Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _____________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ MKUTANO WA KUMI NA MBILI KIKAO CHA ISHIRINI – TAREHE 9 JULAI, 2008 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Nasibu Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 177 Kampeni Dhidi ya Wahujumu Uchumi Mwaka 1983 MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO aliuliza:- Kwa kuwa mwaka 1983 Serikali iliendesha kampeni ya kuwanasa wahujumu uchumi:- (a) Je, ni watu wangapi waliofungwa kwa kuhujumu uchumi? (b) Je, ni watu wangapi walioachiwa na mahakama kwa kutokuwa na kesi na kurejeshewa mali zao? (c) Je, ufisadi uliozuka kwenye miaka hii ya 2000 hauwezi kushughulikiwa kama ilivyofanyika mwaka 1983? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa William H. Shellukindo, Mbunge wa Bumbuli, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- 1 (a) Kampeni ya kuwanasa wahujumu uchumi ya mwaka 1983 ilikuwa ni operesheni ya Serikali katika kukabiliana na wafanyabiashara wa magendo wenye kuhodhi bidhaa na kusababisha upungufu mkubwa wa mahitaji muhimu hususan vyakula, dawa na vifaa vya hospitali kwa ajili ya matibabu na pia kuwadhibiti watoroshaji wa bidhaa nyingi kwenda nchi za nje. Zoezi hilo lilibidi litekelezwe ili kuwashtukia na kuwabaini wahusika wote na wadau wao. Wengi wao walikuwa ni wafanyabiashara wa bidhaa za aina mbalimbali zisizo halali. Kutokana na zoezi la waliotuhumiwa kuhujumu uchumi ni watu wengi walikamatwa. Kati yao walishitakiwa na kupatikana na hatia. Kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama waliohusika walifungwa na kutumikia vifungo vyao magerezani. (b)Idadi ya waliokamatwa mwaka 1983 walikuwa zaidi ya watu 4,000 hii ni kwa mujibu wa Tume ya Jaji Mwita iliyotembelea mikoa yote Tanzania Bara mwaka 1990. Walioachiliwa na mahakama yakiwepo maamuzi ya mahakama ya kurejeshewa mali zao au kulipwa fidia Serikali ilitekeleza maamuzi hayo. Katika uhakiki wa mwisho wa zoezi hilo watu 148 walilipwa kifuta machozi kilichofikia jumla ya shilingi 849 milioni. Hii ni kutokana na mapungufu mengi yaliyojitokeza hususan kukosekana kwa vielelezo na kumbukumbu sahihi. (c) Mheshimiwa Naibu Spika, matukio ya kupotea kwa fedha za umma katika miaka ya 2000 na kuhusishwa na ufisadi yamekuwa yakishughulikiwa kwa utaratibu tofauti na ule wa operesheni ya mwaka 1983. Mazingira ya upotevu wa fedha katika taasisi za umma na sekta binafsi umesababishwa na ubadhirifu, kutokuwajibika na ukiukwaji wa maadili. Tayari Serikali imeunda tume mbalimbali kuchunguza tuhuma hizo na ukweli utakapobainika hatua za kisheria zitachukuliwa. MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, ninapenda kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu nimeingia hapa nimekuta majibu ya swali hili yapo kwenye eneo langu hapa. Kwa hiyo, nashukuru sana na nadhani Mawaziri wengine wafuate mfano huo wa kutekeleza Kanuni zetu. (a)Kwa kuwa zoezi la sasa hivi la kupambana na ufisadi linashughulikiwa katika ngazi ya juu zaidi na kwa kuwa kuna ufisadi mdogo mdogo huko vijijini wa kula michango ya wananchi, kutotoa hesabu za michango ambayo inatakiwa itolewe kisheria. Je, si vizuri zoezi hilo likiendelea mpaka sehemu ya chini na hivyo ikawa ni kampeni ya aina peke yake? (Makofi) (b) Kwa kuwa Serikali imesema kabisa kwamba wale walionekana hawana makosa wameachiliwa na mahakama wamelipwa fidia. Je, ni lini Mzee Omar Mpalahole wa Kijiji cha Manga, Kata ya Funta, tarafa Bumbuli, Jimbo la Bumbuli atalipwa fidia yake kwa sababu ilidhihirika waziwazi kabisa kwamba alikuwa hana kesi na namshukuru sana Msajili wa Mahakama Kuu kwa kumsaidia kutafuta faili la kesi hiyo ya mwaka 2 1983 na ilipatikana mwaka 200. Kuanzia mwaka 2001 mpaka sasa hivi anafuatilia kulipwa fidia yake, ameshakuja Dodoma mara 8 kwa tarehe ambazo ameziandika. Je, ni lini atalipwa fidia yake? Nashukuru sana. (Makofi) NAIBU SPIKA: Hilo la pili tatizo. Lakini la kwanza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, jaribu kujibu. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa William Shellukindo, Mbunge wa Bumbuli, maswali yake mawili kama ifuatavyo:- Kwanza, lile analoliita ufisadi mdogo mdogo ngazi ya chini kwa sasa linashughulikiwa na sheria zilizopo na sheria hizo zinajitosheleza. Pili, kuhusu suala la mpiga kura wake, kutoka Bumbuli ambaye alikumbwa wakati huo na operesheni hii naomba nimkumbushe Mheshimiwa Shellukindo kwamba ule ulikuwa ni wakati muhimu na zoezi hili lilikuwa gumu sana kutekeleza. Kwa hiyo, hata fidia nayo ilikuwa ngumu kwa sababu mbalimbali hasa nyaraka na ushahidi. Hata hivyo na hili analifahamu kwa sababu aliwahi kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu na wengi katika Bunge hili baadhi yetu tumeshughulikia masuala haya. Kwa hiyo, suala lake kama lina ushahidi na kuna jalada tunaomba alete vielelezo hivyo tuone namna ya kumsaidia huyo mpiga kura wake. MHE. ALOYCE B. KIMARO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina swali moja kama ifuatavyo:- Waziri anaweza kuahidi hapa Bungeni kwamba wale waliokamatwa na wana vielelezo kamili na hawajalipwa fidia wakileta vielelezo yuko tayari kuvishughulikia na kuwapa fidia? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Aloyce Kimaro Mbunge wa Vunjo, swali lake la nyongeza kama ifuatavyo:- Nimemwelezea Mheshimiwa William Shellukindo kwamba tutaangalia nyaraka alizonazo mpiga kura wake kwa vile inaonekana nyaraka hizo zilikuwepo kabla mlango wa kutoa kifuta machozi ulikuwa haujafungwa. Kwa kweli masuala yote yanahusu wahujumu uchumi ya mwaka 1983 yalishughulikiwa na hatimaye kufikia mwaka 2000 basi yote yalikuwa yamefungwa na hatushughuliki tena na malalamiko kuhusu wahujumu uchumi kwa makosa yaliyotokea mwaka 1983. NAIBU SPIKA: Dakika za swali hilo zimekwisha. 3 Na. 178 Uboreshaji wa Barabara Vijijini MHE. ANNA RICHARD LUPEMBE aliuliza:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuziboresha barabara za vijijini ambazo ndiyo vyanzo vya mapato kama ilivyo kwa barabara ya Mtimbwa kwenda Chipu na ile ya Sintali kwenda Kala ambako kunapatikana samaki wabichi na dagaa biashara ambazo zinafanywa na wananchi wa maeneo hayo? (b) Je. Serikali haioni kuwa ikitengeneza barabara hizo kutawawezesha wananchi wa maeneo hayo waweze kusafirisha bidhaa zao wakati unaofaa kwenda sokoni na kuongeza ajira kwa vijana? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a)Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba barabara za vijijini ni muhimu kwa wakulima kusafirisha mazao yao na pia kupeleka huduma mbalimbali kwa wananchi kwa maeneo hayo. Mnamo tarehe 23 Juni, 2008 katika Kikao cha Tisa cha Mkutano huu wa kumi na mbili unaeondelea hapa nilijibu swali Na. 75 linalofanana na swali hili kutoka kwa Mheshimiwa Suleiman Omar Kumchaya, Mbunge Lulindi. Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleza Bunge lako tukufu kwamba Serikali imekuwa ikiongeza Bajeti ya matengenezo ya barabara zinazohudumiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hata hivyo ukweli ni kwamba fedha za mfuko wa barabara zilizoidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa mwaka 2008/2009 ni shilingi bilioni 65, kama ilivyokuwa mwaka wa fedha uliopita. Pamoja na hali hiyo, mwaka wa fedha wa 2007/2008 Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imetengewa jumla ya shilingi milioni 323.4na kwa mwaka 2008/2009 imetengewa shilingi milioni 353.94. Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuboresha barabara analozungumzia Mheshimiwa Mbunge, ni jukumu la Halmashauri (Baraza la Madiwani) kuainisha barabara zitakazotengewa Bajeti kwa mwaka husika. Barabara ya Mtimbwa- Chipu aliyoizungumzia Mheshimiwa Mbunge, ni sehemu tu ya barabara ya Mtimbwa – Ntalamila yenye urefu wa km. 42. Barabara hii awali ilikuwa ikihudumiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga. Kwa hivi sasa barabara hii inafanyiwa matengenezo na wakala wa barabara TANROADS Mkoa wa Rukwa. Kwa mwaka huu wa fedha 2008/2009 barabara hii imetengewa shilingi milioni 32 kwa matengenezo ya kawaida (routine maintenance). 4 Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Sintali kwenda Kala ina urefu wa km 67. Barabara hi inahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Katika Bajeti ya mwaka 2007/2008 barabara hii ilitengewa shilingi milioni 48 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum (periodic maintenance) na shilingi milioni 40 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi (spot improvement). Kwa mwaka wa fedha 2008/2009 Serikali imetenga shilingi milioni 44 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum km. 4 na shilingi milioni 30 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi kwenye barabara ya Nkana – Kala yenye urefu wa km. 20 ambayo ni sehemu ya barabara ya Sintali – Kala. (b)Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ikitengeneza barabara hizo itawawezesha wananchi wa maeneo hayo waweze kusafirisha bidhaa zao kwa wakati muafaka kwenda maeneo mbalimbali yakiwemo masoko. Hii itasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na vijana. Pamoja na fedha zilizotengwa kutoka mfuko wa barabara, kwa mwaka 2008/2009 Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pia imetengewa shilingi milioni 80 kutoka programu ya usafiri katika Halmashauri. Juhudi zote hizi ni kielelezo dhihiri kwamba Serikali imedhamiria kufungua barabara za vijiji kwa kuwa ni kiungo muhimu kwa barabara za Wilaya na Mkoa. MHE. ANNA RICHARD LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa