MKUTANO WA ISHIRINI Kikao Cha Ishirin
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA ISHIRINI Kikao cha Ishirini na Mbili - Tarehe 2 Julai, 2010 (Mkutano ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Anna S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILLIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha, 2010/2011. MHE. JOB Y. NDUGAI - MWENYEKITI WA KAMATI YA MALIASILI NA UTALII: Taarifa ya Kamati ya ya Miundombinu Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2009/2010 pamoja na maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011. MHE.MAGDALENA H. SAKAYA, MSEMAJI MKUU WA KAMATI YA UPINZANI KUHUSU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII: Taarifa ya Msemaji wa Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Makadiro ya Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011. NAIBU WAZIRI WA USHIRIKIKANO WA AFRIKA YA MASHARIKI PAMOJA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA: 1 Randama za Makadiro ya Matumizi ya Wizara ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011. MHE SEIF ALI IDDI (K.n.y. WAZIRI WA FEDHA NA UCHUMI): Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Benki Kuu ya Tanzania kwa Mwaka 2008/2009 [The Annual Report and Audit Accounts of the Bank of Tanzania for the Year 2008/2009]. MASWALI NA MAJIBU Na.155 Kampuni za Biashara Kutoa Asilimia 0.3 ya Mapato Yake kwa Halmashauri MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:- Sheria Na. 9n ya LGFA ya Mwaka 1998 inazitaka Kampuni za Biashara kutoa asilimia 0.3 ya Mapato yake (baada ya kulipa kodi zote) kwenye Halmashauri wanapofanyia shughuli zao,lakini zipo kampuni ambazo zimekuwa hazitoi malipo hayo kwa sababu tu shughuli zao ziko kwenye Miji mikubwa kama Mwanza, Dar es Salaam, na baadhi ya kampuni za jinsi hiyo pamoja na TIGO,ZAIN na VODACOM ambazo zimeshindwa kulipa kiasi hicho kwa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo. Je, Serikali iko tayari kufanya marekebisho haraka kwenye utaratibu uliopo sasa ili sheria hiyo iweze kutekelezwa kulingana na kusudi lake? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Mukasa, Mbunge wa Biharamulo napenda kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ya fedha za Seriakli za Mitaa Sura 290 ilitungwa na Bunge mwaka 1982 na hivyo kutumika kwa zaidi ya miaka 28. Kwa muda wote huo yametokea mabadiliko mbalimbali ya kisera, kiuchumi, kijamii, kisheria na kihasibu ambayo yameifanya sheria hiyo kuonekana imepitwa na wakati. Kufuatia hali hiyo na kutokana na hitaji la utekelezaji wa sera ya D by D, ilionekana kuna haja ya kupitia sheria hiyo ili kuyaingiza mabadiliko mbalimbali katika mfumo wa sheria, pamoja na Memorandum ya fedha za Mamlaka za Serikali (Local Authority Financial Memorandum of 1997). 2 Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa Sura ya 290 kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) (z) inazitaka kampuni za biashara kutoa asilimia 0.3 ya mapato yake (baada ya kulipa kodi zote) kwenye Halmashauri wanapofanyia shughuli zao, lakini zipo kampuni ambazo zimekuwa hazitoi malipo hayo kwa sababu tu Makao Makuu ya shughuli zao yako kwenye Miji mikubwa kama vile Mwanza na Dar es Salaam. Tatizo hili sio kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo peke yake bali lipo karibu kwenye Halmashauri nyingi nchini na Wizara yangu imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwenye Halmashauri hizo mfano, Kahama, Mtwara, Mikindani,Geita na kadhalika zikilalamikia baadhi ya makampuni kutolipa kodi ya huduma. Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Halmashauri hazina sheria ndogo zinazoiwezesha kukusanya ushuru huo wa huduma na hivyo makampuni hayo kutumia mwanya huo wa kugoma kulipa na wakati mwingine ni suala la tafsiri ya sheria yenyewe na sheria ndogo za Halmashauri. Napenda kusisitiza kwamba msingi Mkubwa wa ushuru huo ni mahali ambapo kampuni na taasisi inafanyia shughuli au biashara zake ili mradi kampuni na taasisi hizo zina ofisi. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua changamoto hizo Wizara yangu tayari ipo katika mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria ya fedha za Serikali za Mitaa Sura 290. Baadhi ya mambo muhimu katika mapendekezo ya sheria hiyo ni kupanua wigo wa kulipa ushuru na kuweka mfumo mzuri wa ulipaji wa ushuru,(service levy) kwa kuondoa migongano iliyokuwepo ambayo ushuru huo ulikuwa unalipwa kwenye Halmashauri ambayo kampuni hiyo ina Makao Makuu hata kama shughuli zake zinafanywa nje ya Halmashauri. Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo ya marekebisho haya yataziongezea mapato Mamlaka za Serikali za Mitaa, yataziwezesha Serikali za Mitaa hizo kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo, yataziondolea Mamlaka hizo migogoro juu ya Halmashauri ipi inapaswa kulipwa ushuru kwa huduma na kupunguza ukwepaji wa kulipa ushuru mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mapendekezo ya marekebisho hayo kwa sasa yanajadiliwa na wadau mbalimbali kwa kupata maoni ambayo yataboresha utekelezaji mzuri wa sheria hiyo. Baada ya kupokea maoni hayo tutaleta hapa Bungeni mapendekezo ya marekebisho ya sheria. 3 Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati huu ambapo wadau wanaendelea kutoa maoni yao kwa lengo la kuifanyia marekebisho sheria. (Makofi) MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru na nashukuru majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naomba kuwa na swali moja la nyongeza:- Kwa kuwa, Naibu Waziri amekiri hapa kwamba hili ni tatizo na ni tatizo ambalo ni pana kwa maana linatokea kwenye Halmashauri nyingi na kwa kuwa tatizo hili limekuwa la muda mrefu na hivyo Halmashauri zetu zimekuwa zinakosa mapato hasa ukichukulia kuna baadhi ya Halmashauri kama ya Biharamulo ambayo wigo wa mapato ni mdogo. Je, Serikali ipo tayari sasa baada ya kukiri kuanza mchakato wa kurekebisha sheria hii, iko tayari kututhibitishia ni lini mchakato huu unatarajiwa kukamilika ili kuepuka uwezekano wa mchakato kwenda kwa muda mrefu bila ukomo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, labda niweke vizuri hapa jambo hili tusije tukafika mahali watu wakaanza kufikiri kwamba sasa kwa vile tunaanza marekebisho. Kwa hiyo, tunamaanisha kwamba huu ushuru usilipwe. Nimecheki na Dodoma, nimecheki na Arusha, nimecheki na maeneo mbalimbali yanaendelea kuokota ushuru huu pamoja na mapungufu haya ambayo nimekiri kwamba yako hapa. Sasa anataka kujua ni muda gani itachukua, wewe mwenyewe unafahamu na Wabunge wenzangu wote tunafahamu kwamba kipindi hiki huwa hatuleti sheria hapa, tunazungumzia mambo ya Bajeti tu. Kwa hiyo, tuombe tena Mungu akitujalia tena huko mbele ya safari kama tutakwenda, tutapita salama mimi ninaamini Serikali ipo na tutafanya marekebisho hayo. MHE. HAROUB SAID MASOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanaleta mategemeo, na kwa kuwa swali lililoulizwa linahusiana na simu za mkononi na kwa upande wangu mimi naipongeza Serikali kwa kutoa muda wa kutosha kabisa kuhusu usajili wa simu, lakini lililojitokeza ni kwamba wenyewe wenye kampuni za simu watu wamesajili, lakini wanapouliza namba zao na wanapopiga simu wanasema hazijasajiliwa. Je, zitakapofungwa simu zao baada ya tarehe 16 Julai, 2010 nani atachukua dhima ya fidia ya gharama ambazo anakula hasara mteja? WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, juzi wakati nikiwasilisha Bajeti yangu nilieleza kwamba kikomo cha kusajili simu ilikuwa ni siku ya tarehe 30 Juni, 2010 ifikapo saa sita usiku, lakini nikaongeza kwamba kutokana na usikivu ya Serikali ya awamu ya nne ya Chama cha Mapinduzi, imetafakari kilio cha watu walio wengi na kuongeza majuma mawili hadi 4 kufikia tarehe 15 Julai, 2010. Tamko hili limepokelewa kwa hisia mbalimbali, wengi mtakuwa mmesikiliza kipindi cha redio jana asubuhi na kwenye magazeti. Watu walio wengi zaidi wamelaumu kwa kuongeza huo muda kwamba Watanzania tunaonekana kwamba hatupendi kufuata discipline ya maamuzi tunayoyafanya na kwamba tumeongeza muda wa watu kutukana zaidi wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi. Kwa hiyo, sio nia ya Serikali tena kuongeza muda wa kusajili simu na ifikapo tarehe 15 saa sita ya usiku simu ambazo hazijasajiliwa zitazimwa na mpaka pale watu watakapoweza kulipia tena. Mheshimiwa Naibu Spika,napenda kutoa hayo maelezo. Na. 156 Ujenzi wa Kituo cha Afya kila Kata na Zahanati kila Kijiji MHE. RICHARD M. NDASSA (K.n.y. MHE. DR. IBRAHIMU S. MSABAHA) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa ujenzi wa vituo vya Afya katika kila Kata na Zahanati katika Kijiji unatekelezwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dr. Ibrahimu Said Msabaha, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo. Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) umeanza kutekelezwa mwaka 2007 na unategemewa kukamilika mwaka 2017. Moja ya mambo ya muhimu yanayotekelezwa ni ujenzi wa kituo cha Afya katika Kata na Zahanati kwa kila Kijiji na ujenzi wa Hospitali za Wilaya. Ili kuhakikisha kuwa lengo hilo linatimia, Serikali kupitia MMAM imepanga kutekeleza kwa hatua mambo yafuatayo:- 5 (i) Uimarishaji wa vituo vya Afya na Zahanati zilizopo ili ziweze kutoa huduma bora.