MKUTANO WA SABA Kikao Cha Kumi Na Saba – Tarehe 4 Mei, 2017
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA SABA Kikao cha Kumi na Saba – Tarehe 4 Mei, 2017 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Adrew J. Chenge) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa tukae, Katibu. NDG. RAMADHAN ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO:- Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2017/2018. MWENYEKITI: Ahsante, Katibu. NDG. RAMADHAN ISSA ABDALLAH – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Swali la kwanza kwa siku ya leo kama ilivyoada linaelekezwa Ofisi ya Waziri Mkuu na linaulizwa na 1 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde. Kwa niaba yake. MHE. KHATIB SAID HAJI: Nipo. MWENYEKITI: Leo uko upande gani? MBUNGE FULANI: Amebadili chama. (Kicheko) MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo naingia. MWENYEKITI: Ubaki huko huko. (Kicheko) MHE. KHATIB SAID HAJI: Haya ahsante. (Kicheko) Na.140 Umuhimu wa Mwenge wa Uhuru MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- (a) Je, bado kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka, kama zipo ni faida gani? (b) Kama hakuna faida, je, ni lini Mwenge huo wa Uhuru utasitishwa? MWENYEKITI: Ahsante. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista Mhagama majibu. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze muuliza swali leo kwa kukaa upande ule alioulizia swali. (Makofi/Kicheko) 2 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, faida za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na Kimataifa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha ari ya wananchi kujitegemea na kuwekeza katika maeneo mbalimbali katika Taifa letu; kuwa ni chombo pekee cha kujenga umoja, mshikamano na kudumisha amani pale ambapo Mwenge unapita bila kujihusisha na itikadi za kisiasa; kuendelea kuhamasisha na kuimarisha umuhimu wa Muungano kwa Watanzania wa pande mbili za nchi yetu; na kila mwaka hufungua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya wananchi na kuhamasisha uzalendo wa kuendelea kujitolea. Mfano mzuri ni kutokana na takwimu zilizopo ambazo zinaonyesha miradi ya maendeleo iliyozinduliwa pamoja na kuwekwa mawe ya msingi kupitia Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2015/2016 ni pamoja na miradi 1,342 yenye thamani ya shilingi 463,519,966,467. Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Kimataifa Mwenge wa Uhuru umeendelea kusimamia dhana na maudhui yake ya kumulika hata nje ya mipaka yetu kwa kuwa msuluhishi wa amani katika Bara la Afrika na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine ya Afrika duniani kote. Umoja, mshikamano, upendo na ukarimu wa Watanzania ni matunda pia ya Mwenge wa Uhuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na faida na mafanikio makubwa yanayopatikana kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru, Serikali inaamini kuwa zipo faida za kuendelea kukimbiza Mwenge huo wa Uhuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali haina mpango wowote wa kusitisha mbio za Mwenge wa Uhuru. Dhana hii itakuwa ni endelevu na tungependa kuiendeleza kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa kusisitiza misingi hii bila kuchoka. (Makofi) MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Haji. 3 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, malengo, dhamira ya kuanzishwa Mwenge wa Uhuru yameonekana kutotimizwa ikiwemo badala ya kueneza upendo Mwenge wa Uhuru umekuwa unaeneza chuki. Mfano, katika Mkoa wa Rukwa hivi karibuni Wenyeviti na Watendaji waliwekwa ndani kwa kosa la kutochangisha wananchi kuhudumia Mwenge wa Uhuru. Je, kama ni mfano wa kuigwa na katika Afrika na Dunia hakuna nchi iliyotuigiza wakakimbiza Mwenge huu hamuoni kwamba kukimbiza Mwenge sio kuleta maendeleo katika nchi? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili, nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mwenge wa Uhuru historia yake ni kuupamba Uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ina historia yake ya kupata Uhuru kutokana na Mapinduzi. Kwa sababu Mwenge sio jambo la Muungano, hamuoni sasa iko haja ya kuacha kuuleta Mwenge huu kule Zanzibar ambapo hatuoni maana yake yoyote? (Makofi) MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, majibu. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango, uratibu na utekelezaji wa kimfumo na wa kifalsafa wa ukimbizaji wa mbio za Mwenge, huratibiwa kwa kufuata kanuni na utaratibu wa maandalizi uliowekwa kwa nchi nzima ya Tanzania. Hivyo basi, kama ziko dosari ambazo zimekuwa zikijitokeza eneo moja hadi lingine hazitaki kumaanisha kwamba historia ya falsafa ya Mwenge ile ambayo imejengwa katika misingi ya uhuru wa nchi yetu, eti sasa ndiyo iondolewe kwa sababu ya dosari hizo ndogo zinazojitokeza. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali kwenye dosari ndogo tutaendelea kuzipitia na kuziondoa ili falsafa ya Mwenge wa Uhuru iendelee kubaki kama ilivyo. (Makofi) 4 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anasema Zanzibar si sehemu ya Mwenge huu wa Uhuru. Nataka kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya matunda mema ambayo yalizaliwa kwa sababu ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimo la Arusha na ukombozi wa Bara la Afrika. Hivyo, kwa sababu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni matunda ya Mwenge wa Uhuru, Mwenge huu utaendelea kukimbizwa Bara na Visiwani na utaendelea kuenziwa na Watanzania wote Bara na Visiwani ukiwemo wewe Mheshimiwa Mbunge Haji kutoka Visiwani kama Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linaenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru. (Makofi) MWENYEKITI: Hebu tuone Mheshimiwa Getere. MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nataka kuuliza kwa mtu ambaye ni Mtanzania aliyezaliwa katika nchi yetu, anayehoji juu ya Mwenge… WABUNGE FULANI: Aaah! MHE. BONIPHACE M. GETERE: Badala ya kuhoji juu ya mambo mabaya yanayotokea kwenye Mwenge, anayehoji juu ya Mwenge unafanya nini huyu unaweza kumkabidhi hii nchi akaendelea kukaa nayo? Nataka tu kupata ufafanuzi huo. (Makofi) MWENYEKITI: Anataka ufafanuzi. Haya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo linaonyesha jinsi alivyokomaa katika kujua historia ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niwaambie Watanzania, falsafa ya Uhuru wa nchi yetu ya Tanzania haiwezi kutenganishwa na Mwenge wa Uhuru. Naomba 5 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) niwakumbushe, wakati wa Uhuru tarehe 9 Desemba 1961, Marehemu Baba wa Taifa alisema, sisi tutawasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike ndani na nje ya mipaka yetu ulete amani, tumaini, upendo, uondoe chuki na dhuluma, sasa jambo hili si dogo. Kwa Mtanzania anayemuenzi Marehemu Baba wa Taifa itashangaza sana kama hatataka kuenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda tu kuwaomba Watanzania kwa kweli hatuna haja ya kuchukuliana hatua ya namna moja au nyingine lakini wote tutambue Mwenge wa Uhuru ni tunu kubwa ya Uhuru wa nchi yetu na unapaswa kuenziwa na Watanzania wote. (Makofi) MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Suleiman. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kama ziko dosari katika kukimbiza Mwenge basi zitarekebishwa. Mimi nachotaka kumwambia hakuna dosari, dosari ni huu Mwenge wenyewe. Kwa sababu kwanza unapoteza fedha nyingi kupita kiasi na wakati na kwa kule kwetu tunaamini kukimbiza Mwenge ni ibada. Kwa nini tuendelee kulazimishwa kuabudu moto? MWENYEKITI: Uliza swali. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Swali langu ni hilo kwa nini tulazimishwe kuabudu moto? Sisi tunaamini ni ibada ya moto hiyo. (Makofi) MWENYEKITI: Ahsante. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mhagama. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimia Mwenyekiti, labda tu nianze kwa kumnukuu mwanafalsafa mmoja ambaye nilimsoma anasema, vipo vitu vingine vinahesabika lakini huwezi kuvihesabu. Unaweza ukawa na 6 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) vitu vinavyohesabika lakini ukashindwa kuvihesabu na nataka nikuambie hata wewe unaweza kuwa na mtazamo ambao ni hasi kuhusu Mwenge wa Uhuru lakini utashindwa kutekeleza mtizamo huo wa kuufuta Mwenge wa Uhuru katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nakuambia hivi Mheshimiwa Mbunge, mwaka jana wakati tunahitimisha mbio za Mwenge Mkoani Simiyu, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Simiyu, kwa kutumia Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Simiyu umeweza kuzindua viwanda vitatu ambavyo vimeongeza maendeleo ya kiuchumi na vimeongeza ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo, ukiangalia faida za Mwenge huu ni kubwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tumezindua mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Katavi. Mkoa wa Katavi haukuwa na uwanja mkubwa wa michezo wa Mkoa. Nje ya bajeti ya maendeleo ya mkoa, Mkoa wa Katavi umeweza kuanza ujenzi mkubwa wa kiwanja cha mpira katika mkoa huo. Nimeeleza hapa miradi ya kujitegemea ambayo imebuniwa na wananchi ambayo imeongeza chachu ya maendeleo na uchumi wa wananchi katika