1458125901-Hs-15-39
Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ________________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Thelathini na Tisa – Tarehe 24 Juni, 2014 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anna S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu! MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunaanza Maswali na Ofisi ya Waziri Mkuu, atakayeuliza swali la kwanza Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha. Na. 293 Tatizo la Uchafu Katika Jiji la Dar es Salaam MHE. MARYAM S. MSABAHA aliuliza:- Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa uchafu na ombaomba, jambo ambalo linasababisha kero kwa wakazi wake na wageni wanaofika nchini. (a) Je, Serikali ina mikakati gani ya kumaliza tatizo la ukusanyaji wa taka katika Jiji hilo? 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) (b) Je, Serikali inasema nini katika kutumia taka kutengeneza vitu vingine kama mbolea au kutumia taka hizo kufua umeme kama zinavyofanya nchi nyingine? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, changamoto inayolikabili Jiji la Dar es Salaam kuhusu usafi ni kuwepo kwa kiwango kikubwa cha uzalishaji wa taka ikilinganishwa na uwezo wa Jiji kuzoa taka hizo. Uzalishaji wa taka katika Jiji kwa sasa ni wastani wa tani 4,252 kwa siku wakati uwezo uliopo wa kuzoa taka ni wastani wa tani 2,126 kiasi cha 50% kwa siku. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hii Jiji limetumia shilingi bilioni moja (bilioni 1) kwa ajili ya kununulia mtambo mpya wa kusukuma taka, yaani Buldozer D.8, ununuzi wa malori mawili yenye tani 18 kwa ajili ya kuzoa taka na ununuzi wa Compactor moja kwa ajili ya kushindilia taka.
[Show full text]