MAJADILIANO YA BUNGE MKUTANO WA ISHIRINI Kikao
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ MKUTANO WA ISHIRINI Kikao cha Ishirini na Moja – Tarehe 1 Julai, 2010 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA MASOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, naomba kuwasilisha mezani hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. MWENYEKITI WA KAMATI YA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mezani Taarifa ya Kamati ya Viwanda na Biashara Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kwa Mwaka wa Fedha 2009/2010 pamoja na maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU WIZARA YA VIWANDA, BIASHARA NA MASOKO: 1 Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mezani Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kuwasilisha Randama za Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. MASWALI KWA WAZIRI MKUU NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, leo bahati nzuri Kiongozi wa Kambi ya Upinzani yupo. Kwa hiyo, nitamwita awe mwulizaji wa kwanza kufuatana na Kanuni zetu. Mheshimiwa Hamad Rashid Mohammed, mahasimu wawili! (Kicheko) MHE. HAMAD RASHID MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, leo wa Rukwa hawapo.(Kicheko) Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi hivi karibuni imeendelea na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Visiwani Zanzibar. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeupa uwakala Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Daftari la Wapiga Kura la Zanzibar, lina idadi ya wapiga kura wapatao 408,000, Daftari la Wapiga kura la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina wapiga kura kama 465,000. Wakati ZEC ni Wakala wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa Zanzibar, Daftari hilohilo linatumika kwa kuwapigia kura Wabunge wa Jamhuri ya Muungano, lakini lile la Jamhuri ya Muungano linatumika katika Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Je, Mheshimiwa Waziri Mkuu, huoni hapa kuna utata wa Kikatiba na wa Kisheria kwamba, Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatumii Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika kuwapata Wabunge kutoka Zanzibar tofauti na Wabunge wenzao wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inasema nini? WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijaribu kumjibu Mheshimiwa Hamad, swali lake gumu sana kama ifuatavyo:- 2 Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba yetu Bunge limepewa Mamlaka ya kutunga Sheria na moja ya Sheria zilizotungwa ni ile inayohusiana na Uchaguzi Mkuu. Sheria hiyo inatawala taratibu zote za Uchaguzi kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa upande wa Tanzania Visiwani, iko Sheria nyingine ambayo nayo imetungwa kuongoza na kusisimamia taratibu hizo za Uchaguzi. Ile inahusika zaidi na masuala yote ya Uchaguzi yanayohusiana na Zanzibar. Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachokisema Mheshimiwa Hamad kwamba, Sheria hii ambayo sisi tunaitumia hapa kwa ajili ya kupata Wabunge, kwa kuwa ndiyo Sheria hiyo hiyo ambayo inatumika Zanzibar kwa ajili ya Wabunge ambao wanakuja kuingia katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kimantiki ilitakiwa Sheria moja ndiyo isimamie maeneo yote mawili. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu kwa upande wa Sheria ya Zanzibar kwa mfano, masharti kama yale ya ukazi wa miezi 36 sisi huku hatuna. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba iko tofauti kidogo kati ya Sheria hii pamoja na ile ya upande wa Visiwani. Kwa hiyo, mimi ninadhani rai ya msingi ipo kwamba, pengine Serikali ingetazama namna tunavyoweza kuwianisha Sheria hizi mbili kwa upande wa hawa Wabunge wanaotoka upande wa Zanzibar kwa ajili ya kuja kujumuika na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vingenevyo itaendelea kuonekana kwamba, kuna migongano ya kisheria ambayo ingetakiwa kwa kweli kuwa katika Sheria moja. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi ninafikiri ni jambo zuri, tutamwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliangalie, awasiliane na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwenzake waone hii hitilafu ni namna gani inaweza ikarekebishwa. Pengine kitakachohitajika ni marekebisho ya kisheria tu ili Sheria moja tu iweze kutawala kwa maana ya yale ambayo yanahusiana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi) MHE. HAMAD RASHID MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kulielewa hili na kukubali kwamba, kuna tatizo la kimsingi. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuwa Bunge hili sasa lina muda mfupi na hayo ni marekebisho ya kikatiba na kisheria na hatuna muda wa kuyafanya, na kwa kuwa tunaingia kwenye uchaguzi ambao tayari una utata wa kisheria na kikatiba, huoni kwamba inawezekana kabisa Mbunge akachaguliwa na hatimaye watu wakaenda Mahakamani na kudai kwamba, huyu Mbunge hakuchaguliwa kihalali kwa sababu 3 utaratibu wa kupiga kura kumchagua siyo sawa na vile ambavyo Sheria ya Jamhuri ya Muungano inasema. Je, huoni kunaweza kutokea hitilafu ya Wabunge kuondolewa na Mahakama kwa sababu Sheria haikufuatwa? WAZIRI MKUU: Ukiniuliza hilo ni gumu kwa sababu itabidi ningoje sasa nione mkienda Mahakamani, busara za Mahakama zitasema kitu gani, kwa sababu, kikubwa hapa ni kuona masharti ambayo yako kwenye Katiba yetu na yale ambayo yako upande wa Zanzibar. Kama nilivyosema kumbukumbu yangu ya haraka haraka eneo moja ambalo ninaliona kweli linaleta kasoro au tofauti kidogo ni lile la ukazi. Lakini, kama ni la ukazi tu, mimi ukiniuliza nitasema pengine kinachohitajika hapa ni kutafuta tu namna ya kuondoa hiyo hali kwa ajili ya Mbunge huyu. Lakini, kimsingi sidhani kama Wabunge wa upande wa Zanzibar wana tatizo, na hilo la ukazi sidhani kama ni suala kubwa hilo. Hapa ni ile kasoro ya kisheria ambayo nadhani ndiyo ninaiona kama Sheria ni lazima ikae vizuri isiwe na hitilafu ambazo zinaleta kasoro. (Makofi) MHE. DR. WILLIBROD P. SLAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni tumepata taarifa kutoka maeneo mbalimbali na tuna nyaraka zinazohusika na hilo kwamba, Wakuu wa Wilaya wamekuwa wakitumia ofisi za Serikali, muda wa Serikali, vyombo vya Serikali kuwaalika na kuwaita wafanyabiashara katika Ofisi zao au katika Ofisi mbalimbali za Serikali bila hata kuwaambia wanaitiwa nini, jambo linaloashiria kwamba, mtu anaitwa bila hiari yake na wakifika huko wanatakiwa kuchangia Chama cha Mapinduzi. Kwenye maeneo mengine tumepokea pia hata Watendaji wa Vijiji. Mfano halisi ni Nzega, WEO anatakiwa achangie shilingi 20,000/= na VEO achangie shilingi 10,000/= na hata kuna vitisho kwamba wasipofanya hivyo watafutwa kazi. Je, Serikali inatoa tamkoa gani kuhusu hali hii ambayo inatengeneza uwanja usio sawa kwa kutumia Ofisi ya Serikali ambayo ni mlezi wa sisi wote? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ningetaka kumjibu Ndugu yangu Dr. Slaa. Kiungwana ningesema, si na wewe ukawaombe wa kwako. Lakini, ninajua nikisema hivyo atasimama haraka haraka kwamba siyo jibu nililokuwa nataka lipatikane. Mheshimiwa Spika, kwa kifupi ninasema tu kwamba, nichukue hii sehemu ya kwanza ya Mkuu wa Wilaya ambaye anawaita wafanyabiashara, pengine bila kujua 4 unaitiwa nini, anakwenda wanakutana pale na anamwambia bwana ninaomba mchango wako kwa ajili ya Chama cha Mapinduzi, hiari yake kukubali au kukataa. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitafurahi sana kama nitapata mfanyabiashara ambaye anasema alishurutishwa au akafungwa kamba ili aweze kukichangia Chama cha Mapinduzi. Mimi ninadhani hilo ndiyo litakuwa hasa la msingi katika hilo na ninafikiri wafanyabiashara ni watu wazima, na sidhani kama wanaweza wakashurutishwa kama wao mwenyewe hawapendi, sidhani lakini kama wapo fine tunaweza tukalipokea tukamwuliza huyo DC tukapata maelezo. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, Mkuu wa Wilaya huyu, kwa mfumo ulivyo hapa tusije tukasahau kwamba, vile vile ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya na ni Kamisaa wa Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, kwa maana hiyo anao vilevile wajibu wa kusaidia kutafuta michango kama kiongozi ambaye yuko ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Tatizo hapa litakuwa ni moja tu endapo atatumia dola au uwezo wake kumshurutisha mtu kuweza kuchangia. Hilo ndiyo ninaliona litakuwa tatizo.(Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mtendaji wa Serikali ya Kijiji au WEO kwamba na yeye analazimishwa kuchangia. Labda nirudi nyuma kidogo kwamba, kwa taratibu tulizonazo hapa nchini Mtumishi wa Serikali anaruhusiwa kuwa mwanachama wa chama chochote, ndiyo maana huko ndani tunao wanachama wa CUF, CHADEMA na kadhalika na wanaruhusiwa vile vile kuchangia vyama vyao pale watakapokuwa wameombwa na kwa masharti watakayokuwa wamekubaliana kwenye chama kinachohusika. Hapa unaloliona kama tatizo ni pale ambapo umekwenda umemshurutisha huyu mtumishi hata kama ni mwanachama wako wa Chama cha Mapinduzi au hata kama angekuwa mwanachama wa chama kingine. Kama ni hiari halina tatizo, hasa sisi huku ndani Serikalini tunachangia chama chetu kwa hiari