Majadiliano Ya Bunge ______
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ________________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Ishirini – Tarehe 6 Julai, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO): Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), kwa mwaka wa Fedha 2011/2012. MHE. ANGELLA JASMI M. KAIRUKI - (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba Sheria na Utawala kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka 2010/2011 pamoja na maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka 2011/2012. MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA - (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA ARDHI, MALIASI NA MAZINGIRA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka 2010/2011 Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka 2011/2012. MHE. PAULINE P. GEKUL - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO): 1 Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani juu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Kuhusu Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) kwa Mwaka wa Fedha, 2011/2012. MHE. PAULINE P. GEKUL - MSEMAJI WA MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MAZINGIRA): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani juu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Kuhusu Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa Mwaka wa Fedha, 2011/2012. MASWALI NA MAJIBU Na. 185 Uhitaji wa Maji Safi na Salama Geita MHE. JOSEPHINE T. CHAGULLA aliuliza:- Ni sera ya Serikali kuwapatia wananchi wote maji safi na salama kuanzia ngazi ya kila mkoa, wilaya, hadi vijijini, lakini mkoa wa Geita pamoja na wilaya zake Nyang’hwale, Bukombe, Chato na Mbogwe, kuna shida kubwa sana ya maji safi na salama. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa Geita na Wilaya zake Maji Safi na salama? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Thabita Chagulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa maji na usafi wa mazingira vijijini, wilaya za Geita na Nyang’hwale, tayari zimepata mkandarasi aitwae Victoria Drilling Co. Ltd ambaye amesaini mkataba tarehe 20 Juni, 2011 kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa visima vya maji. Uchimbaji unatarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kusaini mkataba wa uchimbaji wa visima 9 katika wilaya ya Nyang’hwale na visima 8 katika wilaya ya Geita. Aidha, ujenzi wa miundombinu ya maji katika vijiji hivyo utafanywa mara baada tu ya shughuli za uchimbaji kukamilika. 2 Mheshimiwa Spika, katika mji wa Geita upo mpango kabambe wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya kuchimba dhahabu ya Geita Gold Mine (GGM) na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikishirikiana na Wizara ya Maji katika mwaka 2011/2012. Mheshimiwa Spika, kazi zinazotarajiwa kutekelezwa kupitia kampuni hiyo ni:- (i) Kujenga pump house; (ii) Kujenga treatment plant; (iii) Kufunga pump za kusukuma maji na; na (iv) Kujenga tanki kubwa la kuhifadhi maji pamoja na kulaza bomba itakalopelekea maji hadi kwenye tanki kubwa. Aidha kazi ya utafiti wa athari za kimazingira (Environment Impact Assessment) imeshafanyika na utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mara baada ya kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano kati ya kampuni ya Geita Gold Mine na Serikali. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa kazi zilizotajwa hapo juu unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2011. Aidha, mradi huu utagharimu jumla ya shilingi bilioni 15.3 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 6 kimetengwa na kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) na kiasi kingine cha shilingi bilioni 9.3 kimeombwa kutoka Serikali Kuu kama maombi maalum (special request) katika mchanganuo ufuatao; kisasi cha bilioni 4.5 kiliombwa katika mwaka wa fedha 2010/2011 na kiasi kilichosalia cha shilingi bilioni 4.8 kimeombwa katika mwaka huu wa fedha 2011/2012. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Geita itajenga mtandao wa mabomba ya kusambaza maji kutoka katika matanki ya kuhifadhi maji hadi kwa mtumiaji (distribution) na mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2011/2012. MHE. JOSEPHINE T. CHAGULLA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri kabisa ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza kama ifuatavyo. Tatizo la ukosefu wa maji katika mkoa mpya wa Geita limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya mkoa na taifa pia. Kinamama ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa wamekuwa wakitumia muda mwingi na nguvu kwa kutafuta maji tu badala ya shughuli zao za ujenzi wa taifa. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kumaliza tatizo hili ili kinamama hawa nao waweze kushirikiki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa lao? 3 NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimwia Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Thabita kama ifuatavyo. Ni kweli Serikali inatambua matatizo ambayo kinamama wanapata na sasa hivi ndiyo maana tumeanzisha huo mradi mkubwa wa kuendeleza sekta ya maji katika kila mji na kila wilaya. Kwa hiyo kwa mwaka wa fedha ambao tunao sasa hivi Serikali imetenga shilingi bilioni 3.5 katika mradi unaoitwa Lake Victoria Commission, Water Facility, kwa hiyo hii ni miradi ambayo tutaendeleza upatikanaji wa maji katika mji wa Nasio, wa Sengerema na Geita. Pia baada ya hapo naomba Mheshimiwa kwa sababu umeuliza mipango tu iliyopo naomba unisubiri wakati Waziri wa Maji atakapowasilisha Bajeti yake na ataelezea mipango ambayo ipo kwa ajili ya miji hiyo ahsante sana. (Makofi) MHE. NYAMBARI CHACHA M. NYANGWINE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona na mimi niweze kuungana na mwuliza swali ili kuuliza swali lingine la nyongeza hasa kuhusiana na wenyeji wa Tarime. Kwa kweli wilaya ya Tarime ina matatizo makubwa ya maji, tangu enzi za uhuru hadi sasa mimi naamini haijawahi kupata maji safi na salama kwa ajili ya afya ya wakazi wa Tarime. Je, Serikali inatoa msimamo gani kuhusiana na tatizo hilo? SPIKA: Yaani ni yale maji ya lake sasa. NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chacha, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo:- Katika mji wa Tarime, pia tumekasimu mamlaka ya maji Musoma ili iweze kusimamia uendelezaji na upatikanaji wa maji katika mji ule. Sasa hivi ameshaajiriwa mtaalam mwelekezi ambaye anatathimini kuweza kujua kabisa kiasi gani cha maji kitakidhi na ongezeko la watu lililopo katika wilaya ya Tarime. Kwa hiyo naomba pia Mheshimiwa Chacha utusubiri kuweza kujua mipango kabambe ambayo Serikali imepanga ambayo tutawasilisha kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji katika mwaka huu wa Fedha. SPIKA: Wanaotaka kuuliza maswali ya nyongeza wanasimama mara ya kwanza wakisimama baadaye huwezi kupata nafasi. 4 Na. 186 Utaratibu wa Ajira za Watumishi wa Halmashauri MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:- Utaratibu wa ajira za watumishi katika Halmashauri ilikuwa ikifanywa na Bodi za Halmashauri husika lakini utaratibu wa sasa ajira zote hutolewa na Idara Kuu ya Utumishi Dar es Salaam. (a) Je, ni utaratibu gani wa uhakika unaotumika kutoa matangazo ya ajira? (b) Je, Serikali inasaidiaje katika gharama za safari na posho ya kujikimu kwa watu walioitwa kwenye usaili? SPIKA: Namba gani? MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Namba 186. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA) alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munde Tambwe lenye, sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Utaratibu wa uhakika wa kutoa matangazo ya ajira unaotumika kwa sasa ni kupitia vyombo vya habari vilivyopo nchini hususan magazeti na tovuti mbalimbali za Serikali. Kwa kupitia matangazo hayo waajiri na hasa Wakurugenzi wa Halmashauri wanaelekezwa kubandika matangazo hayo kwenye mbao za matangazo zilizopo kwenye maeneo yao. (b)Serikali haina utaratibu wa kuwarudishia gharama za safari waombaji wa fursa za ajira. Hata sekretarieti ya ajira imeweka utaratibu wa kuwafanyia usaili waombaji kazi katika makao makuu ya mikoa wanakotoka. Mheshimiwa Spika, kama hatua ya muda mfupi ya kuwapunguzia gharama za waombaji kazi, Sekretarieti ya ajira imefungua ofisi sita za kanda kati mikoa ifuatayo:- Manyara kwa ajili ya mikoa ya kanda ya Kaskazini, Tabora kwa ajili ya Mikoa ya Kanda ya Kati, Mwanza kwa ajili ya Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Morogoro kwa ajili ya Mikoa ya Kanda ya Mashariki na Mbeya kwa ajili ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. 5 MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimwulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo. (i) Hivi Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba Watanzania wengi hawajui hata maana ya tovuti, hasa vijana wetu waliomaliza shule za kata waliopo kule vijijini, lakini atakubaliana na mimi pia kwamba TV hakuna wala magazeti hayafiki kwa wakati? (ii) Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Serikali inaona ugumu gani kurudisha ajira hizi kwenye Halmashauri za Manispaa au Halmashauri za wilaya, lakini Serikali pia inaona basi ugumu gani kupeleka ajira hizi angalau kwenye sekretarieti za mikoa kupunguza urasimu, gharama za kwenda kwenye kanda ili vijana wetu hawa waweze kupata ajira za udereva, uhudumu na kuzing’ang’ania wao kwenye Serikali Kuu? Naomba majibu. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu majibu ya nyongeza ya Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, kama ifuatavyo. Kuhusu suala la tovuti, ni kweli kwamba wapo ambao hawafahamu lakini pia katika dunia ya sasa wapo ambao wanafahamu. Hilo suala la tovuti ni njia moja tu ambayo kama nimeelezea, tumesema tunapitia magazeti, na katika Halmashauri husika, Wakurugenzi wanaagizwa kuweka katika mbao za matangazo.