Tarehe 19 Mei, 2021
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Thelathini na Moja – Tarehe 19 Mei, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Mussa A. Zungu) Alisoma Dua MWENYEKITI: Tukae. Katibu. NDG. NEEMA MSANGI – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilisha Mezani na:- WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/2022. MWENYEKITI: Ahsante. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha 2021/2022. MWENYEKITI: Ahsante. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha 2020/2021 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022. MWENYEKITI: Ahsante. Katibu. NDG. NEEMA MSANGI – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Tunaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba. Na. 263 Kuvutia Wawekezaji kwenye Viwanda vya Kubangua Korosho MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka vivutio maalum ili kuvutia Wawekezaji kwenye viwanda vya kubangua korosho? MWENYEKITI: Waziri. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:- 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kuwa korosho ni miongoni mwa mazao matano ya kimkakati yanayolimwa hapa nchini, kuanzia mwaka 2018 Serikali inatekeleza mpango wa uhamasishaji wa kilimo cha korosho katika mikoa yote inayostawisha kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, huduma za ugani na pembejeo ili kuimarisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda nchini. Hadi sasa, takribani mikoa 20 inazalisha zao hilo kwa viwango tofauti. Msimu wa mwaka 2020/2021 uzalishaji ulikuwa tani 200,010 na kuipatia nchi kiasi cha shilingi bilioni 477. Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha uwekezaji wa viwanda vya kubangua korosho, Serikali imeweka vivutio mbalimbali vikiwemo vivutio visivyo vya kikodi kama vile kuweka mfumo wa soko la awali kwa wabanguaji wa ndani kuanzia mwaka 2020 kwa lengo la kuwawezesha kununua korosho bila kushindana na wanunuzi wanaosafirisha korosho ghafi kwenda masoko ya nje ya nchi na kuwahakikishia malighafi kwa bei nafuu. Katika mnada huo jumla ya tani 2,021.7 kimenunuliwa na viwanda tisa vilivyoshiriki soko hilo la awali. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka pia vivutio vya kikodi kwa viwanda vya kubangua korosho kupitia Sheria ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje Sura 373 ikiwemo: Msamaha wa Kodi ya Makampuni (Corporate Tax) kwa miaka 10; msamaha wa asilimia 100 wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa za mtaji (capital goods); msamaha wa asilimia 100 wa Kodi ya Zuio (Withholding Tax); na riba ya mikopo kutoka nje; pango na gawio; na msamaha wa asilimia 100 wa Kodi ya Ushuru wa Forodha kwa mitambo na vifaa. Kupitia utaratibu huo, jumla ya viwanda vitano vimesajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA). Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kubuni na kuweka vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuvutia zaidi uwekezaji ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwenye Halmashauri zinazolima korosho hapa nchini, ambapo maeneo hayo yatakuwa na huduma muhimu kama vile umeme, maji na barabara; na 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) kupitia kodi mbalimbali zinazotozwa katika mitambo, vipuri na vifungashio. MWENYEKITI: Mheshimiwa Chikota. MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa utaratibu huu wa mfumo wa soko la awali huwa unawakutanisha wenye viwanda na wakulima lakini hauna ushindani kwa sababu bei ni ndogo na wakulima hawavutiwi kupeleka korosho zao kama ilivyo kwenye minada mingine ya kawaida, kwa sababu wakulima wanaona kama ni kangomba ya aina fulani tu: Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka top up kwa bei ile inayotolewa na wawekezaji ili kuhakikisha kwamba wawekezaji hawa wanapata korosho katika soko? Swali la pili, kwa kuwa viwanda hivi vimeajiri vijana wengi na akina mama wengi; na kwa sasa hivi viwanda takriban vyote vinafanya kazi chini ya uwezo wake kwa sababu ya changamoto mbalimbai ikiwemo ukosekanaji wa malighafi kwa sababu hawapati korosho mnadani: Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kwa wawekezaji ambao wameshafungua viwanda nchini na wale ambao wanatarajia kufungua viwanda vipya? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, kwa ufupi. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa korosho kwa sababu wakulima hawana imani na mfumo wa soko la awali, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Chikota kwamba kwa sababu ndiyo mfumo umeanza, Serikali itaendelea kuchukua jitihada kuboresha ili kuweza kuvutia wakulima waone kwamba ile siyo kangomba, bali ni soko ambalo lipo lenye lengo la kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinapata korosho kwanza kabla havijauza nje. 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto hiyo aliyozungumzia kwamba ajira zile hazizalishwi kwa sababu viwanda havipati korosho, naomba nimhakikishie kwamba katika utaratibu huo huo wa kushughulikia changamoto ambazo zipo katika soko la awali, Serikali itaendelea kufikiria namna bora ya kuhakikisha kwamba korosho inapatikana ili viwanda hivi na vingine ambavyo tunategemea kuvutia viwezwe kuanzishwa, viweze kutoa ajira kwa ajili ya vijana wetu. MWENYEKITI: Ahsante. Tunaendelea na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Grace Tendega. Na. 264 Ukosefu wa Huduma za Bure kwa Wazee, Watoto na Wajawazito MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Kumekuwa na changamoto ya huduma za Afya katika Zahanati zetu hasa ukosefu wa dawa pamoja na huduma bure kwa wazee, watoto na akinamama wajawazito. Je, ni lini Serikali itahakikisha Sera ya Afya inatekelezwa bila tatizo lolote? MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) huduma za afya nchini kwa kuongeza bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka wa fedha 2015/2016 hadi shilingi bilioni 270 katika mwaka wa fedha 2020/2021. Ongezeko hilo la fedha limewezesha kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu (tracer medicine) kutoka wastani wa asilimia 31 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 90 kufikia Aprili 30, 2021. Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Mei, 2021 Serikali imetoa huduma ya matibabu bila malipo yenye gharama ya shilingi bilioni 30.1 kwa wananchi wa makundi maalum milioni 12 ikijumlisha wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya dawa za makundi maalum kama wazee, wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwezi Novemba, 2020 Serikali ilitoa shilingi bilioni 41.2, mwezi Februari, 2021 Serikali ilipeleka shilingi bilioni 18.2 katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa na mwezi Mei, 2021 Serikali imepeleka shilingi bilioni 80 na kufanya jumla ya fedha zote zilizopelekwa kwa ajili ya dawa kufikia shilingi bilioni 140. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya ili kuboresha huduma kwa makundi maalum na wananchi kwa ujumla. MWENYEKITI: Mheshimiwa Tendega. MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tumekuwa tunaongeza bajeti ya dawa katika Serikali yetu na tumekuwa tukiona bado zahanati na vituo vya afya havipati dawa. Swali langu: Je, mmefanya utafiti gani wa kuhakikisha kwamba hizo 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) fedha, shilingi bilioni 270 na hiyo shilingi bilioni 140 ndizo zitakwenda kutatua changamoto ya dawa katika zahanati zetu na vituo vya afya? Swali langu la pili; hivi tunavyozungumza wananchi wenye changamoto hizi wa kutoka Jimbo la Kalenga na wengine wengi wanaangalia; je, wananchi wategemee nini kuwa hizi dawa katika zahanati na vituo vya afya itakuwa ni historia? MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Grace Victor Tendega ametangulia kusema, Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba kwa takriban mara tisa ndani ya miaka mitano na hii ni kwa sababu Serikali inajali sana wananchi na inahitaji kuona wananchi wanapata dawa za kutosha ili kuhakikisha kwamba huduma za afya ni bora zaidi. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ni kweli kwamba