utani hapa au silichukulii uzito unaostahili. Serikali inatambua tatizo hilo. Mheshimiwa Mbunge anafahamu kabisa kwamba, lile eneo analolizungumzia wameweka drift. Kwa hiyo, mvua zikinyesha pale watu hawawezi kupita kwenda hospitali, kwenda Makao Makuu ya Wilaya, sokoni na wala sihitaji hata kufika Kilwa. 2 Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua kwamba kuna tatizo kubwa sana na ndiyo maana nimemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hii tukae. Nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kilichotokea; wana daraja lingine ambalo halitaji hapa, linaitwa Mikungo Chapita ambalo ndilo lililochukua fedha nyingi sana na waliliona kama ni kipaumbele, sitaki kutumia takwimu hizi kutetea jambo hili, wakazipeleka fedha kule. Nimewauliza kwamba ni kwanini mlipeleka fedha kule? Wakasema hili daraja ni muhimu sana, sana kwa sababu lile hata kama ni wakati wa kiangazi hawawezi pale. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Murtaza Mangungu kwamba tunatambua daraja hili lina matatizo, kama ni kwenda Kilwa amwambie Mzee Mtopa, mimi nitakuja twende wote tukaone hilo eneo ili tupate tawkimu sahihi. Lakini nataka niseme kwamba anachosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli kuna tatizo pale, kwa hiyo tutakwenda kumsaidia. MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo makubwa ya barabara ambayo watu wa Kilwa Kaskazini wana- face ni matatizo makubwa kwenye barabara zote za halmashauri, manispaa na majiji. Nilikuwa namwuliza Mheshimiwa Waziri, hivi si umefika wakati sasa Serikali ifanye maamuzi ili barabara zote nchini zihudumiwe na mtu mmoja ili iwe rahisi kujua upungufu wa fedha tunazozihitaji? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (TAMISEMI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Peter Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama nitakuwa nimempata vizuri sana, lakini naona anachotaka kusema ni kwamba barabara zote zirudishwe Wizara ya Ujenzi au TAMISEMI. Ninachokifahamu katika jambo hili ambalo analizungumzia Mheshimiwa Mbunge, na labda baadaye nitamfuata ili tujue vizuri anachokisema. Hapo nyuma tuliwambia watu kwamba tunakwenda kwenye kitu kinachoitwa D by D (Decentralisation by Delovution) maana yake unapeleka madaraka kwa wananchi, lakini wakati huohuo unawapelekea nyenzo za kufanyiakazi. Sasa kama utarudi nyuma ukasema tupeleke barabara zote Wizara ya Ujenzi, dhana nzima ya kupeleka madaraka kwa wananchi inakuwa imekufa, inakuwa haipo. Tunachotaka hapa ni kwamba wananchi wenyewe ndiyo wanaojua matatizo waliyonayo kule katika maeneo yao, kwa hiyo wao ndiyo wanaoibua miradi na kusema mradi huu tunadhani sisi kwetu ni kipaumbele. Ukiwaondolea wananchi nafasi hiyo maana yake umewaondolea hata umiliki wa mchakato mzima unaohusikana na maendeleo yao tutakuwa tunarudi kule kule. Makao Makuu Dodoma na Dar es Salaam, ndiyo watakuwa wanafanya maamuzi kwa niaba ya wananchi, kitu ambacho kwa maoni yangu kitakuwa tatizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mheshimiwa Peter Serukamba anazungumzia habari ya kuwa na chombo maalum kitakachosimama kwa ajili ya barabara, lakini ambacho kitabeba mawazo ya wananchi kule waliko, mimi sina tatizo nacho. Hilo ni suala la kisera, tutapokea hayo tutapeleka katika mamlaka tuzungumze vizuri. Nakiri kwamba sikumpata vizuri, lakini hayo ndiyo mawazo ambayo mimi naona yanaweza yakatusaidia. Na. 313 Fedha zilizotengwa kwa ajili ya Uendeshaji wa Shule MHE. TUNDU A. LISSU aliuliza: - 3 Serikali katika mwaka wa fedha 2009/2010 ilitenga jumla ya shilingi 55,553,525,822.75/= kwa ajili ya uendeshaji shule. Kati ya fedha hizo, shilingi 35,656,504,688.15/= ndizo zilizotumika kwa kusudio hilo hadi kufikia mwezi Machi, 2010 na shilingi 21,396,303,806.40/= zilibaki. Lakini licha ya kutengwa fedha hizo, wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakilazimishwa kuchangia ujenzi wa shule za Sekondari za Kata kwa kujenga madarasa, nyumba za Walimu, kununua madawati, karatasi, kulipia taaluma, mitihani na walinzi wa shule hizo:- (a) Je, kwa nini fedha zinazotolewa hazitumiki zote badala yake Wananchi wanachangishwa kwa nguvu kwa kisingizio kuwa Serikali haina fedha za kutosha kujenga na kuendesha shule? (b) Je, kiasi cha shilingi 21,396,303,806.40/= zilizobaki hadi kufikia Machi, 2010 zimepelekwa wapi? (c) Je, Serikali iko tayari kupiga marufuku michango hiyo ya nguvu na kueleza sababu za kubaki kwa fedha hizo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tundu Antiphas Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, lenye sehemu (a), (b) na ( c ) kwa pamoja kama ifuatavyo. (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM),