Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA TANO Kikao cha Tisa – Tarehe 18 Novemba, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI: Hati zifuatazo ziliwasilishwa mezani na:- MHE. ENG. RAMO M. MAKANI - MWENYEKITI WA KAMATI TEULE YA BUNGE: Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge. MHE. JANUARY Y. MAKAMBA - MWENYEKITI WA KAMATI YA NISHATI NA MADINI: Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini juu ya Uendeshaji wa Sekta Ndogo ya Gesi Nchini. MASWALI NA MAJIBU Na. 109 Mikopo ya Wajasiriamali iliyotolewa na Mheshimiwa Rais MHE. MCH. LUCKSON N. MWANJALE (K.n.y. MHE. JAMES D. LEMBELI) aliuliza:- (a) Je, ni wananchi wangapi wa Wilaya ya Kahama walionufaika na fedha za mikopo ya wajasiriamali, maarufu kama mamilioni ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete? (b) Je, ni wananchi wa makundi gani kutoka maeneo gani ya Wilaya walinufaika na mamilioni hayo? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE alijibu:- Mshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa James Daudi Lembeli, Mbunge wa Kahama lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a)Mheshimiwa Spika, wananchi wa Wilaya ya Kahama walionufaika na fedha za mikopo ya wajasiriamali maarufu kama Mabilioni ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, hadi kufikia Disemba, 2010 ni 1,357. Wananchi hawa kwa ujumla waliokopeshwa shilingi 753,840,000 kupitia Benki ya NMB. (b)Mheshimiwa Spika, wananchi walionufaika na mikopo kwa kuzingatia wingi ni vijana na wanawake kutoka maeneo ya mijini na vijijini. 1 MHE. MCH. LUCKSON N. MWANJALE:Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa jibu zuri ambalo Waziri amejibu, lakini naomba niulize swali la nyongeza; Kwa kuwa, mikopo hii iliwanufaisha zaidi wananchi wanaokaa mijini na vijijini kwa sehemu kubwa walikosa, Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba hawa wananchi wanaokaa vijijini hasa wajasiriamali nao wanapata? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Spika, fedha hizi zilianza kutumika mwaka 2007 na kuishia Oktoba, 2009 awamu ya kwanza na kwa ujumla Benki ya NMB ilitoa shilingi bilioni 16.3 na CRDB ilitoa shilingi bilioni 29.94. Kwa hiyo, jumla ya fedha zote zilizotumika katika awamu ya kwanza ni bilioni 37.17. Awamu ya pili ilianza ilianza mwaka 2007 na kuna fedha zilizotenga bilioni 11.3 na awamu hii inakamilika mwezi Machi. Baada ya hapo kutafanywa tathmini kwa maagizo ya Rais ili tuone watu gani wamenufaika zaidi katika mpango huu ili awamu inayofuata sasa tuelekeze kwa watu hawa ambao watakuwa hawajanufaika zaidi wakiwemo hawa wa vijijini. MHE. HAMAD RASHID MOHAMED:Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza; Mheshimiwa Spika, suala la kunufaika ni moja na suala la impact ya kila pesa zinapotolewa, Je katika kipindi chote hiki kabla ya kutolewa kwa awamu ya pili, ile awamu ya kwanza impact yake ya 37 bilioni ilikuwa ni nini na hatimaye Serikali ikaridhika kuendelea na kutoa mikopo hiyo? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Spika, kwa takwimu inaonesha kwamba mikopo hii imeleta impact kubwa sana. kwanza kutokana na riba yake kuwa tofauti na riba ya kawaida ya mabenki, lakini pili urasimu wake kuwa mfupi na tatu fedha hizi zimeweza kuwafikia wananchi wengi sana kwa muda mfupi sana. Kwa hiyo impact yake ni kubwa lakini hasa impact imejionesha kwa akina mama kwa sababu asilimia zaidi ya hamsini wamekopeshwa akina mama na ulipaji wao ambao umeonesha faida kutokana na miradi yao inazidi asilimia themanini. Na. 110 Wananchi Kuchimbiwa Visima Virefu vya Maji MHE. SELEMANI J. ZED aliuliza:- Katika Kata za Semembela, Karitu, Igusule na Sigili katika Jimbo la Bukene kuna matatizo makubwa ya upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzipatia Kata hizo visima virefu vya maji ili wananchi wapate huduma kwa mwaka mzima? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:- Mhehsimiwa Spika, Wilaya ya Nzega ina jumla ya visima virefu 197, visima 315 na miradi ya maji ya bomba minne (4) inayofanya kazi ambapo jumla ya wakazi 195,934 wanaopata huduma ya maji safi na salama sawa na asilimia 37 ya wakazi wote. Kati ya visima virefu 197 na vifupi 315, visima virefu 71 na visima vifupi 211 vipo katika Jimbo la Bukene. 2 Mheshimiwa Spika, katika programu ya maendeleo ya sekta ya maji, miradi mbalimbali imetekelezwa katika Jimbo la Bukene ikiwemo miradi ya quick wins, programu ya maji na usafi wa mazingira vijijini na mradi wa maji vijijini unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali za Tanzania na Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA kama ifuatavyo:- (i) Miradi ya Quick wins (a) Uchimbaji wa visima 20 na kufungwa pampu za mkono kwenye kata za Karitu, Isaganhe, Mogwa na Kahama ya Nhalanga. Gharama iliyotumika ni shilingi 90,654,000 mwaka 2008/2009. (Makofi) (b)Uchimbaji wa visima virefu viwili katika Kata ya Bukene ambao umegharimu kiasi cha shilingi 34,930,000 mwaka 2008/2009 ambapo kisima 1 kinatumika kama chanzo cha maji ya bomba. (c)Ukarabati wa miradi miwili ya maji ya bomba katika Kata za Bukene na Igusule. Mradi wa Kata ya Bukene uligharimu shilingi 24,300,000 mwaka 2008/2009 na ule wa Igusule uligharimu shilingi 80,753,000 mwaka 2009/2010. Upatikanaji wa maji katika mradi wa Bukene ni kidogo kutokana na eneo la chanzo cha maji kutumika kwa shughuli za kilimo zinazofanywa na mwananchi mmoja ambaye ni mmiliki wa eneo hilo. (ii)Program ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini. Kupitia programu ya maji na usafi wa mazingira Vijijini visima virefu 10 vimechimbwa katika Kata za Itobo, Sigili, Ikindwa na Mwamala ambapo kati ya visima 10 vilivyochimbwa visima 6 vimepata maji na visima 4 havikupata maji. Katika visima 6 vilivyopata maji visima 5 vinategemewa kutumika kama vyanzo vya miradi ya maji ya bomba. Hii inatokana na kisima kimoja katika Kata ya Sigili kutokuwa na maji ya kutosha hivyo kilipendekezwa kufungwa pampu ya mkono. Gharama iliyotumika katika mradi huu ni shilingi 269,270,000 kwa mwaka 2010. Katika mwaka 2011 /2012 Halmashauri ya Wilaya Nzega imeidhinisha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa maji. (iii) Miradi ya maji unaohisaniwa na JICA. Ipo miradi ya maji inayohisaniwa kati ya Serikali za Tanzania na Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA. Mradi huu umesaidia kukarabati visima 11 katika Jimbo la Bukene kati ya visima 23 vilivyokarabatiwa katika Wilaya ya Nzega. Mradi uliokarabati una jumla ya visima 45 Mkoa wa Tabora kwa gharama ya dola za kimarekani 35,000 mwaka 2010. Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuvipatia vijiji vyote huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao. Aidha, kutokana na ufinyu wa bajeti Serikali itatekeleza miradi hii kwa awamu. MHE. SELEMAN J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Waziri nina swali la nyongeza:- Tofauti na visima vifupi, visima virefu vinapaswa kutoa maji mwaka mzima, lakini visima vingi kati ya visima hivi vinavyotajwa kuwa ni virefu sehemu kubwa ya mwaka havina maji, kwa mfano kisima cha Bukene ambacho kimetajwa kwamba ni kisima kirefu, wiki tatu zilizopita nilikuwa Bukene, maji yapo chini na pampu iko juu haiwezi kuyavuta. Je, Serikali iko tayari kuteua Tume ya Watalaam waende katika Jimbo la Bukene na Wilaya ya Nzega kwa ujumla wavikague hivi visima vinavyoitwa virefu na kujua sababu ni kwanini visima vinachimbwa kama virefu lakini sehemu kubwa ya mwaka havina maji na wananchi wanapata matumaini kwamba wana visima virefu. Lakini bado wanapata kero ile ile kwa sehemu kubwa ya mwaka kutokuwa na maji. 3 NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nikubaliane naye kwamba kwa Mkoa wa Tabora kwa sehemu kubwa maji chini ya ardhi ni tatizo na visima vingi tumejaribu kuchimba na maji yanapatikana kwa asilimia labda hamsini. Sasa ndiyo tunatafuta njia kwamba tunafanyaje mahali ambapo tumechimba visima na maji hakuna. Mheshimiwa Spika, tunatafuta vyanzo vingine kama mabwawa au kuyachukua maji kama ambavyo sasa hivi tunataka kuchukua maji ya Ziwa Victoria kwa mradi wa kutoka Kahama, Nzega, Tabora na Igunga, hili litasaidia vijiji vingi vilivyopo kandokando ya lile bomba kupata maji. Hiyo ni njia moja ambayo nafikiri ni ya uhakika zaidi. Lakini kwa hili la visima, kwa kweli kwa sehemu kubwa kwa Mkoa wa Tabora ni tatizo, watalaam wameshakwenda na taarifa tulizo nazo ndiyo hizo. (Makofi) Na. 111 Mnada wa Wafanya Biashara Ndogondogo Msalato MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza:- (a) Je, mnada wa wafanyabiashara ndogo ndogo wa Msalato, ambao hufanyika kila siku ya Jumamosi ni wa kudumu au ni wa muda? (b) Kama ni wa kudumu. Je, ni kwa nini mazingira ya biashara hususani vibanda yasiboreshwe na kufanywa ya kudumu? (c) Je, ni kiasi gani cha ushuru hukusanywa kila siku ya mnada na fedha hizo zinatumikaje? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:- (a)Mheshimiwa Spika, soko la wafanyabiashara ndogo ndogo Msalato ni Gulio ambalo kwa tafsiri sahihi ni mahali ambapo watu wanakutana kwa shughuli za kibiashara kwa juma au mwezi mara moja. Gulio hili lilianzishwa mwaka 2005 kwa lengo la kusogeza karibu huduma za soko kwa wananchi wa Kata ya Msalato na Kata jirani kupata bidhaa katika gulio hilo. Gulio la Msalato kwa sasa ni la kudumu na linafanyika kila siku ya Jumamosi. (b)Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imekuwa ikiboresha soko hili ili kuwawezesha wananchi wanaokwenda katika soko hili kupata huduma zote muhimu kama kuwepo kwa maji na vyoo.