Hotuba Ya Waziri Wa Uchukuzi, Mhe. Dkt
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
HOTUBA YA WAZIRI WA UCHUKUZI, MHE. DKT. HARRISON G. MWAKYEMBE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014 UTANGULIZI 1. Mheshimiwa Spika, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyochambua bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kuweka mezani taarifa ya Kamati mbele ya Bunge lako Tukufu, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako likubali kupokea, kujadili na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2013/2014. 2. Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kukutana tena leo kujadili maendeleo ya Sekta ya Uchukuzi, Hali ya Hewa na Taifa letu kwa ujumla. 3. Mheshimiwa Spika, napenda vilevile nimpongeze kwa namna ya pekee Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa Mwenyekiti wa Chama 1 cha Mapinduzi. Kuchaguliwa kwake, tena kwa kishindo, ni ushahidi tosha wa imani kubwa waliyonayo wana CCM kwake kutokana na kazi nzuri aliyoifanya miaka mitano ya kwanza ya uongozi wake. Aidha, nawapongeza Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Mhe. Philip Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara) na Mhe. Abdulrahman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM. Binafsi nina imani kubwa kuwa safu hii mpya ya uongozi yenye rekodi ndefu ya utendaji uliotukuka nje na ndani ya Chama cha Mapinduzi itatusogeza karibu zaidi na malengo tuliyojiwekea kama Taifa ya kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. 4. Mheshimiwa Spika, niruhusu vilevile nitumie fursa hii kuwashukuru Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wao imara na wa mfano ambao umeisaidia sana Wizara ya uchukuzi katika utekelezaji wa majukumu yake. 5. Mheshimiwa Spika , naomba nimalizie kwa pongezi zifuatazo: kwanza kwako wewe binafsi Mhe. Spika, Naibu wako, Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb) na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendelea kuliongoza Bunge letu kwa staha, 2 uvumilivu mkubwa na bila kuyumba katika kusimamia Kanuni tulizojiwekea. Pili, Mawaziri wenzangu na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri wanayofanya na kwa ushirikiano mzuri wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu kama Waziri wa Uchukuzi. Tatu na mwisho, familia yangu na wapiga kura wa Jimbo la Uchaguzi la Kyela ambao wameendelea kunionyesha upendo na ushirikiano mkubwa hata pale ninapokuwa nimebanwa na majukumu ya Kitaifa nje ya Jimbo langu la uchaguzi. 6. Mheshimiwa Spika, hotuba hii imezingatia kikamilifu maudhui yaliyomo kwenye Hotuba ya Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu na Mbunge wa Katavi iliyowasilishwa katika Bunge lako Tukufu tarehe 10 Aprili, 2013. Naomba kumshukuru na kumpongeza kwa hotuba nzuri iliyotoa ufafanuzi wa kina kuhusu utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa mwaka 2012/2013 na mwelekeo wa shughuli za Serikali na dira ya Bajeti ya Serikali katika mwaka 2013/2014. 7. Mheshimiwa Spika, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Prof. Juma Athuman Kapuya, Mbunge wa Urambo Magharibi nayo imefanya kazi nzuri na kubwa ya uchambuzi wa kina wa 3 Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Sekta katika mwaka 2012/2013 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2013/2014. Pamoja na kuipongeza Kamati kwa kazi nzuri, Wizara itazingatia maoni na ushauri wa Kamati katika kuboresha utendaji wa Sekta za Uchukuzi na Hali ya Hewa. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA WIZARA KWA MWAKA 2012/2013 NA MALENGO YA MWAKA 2013/2014 8. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya awali, niruhusu sasa nifanye mapitio ya utekelezaji wa mipango ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2012/2013 na kutoa maelezo kuhusu Malengo na Makadirio ya bajeti ya Wizara kwa mwaka 2013/2014. Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2012/2013 ulizingatia: Dira ya Taifa ya mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, Malengo ya MKUKUTA II, Ahadi na Maagizo ya Serikali pamoja na Sera za Kisekta, Kitaifa na Kimataifa. HUDUMA ZA UCHUKUZI KWA NJIA YA NCHI KAVU Usafiri na Uchukuzi kwa Njia ya Reli 9. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuboresha na kukuza kiwango cha utoaji wa huduma ya 4 usafiri wa reli nchini. Pamoja na jitihada hizo, utoaji wa huduma katika sekta hii kwa kipindi kirefu umekuwa hauridhishi kutokana na kuchakaa kwa miundombinu ya reli, uchakavu na uchache wa vifaa vya uendeshaji kama vile vichwa vya treni, mabehewa, mashine na mitambo ya kufanyia kazi. Hali hiyo imelazimu, katika sehemu mbalimbali za njia ya reli, treni kupunguza mwendo hadi wastani wa Kilometa 15 tu kwa saa ili kuzuia ajali, na hivyo kulinda usalama wa abiria na mizigo. 10. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara kupitia taasisi zake zinazohusika na uchukuzi kwa njia ya reli, imechukua hatua kadhaa ili kudhibiti hali hiyo. Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO) iliendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uimarishaji wa miundombinu ya reli: kuondoa reli nyepesi na chakavu na kutandika reli mpya na nzito zaidi; kuimarisha madaraja yaliyopo na kujenga mengine mapya; kuimarisha tuta la reli na kuendelea na ujenzi wa vituo vya upakiaji na upakuaji wa makontena. 11. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kulifanyia kazi eneo kati ya stesheni za Kitaraka na Malongwe lenye urefu wa Kilometa 89 ambalo lina reli kuukuu na nyepesi za ratili 56.2 kwa yadi (sawa na kilo 28 kwa mita), hivyo kuwa chanzo cha ajali za treni za mara kwa mara. 5 Kazi ya kutandika reli mpya na nzito za ratili 80 kwa yadi (kilo 40 kwa mita) ambayo tuliiombea fedha hapa Bungeni na tukapewa, ilianza Septemba, 2012 kwa kutumia mikono (manual relaying) badala ya kusubiri mashine maalum kwa kazi hiyo. Utaratibu huo umetuwezesha kung'oa reli zisizohitajika na kutandika nyingine kwa umbali wa Kilometa 13 na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa vijana 250 wa Ki-Tanzania. 12. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mkandarasi, Kampuni ya ujenzi kutoka China iitwayo China Civil Engineering Construction Company (CCECC), ameshafikisha kwenye eneo la mradi mashine maalum ya kutandikia reli yenye uwezo wa kutandika Kilometa 1 ya reli kwa siku, kreni 2 za kupakia paneli zilizokwisha unganishwa kwenye mabehewa na viberenge vikubwa viwili kila kimoja kina uwezo wa kuvuta mabehewa 4 yenye reli na mataruma, na mitambo midogo ya kushindilia kokoto baada ya kutandika reli. Tunatarajia mradi kukamilika mwezi Oktoba 2013 kwa gharama ya Shilingi bilioni 29.2. 13. Mheshimiwa Spika, katika maombi yetu ya fedha kwa mwaka 2012/2013, tulilieleza Bunge lako Tukufu kuhusu uharibifu mkubwa wa miundombinu uliotokea kwenye maeneo 32 ya Reli ya Kati, kati ya stesheni za Kilosa na Gulwe kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2009 na 2010 na maeneo 13 kati ya 6 Gulwe na Godegode kutokana na mvua za mwaka 2011. Pia tulieleza jitihada zilizofanyika za ukarabati wa reli, madaraja na ujenzi wa kingo za tuta la reli kwenye maeneo hayo. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, mbali na ujenzi wa madaraja unaoendelea, kazi zingine zote za ukarabati wa mindombinu ya reli na udhibiti wa mto Mkondoa, zimekamilishwa vizuri. Tatizo lililobaki katika eneo hilo na ambalo tunalifanyia kazi ni la mchanga kujaa kwenye makalavati kila mvua inaponyesha. Mathalan, makalavati yaliyopo stesheni ya Gulwe, pamoja na kwamba yalisafishwa kikamilifu, kwa sasa yamejaa mchanga kwa karibu asilimia 50. 14. Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishadokeza awali, kazi kubwa inayoendelea eneo hilo hivi sasa ni ujenzi wa madaraja mawili makubwa kati ya Kilosa na Gulwe na daraja moja kati ya stesheni za Bahi na Kintinku. Kazi ya awali, ambayo inaendelea ni ujenzi wa nguzo za madaraja hayo na udhibiti wa uimara wake. Juu ya nguzo hizo, patafungwa madaraja ya vyuma (bridge steel girders) ambayo kwa sasa yanamaliziwa kutengenezwa nchini China. Mkandarasi, CCECC, anatarajia kuwa ifikapo mwishoni mwa Juni, 2013 tayari madaraja hayo ya vyuma yatakuwa yameshawasili nchini tayari kwa kazi ya 7 kuyafunga. Gharama za ujenzi wa madaraja hayo matatu ni Shilingi bilioni 14.45. 15. Mheshimiwa Spika, mwaka jana nilipokuwa nawasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2012/2013, nilielezea kuwa pamoja na mabadiliko makubwa ya tabia nchi ambayo husababisha mvua kubwa kunyesha bila matarajio, shughuli za binadamu hususan ufugaji na kilimo kinachoambatana na ukataji miti milimani na uedeshaji wa kilimo na ufugaji karibu kabisa na tuta la reli, ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha mvua zinazonyesha maeneo hayo kuwa na athari kubwa kwenye miundombinu ya Reli ya Kati hasa kati ya stesheni za Kilosa na Gulwe. Natumia fursa hii kuwaomba wananchi walio karibu na njia za reli nchini kutunza mazingira na kuepukana na shughuli zozote ndani ya eneo la hifadhi ya reli ambalo kwa mujibu wa sheria ni mita 15 pande zote za reli kwa sehemu za miji na mita 30 kila upande nje ya miji. 16. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali lakini kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na sheria ili kulinda miundombinu ya reli. Mathalan, tarehe 14 Septemba, 2012, Wizara kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Morogoro na Dodoma, Wah.Wabunge, Madiwani na Makatibu 8 Tarafa wa maeneo kutoka Kilosa hadi Gulwe walishiriki mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Gulwe kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wao juu ya athari zitokanazo na shughuli za kilimo na ufugaji zisizozingatia masharti ya sheria na kuzembea utunzaji wa mazingira. 17. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kuwakumbusha wananchi kuwa, kutokana na shughuli za binadamu zisizofuata sheria wala utaratibu, mvua zikinyesha husomba magogo, udongo na mchanga mwingi kutoka milimani. Mzigo wote huo huishia kwenye tuta la reli na kusababisha makalvati na madaraja kuziba hivyo kulazimisha maji kupita juu ya tuta la reli na hatimaye kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya reli.