Online Document)
Hii ni nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________ MAJADILIANO YA BUNGE ________ MKUTANO WA KUMI NA TATU Kikao cha Sita - Tarehe 11 Novemba, 2003 (Mkutano Ulianza Saa Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Juma J. Akukweti) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kabla sijamwita muuliza swali wa kwanza, leo kama mlivyoona kwenye Order Paper, badala ya maswali 15 yapo 16 kwa hiyo, mtaona hali itakavyokuwa katika taratibu zetu. Na. 73 Daftari la Wapiga Kura MHE. DR. THADEUS M. LUOGA aliuliza:- Kwa kuwa ikiwa kila Kata au Kijiji kitakuwa na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura itapunguza gharama ya uchaguzi kwa kiwango fulani:- Je, kazi hii itafanyika lini? WAZIRI WA NCHI, OFISI WA WAZIRI MKUU (MHE. MUHAMMED SEIF KHATIB) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dr. Thadeus Luoga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya jitihada kubwa katika maandalizi ya jambo hili. Aidha, tarehe 4 Februari, 2003 wakati najibu swali Na. 2442 la Mheshimiwa Wilfred Muganyizi Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini katika Mkutano wa Kumi wa Bunge hili nilisema kuwa Tume ya Uchaguzi imekwishafanya maandalizi makubwa katika kuanzisha daftari hilo. Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, nilisema kuwa Tume itakamilisha maandalizi kwa kufanya semina ya mwisho mwezi Februari, 2003. Vyama vya Siasa, Mashirika ya Kiserikali na vyombo vya Habari walishirikishwa ili kupata maoni na michango yao katika kukamilisha maandalizi ya uanzishaji wa daftari hili. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwa semina iliyopangwa kufanyika mwezi Februari, 2003 ilifanyika tarehe 24 Machi, 2003 ambapo maoni na michapo ya wadau walioshiriki yamesaidia sana kukamilisha maandalizi.
[Show full text]