Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO-(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA SITA Kikao cha Kumi – Tarehe 10 Februari, 2017 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Najma Murtaza Giga) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tukae. (Makofi) Katibu! NDG. CHARLES MLOKA – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Taarifa ya Serikali kuhusu Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 na 2014/2015. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Taarifa ya Serikali kuhusu majibu ya Serikali juu ya Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa Mwaka wa Fedha ulioisha tarehe 30 Juni, 2015. NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Chuo Kikuu Mzumbe kwa Mwaka wa Fedha ulioisha tarehe 30 Juni, 2015 (The Annual Report and Audited Accounts of Mzumbe University for the Financial Year ended 30th June, 2015). Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Chuo Kikuu cha Ardhi kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015 (The Annual Report and Audited Accounts of Ardhi University for the Financial Year 2014/2015). NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Taarifa ya Mwaka na Hesabu zalizokaguliwa za Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 (The Annual Report and Audited Accounts of Road Fund Board for the Financial Year 2012/2013) MHE. WILLIAM M. NGELEJA - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kwa Kipindi cha kuanzia Januari, 2016 hadi Januari, 2017. 0 NAKALA YA MTANDAO-(ONLINE DOCUMENT) MHE. CAPT. (MST.) GEORGE H. MKUCHIKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2016 hadi Januari, 2017. MHE. KANALI (MST.) MASOUD ALI KHAMIS – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2016 hadi Januari, 2017. MWENYEKITI: Ahsante. Katibu! NDG. CHARLES MLOKA – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU Na. 105 Ujenzi wa Barabara ya Kibiti – Nyamisati MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kwa changarawe barabara ya Kibiti – Nyamisati. (a) Je, ni sababu zipi zilizochelewesha kukamilika kwa ahadi hiyo? (b) Je, ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za kuchelewa kwa matengenezo ya barabara ya Kibiti – Nyamisati kwa kiwango cha changarawe ni upatikanaji wa fedha. Tathmini iliyofanyika imebainisha kwamba barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 40.8 inahitaji shilingi bilioni 1.2 ili kufanyiwa matengenezo kwa kiwango cha changarawe. Hata hivyo, ili kuifanya barabara hiyo angalau iweze kupitika Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 iliitengea barabara hiyo shilingi milioni 45.79 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya kilometa 38.31 na katika mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 24 zilitumika kwa marekebisho ya sehemu korofi yenye urefu wa kilometa mbili na matengenezo ya kawaida ya kilometa 15. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matengenezo ya barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Serikali itajitahidi kutenga fedha za matengenezo kwa awamu ndani ya kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipande cha kilometa 32.8 kilichobaki baada ya hapo awali kufanyika matengenezo ya kilometa nane kwa kiwango cha changarawe kutoka Kibiti mpaka Ruaruke yaliyofanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani. MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nianze kusema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Waziri huyu ni mchapakazi, kweli tarehe 5 Januari, ni Waziri wa kwanza aliyefika maeneo ya Delta na nilifanya naye kazi na nikaonesha kweli kauli ya hapa kazi inatekelezeka. (Makofi) 1 NAKALA YA MTANDAO-(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize maswali yangu mawili; moja, je, kutokana na barabara hii kwamba kwa sasa ina maeneo mawili ya daraja hayapitiki, je, Serikali haioni kwamba ina kila sababu ya kukarabati madaraja hayo? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Barabara ya kutoka Muhoro kwenda Mbwela ina matatizo makubwa hasa kwenye Daraja la Mbuchi, je, Serikali itatusaidiaje katika hilo la Mbuchi? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kupokea shukrani zake ndugu yangu Mheshimiwa Ungando, naomba nikiri, kweli nilikuwepo kule na tulitembelea visiwa 40 vya Deltakatika Jimbo lile la Kibiti. Barabara ya kutoka hapa Bunju mpaka Nyamisati kule ndani kwa kweli ina changamoto kubwa sana naomba tulipokee jambo hili kwa sababu katika programu yetu ya uondoaji wa vikwazo tutajitahidi ofisi yetu tufanye kila liwezekanalo kwa sababu tukiwasaidia wananchi wa eneo lile tutakuwa hata tumewasaidia wananchi wa Mafia kwa sababu wanaposafiri kutoka Nyamisati kwenda Mafia lazima watumie barabara ile. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika suala zima la Daraja la Mbuchi, na kwa sababu tulipita kule na vilevile tunajua kuwa tuna harakati ofisi yetu kutengeneza Daraja la Mbwela, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kuhakikisha mambo haya yote ofisi yetu inayashughulikia na Mheshimiwa Ungando amini Serikali yako tutakupa ushirikiano kwa sababu jimbo lako ni miongoni mwa majimbo yenye changamoto kubwa. MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Barabara ya Tanga - Pangani - Bagamoyo ni barabara ambayo imekuwa ikitolewa ahadi kila chaguzi kuu zinapofika na Uchaguzi Mkuu uliopita pia ahadi hiyo ilitolewa ya kwamba itaanza kutengenezwa na tayari tunaambiwa upembuzi yakinifu umekwishafanyika, sasa je, ni lini utengenezaji wa barabara hiyo utaanza ikiwa tayari upembuzi yakinifu umekwishafanyika? Ahsante. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii nimepita mara kadhaa na juzijuzi nilivyokuwa natembelea Mkoa wa Tanga, ni miongoni mwa barabara niliyoipita kutoka Bagamoyo mpaka pale Pangani na kikubwa zaidi katika kufika pale nilikuta reference ya Waziri wa Miundombinu aliyekuwa akipita pale na kutoa ahadi hiyo ya ujenzi wa barabara hiyo lakini ikiwa sambamba na ujenzi wa daraja lile la pale Pangani. Mheshimiwa Mawenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu ni commitment ya Serikali na kipindi cha sasa kwa sababu ujenzi wa barabara ya lami lazima kwanza upembuzi yakinifu ufanyike na jambo hilo limekamilika, ninaamini suala la barabara hii kwa sababu ni barabara ya kimkakati, kwamba hata kwenda Mombasa ni barabara ya shortcut naamini Serikali hii itafanya kila liwezekanalo ujenzi wa barabara hii uweze kukamilika. MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la dogo nyongeza. Barabara ya kutoka Mkuranga Mjini mpaka Kisiju Pwani ni miongoni mwa barabara ambayo zimekuwa zikiahidiwa pia kuwekwa lami na Awamu ya Nne na hata Awamu hii ya Tano. Barabara hii inapita katika Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Mkuranga lakini pia inapita katika Hospitali yetu Kuu ya Wilaya ya Mkuranga. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itatusaidia kuhakikisha barabara hii inawekwa lami kutoka Mkuranga Mjini kupita Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Hospitali ya Wilaya mpaka Kisiju Pwani? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niweke kumbukumbu sawa, kwanza Mheshimiwa Ulega juzi kwa uchapakazi wake mzuri juzi alikuja ofisini kwetu kwa ajili ya kuhakikisha suala zima la miundombinu ya barabara katika jimbo lake na hii ni miongoni mwa barabara ambayo tulikuwa tukiijadili na Katibu Mkuu wangu pale jinsi gani tutafanya, kwa sababu yale ni Makao Makuu ya Halmashauri na kila Makao Makuu ya Halmashauri lazima angalau barabara ya lami iweze kufikika. (Makofi) 2 NAKALA YA MTANDAO-(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tutaangalia jinsi gani tutafanya lakini nikijua wazi barabara ile ambayo inaenda mpaka Kisiju Pwani ni jambo la mkakati mkubwa sana na kuna barabara nyingine kutoka Kimanzichana inapita katikati kule mpaka inakuja maeneo ya Msanga katika Jimbo la Kisarawe, hizi zote ni barabara za kimkakati kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Mkoa wa Pwani unafunguka, lengo kubwa ni kwamba katika uchumi unaofunguka wa viwanda sasa wananchi waweze kushiriki vizuri katika mchakato wa viwanda. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ulega naomba nikuahidi tutakupa ushirikiano wa kutosha kujenga miundombinu yetu ya barabara za lami katika maeneo yetu. Na. 106 Ahadi ya Kuboresha Maisha ya Wavuvi na Wakulima Nchini MHE. QAMBALO W. QULWI (K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO) aliuliza:- Wilaya ya Karatu inapakana na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro ambapo watalii wengi hutembelea hifadhi na kufanya Wilaya hii kupata fursa ya kujengwa hoteli za kitalii, pamoja na hoteli hizo kujengwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya, Halmashauri hiyo hainufaiki na uwekezaji huo. (a) Je, Halmashauri hiyo hairuhusiwi kutoza hotel levy? (b) Je, nini mkakati wa Serikali