Tarehe 12 Aprili, 2021
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Saba – Tarehe 12 Aprili, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Mkutano wetu wa Tatu, leo ni Kikao cha Saba. Natumaini mlikuwa na weekend njema Waheshimiwa Wabunge, ingawaje weekend ilikuwa na mambo yake hii. Jana nilimtafuta Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa mambo yetu haya ya Bunge kuhusiana na uchangiaji wa Mpango wa Maendeleo akaniambia Mheshimiwa Spika tafadhali niache. Aah! Sasa nakuacha kuna nini tena? Anasema nina stress. Kumbe matokeo ya juzi yamempa stress. (Makofi/Kicheko) Pole sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, na Wanayanga wote poleni sana. Taarifa tulizonazo ni kwamba wachezaji wana njaa, hali yao kidogo, maana yake wamelegealegea hivi. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge baadaye tunaweza tukafanya mchango kidogo tuwasaidie Yanga ili wachezaji… (Kicheko) Katibu, tuendelee. (Kicheko) NDG. EMMANUEL MPANDA – KATIBU MEZANI: 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA VIJANA) (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2021/2022. NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu. Katibu! NDG. EMMANUEL MPANDA – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Swali la kwanza linaelekea TAMISEMI na litaulizwa na Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge kutoka kule Ruvuma. Na. 49 Hitaji la Vituo vya Afya – Tunduru MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya afya katika Kata za Tinginya, Muhimba, Kalulu, Mindu, Nalasi Magharibi na Nalasi Mashariki Wilayani Tunduru? SPIKA: Majibu ya Serikali kuhusu ujenzi wa vituo vya afya Ruvuma na nchi nzima, Mheshimiwa Naibu Waziri TAMISEMI, Mheshimiwa David Silinde, tafadhali.
[Show full text]