http://www.fortunecity.com/victorian/abbey/313/ukweli.html

UKWELI NI HUU (KUUSUTA UWONGO) Aman Thani Fairooz

Dibaji Kitabu Hichi Ukweli Ni Huu (Kuusuta Uwongo) Utukufu Na Neema Ya Zanzibar Na Ubaguzi Kabla Ya Mavamizi Ubaguzi Umeanzishwa Zanzibar Wakati Wa Serikali Yenye Kujiita Ya "Mapinduzi" Elimu Na Matibabu Bure! Taalimu Matibabu Hali Za Maisha Neema Zilikuwepo Kuanza Harakati Za Siasa Sheikh Ali Muhsin Kwenda Nchi Za Ulaya Ikiwemo Na Uingereza Kupigania Uchaguzi Wa "Common Roll" (Mtu Mmoja Kura Moja). Kuasisiwa HizbulWattan (Zanzibar Nationalist Party) Wakoloni Dhidi Ya Hizbu, Uhuru Na Umoja Wa Zanzibar Makao Makuu Ya Hizbu Hizbu Kumleta Zanzibar Seyyid AbdulRahman (Babu) Natija Ya Safari Ya Sheikh Ali Muhsin Wakoloni Na Nyerere Ndio Waasisi Wa AfroShirazi Uchaguzi Wa Mwanzo Juni 1957 Kwanini Sheikh Ali Muhsin Aliamua Kusimama N'gambo Badala Ya Majumba Ya Mawe? Kwenye Shari Huzaliwa Kheri Kukuwa Kwa Harakati Za Siasa Ati Husemwa Kuwa Hizbu Imefeli! Kugawanyika Kwa AfroShirazi Kuasisiwa Kwa Zanzibar And Pemba Peoples' Party (ZPPP) Tume Ya Sir Hillary Blood Uchaguzi Wa Pili, Januari 1961 Uchaguzi Wa Tatu Juni 1961 Ushirikiano Wa ZNP/ZPPP Kutokufaulu Mazungumzo Ya Mwanzo Ya Katiba Ya Uhuru AfroShirazi Iliandaa Machafuko Siku Ya Uchaguzi Muungano Wa ZNP/ZPPP, Waunda Serikali Kutokufaulu Mazungumzo Ya Mwanzo Ya Katiba Ya Uhuru Babu Kutoka Katika Hizbu Dhamiri Za Babu Kufungwa Gerezani Kwa Seyyid AbdulRahman Babu Kutolewa Gerezani Babu Babu Na Fisadi Yake Ya Mwisho Kipi Kilicho Mpelekea Babu Kuchukua Khatua Kama Hizo Uchaguzi Wa Julai 1963 Nyerere Anasema Wakoloni Walipendelea Kuiacha Serikali Ya Zanzibar Mikononi Mwa Hizbu Mkutano Wa Katiba Ya Uhuru. Uhuru Wa Zanzibar Sherehe Za Uhuru Yaitwayo "Mapinduzi" Kuuliwa Kwa Muhsin, Suleiman Na Ahmed

1

Kifo Cha Ali Mzee Mbalia "Skolashipu" Za Misri Yaliyo Nifika Nafsi Yangu Na Hayo Yenye Kuitwa "Mapinduzi" Maafa Ya Gerezani Kufungwa Kifungo Cha Miaka 10 Gerezani Kiasi Cha Kazi Alichokuwa Akifanyishwa Mfungwa Maovu Waliyotendewa "Wafungwa Wa Kisiasa" Kutolewa Gerezani Nakimbilia DarEsSalaam Mahabusi Wadhulumiwa Wa Mwalimu Nyerere Mateso Ya "Kwa Ba Mkwe" Maisha Ya Gereza Langoni Nyakati Za Kufanyishwa Kazi "Wafungwa Wa Sisasa" Ufungwa Wa Karume Ni Zaidi Ya Utumwa Kurejeshewa Uhuru Wetu Kuuliwa Wananchi Msikitini Kuuliwa Kwa Wananchi Wengine Namna Walivyo Uliwa Wafungwa Waliyokufa Gerezani (1) Mzee Mohammed Mbaba (2) Maalim Harun Ustadh (3) Idi Hassan (4) Ramadhan Ibrahim Saadalla Wameuliwa Vifungoni Wafungwa Wengine Wauliwa "Wafungwa Wa Siasa" Bado Waendelea Kuuliwa Aliyonizungumziya Twala Yalomfika Othman Shariff Kuteswa Na Kuuliwa Othman Shariff Kufungwa Na Kuuliwa Saleh Saadalla Karume Kuanza Kumbadilikia Twala Mwisho Wa Twala Makomred Wamechangia Maafa Yaliopo Nchini Kwanini Mwalimu Nyerere Alikataa Kuwapeleka Zanzibar Watuhumiwa Wa Kesi Ya Ukhaini? Siri Hii Ni Kubwa Sana!! Serikali Ya Mavamizi Ya Zanzibar Bado Imo Na Ubaguzi Wake Nilitakiwa Nitoke Nchini Namna Nilivyoondoka Kuukimbia Wattani Wangu Kuleta Ahli Zangu Dubai Mengineyo Kwa Ufupi Mwalimu Na Uislamu Mwalimu Na Utumwa Porojo La Mitaani Demokrasi Ya Vyama Vingi (MultiParty Democracy) Vipi Kuifikilia Demokrasi Shukrani

DIBAJI Namshukuru Mwenye Enzi Mungu Mwenye Wingi wa Rehema Kubwa na Ndogo kuniwezesha kuandika kijitabu hiki ambacho nimejaribu kiasi nilichoweza kuyaeleza yale yaliyotokea katika Nchi yetu, Zanzibar. Na yaliyonitokelea mimi mwenyewe na yaliyowatokelea Wananchi wenzangu kutokana na hayo yenye kuitwa, "Mapinduzi" yaliyofanyika katika Visiwa vyetu mnamo taarikh 12 Januari, 1964. Haya ninayoyaandika ni kiasi ya hayo niyajuayo mimi tu; hapana shaka yapo mengi ambayo sikupata kuyajuwa. Bali nataraji watatokea wenzangu nao, wakayaeleza waliyotendewa au waliyoyaona yakitendwa.

2

Nafanya haya si kwa makusudio yoyote mengine zaidi ya kutaka kueleza ukweli wa yaliyotendeka katika Nchi yetu ili Wananchi wenzangu (na ndugu zetu wa , bali na ulimwengu, pia) na khasa wale waliokuwa wadogo, na wale ambao hawajaja duniani wakati huo waweze kuyafahamu japo kwa uchache yaliyotendeka katika Nchi yao kwa hayo yenyekuitwa "Mapinduzi". Ikiwa katika kuyaelezea haya, kutahitajia kumtaja mtu au watu kwa njia yoyote, itakuwa nafanya hivyo kwa kutokana na maudhui ninayo izungumza wala si kwa ajili ya kusengenya au kukejeli au kudharau au kwa kutia illa za namna fulani, hashaa! Bali kwa vile dhamiri ya kukiandika kijitabu hiki ni kuelezea ukweli wa mambo yalivyokuwa, basi sitochelea kulieleza lolote madhali kwa kufanya hivyo ndio itakuwa natimiliza lengo nililolikusudia, nalo ni kuueleza ukweli. Kutokana na hayo, nachukuwa nafsi yangu masuliya yote yatayotokea katika maandishi haya.

Muhimu, nawaomba wasomaji wangu wajishughulishe zaidi na hayo niliyokusudia kuyaeleza, kwani hayo hayana shaka yoyote, ni kweli tupu. Na nawaomba wasijishughulishe na makosa madogo madogo, kama vile ya upigaji chapa, makosa ya lugha au juu ya utaratibu wa uwandishi. Ikiwa litatokea suala lolote, au ikiwa lolote halitafahamika, basi wakurejelewa ni mimi. Inshallah, nitajaribu kama nitavyoweza kutanzua kila lililotanzika na ikiwa nitashindwa, basi sitoona taabu kutaka msamaha. Mwenye kukamilika kwa yote ni Mwenye Enzi Mungu. Tunamuomba Mwenye Enzi Mungu ajaaliye haya tunayoyaeleza yapate kusomwa, kuzingatiwa na kufahamika na ipatikane faida ndani yake kwa kutumiwa kwa kheri. Kubwa ya kheri hizo ni kusahihisha palipo haribika, kuiondosha haramu, kuomba toba na kutenda mema, kwani mema huondowa mabaya. Mwenye Enzi Mungu atupe taufiq, Amin. Aman Thani Fairooz P.O. Box 10836 Telephone 04850802 Dubai United Arab Emirates Januari, 1995

3

KITABU HICHI Kidogobasi, Chungutamu. Kwa hakika Kitabu hichi ni kidogo basi. Lakini, kama alivyosema muandishi kuwa kaandika kwa ufupi, bali ufupi wa kutosheleza faida yake. Yoyote atakaye kisoma kitabu hichi kwa kutaka kufahamu na bila ya mawazo yake kudhibitiwa na kupenda au kuchukiya, basi hapana shaka atapata faida. Atafahamu jinsi wananchi wa Zanzibar walivyokuwa katika harakati zao za kuwania uhuru wa nchi yao kutokana na ukoloni wa Muingereza. Harakati ambazo zalianza kabla ya miaka ya 1940. Pia ataweza kufahamu ni nani walioanzisha harakati hizo, namna zilivyopata kuungwa mkono na wananchi na namna zilivyokuwa zikiendeleya. Pia atapata kufahamu jinsi ya pingamizi zilivyokuwa. Atafahamu pingamizi hizo zilivyoanzia, nani aliyezianzisha na kuzipalilia na kuzikuza. Atafahamu natija yake! Pia atafahamu vipi wananchi chini ya uwongozi wa vyama vyao ZNP/ZPPP walivyokuwa wakizikabili pingamizi hizo. Na zaidi atafahamu juhudi za waongozi wa ZNP/ZPPP katika kutaka mafahamiano na ushirikiano na wananchi wenziao ASP na nini ulikuwa muelekeo wa waongozi wa ASP, muelekeo ambao mara nyingi ulikuwa ukiathirika kwa uwongozi na fikra zilizokuwa zikipangwa na kuletwa kutoka nje ya nchi.

Chungutamu. Kweli ni chungu! Lakini ni wajibu isemwe na kubainishwa. Uchungu uliyomo ndani ya kitabu hichi ni kuona jinsi wananchi walivyohangaika kwa jasho, mali na hata damu zao kwa kuwania uhuru wao kutokana na ukoloni wa Muingereza, lakini kwa sababu ya husda, chuki na ufisadi uhuru huo haukuachiwa kuishi zaidi ya siku thalathini! Isitoshe, sio kuwa uhuru huo ulipotezwa kwa kutumiliwa njiya za usalama, sivyo, bali kwa fujo! Fujo ambalo natija yake ni kupotezwa Dola ya Zanzibar, roho za wananchi, heshima ya binaadamu, mali za watu na mwisho kuwachwa wananchi kuishi ndani ya haramu. Utamu japo kwa hakika sio utamu ni kwa vile kuweza wananchi kupata kuufahamu UKWELI ambao kwa muda wa zaidi ya miaka thalathini umekuwa ukifunikwa kwa UWONGO. Lakini, kama yalivyo maumbile, kweli daima huibuka.

Tunamshukuru Mwenye Enzi Mungu kwa kudhihiri kitabu hichi na kuweza kuufahamisha umma, bali na ulimwengu, maafa yaliofikishiwa Zanzibar, Nchi na Wananchi. Msomaji, na pengine hata asimuliwaye haya, huenda akasema, yaaleiti yalielezwa haya kiasi cha miaka ishirini liyopita, au kabla ya hapo. Hivyo ni kweli! Lakini kila kitu kwa majaaliwa, na kuchelewa kwengine kuna kheri zake kama kwengine kunavyo shari zake. Kheri katika kuchelewa kudhihiri kitabu hichi ni kuwa vijana waliokuwa wadogo wakati wa maafa ya Zanzibar leo ni watu wazima, wenye uwezo wa kufikiri, kuamua na kutenda. Kwa hivyo wanahitajia kuujuwa Ukweli. Wao si kwa ajili ya Kuusuta Uwongo, hashaa!! Bali ni kwa ajili ya kuujuwa ukweli, kisha iwe ni mafunzo kutokana na yaliotendeka. Watasoma, na Inshallah watayafahamu na kuyatumia. Na haya ndio khasa makusudio na faida ya kitabu hichi. Kutumia kwao huko kwanza iwe ni kwa kuepusha yasitendeke tena maafa yaliyotendwa, kufuatilia hilo au yote mawili sambamba ni kwa kufanyakazi katika kujenga palipo bomolewa. Kubomowa daima ni rahisi kuliko kujenga, kujenga kunataka umoja na ushirikano wa kila mmoja wetu. Kwa hivyo ni waajibu wa kila mmoja wetu kushirikiana, bega kwa bega, kwa nia na nguvu moja kufanyakazi kuirejesha Zanzibar. Kwanza, kuirejesha katika ramani ya ulimwengu ili iwe na jina na pahala pake kuwa ni Dola kaamili na iliyo huru. Kisha, bali ndio la muhimu, kuirejesha katika neema zake.

Hichi ni kitabu cha kusomwa na kila Mzanzibari, bali na ndugu zetu wa Tanganyika, pia. Abdulla Ali (Baba)

4

UKWELI NI HUU (KUUSUTA UWONGO)

Nimelichagua jina hili la UKWELI NI HUU KUUSUTA UWONGO, baada ya kuyasikia na kuyasoma me ngi ya uwongo na hata yakafika kusomeshwa watoto wetu katika maskuli ya Zanzibar kukhusu hayo yenye kuitwa "MAPINDUZI" yaliyofanyika katika visiwa vyetu vya Zanzibar mnamo taarikh 12 Januari 1964. Kabla ya kuingia katika hayo, ningependa ku waambia wasomaji wangu wote kuwa mimi si mjuzi hata kidogo wa fani hii ya uandishi; tena ni mbovu sana katika "spellings" na ka tika "nahau" za Kiswahili cha kisasa. Pia nawaomba radhi kwa Kiswahili changu cha kizamani. Bali, kutokana na huo uzushi na kupotezwa kwa makusudi ukweli wa hayo yaliofanyika kukhusu hayo yenye kuitwa "mapinduzi" nimeona sina budi illa ni kujitolea hivyo hivyo juu ya upungufu wangu katika fani hii ya uandishi. Lakini ukweli lazima niudhihirishe ili vichipukizi vyetu viweze kuyaelewa vilivyo yaliyotendeka katika nchi yao. Kwani wengi walikuwa wadogo na wengine walikuwa hata hawajazaliwa katika wakati huo.

Ilivyokuwa Kiswahili ni lugha yangu ya kuzaliwa, basi ninaiandika kama ninavyoisema. Si shughuliki na "kua au kuwa, aliniambia au aliniambiya, ameuawa au ameuwawa kenda au kaenda, amekwenda au ameenda". Hayo kwa wataalamu wa lugha ni mambo muhimu lakini kwa mimi nakutakeni msamaha juu ya hayo. Muhimu ya kuyaangaliya na kuyazingatiya ni yale nikusudiayo kuyaeleza, kwani hayo ndio muhimu na ndio ya kweli tupu isiyokuwa na dosari hata chembe.

La mwanzo nitakalo kuombeni mlifahamu uzuri ni ile hakika kuwa hayo yaliyofanyika katika visiwa vyetu taarikh 12 Januari 1964, hayakuwa "MAPINDUZI" wala hayafai hata kidogo kuitwa 'mapinduzi' kwa maana asili ya neno. Bali kwa maana zote yalikuwa khasa ni "MAVAMIZI", yaani kwa Kiingereza "INVASION". Mapinduzi lazima yapangwe, yaongozwe na yatekelezwe na wananchi wenyewe kwa maslaha ya nchi na wananchi wake. Sasa tukiangalia hayo yaliotendeka Zanzibar, yalipangwa, yaliongozwa na yalitekelezwa na WAGENI kutoka nchi za nje za jirani zetu. (Ni wao wala si wananchi ndio waliochukua ngawira kubwa kubwa). Haya yanathibitika zaidi kwa vile kuwa huyo jamadari aliyeyaongoza hayo 'mavamizi' ni John Okello na wa chini yake walikuwa Injini na Mfaranyaki. Nani kati ya hao aliyekuwa kitovu chake kimezikwa visiwani? Okello amezaliwa na amekulia kwao Uganda, Injini amezaliwa na amekuliya kwao Kenya na Mfaranyaki amezaliwa na amekuliya kwao Tanganyika. Wote hao walikuja Zanzibar wakiwa watu wazima na shughuli zao, wamekuja kutafuta kibarua na kukimbia kodi za kichwa katika nchi zao.

Liangalie hilo waliloliita "Baraza la Mapinduzi". Utaona sehemu kubwa ya wanachama wa Baraza hilo walikuwa si Wazanzibari, laa kwa kuzaliwa wala kwa kuchukua Tajnisi (Kuandikisha Uraia). John Okello, Khamis Darweshi, Seif Bakari, Said Natepe, Said Washoto, Muhammed Mfaume, Edington Kisasi, Mohammed Abdalla Kaujore. Ukiwaacha wengineo ambao nao vile vile walikuwa si wananchi wa Zanzibar kwa kuzaliwa, bali wao walikuja Zanzibar wakiwa katika migongo ya wazee wao na waliendelea kuishi humo visiwani kwa maisha yao yote. Na wakachukuliwa kama ni Wazanzibari.

UTUKUFU NA NEEMA YA ZANZIBAR Mwenyezi Mungu amevipa visiwa hivi viwili yaani Unguja na Pemba bahati ya utukufu kwa kila jambo lake. Hayo yaliendelea tokea karne na karne mpaka pale ulipotendwa ufisadi wa taarikh 12 Januari 1964, ndipo neema na utukufu wa Zanzibar ulipoanza kutoweka. Hapo tena, badala ya zumari kuwa likipulizwa Zanzibar, watu wa maziwani (Bara) walikuwa wakihemkwa, ikawa linapulizwa Bara, tuliopo visiwani tunahemkwa!

ZANZIBAR NA UBAGUZI KABLA YA MAVAMIZI Nathubutu kusema bila ya wasiwasi wowote kuwa Zanzibar hakukuwepo ubaguzi wa namna yoyote kwa maana khasa na ya wazi ya neno UBAGUZI. Kwanza Wazanzibari ni watu waliochanganya sana damu hata sio rahisi kuweza kumtambua mtu kuwa ni mwenye kutokana na asili ya kabila fulani kwa kuangalia rangi yake au pua yake au masikio yake au kimo chake au kwa jina lake. Jee, watu hao watabaguana namna gani? Malipo ya wafanyakazi serikalini yalikuwa hayakupangwa kiukabila. Wala serikali haikuwa na sehemu maalumu katika maskuli wala katika mahospitali kuwa zimetengwa kwa ajili ya watu wa makabila fulani.

5

Katika nchi za jirani zetu, Tanganyika, Kenya na Uganda kote huko kulikuwepo na ubaguzi uliyokuwa ukiongozwa na serikali za nchi hizo. Malipo ya mishahara ya wafanyakazi yalikuwa yakilipwa kutokana na makabila yao wala si kutokana na ujuzi wao wa kazi. Kulikuwepo "African Scale, Asian Scale na European Scale". Madaktari, Mainjinia, Waalimu na wowote nawawe wana elimu na ujuzi na maarifa ya namna moja, yaani wote sawa sawa kwa elimu na ujuzi wa kazi zao, lakini mishahara yao ilikuwa tafauti kutokana na makabila yao. Waafrika ndio wenye kulipwa malipo ya chini kabisa kuliko wote. Wazungu walikuwa ndio wenye kulipwa mishahara minono (hata baadhi yao walikuwa hawana elimu yoyote isipokuwa huwo Uzungu wao), waliowafuatia ni Waasia.

Vyoo vya njiani (Public Toilets) na sehemu za kungojelea usafiri wa reli navyo vile vile vilikuwa vikitumika kwa ubaguzi wa kikabila. Waafrika waliekewa vyoo vyao na sehemu zao za kungojelea usafiri. Wazungu walikuwa na sehemu zao na Waasia walikuwa na sehemu zao, wote mbali mbali. Lilikuwa ni kosa na kuvunja sheria ikiwa imetokea kwa yoyote kuingia katika sehemu isiyo kuwa amekhusika nayo. Khasa Muafrika awe ameingia au amekaa katika sehemu za Waasia au za Wazungu. Katika Tanganyika, Kenya na Uganda kote huko kulikuwa na Kodi ya Kichwa. Kodi hiyo ilikuwa ikilipwa na kila mtu aliyekwishafika balegh katika umri wake. Nayo pia ikitekelezwa kwa njia za ubaguzi wa kikabila. Waasia na Wazungu, wao hata ikiwa wamechelewa kulipa kodi zao, basi walikuwa hawakamatwi majiani wala hawaendewi majumbani mwao kukamatwa. Lakini, Waafrika walikuwa wakisakwa majiani na wakiendewa majumbani mwao mnamo pinga pinga za usiku. Na wakikamatwa, basi walikuwa wakifungwa kamba za viunoni au hufungwa ncha ya shati la huyu na la huyu kisha walikuwa wakiongozwa mmoja nyuma ya mmoja na huku wakipigwa mateke na kusukumwa mpaka wakifikishwa Bomani. Huko ikiwa hawatokuwa na cha kulipa basi walikuwa wakihukumiwa na kufungwa. Kutokana na hali kama hizo, ndipo wengi kati ya wananchi wa nchi hizo, khasa kutoka Tanganyika walikimbia kutoka makwao na kuhamia Zanzibar kwa sababu ya kufuata hali njema za kimaisha. Zanzibar hakukuwepo kodi za kichwa wala ubaguzi wa vyooni wala malipo ya mishahara wala wa namna yo yote. Ilikuwa njema atakae naaje.

UBAGUZI UMEANZISHWA ZANZIBAR WAKATI WA SERIKALI YENYE KUJIITA YA "MAPINDUZI" Mara tu baada ya kufika hiyo serikali ya 'mavamizi' katika Zanzibar ubaguzi wa ukabila ulianzishwa. Kila "mrangi rangi" kama walivyokuwa wakiwaita wenyewe, yaani wenye asili za Kiarabu, za Kihindi na za Kingazija walianza kutolewa makazini bila ya kupewa hata haki zao za ufanyaji wa kazi. Mashamba, majumba na hata mabiashara yao yalichukuliwa kwa nguvu na kupewa wageni ikiwa ni tunzo la ukatili na maovu waliyowafanyia wananchi katika nchi yao. Serikali ya 'mavamizi' ya Zanzibar ilitangaza rasmi kupitia vyombo vya khabari vya serikali kukhusu ubaguzi katika Taalimu. Waafrika, wakipasi au wasipasi bali idadi yao ya kuingia katika "Form One" ya "secondary school" ilikuwa ni 77 katika mia (77%), Waarabu 16 katika asili mia (16%), Wahindi 6 katika mia (6%), na Wangazija MMOJA katika mia! (1%). Si hayo tu, bali serikali ya 'mavamizi' imetumia fedha za umma kwa ajili ya kujijengea hospitali yao wao tu Wanachama wa Baraza la Mapinduzi na familia zao na wameita, "Mapinduzi Wing". Vitanda, mabetishiti, foronya za mito, vyombo vya kulia kama sahani, vikombe, visu na nyuma (forks) vyote viliagiziwa kutoka Ulaya. Ilikuwa ikitokea Mheshimiwa kulazwa huko, basi na mkewe alikuwa akihamia huko huko na kulala kitanda kimoja kama kwamba wamo katika siku za fungati! Haya yakitendeka wakati wananchi wanyonge hawana hata dawa mahospitalini! Huo ulikuwa ndio usawa, sio ubaguzi!

ELIMU NA MATIBABU BURE! Tunaambiwa na serikali yenye kujiita ya 'mapinduzi' kuwa elimu na matibabu yameanza kuwa bure kwa wananchi baada ya kupatikana kwa Serikali ya 'mapinduzi'! Huu ni uwongo uliokuwa hauna hata kifuniko. Toka lini elimu na matibabu yalikuwa kwa malipo katika Zanzibar? Tangu kuanzishwa kwa skuli ya serikali na Sayyid Ali bin Hamoud na toka kuanzishwa kwa matibabu katika mahospitali, kamwe hayajapata kuwa ya malipo. Toka kwa kuangaliwa na madaktari mpaka kwa madawa, chakula, na mpaka kulala kwa kutibiwa katika mahospitali kulikuwa bure.

TAALIMU Wananchi na wageni, kuanzia chumba cha kwanza yaani (standard one) mpaka kufikia chumba cha nane (standard eight), masomo yalikuwa bure kwa wote. Sio hivyo tu, kila mwanafunzi alikuwa na deski lake peke yake la kukalia na kila mwanafunzi alikuwa akipewa madaftari ya kuandikia bure, vitabu vya

6 kusomea bure, kalamu za kuandikia bure, vidawa vya wino na wino wake bure hata blotting papers (la kukaushia wino) pia wakipewa bure. Na kila Ijumaa wanafunzi walikuwa wakipewa sabuni za kufulia bure. Skuli za mashamba, wanafunzi walikuwa wakipewa kifungua kinywa kunde na uji kabla ya kuingia katika vyumba vya masomo, bure.

Kuanzia chumba cha tisa mpaka cha 12, na baada ya muda katika miaka ya 1950 kuanzia chumba cha saba mpaka cha 12, wazee walitakiwa wasaidie kitu kidogo katika masomo ya watoto wao. Malipo hayo yalikuwa ya kitu kidogo sana na si kila mzee alikuwa akilipa ada hizo. Wengi sana katika wazee walikuwa hawalipi hata senti moja. Na hao waliokuwa wakilipa, wengi wao walikuwa wakilipa kuanzia Shs. tano mpaka Shs. 20 kwa wingi kila baada ya miezi mitatu au mine. Kabla ya mzee kuwa alipe au asilipe, kulikuwepo taratibu maalumu zilizokuwa zikifanywa. Mzee wa mtoto alikuwa akipelekewa "questionnaire" (karatasi) yenye masuala yaliyokhusu mapato yake, kazi yake na idadi ya watu wake wa nyumbani. Kwa kutaka kuhakikisha uwezo wa mzee huyo, basi akipelekewa waraka huo kwanza Sheha wa mtaa kuhakikisha yale yalioandikwa na akisha Sheha humpelekea Mudiri wake na Mudiri humpelekea D.C. wake. Baada ya khatuwa hizi ndio tena hapo hutolewa uamuzi wa kulipa au wa kutokulipa, na kama kulipa alipe kiwango gani.

Kutokana na mipango kama hiyo, zaidi ya 70 katika mia (70%) ya wazee watoto wao walikuwa wakisoma bila ya kulipiwa kitu chochote na kiasi cha 20 katika mia (20%) walikuwa wakilipiwa kitu kidogo na kiasi cha 10 katika mia (10%) ndio waliyokuwa wakilipiwa idadi kamili ambayo ilikuwa chini ya Shillingi 200, kwa mwaka mzima. Wengi waliokuwa wakilipa kima hicho, walikuwa ni wazee wenye asili za Kihindi. Wanaoitwa Waafrika na wanaoitwa Waarabu hayo yalikuwa si maji yao. Muhimu katika hayo si kulipa au kuto kulipa, muhimu ni thamani (quality) ya elimu iliyokuwa ikipatikana siku hizo, jee leo inapatikana? Hilo ndilo suala muhimu la kujiuliza na kulizingatia. Ikiwa hiyo isemwayo leo kuwa elimu bure, na imekuwa wanafunzi hawana madeski ya kukalia, hawana vitabu vya kusomea, wala chochote cha kusomea, bali zaidi hawana hata walimu wenye ujuzi wa kusomesha; basi bure kama hiyo ni "bure ghali". Kwa hiyo bure, basi watoto wetu leo wametokwa na vibyongo kwa kuinama wakati wa kuandika. Wakirejea kutoka maskuli utadhania wanatoka kuchimba makaburi kwa mavumbi yalivyo watapakaa kwa kusota chini.

Elimu bure! Wanafunzi wakipotezewa wakati wao wa masomo kwa kuchezeshwa ngoma za sindimba na kuimbishwa majimbo ya kanisani ati huitwa, "Kwaya". Kuanzia Disemba wanafunzi walikuwa wakianzishwa mazowezi ya kucheza ngoma na kuimba hizo kwaya pamoja na magwaride kwa ajili ya kujiweka tayari kwa sherehe za hayo yenye kuitwa 'mapinduzi' katika mwezi wa Januari. Wakimaliza tu, hawawahi hata kushusha pumzi wanangojewa kwa sherehe za kuasisiwa kwa Chama cha AfroShirazi, 2 2 (February 2). Wakimaliza tu, hawawahi hata kunywa maji, wanazolewa tena kwa mazowezi ya sherehe za "Muungano" April 26. Hawawahi hata kukaa kitako, wanabebwa tena kwa mazowezi ya Sikukuu ya Wafanyakazi "May Day". Hapo hupumua kidogo kisha huzolewa tena kwa mazowezi ya kusherehekea, "Saba Saba", July 7. Hawawahi hata kwenda chafya, hunyakuliwa tena kwa mazowezi ya sherehe za "Elimu Bure"! Septemba. Wakimaliza hapo wanazolewa tena kwa mazowezi ya sherehe za "Uhuru wa Tanganyika" Desemba. Ukiangalia utaona kuwa mwaka mzima badala ya watoto wetu kusomeshwa, walikuwa wakichezeshwa ngoma, kuchezeshwa magwaride na kuimbishwa manyimbo ya kanisani. Bado ati husemwa ELIMU BURE, kweli bure, lakini BURE KWA MJINGA!

Kwa kweli kiwango cha elimu Zanzibar kimeanguka kiasi kikubwa sana, kiasi cha kuitwa, "chini ya sufuri". Imefika hadi leo kuwa mwanafunzi aliyemaliza hicho wanachokiita, "kidato cha nne" (Form IV), ukimwambia aandike barua ya kuomba kazi kwa lugha ya Kiingereza, anashindwa hata kujaribu kuandika na ikiwa atajaribu, basi kichwa huwa miguu na miguu huwa kichwa. Hapo yalipokuwepo masomo ya kweli na walimu wa kweli wenye kufunzwa wakafunzika katika fani ya kusomesha, wanafunzi waliyomaliza chumba cha nane ilikuwa wakiandika Kiingereza, utawavulia kofia.

MATIBABU Tukija katika matibabu, ndiko tutakako kukuta kumeporomoka vibaya kabisa. Hospitali hazina madawa, hazina vifaa vya matibabu, hakuna hata vitanda na mabetishiti ya kutosha. Wagonjwa wanatakiwa wakenda kutaka matibabu, wachukue zana zao wenyewe tokea pamba, gauze, vijembe vya kunyolea na

7 hata chupa za "Drips" pia wende nazo. Shuka za kutandika vitandani, mito na foronya zake na nguo za kujifunikia wakati wa kulala vyote hivyo lazima wendenavyo mwenyewe; kama si hivyo basi hatapata matibabu. Ubavuni mwao wakitazama wanaiyona "Mapinduzi Wing" bwana na bibi wanaingia na kutoka! Tokea miaka yalipoanzishwa mahospitali ya serikali Zanzibar, matibabu yalikuwa bure kwa wote. Kwa wananchi, kwa wageni na hata kwa wapita njia. Kuangaliwa na daktari kulikuwa bure, dawa bure, ukilazwa kwa ajili ya matibabu, bure. Na hospitali zilikuwa hospitali kweli kwa kila kitu. Madawa ya kila maradhi yalikuwepo. Madaktari wenye ujuzi wa kazi zao, waliosomeshwa wakakhitimu walikuwepo wa kutosha. Sivyo kama ilivyo hivi sasa, wauguzaji (Staff Nurses) ndio madaktari, tena wa kufika kuuchana na kuupasua mwili wa binadamu! Kwenye nchi yenye sheria, pindi likitokea lolote, basi ushahidi wa watu kama hao, hauwezi kukubalika katika mahakama za sheria, kuwa ni ushahidi wa kidaktari. Lakini ndio kama ule msemo wa Kiswahili, "likikosekana la mama, hata la punda hufaa".

Ni kweli kulikuwepo katika hospitali kuu ya serikali sehemu maalumu za kulala wagonjwa wa kulipa. Lakini hayo yalikuwa kwa kupenda kwake mwenyewe huyo mgonjwa. Malipo yenyewe yalikuwa kwa watu wenye kufanyakazi za serikali, walikuwa wakilipa Shs. sita kwa siku, na waliyokuwa hawafanyi kazi za serikali, walikuwa wakilipa Shs.12 kwa siku. Kwa hakika hakukuepo tafauti kubwa baina ya huko kwa malipo na kwa bila ya malipo. Tafauti ziliyokuwepo baina ya sehemu za kulala wagonjwa kwa malipo na sehemu za bure ni za nyongeza tu, sio kwa ya lazima. Kwa mahitajio ya kimatibabu kulikuwa hakuna tafauti hata kidogo. Tafauti zenyewe zilikuwa kama hizi: Katika upande wa malipo, wagonjwa walikuwa wakipewa panjama za kulalia, vyakula vyao wakiletewa katika sinia na sahani zao zilikuwa za kaure na walikuwa wakipewa chai ya kitandani (bedtea) na pia walikuwa wakipewa chai ya alaasiri (afternoon tea). Pia walikuwa wakipewa taula ya kujifutia maji baada ya kukoga. Chakula kikubwa kilikuwa wali na mchuzi wa nyama na kibakuli cha puding.

Upande wa wagonjwa wa bure, wao walikuwa wakiletewa vyakula vyao bila ya kutiliwa katika sinia na sahani zao zilikuwa za senti (aluminium), chai walikuwa wakitiliwa katika makopo ya senti. Hapakuwa na tafauti kubwa ya chakula isipokuwa wao badala ya kupewa chai ya kitandani, wakipewa uji. Wagonjwa wote wa kulipa na wa bure walikuwa wakipewa matunda na mboga. Na ikiwa mgonjwa ameandikiwa na daktari chakula maalumu kutokana na maradhi yake, basi alikuwa akipewa chakula hicho (bila ya malipo) sawa sawa na mgonjwa aliyekuwa katika sehemu za malipo ikiwa maradhi yao ni ya namna moja. Madaktari na wauguzaji walikuwa ndio hao hao na matibabu yalikuwa ndio hayo hayo kwa wote, wa kulipa na wa bure.

Leo tuambiwayo kuwa matibabu bure, mgonjwa akenda hospitali baada ya kuangaliwa na daktari (pengine na muuguzaji "nurse" tu) na akaandikiwa dawa, akifika kwa watoa dawa jawabu analolipata ni kuwa, "dawa hizi hazipo. Kanunue nje"! Jawabu kama hizo ni za kila siku. Ukenda kuwaangalia wagonjwa waliolazwa, ukianza tu kupanda ngazi, unakaribishwa na harufu za mikojo na za mashonde kutoka vyooni. Hospitali haina maji ya kutosha. Ukiingia katika vyumba vya kulala wagonjwa, unawakuta mapaka wanacheza foliti kwa jinsi ya uchafu uliomo ndani. Makunguru wanaruka huku na huku humo vyumbani, wanapitia dirisha hili na kutokea jengine. Sakafu zinanata kwa uchafu. Sasa watizame hao wagonjwa namna walivyo lala humo vitandani. Vichekesho khasa. Wengine wamejifunika kanga za kisutu, wengine za mkeka, wengine za visima, na za namna mbali mbali. Utadhania watoto wa kizamani walipokuwa wakitiwa kumbini (kutahiriwa) Mabetishiti yaliyotandikwa vitandani kwa ilivyokuwa kila mmoja amekuja na lake, basi, huyu katandika jeupe la mfuto, huyu lililofumwa tausi na huku limeandikwa KARIBU MGENI, na kwa kipembeni ya chumba utaona mengine yameandikwa FURAHA YA BIHARUSI, na jengine limeandikwa kwa maandishi ya nakshi SINA MWENGINEWE, au MAPENZI YETU YA UTOTONI, au MIMI NA WEWE HATULISHANI YAMINI, mradi huwa rangi rangire. Hospital zimepoteza jina na thamani yake kwa kila upande, haziwezi hata kidogo kutowa huduma zitarajiwazo.

Hiyo ndio hali ya hayo yanayoambiwa matibabu ya bure! Lakini haya yote yanaowapata ni wananchi wa kawaida tu. Ama wenyewe wakina fulani na fulani pamoja na watoto wao, wao bukheri wa sururu hata hawana khabari nayo wala hawayasikii licha kuyaona. Khalafu kwa kuudanganya umma ati husema, "Tumeondoa serikali ya kisultani na kibwanyenye!". Wakati wa huo Usultan, Mfalme wa nchi hajapata kuwa na hospitali yake peke yake. Yeye pamoja na ukoo wake wakenda katika hospitali hiyo hiyo wanayokwenda watu wa kawaida. Aliyekuwa Mfalme wa nchi, Seyyid Abdulla Bin Khalifa Bin Haroub,

8 alipopata maradhi, alilala katika hospitali hiyo hiyo na alifanyiwa operesheni katika hospitali hiyo hiyo wanayotibiwa watu wa kawaida.

Wakoloni wa Kiingereza waliweka sehemu yao ya kutibiwa waliita "European Wing". Kutokana na makelele ya wananchi, khasa kutokana na makala yaliyokuwa yakiandikwa katika gazeti la wananchi la "Mwongozi", sehemu hiyo ilibadilishwa jina na badala ya kuitwa "European Wing", ikaitwa "West Wing". Kutokea wakati huo ilikuwa wazi kwa yoyote mwenye kupenda kwenda katika sehemu hiyo ikiwa yutayari kulipa ada zilizowekwa. Leo baada ya mapinduzi ya kuleta usawa na kuondoa usultani na ubwanyenye, mheshimiwa akiumwa na mdudu upande basi mbio anachukua ndege anakwenda zake Uingereza au Ujarumani kwa matibabu. Ikiwa matibabu yapo nchini bure, mbona wao wanayakimbia na kuyafuatia ya malipo, tena katika nchi za n'gambu na kwa kutumia pesa za wanyonge kwa matibabu yao? Sasa ipi inayostahiki kuitwa serikali ya kibwanyenye? Hii ya waheshimiwa waliyojitenga mbali na umma au ile ya waliyokuwa wakiishi pamoja na umma? Mwenye macho haambiwi tizama! Unaweza kuwadanganya baadhi ya watu baadhi ya siku, lakini huwezi kuwadanganya watu wote siku zote.

HALI ZA MAISHA Matunda makubwa waliyopata wananchi wa visiwani wa Unguja na Pemba kutokana na hayo yenyekuitwa, 'mapinduzi', ni shida za kimaisha katika kila upande. Vyakula havinunuliki, nguo hazikamatiki. Mradi wananchi wamo katika kuhiliki kwa maisha yalivyo magumu. Vijana wamekuwa wazee kwa shida. Sokoni kunaitwa, "Uwanja wa Mapambano". Na kweli, ukenda sokoni basi upanie kweli kweli kwani fungu la mihogo sita ikiwa huna Shs.200, hulichukui. Mkungu wa ndizi ya mtwike, Shs.3000, nazi moja Shs.50, pilipili za mchuzi fungu Shs.30 mpaka 50, kicha cha mboga ya mchicha kuanzia Shs.70 mpaka kuteremka Shs.50. Fungu la machungwa sita yaliyotukuka kidogo, Shs.200 na yaliyokuwa madogo, Shs.100. Takriban watu wote wamekuwa Mabaniani, hawali nyama kwani kilo ya nyama ni Shs.1200!

Mishahara ya wafanyakazi wa serikali ya kiwango cha chini ambao ndio wengi, ni Shs.7000! Mtu, yeye na mkewe na watoto wawili, inambidi, tena kwa kujibana, atumie Shs.1000 kwa siku kwa chakula cha asubuhi na cha mchana. Kwa hivyo inamlazimu apate Shs.30,000 kwa mwezi. Ikishakuwa mshahara wake ni Shs.7000 kwa mwezi, hizo 23,000, atazipata wapi? Kutokana na hali kama hizo za kimaisha, ndio utaona kuwa toka waongozi wa serikali mpaka wafanyajikazi wa chini wanaishi kwa magendo. "Corruption" (rushwa) katika nchi imefika katika kilele cha juu kabisa. Tunakubali kuwa ulimwengu wote umeingiwa na shida za kimaisha lakini huwepo sababu maalumu ambazo kwa Zanzibar Alhamdulillahi hazijatokea na Inshallah zisitokee. Mara nyingi watu hukutwa na shida za kimaisha katika nchi zao kwa kutokana na hali za mabadiliko kama kutokupata mvua, kutokea mifuriko ya maji, kutokea moto wa misituni, kutokea mitetemeko ya ardhi au vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kama nilivyo tangulia kusema shida kama hizo, Alhamdulilah hazikufika katika nchi yetu.

Sasa kipi kilicho sababisha taabu na dhiki zote hizi za kimaisha? Hili ni suala ambalo kila mwananchi lazima ajiulize, ikiwa tutajiuliza kwa insafu basi jawabu halitokuwa zito kulipata. Mpaka Januari 11, 1964, pishi moja ya mchele ilikuwa baina ya Shs. nne mpaka tano. (Pishi moja ni sawa na kilo tatu). Ina maana ya kuwa kilo tatu za mchele zilikuwa Shs. nne mpaka tano. Na zilikuwepo kabila mbali mbali za mchele yaani namna kwa namna. Neema zote zilizokuwepo Visiwani Zanzibar, Mwenyezi Mungu ameziondosha kwa kutokana na maovu yaliyoletwa na hayo yenye kuitwa "Mapinduzi". Ni kama wale watu waliyo mchinja bata aliyekuwa akitaga mayai ya dhahabu. Dhulma zilizofanywa za kupoteza roho za viumbe wa Mwenyezi Mungu, bila ya kuwa na kosa lolote la kisheria, mali za watu zimechukuliwa kwa nguvu kutokana na wenye haki nazo. Natija ya hayo imekuwa leo sehemu kubwa sana ya vyakula vinavyouzwa masokoni vinatokana na ardhi zilizoporwa.

Kwa hivyo, wananchi wanalishwa vyakula vya haramu. Na wale waliokuwa wamenunua majumba ambayo wanajua ni yenye kutokana na kuibiwa kutoka kwa wenye haki nayo, basi wajue kuwa Sala zao wanazo zisali katika majumba hayo, Mwenyezi Mungu hazikubali. Na ni hivyo hivyo, kwa wale walionunua mashamba yaliyoporwa kutokana na wenye haki nayo, basi na wao wajue kuwa vyakula wanavyo vivuna katika mashamba hayo ni vyakula vya haramu. Kwa hivyo, wao wanakula haramu na wakiviuza, wao, ndio watao chukua dhima ya kuwalisha wenziwao vyakula vya haramu. Kutokana na

9 hali kama hizo zilizokuwa zimefanyika katika nchi, ndio ikawa kila lifanywalo haliwi. Na ikiwa hapatofanywa TOBA ya kweli, basi nawaje wowote wataokuja, ikiwa wataendelea na mwendo wa kurithi mwendo wa kidhalimu waliyoukuta, basi hapana litalo weza kutengenea ila itakuwa kuziba kiraka hapa na kupasuka pengine. Kauli ya Mwenyezi Mungu kattu haiwezi kwenda kombo. Mwenyezi Mungu Anasema kuwa: "Hazidi mwenye kudhulumu illa khasara".

NEEMA ZILIKUWEPO Katika huo wakati unaoitwa wa kikoloni, Serikali ya Zanzibar ilikuwa ikiendesha mambo yake yote kama kujenga maskuli, mahospitali, mabarabara, kununua meli za usafiri, pamoja na kuyahudumia na kulipa mishahara ya wafanyakazi tokea wa kigeni mpaka wananchi. Na hao wafanyakazi wa kigeni ambao wengi wao walikuwa Wazungu, basi juu ya mishahara yao walikuwa wakipewa posho maalumu (Inducement Allowances), pia walikuwa wakilipiwa nauli za kuwaleta na kuwarejesha na za wakati wa likizo zao. Yote hayo na mengineyo yakifanywa kutokana na mapato ya ushuru tu wa forodha.

Serikali hii yenye kujiita ya "Mapinduzi", ni wao peke yao ndio wenye kununua bidhaa muhimu zote za nchi kama vile, karafuu, mbata na pilipili hoho kutoka kwa wananchi kwa bei wazitakazo wao wenyewe na wakaziuza kwa bei ziliopo katika masoko ya ulimwengu. Isitoshe, serikali hii haina gharama za kuwalipa hao Wazungu kama ilivyokuwa hapo zamani, sasa ilikuwaje hata ifike serikali kuwa haina fedha hata za kuwalipa mishahara wafanyakazi wake wa kienyeji? Hapana shaka sababu kubwa ya hayo ni hii dhulma iendeleayo hadi hii leo, uwendeshaji mpotofu, ukiongozwa na siasa ya husda na uroho wa madaraka na kipato, siasa ya "Chukuwa Chako Mapema"! (CCM). Siasa ambayo immefanya mwananchi kuwa hana uwezo wala itibari yoyote katika nchi yake. Kwa hali za kimaisha nchini mwananchi hawezi kukaa akatua na kufikiri na kupanga juu ya maendeleo ya nchi yake, yeye anafikiri juu ya cha jiyo tu! Siasa mbovu hii iliopangwa makusudi imemzuiliya na kumnyima mwananchi uwezo na njia za kujiendeleza, laa si katika kimaisha, walaa si katika kiutamaduni au kielimu. Inatilia nguvu mizizi ya siasa yake ile ile ilioanziwa, nayo ni "Mwenye Elimu ni Aduwi"

KUANZA HARAKATI ZA SIASA Kabla ya Serikali ya Kiingereza kuiingiza Zanzibar chini ya Himaya yake, Zanzibar ilikuwa ni Dola kamili iliyokuwa ina shughuli zake (ikiamiliana) na ulimwengu wote. Mara tu Muingereza alipoitia Zanzibar katika makucha yake mnano mwaka 1890, kila jambo kubwa na dogo lilikuwa lazima liamuliwe kutoka Uingereza. Mfalme wa nchi alifanywa kuwa ni alama tu ya Dola, hakuwa na uwezo katika kukata shauri juu ya uwendeshaji wa nchi. Kama ilivyo kawaida ya wakoloni popote ulimwenguni wanapotawala, lazima watumie mbinu za kuwagawa wananchi (ili waendeleze utawala wao) kutokana na hali za namna fulani ziliopo katika nchi. Ikiwa kwa njia za kidini, ukabila, urangi, utajiri, uwezo wa kimaisha na hata umadhehebu.

Katika Zanzibar Muingereza alitumia njia za kuwagawa wananchi kwa kutumia asili za makabila yao. Aliwafanya wenye asili za Kiarabu wajione kuwa wao tu ndio wenye haki za utawala kwa vile ilivyokuwa Mfalme wa nchi anatokana na asili zao. Aliwafanya Washirazi yaani, Wahadimu, Watumbatu na Wapemba wajione kuwa wao tu ndio wenye kila haki za nchi kwa vile ilivyokuwa wao ndio waliyokwenda kuwaita Waarabu (kutoka kwao Oman) kuja kuwasaidia kumuondoa Mreno. Aliwafanya Waafrika (weusi) wajione kuwa wao tu ndio wenye kusitahiki utawala wa Zanzibar kwa vile Zanzibar imo katika Bara la Afrika. Na alichukua uchumi wote wa nchi na kuuweka katika mikono ya wenye asili za Kihindi kuwa wao ndio raia wa Kiingereza sahihi wa tangu asli, kwa uwezo wao wa kimaisha wakajiona kuwa wao ni wabora kuliko wengine katika nchi. Kutokana na hali kama hizo, wananchi walianza kujigawa mafungu kwa mafungu na walianza kufungua Jumuiya zao za Kikabila. Waarabu walifungua yao, Washirazi walifungua yao, Waafrika walifungua yao na Wahindi walifungua yao na Wangazija wakafungua yao. Na ndani ya hizo hizo, zilijitokeza zengine na kila moja ilikuwa ikijitapa kwa upande wake.

Kwa muda mkubwa jumuiya hizo zilikuwepo katika nchi na hazikuweza kupata wala kufanya lolote kwa maslahi ya nchi. Kubwa walilokuwa wakilipata ni kualikwa chai ya alaasiri kwenye Bustani ya Jumba la Balozi wa Kiingereza, na kualikwa katika siku ya kuzaliwa Mfalme wa Kiingereza na Mfalme wa nchi na kualikwa kutembelea manuwari za Kiingereza zinapofanya ziara kuitembelea Zanzibar. Katika miaka ya

10

1920 Muingereza katika njama zake za kuzidi kuwafarikisha wananchi ili aendelee kuwatumia katika kuendeleza utawala wake, alianzisha kuwateuwa (appoint) wananchi kwa kuwatia katika Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council) kwa njia za kikabila. Aliwateua hatimaye Waarabu wane, Waafrika wane, Wahindi watatu na Mzungu mmoja. Na upande wa Serikali walikuwemo wakurugenzi wa idara wa Kiingereza kutoka idara mbali mbali za serikali walioteuliwa vile vile, hao walizidi kwa wingi katika baraza hilo kuliko raia. Mwendo huo uliendelezwa kwa muda wa miaka 28 na hapakuweza kupatikana lolote la maslaha ya nchi. Miaka nenda miaka rudi, nchi haikuwa na maendeleo yoyote kukhusu mabadiliko ya Katiba itayo wawezesha wananchi kuendesha wenyewe shughuli za nchi yao bila ya kuingiliwa na yoyote.

Katika mwaka 1953 na 1954, Jumuiya ya Waarabu (Arab Association) iliamua kumpelekea Balozi wa Kiingereza madai ya kutaka yaletwe mabadiliko ya Katiba yatayo wawezesha wananchi wa Zanzibar kuchagua wajumbe wao wa kuwapeleka katika Baraza la Kutunga Sheria kwa njia ya uchaguzi wa Kura Moja Kwa Mtu Mmoja (One Man One Vote). Na miongoni mwa madai yao, walidai uondolewe mtindo wa kuwateua wananchi kwa njia za kikabila katika kila jambo la nchi. Pia walitaka baada ya kupatikana kwa matokeo ya uchaguzi huo, paanzishwe mazungumzo ya taratibu za kupatikana kwa Uhuru kamili wa Zanzibar.

Balozi wa Serikali ya Kiingereza aliyekuwepo Zanzibar wakati huo akiitwa Mr. Renkin. Balozi huyo alikataa hata kuyatia maanani madai hayo. Jumuiya ya Waarabu walipoona hawakuweza kupata natija yoyote katika madai yao, bali hata hayakuzingatiwa, waliamua kuanzisha mgomo kwa kuwazuia wajumbe wao kushiriki katika vikao vya Baraza la Kutunga Sheria na katika vikao vya Kamati za Mabaraza yote waliyoteuliwa kushiriki. Mgomo huo ulichukua muda wa miezi 18 bara bara. Jambo la kulizingatia katika suala hili ni kuwa, madai hayo kutokana na Jumuiya ya Waarabu hawakuyafanya kwa maslahi yao binafsi zao, bali kwa maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari wote bila ya kujali asili za makabila yao. Haya yanajithibisha zaidi kwa vile ukiangaliya idadi ya hao waliyokuwa wakiitwa (au wanaoitwa) Waarabu katika Zanzibar, walikuwa ni kiasi cha 16 katika 100 (16%). Juu ya hivyo waliamua kuziachilia mbali nyadhifa walizopewa, sio hivyo tu, bali kutoa muhanga nafsi zao wakiweka mbele maslahi ya nchi. Bahati mbaya hawakupata kuungwa mkono na wananchi wenziwao wenye asili za makabila mengine juu yakuwa walizungumza nao na waliwataka washirikiane katika madai hayo. Mmoja kati yao (alioteuliwa kushiriki katika Baraza la Kutunga Sheria akiwa ni mwenye asili ya Kiarabu), alipinga uamuzi wa Jumuiya yake na alihudhuria katika kikao cha Baraza la Kutunga Sheria wakati wenzake walipokuwa wamesha amua kugomea. Matokeo yake, alitokea mwananchi mwenye uchungu na nchi yake na kumpiga bwana huyu kwa visu. Kwa bahati mbaya alikufa kutokana na pigo hilo.

SHEIKH ALI MUHSIN KWENDA NCHI ZA ULAYA IKIWEMO NA UINGEREZA KUPIGANIA UCHAGUZI WA "COMMON ROLL" (MTU MMOJA KURA MOJA). Wakati Jumuiya ya Waarabu ilipokuwa katika hekaheka za mgomo wao wa kuto kushiriki katika Mabaraza yote ya Serikali kwa madai ya kutaka papatikane mabadiliko ya Katiba yatayo wawezesha wananchi kuchagua wawakilishi wao wa Baraza la Kutunga Sheria kwa njia ya uchaguzi wa "One Man One Vote" na kusita kuteuliwa kutokana na asili ya makabila yao, mwananchi mwenzao mwenye uchungu wa nchi yake alifunga safari (kwa gharama zake mwenyewe) kwenda kupigania maslahi ya nchi yake, akiendeleza madai ya wananchi wenziwe huko nyumbani. Wakati Sheikh Ali Muhsin alipokuwa katika hekaheka hizo huko Uingereza, alikutana na Seyyid AbdulRahman Mohammed (Babu) na waliweza kushirikiana katika juhudi hizo. Katika harakati hizo Sheikh Ali alikutana na waongozi mbali mbali wa kisiasa na wengi wao walimshajiisha juu ya kuendelea na juhudi za ugombozi wa nchi yake na walimpa kila msaada (moral support). Huko Uingereza alipata kuzungumza na wakuu wa Serikali ya Kiingereza, wakuu wa upande wa Upinzani na wakuu wa Vyama vya Wafanyakazi. Pia alikutana na wakuu wa vyama na jumuiya mbali mbali zenye kupigania kuondoka kwa ukoloni katika Afrika na katika sehemu zengine za ulimwengu.

KUASISIWA HIZBULWATTAN (ZANZIBAR NATIONALIST PARTY) Wakati Sheikh Ali Muhsin akiwemo katika safari zake huko nchi za Ulaya, huko nyumbani walichomoza wananchi wengine waliokuwa nao na ghera na mapenzi ya nchi yao. (wote, isipokuwa mmoja tu kati

11 yao Sheikh Abdalla Mahmoud walikuwa si Waarabu) Wananchi hao walikutana kuzingatia na kutafakari juu ya kupotea kwa nchi yao kutokana na mbinu za mkoloni za kuwagawa wananchi kwa kutumia asili za makabila yao. Wananchi hao waliibuka na amuo la kuanzisha Umoja wa Wananchi wa Unguja na Pemba. Umoja ambao kila raia wa Zanzibar atastahiki kuwemo bila ya kujali asili ya kabila yake wala Imani ya Dini yake, la umuhimu ni URAIA wake. Hichi kilikuwa ndio chama cha kwanza na pekee katika nchi kuasisiwa kwa kufuatia misingi ya Uwananchi.

Wananchi waasisi hao walikuwa ni, Sheikh Vuai Kiteweo, Sheikh Miraj Shaalab, Maalim Zaid Mbarouk, Maalim Maksud Fikirini, Maalim Mwandoa Khamis, Maalim Wazir Ali bin Maalim, Sheikh Haji Hussain Ahmed, Sheikh Othman Soud, Sheikh Abdulla Mahmoud Kombo (wa Makunduchi), Sheikh Ramadhan Tosir (Ramadhan Madafu), Maalim Hija (wa Ndijani), Sheikh Ame, Sheikh Abdulla Mali, Sheikh Haji Kombo (wa Kiboje), Sheikh Abdalla Mahmoud na wenziwe wachache. Kwahivyo wale wenye kusema na kutangaza kuwa Hizbu (ZNP) iliasisiwa na Waarabu au kilikuwa chama cha Waarabu, hapana shaka wanakosea, amma kwa kutokujuwa ukweli ulivyo au wanasema hivyo kwa makusudio ya kutafuta maslaha yao. Ukweli na hakika ilivyo ni kuwa Hizbu haikuasisiwa na Waarabu wala hakijapata kuwa Chama cha Waarabu. Na kama Hizbu kingelikuwa ni Chama cha Waarabu, basi kisingeweza kupata ushindi katika chaguzi zilizofanyika za (One Man One Vote) kwani idadi ya hao wenyekuitwa Waarabu nchini ilikuwa ndogo; kwahivyo idadi yao hiyo haingaliwezesha kukipa (hicho kisemwacho ni chama chao) voti za ushindi.

Madai hayo ni miongoni mwa maneno na mbinu za kufitinisha na kuwagawa wananchi kwa kuuwogopa umoja wao. Hapana shaka zimetungwa na wakoloni na kuimbwa na vibaraka vyao, kwa maslahi yao. Mabwana hao tuliowataja hapo juu wakiwa ndio waasisi wa Chama cha HizbulWattan, wao ndio waliyomuendea Sheikh Ali Muhsin nyumbani kwake baada ya kurejea kutoka safarini na kumueleza kukhusu kuasisi kwa chama chao na nini dhamiri zilizo wapelekea kuasisi chama hicho. Baada ya kumueleza, walimtaka na yeye awaunge mkono kwa kujiunga katika chama. Sheikh Ali Muhsin alipoona kuwa hayo wayatakayo wananchi wenzake ndio hayo hayo ayatakayo na kuyapigia mbio daima basi, hapo hapo aliamua kujiunga na kushirikiana nao. Baada yakujiunga, waasisi hao walimtaka Sheikh Ali Muhsin aanze kuzungumza na nduguze wenye asili za Kiarabu bali na kila anaefahamiana nae ili wajiunge na wananchi wenziwao. Sheikh Ali aliupokea na kuanza kuutekeleza ujumbe huo. Miongoni mwa wa mwanzo (kati ya hao wenye kuitwa Waarabu) kujiunga na Umoja huo ni, Sheikh Badr Muhammed Barwani, Sheikh Ahmed Seif Kharusi, Sheikh Amour Zahor Ismaily, Sheikh Ali Ahmed Riyamy Sheikh Nassor bin Isa Ismaily na Sheikh Ahmed Khalfan Naamani haikuchukuwa muda ila nao walijiunga.

WAKOLONI DHIDI YA HIZBU, UHURU NA UMOJA WA ZANZIBAR Serikali ya kikoloni ilipoona Umoja wa Hizbu umesimama na kila siku unazidi kuungwa mkono na wananchi wa kila pembe na kila aina, walizidi kuogopea maslahi yao. Kwa kuhifadhi maslahi yao walianza kuuandama Umoja huo HizbulWattan nje ndani, usiku na mchana kwa kuwatumilia baadhi ya wananchi wafanyakazi wa Idara ya Utawala khasa Mamudiri na Masheha. Vitumishi hivyo vilifunga njuga na kuingia mitaani na viamboni katika juhudi za kuuvunja Umoja huo wa HizbulWattan. Kwa kiasi fulani hapo mwanzoni waliweza kufanikiwa, kwani walitumilia mbinu za kuwatisha wananchi; baadhi kwa kuwaambia kuwa, chama hiki azma zake ni kuleta michafuko katika nchi na kwa baadhi ya wananchi wakiwaambia kuwa chama hiki kinataka kumuondoa Mfalme. Kila mmoja wakimpigia mdundo waliofikiria kuwa utaweza kumshitusha na kukiepuka chama hiki. Bali wananchi hawakuchukuwa muda illa waliweza kuzielewa mbinu zao hizo na kuwaepuka na badala yake kuzidi kuungana na wananchi wenziwao.

MAKAO MAKUU YA HIZBU Kabla ya uchaguzi wa mwanzo wa "Common Roll Election, yaani, "Mtu Mmoja Kura Moja", katika Zanzibar mnamo mwaka 1957, mwananchi, mzalendo Sheikh Mahmoud wa Mtendeni aliyekuwa mwishoni akijishughulisha na utengezaji wa saa, alijitolea kwa kukipa Chama jumba lake la ghorofa moja lililokuwepo mtaa wa Mwembetanga kuwa ni Makao Makuu ya Chama. Alilitoa jumba hilo bila ya kupokea kodi hata senti moja. Baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwanzo wa 1957, Hizbu iliyaondoa Makao Makuu yake kutoka Mwembetanga na kuhamia Mkunazini karibu na Msikiti Gofu. Baada ya kuwepo hapo kwa muda, ndio iliweza kununua jumba lake wenyewe katika mtaa wa Darajani

12 na kulifanya ndio Makao Makuu ya Chama. Jumba hilo, baada ya 'Mavamizi' ya Januari 12, 1964, liliporwa na Serikali ya 'Mavamizi' na kufanywa Makao Makuu ya AfroShirazi Youth League. Kama ilivyo hali ya majengo mengi mengineo humo nchini, jumba hilo limetupwa bila ya matengenezo wala matumizi ya faida. Na linaachwa kubomka pole pole. Haya sio ajabu, bali haya yanazidi kuthibitisha jinsi hao viongozi wa Zanzibar walivyokuwa hawana uchungu na Nchi bali na chochote cha nchi.

HIZBU KUMLETA ZANZIBAR SEYYID ABDULRAHMAN (BABU) Miezi michache kabla ya uchaguzi wa mwanzo wa 1957, Chama cha HizbulWattan kilimleta Babu Zanzibar ili ashirikiane na wananchi wenziwe katika harakati za kisiasa. Baada ya kufika Zanzibar, Hizbu ilimteuwa kuwa Katibu Mtendaji wa Chama (Excutive Secretary). Kutokana na maarifa aliyokuwa nayo katika mipango ya kuendesha chama cha kisiasa, Babu baada ya muda mdogo alianzisha Umoja wa Vijana (Youth Own Union) (YOU). Kwa msaada na ushirikiano wa waongozi wenziwe na wananchi Babu alifanya kazi kubwa katika kukijenga Chama cha Hizbu ndani na nje ya nchi. Lakini, kwa bahati mbaya, kama alivyokuwa hodari katika kukijenga, ndivyo alivyojaribu kwa uhodari au ilivyo khasa kwa kiujanja kutaka kukibomoa baada ya kushindwa kufikilia maslahi yake binafsi kwa kukitumilia chama. (Baadae tutaeleza aliyoyatenda katika kukibomoa chama na kuifisidi nchi).

Alipojiunga Sheikh Ali Muhsin katika chama cha HizbulWattan Zanzibar Nationalist Party (ZNP) aliwapa shauri wakuu wa Chama kumtaka Babu achukue mafunzo katika kuendesha chama na baadae aje asaidie katika uendeshaji wa ZNP. Wakuu wakapendezewa na shauri hiyo, na Babu akawafik. Sheikh Ali hapo tena aliiomba Labour Party ya huko Uingereza kwa kupitia kwa (wasta wa) Mr. John Hatch na Mrs. Eirene White M.P. na Labour Party ikakubali kumpokea Babu kwa mafunzo. Mafunzo hayo yalikuwa ya muda wa miezi sita. ZNP (Hizbu) ililipia gharama zote za kimaisha kwa muda huo na za safari. Katika muda huo pia aliendelea kulipwa mshahara akiwa ni Executive Secretary wa Chama ZNP. Utaona dhahiri kuwa imani ya Hizbu juu ya elimu na maarifa haikufungika sehemu mmoja tu, bali ilikuwa ni kwa kila upande. Hizbu iliamini kuwa uwongozi mwema wa chama na nchi utapatikana kutokana na watu wenye ujuzi na maarifa, kwa hivyo iliona umuhimu wa kumpatia mafunzo na elimu ifaayo Katibu Mtendaji wake khasa, na wengine wafuatie.

NATIJA YA SAFARI YA SHEIKH ALI MUHSIN Kama tulivyoeleza hapo mwanzoni kuwa Sheikh Ali Muhsin alizitembelea baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na Uingereza kwa ajili ya kugombania kupatikana kwa mabadiliko ya Katiba ya Kuanzishwa kwa uchaguzi wa "Common Roll" yaani "One Man One Vote" katika Zanzibar. Natija ya safari hiyo, Serikali ya Kiingereza, ilimleta Zanzibar Mr. Coutts akiwa ni mchunguzi juu ya maendeleo ya Katiba. Mchunguzi huyo alifika Zanzibar kati ya mwaka wa 1956. Chama cha Hizbu kilifanya maandamano makubwa kwa kumpokea Mr. Coutts hapo kiwanja cha Ndege cha Kiembe Samaki siku aliyofika Zanzibar. Waandamanaji walichukuwa mabango yaliyokuwa yameandikwa:

"TUNATAKA UCHAGUZI WA ONE MAN ONE VOTE" "TUNATAKA UHURU WA NCHI YETU" "TUMECHOKA KUTAWALIWA'' ''TUNAPINGA "UBAGUZI WA RANGI NA WA UKABILA"

Mjumbe huyo alipokuwa nchini alikutana na wananchi pamoja na wakaazi mbali mbali wa nchini. Alionana hata na watu binafsi. Na alipokea risala (za maandishi na za mdomo) kutoka vyama mbali mbali vya kikabila na vya kidini. Chama cha Hizbu nao walionana na mjumbe huyo na walimkabidhi risala yao yenye kutilia nguvu matakwa yao, matakwa ambayo ndio msingi wa ujumbe wake wa kuja Zanzibar. Inafaa ifahamike kuwa tangu kufika kwa mchunguzi huyo na mpaka kuondoka hapakuwepo chama cha kisiasa nchini isipokuwa kimoja tu HizbulWattan. Vyama vyote vya kisiasa vyengine viliasisiwa baadae. Kwahivyo HizbulWattan ndicho chama cha mwanzo cha kisiasa kuasisiwa Zanzibar.

Mr. Coutts alipomaliza shughuli zake alirejea kwao. Baada ya muda alileta mapendekezo ya uchunguzi wake kwa Balozi wa Serikali ya Kiingereza aliyekuwepo Zanzibar. Katika mapendekezo yake hayo, Mr. Coutts alikubali kuwa Zanzibar inafaa kuanzishwa uchaguzi wa "Common Roll" yaani uchaguzi wa kwa pamoja, bila ya kujali khitilafu za kabila. Lakini alipendekeza kuwa uchaguzi uanzie kwa viti sita na vilivyobakia viendelee katika mpango ule ule wa kuteuliwa na Balozi wa Serikali ya Kiingereza kwa kushauriana na Mfalme wa nchi. Pia katika mapendekezo yake, Bwana Coutts alitaka Balozi wa

13

Kiingereza aendelee kuwa Mwenye Kiti wa Baraza la Kutunga Sheria na watumishi wa Serikali ya Kiingereza waendelee kuwa waongozi wa upande wa Serikali.

Hizbu haikuridhika hata kidogo na mapendekezo hayo, kwa vile asli ya madaai yao ni kuwa Wawakilishi wote wa Baraza la Kutunga Sheria wawe ni wananchi waliyo chaguliwa na wananchi kwa uchaguzi wa "One Man One Vote". Juu ya hivyo, Hizbu ilikubali kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuona kuwa msingi wa matakwa yao ulipatikana; nao ni kuanzishwa kwa uchaguzi wa "Common Roll". Kwa kukubaliwa misingi hii Zanzibar ikawa ndiyo nchi ya mwanzo katika Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na ya Kusini kuanzishwa uchguzi kama huo. Baada ya kupatikana haya HizbulWattan ilizidisha juhudi za kuwafahamisha wananchi misingi na faida ya kuchaguwa Wawakilishi wao kwa kupitia uchaguzi huo.

WAKOLONI NA NYERERE NDIO WAASISI WA AFROSHIRAZI Wakuu wa Serikali wa Idara ya Utawala, Zanzibar baada ya kuona kuwa mpaka kuondoka kwa mchunguzi Coutts Zanzibar na mpaka kuleta mapendekezo ya uchunguzi wake, hapakuweza kuasisiwa chama chengine cha kisiasa nchni ili kipate kushindana na HizbulWattan (ZNP), waliamua kumtumilia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wakoloni walimtumilia Mwalimu kwa kuja Zanzibar kujaribu kuwashawishi waongozi wa vyama viwili vya kikabila waweze kuungana na kuasisi chama kimoja cha kisiasa ili kiweze kushiriki katika uchaguzi na kiweze kuwa pingamizi kwa Chama cha Hizbu. Katika ripoti ya Mr. Penny aliyekuwa Muangalizi wa Uchaguzi aliandika, "Ofisi yangu na Idara ya Utawala zilisaidia kuundwa kwa AfroShirazi na kwahivyo ikaokolewa Zanzibar na kuwa na utawala wa chama kimoja wa namna ya khatari."

Mwalimu Nyerere alikuja Zanzibar pamoja na Sheikh Zubeir Mtemvu mnamo mwisho wa mwaka 1956. Mwalimu pamoja na ujumbe wake alikutana na waongozi wa African Association, Sheikh Abeid Amani Karume, Bwana Mtumwa Borafia na Bwana Boniface. Waongozi wa Shirazi Association aliokutana nao Nyerere katika ujumbe wake huo ni, Sheikh Ameir Tajo, Sheikh Thabit Kombo Jecha na Sheikh Othman Shariff Musa. Mkutano huo ulifanyika katika nyumba ya Sheikh Abeid Amani Karume iliyokuwepo mtaa wa Kachorora, Mwembe Kisonge. Nyumba hiyo kwa wakati huo, ilikuwa ikikaliwa na Maalim Haji Ali Mnoga na Bwana Hija Saleh Hija. Njama hizo za wakoloni pamoja na Mwalimu Nyerere zilifanikiwa. Taarikhi 2 Februari 1957, miezi michache tu kabla ya kufikia uchaguzi wa mwanzo wa Juni, 1957 Chama cha AfroShirazi kiliasisiwa rasmi (kikiwa ni muungano wa jumuiya mbili za kikabila yaani "African Association na Shirazi Association"). Karume akawa Rais wa chama, Sheikh Ameir Tajo Makamo wa Rais na Sheikh Thabit Kombo Katibu Mkuu. Uwongozi wa chama haukwenda kwa mzalendo, haukwenda laa kwa Sheikh Ameir Tajo walaa kwa Sheikh Thabit Kombo, walaa kwa Sheikh Othaman Shariff, bali kwa Mzee Karume. Mbinu na njama za kuuwangamiza Uzanzibari zilianzwa zamani.

UCHAGUZI WA MWANZO JUNI 1957 Kutokana na mapendekezo ya uchunguzi wa Bwana Coutts kukhusu uchaguzi, uchaguzi wa mwanzo ulifanyika, June, 1957. Na kwa uchaguzi huo ndio wananchi wa Unguja na Pemba kwa mara ya kwanza waliweza kushiriki katika kuwachagua Wawakilishi wao wa Baraza la Kutunga Sheria la nchi yao. Uchaguzi huu ulikuwa wa viti sita. Majimbo mane yalikuwa kwa Unguja na mawili Pemba. Majimbo sita hayo yaligaiwa kama hivi:

Unguja: Majumba ya Mawe Unguja: N'gambo Unguja: Kaskazini Unguja: Kusini Pemba: Kaskazini Pemba: Kusini

Sheikh Ali Muhsin alisimama katika jimbo la N'gambo akiwa ni Mwakilishi wa HizbulWattan, akishindania na Sheikh Abeid Karume akiwa Mwakilishi wa AfroShirazi, na Sheikh Ibuni Saleh alisimama katika jimbo hilo hilo akiwa ni mgombea huru. (independent candidate). Bwana Rutti Bulsara alisimama katika jimbo la Majumba ya Mawe akiwa Mwakilishi wa Hizbu na washindani wake wakiwa, Bwana Choudhry, Mwakilishi wa Muslim Association, Bwana Anverali Hassan Virji, mgombea huru na Bwana AbdulQadir

14

Mukri, akiwa naye pia ni mgombea huru. Sheikh Amour Zahor alisimama jimbo la Kusini akiwa ni Mwakilishi wa Hizbu na Sheikh Ameir Tajo akiwa ni Mwakilishi wa AfroShirazi katika jimbo hilo. Sheikh Haji Muhammad alisimama katika jimbo la Kaskazini akiwa mgombea huru akiungwa mkono na Hizbu, Sheikh Daud Mahmoud yeye alikuwa Mwakilishi wa AfroShirazi katika jimbo hilo. Hizbu ilimuunga mkono Sheikh Haji Muhammad kwa kuamini kuwa ana fikra za kizalendo, na kutarajia kuwa hayuko mbali bali naye atajiunga na wananchi wenziwe ndani ya HizbulWattan; na hakika ikawa hivyo.

Pemba Kusini alisimama Sheikh Rashid bin Ali Khaify akiwa Mwakilishi wa Hizbu na Sheikh Muhammed Shamte Hamad alisimama jimbo hilo akiwa mgombea huru. Pia alisimama katika jimbo hilo Sheikh Abdalla bin Suleiman Busaidy, akiwa naye ni mgombea huru. Pemba Kaskazini, alisimama Sheikh Rashid Hamad Othman akiwa Mwakilishi wa Hizbu, Sheikh Ali Shariff Musa akiwa mgombea huru na Sheikh Shaaban Soud Mponda akiwa Mwakilishi wa AfroShirazi. Matokeo ya uchaguzi huo, Chama cha AfroShirazi kilipata viti vitatu Unguja na hakikuweza kupata hata kiti kimoja Pemba. HizbulWattan ilishindwa kupata hata kiti kimoja laa Unguja wala Pemba. Viti viwili vya Pemba vilichukuliwa na wagombea huru wake, yaani Sheikh Muhammed Shamte na Sheikh Ali Shariff, baadae waliviunga viti vyao kwenye AfroShirazi na kuwa na viti vitano katika Baraza jipya la Kutunga Sheria. Kiti kimoja cha Nyumba za Mawe, kilichukuliwa na Bwana Chodhry Mwakilishi wa Muslim Association. Natija hii ya uchaguzi inathibitisha kuwa Hizbu ni chama kilicho asisiwa bila ya kutokana na asili ya chama au jumuiya ya kikabila iliyokuwepo nchini kwa muda, kama vile ilivyokuwa hali kwa AfroShirazi. Na kwa vile HizbulWattan ilikuwa ndio kwanza chama kichanga haikustaajbu kwa kutopata hata kiti kimoja katika uchaguzi huu, kwani kilikuwa bado hakijawafikilia wananchi kwa wingi. Amma AfroShirazi ambayo ni muungano wa jumuiya mbili za kikabila, jumuiya ambazo kwa muda zilikuwa zishakuwepo nchini hakikupata taabu kupata ushindi wa uchaguzi huu, kwani wanachama wake ndio walewale. Tafauti na HizbulWattan ambayo ilibidi ikuwe kwa kupitia kwa wananchi pole pole.

KWANINI SHEIKH ALI MUHSIN ALIAMUA KUSIMAMA N'GAMBO BADALA YA MAJUMBA YA MAWE? Sheikh Ali alikuwa na hakika mia juu ya mia kuwa hatoweza kumshinda mpinzani wake katika sehemu hiyo kama alivyokuwa na hakika kuwa angeweza kupata ushinde ingekuwa amesimama katika Jimbo la Majumba ya Mawe. Lakini alitaka kuthibitisha kuwa kura chache za wananchi wenye asili mbali mbali zilikuwa pia nazo zina umuhimu katika kuendeleza siasa ya chama, si kasoro kuliko kura nyingi ambazo angeweza kuzipata katika Majumba ya Mawe. Lengo lilikuwa ni kuondoa ukabila na urangi. Kura 918 ndizo alizozipata, lakini zilikuwa na umuhimu mkubwa kwa chama na ziliongezea kumpa moyo zaidi katika kuendelea na juhudi za ugombozi wa nchi.

Uchaguzi ulifanyika kwa salama na ulimalizika kwa salama ingawa wakoloni walijaribu kutaka zitokee fujo wakati wa uandikishaji wa uchaguzi. Kwani badala ya wao (wakiwa ndio serikali) kuchukua dhamana ya kuchunguwa na kuhakikisha ni nani mwenye kustahiki kuchagua na kuchaguliwa, kazi hiyo waliitupia vyama vya siasa. Kweli sheria waliziweka za kuwa ni raia wa Zanzibar tu ndiye mwenye haki ya uandikishaji na upigaji wa kura, lakini sharia hizo hawakuzilinda na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa. Matokeo yake kulitokea kupingana na kuzozana baina ya watu wenyewe kwa wenyewe na hayo ndiyo yaliyozidi kupalilia chuki na ukhasama. Katika uchaguzi huu, wageni wengi khasa kutoka Tanganyika ambao walikuwa wakiishi Zanzibar walipenya katika kujiandikisha na walipiga kura. Hata hivyo, si haba uchaguzi uliweza kufanyika kwa salama bila ya kutokea fujo la namna yoyote.

KWENYE SHARI HUZALIWA KHERI Kushindwa HizbulWattan katika uchaguzi wa mwanzo, ndiko kuliko zidi kuwazinduwa wananchi na kujitokeza paruwanja katika kusimama bega kwa bega na wananchi, wazalendo wenziwao katika juhudi za kuigomboa nchi yao kutokana na ukoloni wa Kiingereza. Baada ya kumalizika kwa machofu ya pirika pirika za uchaguzi, Chama cha Hizbu kilitayarisha mkutano maalumu wa hadhara katika Jumba la Seyyid Khalifa Hall (sasa ati linaitwa "Karume House"). Umma wa kike na wa kiume uliomiminika siku hiyo ulikuwa wa aina ya peke yake. Haukupata kutokea tangu kuanza kwa harakati za kisiasa katika Zanzibar. Kwa jinsi mabibi walivyokuja kwa wingi kwenye mkutana huo, ililazimu wanaume wote waliyokuwemo katika ukumbi wa jumba hilo watoke nje kwa kuwapisha mabibi. Wanaume, wao walikaa katika uwanja wa Bustani ya jumba hilo. Siku hiyo ndipo wanawake walipodai wawe na Sehemu yao katika Chama, na wapate kura sawa na wanaume. Waliopiga kifua mbele kati yao ni BiZuhura bt Saleh,

15

BiSharifa Ahmed na BiZamzam Sultan. Kuanzia siku hiyo, kila usiku uchao, wananchi wake kwa waume walikuwa wakijitokeza kwa wingi katika kujiunga na Chama cha Wazalendo wenziwao. Waongozi wa chama kwa kulingana na umma unavyozidi kujiunga na chama kila siku ilibidi watengeneze mipango kukhusu kueneza mafunzo na siasa ya chama kila upande.

KUKUWA KWA HARAKATI ZA SIASA Baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Juni 1957, Hizbu ilianza kutayarisha mipango ya kueneza fikra na siasa ya chama kwa Unguja na Pemba kwa mjini na mashamba. Natija ya juhudi hizo haikuchukuwa muda illa zilidhihiri. Matawi ya Hizbu yalikuwa yakifunguliwa kila siku Unguja na Pemba, mjini na mashamba. Kila Tawi lilikuwa na skuli ya kusomeshea vijana na watu wazima (wa kike na wa kiume) waliokuwa hawakuwahi kuingia skuli wakati wa udogo wao. Vilevile kila Tawi lilikuwa ni kituo cha kutoa "Huduma ya Kwanza" (First Aid) kwa wenye kufikwa na maradhi madogo madogo. Vijana wa Youth Own Union ndio waliyokuwa walimu wa kusomesha na ndio waliyokuwa waganga wa kutibu maradhi madogo madogo.

Sheikh Juma Aley, aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya ZNP/ZPPP, yeye ndiye aliyekuwa akiwapa vijana hao mafunzo ya haraka juu ya namna ya kusomesha. Dr. Said Aboud Bin Tahir, yeye alikuwa akiwapa mafunzo juu ya matibabu madogo madogo. Sheikh Ali Makka na Sheikh Juma Ali (dogo dogo), wao wakijitolea kwa kuwapa wogonjwa matibabu katika kituo cha matibabu cha Hizbu kilichokuwepo katika jumba la Makao Makuu ya Chama, hapo Darajani. Katika kituo hicho vilikuwepo kila vifao vyenye kuhitajika kwa matibabu. Wagonjwa walikuwa wakiangaliwa na wakitibiwa bila ya malipo yoyote na bila ya kutizamwa msimamo wao wa kisiasa. MuHizbu na MuAfro wote walikuwa wakipata matibabu sawa sawa.

Pia katika Makao Makuu hayo ya chama kulikuwepo na sehemu ya "Welfare" ambayo ilikuwa ikijishughulisha na mambo ya kutoa misaada ya dharura kwa mwananchi yoyote (si kwa wananchama wa Hizbu tu). Sehemu hiyo ya "Welfare" ilikuwa na gari mbili za kuchukulia wagonjwa (ambulance) kutoka majumbani mwao kwa wale waliokuwa hawawezi kwenda kwa miguu yao au wanaishi katika sehemu zilizo mbali na hospitali, kama mashamba na sehemu zengine. Pia sehemu hiyo ya "Welfare" ilikuwa ikishughulikia kuweka majina ya wananchi wanaojitolea kutoa damu kwa kuwasaidia wagonjwa. Ilifika hadi hospitali kuu ya serikali wakihitajia damu kwa sababu ya wagonjwa, wakenda katika sehemu hiyo ya "Welfare" ya Hizbu kuomba watu wa kutoa damu. Vilevile ilifika wakati mmoja hospitali ya serikali kuazima dawa fulani kutoka katika kituo cha Hizbu cha matibabu. Sehemu hiyo ya "Welfare" ilikuwa chini ya uangalizi wa Seyyid Hashim Bin Abubakar Bin Salim, Bibi Aisha Salim (maarufu Bibi Aisha wa YOU au Aisha Mtumbatu) na Bibi Azza Mohammed Seif (mamewatoto wa Sheikh Ali Muhsin).

Miongoni mwa harakati za Hizbu katika kuwahudumia wananchi, wazee na vijana wa kiume na wa kike walijitolea bila ya malipo kwa ujenzi wa njia ya Nungwi. Mwishowe Serikali ikaingia kusaidia katika ujenzi huo kwa kuleta mipango ya siku moja kuwalipa na siku moja ya kujitolea. Yaani katika siku 30, wakilipwa siku 15. Mpango huo ukiitwa "Jisaidie Nikusaidie". Vilevile Mahizbu kwa kuendeleza huduma kwa wananchi wenziwao walijitolea kuijenga njia ya Uzi toka mwanzo mpaka mwisho, kwa kuunganisha kisiwa cha Uzi na kisiwa kikubwa cha Unguja hapo Unguja Ukuu. Pia walijitolea kuwapelekea maji ndugu zao wa Tumbatu. Wakati wananchi wa Tumbatu walipokuwa na shida kubwa ya maji Chama kilikodi matishali na kupakia mapipa ya maji kutoka mjini mpaka Tumbatu. Ikiwa nitaendelea kutaja ya kheri yaliokuwa yakifanywa na Chama cha Hizbu katika kuwahudumia wananchi, basi itanifanya nisiendelee na hayo niliyo yakusudia khasa kuzungumza na wananchi wenzangu. Kwahivyo, haya machache yanatosha kukupeni sura na fikra namna gani Chama cha Hizbu kilivyokuwa kikiendeshwa. Na kutokana na maendesho kama hayo, ndipo kila uchao wananchi walikuwa wakijiunga na Wazalendo wenziwao.

ATI HUSEMWA KUWA HIZBU IMEFELI! Ikiwa Hizbu imefeli, iliyofuzu ni ipi!? Yaliyofanywa na Hizbu kikiwa ni chama tu cha siasa, basi serikali ya Zanzibar hii iliyokuwepo ya "Mavamizi" kwa muda wa miaka 30 (1964 - 1994) haijaweza kuyafanya. Hospitali za serikali kuwa hazina hata vidonge vya Panadol licha ya Penicillin, ndio kufuzu huko? Skuli za serikali kuwa hazina hata madeski ya kukalia, licha walimu wajuzi wa kusomesha, ndio kufuzu huko?

16

Wanafunzi wa Chuo cha Kujifunza Uwalimu hawana hata matandiko wala mashuka katika vitanda vyao. Chakula ni cha mipango mipango na wakati mwingi wanafunzi wanalala na njaa kwa ukosefu wa chakula cha kutosha. Huko, ndiko kuffuzu! Barabara hazipitiki kwa uchafu wa maji ya makaro. Katika kila taa 10 za njiani, taa mbili tu ndizo zinazowaka na muwako wenyewe utadhani globu ya kurunzi (tochi) uchwara. Huko ndio kufuzu? Baada ya miaka 30 ya utawala wa Serikali yenye kujiita ya 'mapinduzi', kiwanja cha ndege cha Zanzibar hakina hata kiti kimoja cha kukalia wajao kuwashindikiza wasafiri wao. Ikiwa huko ndio kufuzu, basi hatujui kufeli kutakuwa na sura gani! Inaweza kuwa huko ndio kufuzu, yategemea nia na azma za waongozi wa hizo serikali. Bali kwa nchi na wananchi huko hata kwa lugha gani hakuitwi kufuzu, bali ni kudamirika. Kudamirika ambako ni sawa na kuteremkiwa na balaa, kwani iteremkapo balaa ya Mwenye Enzi Mungu (kwa maasi ya binaadamu) humfika mwema na mbaya. Maafa ya Zanzibar yamemteremkia kila mwananchi, mwema na mbaya, (Inshallah wako hao wema). Sababu kubwa ya hivyo ni kuwa juu ya maovu yaliofanywa na yaendeleayo kufanywa hakuna tena kukatazana maovu na kufahamishana kutenda mema, na hapo ndipo Mwenye Enzi Mungu azidishapo nakama Zake. Mwenye Enzi Mungu tunakuomba utunusuru.

KUGAWANYIKA KWA AFROSHIRAZI Mwanzoni mwa 1959 kulitokea mgawanyiko wa waongozi wa Chama cha AfroShirazi. Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Ali Shariff waliamua kujitoa katika chama na kwa kutoka kwao, kulifuatiwa na wanachama wengi nyuma yao khasa Pemba. Katika wakati huo huo, Chama cha AfroShirazi kilimfukuza katika chama Sheikh Ameir Tajo kwa singizio la kuwa alikwenda kuwaombea msaada wa fedha vijana wa YASU (Young African Social Union) kwa Sir Tayabali Karemjee kwa ajili ya ujenzi wa klabu (club) yao iliyokuwepo Miembeni, bila ya kuiarifu kamati kuu ya AfroShirazi. Sababu kubwa zilizompelekea Sheikh Mohammed Shamte na wenziwe kujitoa katika Chama cha AfroShirazi ni zenye kutokana na hisia za uwananchi khalisi kwa nchi yake. Hisia zake za kisiasa na nyendo zake pamoja na matarajio yake juu ya nchi yake yalikuwa ya kutaka kutumikia upatikane uhuru wa Zanzibar. Uhuru utaongozwa na Wazanzibari wenyewe bila ya kuchukua amri au shauri kutoka pahala pengine popote.

Sheikh Karume yeye alikuwa hawezi kufanya lolote bila ya kuzungumza na Mwalimu Nyerere na kama itavyoamuliwa na Mwalimu, ndivyo hivyo hivyo atavyofuata hata ikiwa si maslahi kwa Zanzibar (na mara nyingi hivyo ndivyo ilivyokuwa). Sheikh Mohammed Shamte, hayo yeye alikuwa hayakubali; kwahivyo daima walikuwa wakibuburushana mpaka mambo yalipofika hadi ya kufanywa mikutano ya Kamati Kuu ya Chama bila ya kuarifiwa Sheikh Mohammed kwa kukhofiwa kuwa akiwepo ataleta upingaji juu ya baadhi ya mambo. Ilipofika kiwango hichi, maji kuzidi unga, Sheikh Mohammed na Sheikh Ali Shariff walijitoa katika AfroShirazi.

KUASISIWA KWA ZANZIBAR AND PEMBA PEOPLES' PARTY (ZPPP) Chama cha Z.P.P.P. kiliasisiwa Novemba, 1959. Raisi wa Chama alikuwa Sheikh Mohammed Shamte Hamad na Naibu Raisi alikuwa Sheikh Ameir Tajo. Makao Makuu ya Chama yalikuwa Malindi Zanzibar. Z.P.P.P. kilikuwa Chama cha wananchi wa Unguja na Pemba. Kwa Unguja hakikuweza kupata wanachama wengi kwa wakati huo lakini kwa Pemba kiliweza kupata wananchi wengi kujiunga katika chama. Misingi na dhamiri ya Z.P.P.P. ikilingana na ya HizbulWattan. Nayo ni kufanyakazi kwa pamoja Wazanzibari wote, bila ya kubali rangi, kabila au imani zao za kidini katika kugombania kupatikana Uhuru wa Zanzibar kwa ajili ya mslahi ya wananchi wote. Waongozi wa HizbulWattan hawakuwa na shaka yoyote juu ya uzalendo wa Sheikh Muhammed Shamte na wenziwe, kwahivyo walikuwa wakiamini kuwa iko siku wataweza kufanyakazi pamoja.

TUME YA SIR HILLARY BLOOD Katika Mei, 1960 Serikali ya Kiingereza baada ya juhudi kubwa zilizokuwa zikifanywa na Chama cha Hizbu juu ya kutaka yapatikane maendeleo zaidi juu ya mabadiliko ya Katiba katika nchi, walimleta Sir Hillary Blood kutoka Uingereza akiwa ni mchunguzi wa mabadiliko ya Katiba. (Huyu ni wa pili, wa kwanza alikuwa Mr. Coutts). Hizbu kama kawaida yao waliandaa maandamano makubwa kutoka kiwanja cha ndege cha Kiembe Samaki mpaka mbele ya nyumba ya Balozi wa Kiingereza. Waandamanaji wote wa kike na wa kiume, walichukuwa mabango yaliyoandikwa neno moja tu, "UHURU 1960".

17

Sir Hillary Blood alipofika Zanzibar alivikuta vyama vitatu vya siasa, Zanzibar Nationalist Party (ZNP) yaani HizbulWattan, AfroShirazi Party yaani A.S.P. na Zanzibar and Pemba Peoples' Party yaani Z.P.P.P. Vyama vyote vitatu vilimpelekea Sir Hillary Blood risala za matakwa yao na vilevile Sir Hillary alipokea risala kutoka katika vyama vya wafanyakazi na kutoka kwa watu binafsi. Pia alizungumza na kuchukua fikra na nasaha kutoka kwa watu mbali mbali. Risala ya Hizbu na risala ya Z.P.P.P. zililingana sana katika matakwa yao. Zote mbili zilitaka Wawakilishi wote wa Baraza la Kutunga Sheria wawe wananchi waliyochaguliwa katika uchaguzi wa "One Man One Vote". Na baada ya matokeo ya uchaguzi huo yafuatiye mazungumzo ya Uhuru kamili wa Zanzibar. Ama risala ya AfroShirazi Party, ilitaka Wawakilishi wote wa Baraza la Kutunga Sheria wawe 25 na katika hao 22 wawe ndio wa kuchaguliwa kwa njia ya uchaguzi na watatu waliyobakia wawe miongoni mwa wafanyakazi wa Serikali ya Kiingereza waliopo nchini, hawa wateuliwe na Balozi wa Kiingereza.

Kwa faida ya wasomaji, nitazinukulu sehemu muhimu za risala zote tatu, yaani ya Hizbu, ya AfroShirazi na ya ZPPP. Kwa kufanya hivyo hapana shaka itakuwa faida zaidi kwa wananchi na khasa kwa vichipukizi vyetu, na wao wapate kujionea kwa macho yao, chama gani kilichokuwa kikiwakumbatia na kuwataka wakoloni waendelee katika uwongozi wa Serikali ya Zanzibar. Pia wapate vilevile kujionea wenyewe vyama gani vilivyokuwa vikitaka upatikane Uhuru kamili wa nchi.

Risala ya Hizbu ilikuwa kama hivi: "...... It is unnecessary now to argue whether or not it is our right to rule ourselves compeletely and whether or not we have the capacity to do so. Those days are over. There are now no two sides to the question. "...... In framing the recomendations regard should be paid to Her Majesty's Government's view that the legislature should become predominantly elective in character and that the executive should be reorganized to permit the establishment of a ministerial system. "...... Under any circumstances you will be failing in your duty and mocking the people of Zanzibar if you recommand anything less than full independence for the country".

Risala ya Z.P.P.P. ilikuwa kama hivi:

".....That the Zanzibar and Pemba Peoples' Party feels that this Sultanate should be given full independence within the British Commonwealth soon after the next election. "....That the Legislative Council should be of 30 members and that all 30 seats should be contested on Common Roll Election as stipulated in your terms of reference". Risala ya AfroShirazi Party ilikuwa kama hivi: "...... the AfroShirazi Party believes and recommends that the Legislative Assembly should consist of no more than 25 seats of which three seats should be reserved for exofficio members. The rest should all be open seats to be fought in Common Roll Election. "...... The exOfficio members should be the Minister for Justice, Minister of Finance and Minister of Defence and External Affairs. "...... It will indeed be fitting, and we entreat Her Majesty's Government, that 30th October, 1960, should mark the granting of selfgovernment to the people of these islands".

Mimi sitoongeza langu ila ninawaachia wasomaji baada ya kuzisoma risala zote tatu waamuwe wenyewe, ni wepi hao waliyokuwa bado wakitaka kurambatia urojo wa wakoloni. Ikiwa Wizara ya Uadilifu, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ulinzi na Mambo ya Nje, ziwe katika mikono ya wakoloni, sasa wananchi watakuwa wamejitawala kitu gani? Ndio wenye kuitambua siasa ya AfroShirazi, na kwa kujidhihirisha zaidi kwa kimaandishi kama hivi, hawakustaajabu walipomuona Karume ameyatia mambo yote muhimu kwa nchi, chini ya amri ya Serikali ya Muungano ambayo kwa ukweli ni Serikali ya Tanganyika, chini ya amri ya kidikteta ya Bwana Nyerere.

Umoja wa Vijana wa Youth Own Union walikasirishwa sana na mapendekezo ya Sir Hillary Blood. Kwa kuthibitisha uchukivu wao, waliandaa mkutano maalumu wa hadhara katika mtaa wa Mwembe Sanda, Miembeni, mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi. Baada ya kusomwa mapendekezo ya

18

Mchunguzi huyo mbele ya wananchi, ilikubaliwa kuilani na kuichoma moto ripoti hiyo, kwa vile ilivyo kwenda sana katika kudharau matakwa ya wananchi. Pia ilikubaliwa katika mkutano huo kumpelekea Sir Hillary risala maalumu kutoka kwa Umoja wa Vijana wa Youth Own Union ya kupinga mapendekezo yake aliyoyatoa kukhusu maendeleo ya Katiba katika Zanzibar.

Mapendekezo aliyoyatoa Sir Hillary Blood katika uchunguzi wake ni kuwa viti 22 tu viwe vya kuchaguliwa katika uchaguzi wa "Common Roll Election" na viti vinane viendelee kuwa vya kuteuliwa na Balozi wa Kiingereza kwa kushauriana na Mfalme wa nchi, yaani vyote viwe 30. Mapendekezo yake haya hayakuwa mbali na yale ya Chama cha AfroShirazi. Kama tulivyoona hapo juu katika risala yao, AfroShirazi wao walipendekeza kuwa viti vyote visizidi 25, kati ya hivyo vitatu viwe vya wajumbe wa kuteuliwa na kuchukuwa nafasi muhimu katika serikali.

UCHAGUZI WA PILI, JANUARI 1961 Baada ya miaka mitatu unusu tokea kufanyika kwa uchaguzi wa mara ya mwanzo, Juni 1957, ulifanywa uchaguzi mwengine, katika Januari, 1961. Safari hii, mabibi nao walipata fursa ya kushiriki katika uchaguzi. Uchaguzi huu ulikuwa wa viti 22. Vyama vyote vitatu vilishiriki kwa ukamilifu. Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa, AfroShirazi walipata viti 10, Hizbu viti tisa na ZPPP viti vitatu. Kwa natija hii, hapakuwa na chama kilichoweza kuunda Serikali ila kwa kushirikiana na chama chengine. Balozi wa Kiingereza Sir George Mooring aliwaalika waongozi wa vyama viwili vikubwa, yaani Hizbu na AfroShirazi kwa kuzungumzia tatizo liliokuwepo juu ya utaratibu wa kuweza kuunda serikali. Baada ya mazungumzo marefu ya hivi na hivi mwongozi wa Chama cha Hizbu, Sheikh Ali Muhsin alitoa shauri la kutaka ifanywe serikali ya pamoja ya vyama vyote vitatu. Mwongozi wa Chama cha AfroShirazi, Sheikh Abeid Amani Karume, yeye aliipinga shauri hiyo na badala yake alitaka matokeo ya uchaguzi huo yafutwe na pafanywe uchaguzi mwengine.

Baada ya kuzozana zozana na pasipatikane natija yoyote ya kurahisisha tatizo hilo, Balozi wa Kiingereza, Sir George Mooring alimpa kila kiongozi katika hao wawili muda wa wiki moja ajaribu kupata waakilishi waliyochaguliwa kuchanganya viti vyao pamoja naye ili aweze kupata wingi wa viti vya kumuwezesha kuunda serikali. Fursa hiyo kwanza alipewa Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuwa Chama chake kilipata kiti kimoja zaidi kuliko Chama cha Hizbu.

Wakati Karume alipokuwa katika juhudi za kuzungumza na Chama cha ZPPP, kwa kuwataka waviunge viti vyao vitatu upande wa Chama cha AfroShirazi, baadhi ya watumishi wa Serikali wa kikoloni na khasa wa Idara ya Utawala, nao waliingia kazini kwa kufunga njuga kwa njia za siri siri. Miongoni mwa utumishi wao ilikuwa ni kukisaidia Chama cha Afro waweze kupata viti vya kutosha waunde serikali. Kwa kutaka kutekeleza utumishi wao huo walizungumza na Sheikh Othman Shariff na walimtaka afanye kila njia na kila jitihada mpaka ampate Sheikh Mohammed Shamte akubali kuvipeleka viti vyao (vya ZPPP) vitatu upande wa AfroShirazi.

Kwa ilivyokuwa Sheikh Othman aliahidiwa malipo fulani fulani kama vile kulipiwa deni la nyumba yake ya "Kijipu House" iliyokuwepo Gongoni, Zanzibar, na mengineyo yaliyokhusika na mambo ya kisiasa, aliukubali utumwa huo. Na kwa kuwepo makhusiano ya kuowana baina yake na Sheikh Mohammed Shamte, yaani Sheikh Mohammed Shamte alimuowa binti wa Sheikh Issa Shariff (mtoto wa kaka yake Sheikh Othman Shariff), na vilevile mmoja katika hao washindi watatu wa ZPPP, alikuwa ni kaka yake yeye Othman, yaani, Sheikh Ali Shariff, basi Sheikh Othaman aliona itamuwiya rakhisi kufuzu utumwa huo. Othman aliingia mbioni kwa "Full speed". Baada ya kuona jitihada zake zote alizozifanya za kumtaka Sheikh Mohammed Shamte ayakubali matakwa yake zimefeli, alianza kumtishia kaka yake Sheikh Ali Shariff kwa kumwambia kuwa, "Ikiwa na wewe hukubali kufuata shauri yangu, basi hutoniona tena baada ya leo. Afadhali nijiuwe kuliko kuona umeungana na Hizbu".

Kwa kutaka kutimiza tishio lake hilo kwa kaka yake, Sheikh Othman alitoka kwake na asijulikane aliko kwenda, kwa muda mkubwa sana. Alijificha! Zogo la kutafutwa Sheikh Othman lilianza mjini, vijana wa YASU upande wao na Polisi upande wake. Kaka yake, Sheikh Ali Shariff aliingiwa na khofu na kihoro kwa mapenzi ya ndugu yake. Aliwambia vijana wa YASU wamtafute Sheikh Othman na watapomwona wamwambie kuwa yeye (Ali Shariff) ameikubali shauri yake ya kukiunga kiti chake katika upande wa

19

AfroShirazi. Haukupita muda mkubwa baada ya hapo, ila Sheikh Othman alirejea kwake kutoka huko alikojificha, kwani baadhi ya hao vijana wa YASU walikuwa wakijuwa mpango huo alioufanya Sheikh Othman na wakijua wapi alipojificha. Kwa hivyo, walipopata uhakika kwa Sheikh Ali Shariff wa kukubali kujiunga na AfroShirazi, mara tu walizifikisha salamu hizo kwa Sheikh Othman. Muda wa wiki aliopewa Karume ulimalizika kwa kupata kiti kimoja tu zaidi, yaani kiti cha Sheikh Ali Shariff.

Kwa kutowezakana kuunda Serikali kwa viti walivyokuwa navyo AfroShirazi hadi wakati huo, basi Balozi wa Kiingereza alimpa Sheikh Ali Muhsin naye muda wa wiki ajaribu kupata waakilishi wa kujiunga naye ili aweze kupata wingi wa kutosha wa kuwezesha kuunda serikali. Sheikh Ali pamoja na wenziwe hawakuchukua muda mrefu ila waliweza kukubaliana na Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Bakari Mohammed wote wawili hao wakiwa ni washindi wa ZPPP kuviunga viti vyao upande wa Hizbu. Muda wa wiki mbili ulimalizika na ikawa kila upande wanavyo viti kumi na moja.

Ilivyokuwa hali ndio hivyo, Balozi wa Kiingereza alitoa uamuzi wake kuwa pafanywe Serikali ya Mshikizo ya muda wa miezi sita na baada ya hapo pafanywe uchaguzi mwengine. Mwongozi wa Hizbu, Sheikh Ali Muhsin, ilipokuwa hali imefika hadi hii alizidi kumnasihi mwongozi mwenziwe Sheikh Karume kwa kumtaka atizame na kuyapa umuhimu maslahi ya nchi kuliko ya vyama. Alimnasihi waondoe mzozo na wakubaliane kuunda Serikali ya pamoja. Alizidi kwa kumfahamisha Sheikh Karume kuwa kufanya hivyo kutainusuru nchi na kuingia katika uchaguzi mwengine, ambao ni gharama na pia kukhatarisha usalama. Pia alimueleza kuwa kuunda Serikali ya pamoja itawezesha nchi bila ya kuchelewa zaidi kufikilia Uhuru. Sheikh Karume akiwa keshakuwa na mipango na matakwa yake, mbali na maslahi ya nchi, yote haya aliyakataa katakata na alishikilia fikra iliyotolewa na Balozi wa Kiingereza ya kufanywa Serikali ya Mshikizo na kufanywa uchaguzi baada ya miezi sita.

Baada ya kuwa hakuna jengine isipokuwa kutekelezeka shauri hiyo iliyotolewa na Balozi, lilizuka tatizo jengine nalo ni, nani ataye kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali hiyo ya Mshikizo? Sheikh Ali Muhsin alipendelea nafasi hiyo apewe raia aliyekuwa na uzowevu juu ya mambo au uwendeshaji wa serikali. Kwahivyo, alipendelea nafasi hiyo ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mshikizo apewe Sheikh Ahmed Lakha, ambaye ni Mzanzibari, mwenye ujuzi, maarifa, itibari na hakuwa mwenye kujiambatisha na chama chochote. Mwongozi wa AfroShirazi Sheikh Abeid Amani Karume alikataa katakata kukhusu nafasi hiyo kupewa Sheikh Ahmed Lakha. Yeye alitaka nafasi hiyo apewe Bwana Roberts, mfanyakazi wa Serikali ya Kiingereza ambaye wakati huo alikuwa ni "Chief Secretary" wa Serikali ya Zanzibar na pia ndiye aliyekuwa akikamata nafasi ya Ubalozi wa Kiingereza wakati Balozi akiwa katika likizo. Shauri ya mzee Karume ndiyo iliyokubaliwa na Balozi, Sir George Mooring na Bwana Roberts akawa Waziri Kiongozi wa mwanzo wa Serikali ya Mshikizo ya Zanzibar.

Ukifuatia na kuzingatia utatambua kuwa katika harakati za kisiasa hizi zilizopita muda wote huu, fikra za ASP daima zilikuwa zikilingana na kukubaliana na fikra na matakwa ya kikoloni.

UCHAGUZI WA TATU JUNI 1961 Kwa kuchelea natija ya uchaguzi huu kutokea kama ile ya uchaguzi uliopita (wa Januari, 1961) hata kutokumkinika chama kimoja pekee kuunda Serikali kwa idadi ya viti walivyokuwa navyo, katika uchaguzi huu liliongezwa jimbo moja na kufanya idadi ya viti vyote 23 badala ya 22.

Ushirikiano Wa ZNP/ZPPP Katika uchaguzi huu, Hizbu na ZPPP walikubaliana na walitangaza rasmi kuwa watashirikiana katika kusimamisha wagombea wao kwa pamoja. Yaani, jimbo litalo simamiwa na mgombea wa Hizbu, ZPPP haitoweka mgombea wake bali wanachama wote wa Hizbu na wa ZPPP watampigia kura mjumbe huyo na hivyo hivyo kwa mgombea wa ZPPP. Fikra hii ilifanyika kwa kuzidi kutilia nguvu umoja na vile kila siku idhihirivyo kuwa misingi na matakwa ya ZNP/ZPPP juu ya maslahi ya nchi yakilingana. Ndugu zetu ASP wao daima muelekeo wao (kama tulivyoona na tutavyozidi kuoona) ulikuwa kinyume na hivyo, maslahi yao binafsi ndio yaliokuwa mbele.

20

AfroShirazi Iliandaa Machafuko Siku ya Uchaguzi Waongozi wa Chama cha AfroShirazi walipoona ushirikiano wa Hizbu na ZPPP katika uchaguzi, walijua kuwa hawatoweza kushinda, kwa hivyo waliandaa kufanya machafuko katika vituo vya uchaguzi. Walianza kwa kuwasukuma sukuma wanachama wa Hizbu na wa ZPPP khasa mabibi na vizee. Waliendelea katika mipango yao hiyo ya fujo kwa kuwatowa wanachama wa ZPPP/ZNP katika mistari waliyokuwa wamejipanga kwendea kwenye masanduku ya kutilia kura. Ilipokuwa wanachama wa Hizbu na ZPPP hawakukubali kutolewa katika mistari, hapo tena wanachama wa AfroShirazi walianza kuwapiga wanachama wa ZNP/ZPPP kwa magumi, mateke na mwisho walianza kutumia silaha kama visu, mapanga na mawe. Michafuko hiyo ilianza katika vituo vya uchaguzi na baadae iliendelea majumbani, mitaani na viamboni.

Waongozi wa Hizbu na ZPPP, walipoona wenziwao wao wanauliwa na kujeruhiwa, waliwatangazia wao wote waondoke katika vituo vya upigaji kura na waliwazuia waliyokuwa bado hawajafika katika vituo vya upigaji kura, wasende mpaka watapoambiwa na chama chao ZNP/ZPPP kuwa wende ndio wende. Michafuko hiyo ilimalizikia kwa kuuawa MaHizbu na MaZPPP 68 na mamia kujeruhiwa vibaya vibaya. Wengi wao walibakia na vilema vya muda na wengine vya milele.

Michafuko hiyo ilianza tokea saa 12 za asubuhi kabla hata kufunguliwa hivyo vituo. Na tokea wakati huo, askari wa polisi walikuwa wamesha kuwepo katika vituo vyote vya mjini na mashamba lakini walijifanya kama hawayaoni yenye kutokea. Serikali ya kikoloni walipoona mambo yamezidi watu wanauliwa na kujeruhiwa kwa wingi, ndipo walipoagizia kikosi cha askari wa kuzuwia fujo (GSU) kutoka Kenya. Askari hao walifika Zanzibar kiasi cha saa saba za mchana. Baada ya kuingia mitaani waliweza kutuliza michafuko na kurejesha hali ya kawaida. Lakini wakati huo waliyokuwa wameuliwa, wamesha uliwa na waliyokuwa wamejeruhiwa, wameshajeruhiwa. Juu ya fujo hilo lililoandaliwa na AfroShirazi katika uchaguzi huo kwa kufikiria kuwa kwa kufanya hivyo watapata ushindi, wanachama wa ZPPP na Hizbu walisema, Mungu Mmoja kheri tufe lakini hatutowacha kwenda kuzitia kura zetu. Baada ya kuhisabiwa kura, AfroShirazi walijikuta na viti vyao vilevile 10 walivyovipata katika uchaguzi wa Januari 1961. ZNP/ZPPP walijipatia viti 13.

Katika sehemu ya Zanzibar kulikofanywa ukatili mkubwa sana siku hiyo ya uchaguzi wa taarikh moja Juni 1961, hapakutokea kuliko Bambi. Huko Mwalimu mmoja wa skuli, anayeitwa Bwana Ali Muhsin Mshirazi (bwana huyu pia alishiriki katika mauwaji ya Januari 12, 1964) alishirikiana na makatili wenzake kwa kuwachukua vijana wadogo, ambao wengi wao walikuwa ni miongoni mwa wanafuzi wake na kuwatia ndani ya tanuri la kuchomea mbata kwa kuwadanganya ati kuwa "anawahifadhi na ghasia ziliopo katika mji". Baada ya kuwatia humo, waliiondoa ngazi waliyo wateremshia kisha waliwamiminia geloni kwa mageloni ya petroli kisha wakawawasha moto. Vijana hao waliachwa wakiteketea mpaka kuwa majivu. Tanuri hilo ndilo lililokuwa kaburi lao. Jee nini kosa la vijana hao? Na wawe wana makosa ya aina yoyote, jee ulimwenguni huu tuishio iko kanuni ya adhabu ya aina hiyo? Kwa Kiislamu haifai kuadhibu kwa moto hata kwa mnyama mwenye kudhuru. Seuze binaadamu, tena watoto wadogo! Malipo ya Mwenyezi yanaanza tangu hapa duniani, natunayaona, kesho ndio hesabu na malipo ya milele.

Kwa bahati, mmoja kati ya vijana hao ambaye siku yake ilikuwa bado Mwenye Enzi Mungu hajamuandikia, aliweza kupenya wakati walipokuwa wenzake wana teremshwa ndani ya tanuri mmoja mmoja. Kijana huyo, ndiye baadae aliyeweza kuzifikisha khabari hizo katika mikono ya polisi na kuweza kukamatwa mikatili hiyo. Jambo la kustaajabisha na kusikitisha ni kuwa mahakama iliyokuwa ikiendeshwa na Naibu Jaji Mkuu mkoloni, Muingereza haikuweza kupata hata mshitakiwa mmoja kati ya wote waliyopelekwa mbele yake kwa mashitaka ya kuuwa, kuwa ni mukhalifu. Hakutokea hata muuwaji mmoja aliyepewa adabu ya kuuliwa au hata ya kufungwa gerezani kifungo kikubwa. Wote waliachiliwa huru.

Katika kesi ya mwalimu (Ali Muhsin Mshirazi) na mikatili wenzake, ushahidi aliyoutoa kijana yule mdogo mbele ya mahakama, kila aliyekuwepo na kumsikia kijana huyo jinsi alivyotoa ushahidi wake dhidi ya mikatili hiyo, aliona mikatili hiyo itapewa adabu inayo wasitahikia. Hakimu wa kesi hiyo alipokuwa anatoa hukumu yake alisema kuwa, "Ushahidi nilioupata kutokana na kijana huyu ni ushahidi mzuri, na

21 nampa sifa kwa kutokana na umri wake na alivyoweza kutoa ushahidi wake na alivyoweza kuikabili mahakama kwa ushujaa. Lakini, nasikitika ushahidi wake haukuweza kupata kusaidiwa na mtu mwengine ambaye mwenye umri mkubwa. Kwa kuwa huyu ni kijana mdogo, nashindwa kuamini ushahidi wake peke yake. Kwa hivyo basi, sina budi na kuwaachilia huru washitakiwa hawa"!!

Yote haya tuliokuwa tukitendewa na wakoloni, bado utamsikia Mwalimu Nyerere akidanganya na akikejeli kwa kusema kuwa Chama cha HizbulWattan kikipendelewa na wakoloni! Nyimbo hii ya kijanja na ya kejeli pia ikiimbwa na waongozi wa hii serikali inayojiita ya 'mapinduzi'. Haikuimbwa na hao tu, bali hata wale ndugu zetu tuliyokuwa pamoja kwa muda hapo mwanzoni walikuwa shangweni kwa kujitafutia maslahi ya nafsi zao. Maneno haya ni istihzai ya dhahiri, kwani ingelikuwa wakoloni wameipendelea Hizbu bali sio kuipendelea, lakini lau wangelifanya insafu na uaminifu tu basi hata hayo yenye kuitwa 'mapinduzi' yasingeweza kutokea.

MUUNGANO WA ZNP/ZPPP, WAUNDA SERIKALI Waswahili wanasema, "Wanja wa Manga, si Dawa ya Chongo". Fujo lote walilolifanya AfroShirazi kwa kutarajia kupata ushindi, hawakupata ushindi. ZNP/ZPPP, waliunda Serikali kwa kupata viti 13 kwa viti 10 vya AfroShirazi. Serikali hii ikiitwa, "Responsible Government" yaani "Serikali ya Madaraka" kufikilia Uhuru. Sheikh Mohammed Shamte Hamad ndiye aliyekuwa Waziri Kiongozi (Chief Minister) wa Serikali hiyo.

KUTOKUFAULU MAZUNGUMZO YA MWANZO YA KATIBA YA UHURU Baada ya miezi 10 mpaka 11 tokea Serikali ya Muungano wa ZPPP/ZNP "Serikali Ya Madaraka" kuwa katika madaraka, Serikali ya Kiingereza ilikubali baada ya kushikiliwa na serikali hiyo ya madaraka kufanya mkutano wa mazungumzo ya uhuru. Mkutano huo wa Katiba ya Uhuru ulifanywa katika miezi ya Machi na April 1962 huko Lancaster House, London. Pande zote mbili yaani upande wa Serikali na upande wa Upinzani walihudhuria kwenye mkutano huo. Kwa bakhti mbaya mkutano huo haukuendelea kwa siku nyingi illa ulivunjika bila ya kukubaliana kwa kuwekwa kwa taarikh ya Uhuru. Waongozi wa AfroShirazi walikataa kuzungumzwa chochote kilicho khusika na kutolewa taarikh ya Uhuru mpaka kwanza pafanywe uchaguzi mwengine. Baada ya matokeo ya uchaguzi huo, ndio yafuatie mazungumzo ya kutolewa kwa taarikh ya Uhuru. Waongozi wa upande wa Serikali waliwanasihi mwisho wa uwezo wao waongozi wa upande wa Upinzani yaani AfroShirazi waache kuleta vizingiti vitavyo sababisha kuchelewa kwa Uhuru wa Zanzibar. Bali waongozi wa AfroShirazi walin'gan'gania uzi wao huo huo wa kupinga kuzungumzwa chochote kitachofikilia kutolewa kwa taarikh ya Serikali ya Ndani kabla ya kufanywa uchaguzi mwengine.

Waongozi wa upande wa Serikali, walipoona waongozi wa upande wa Upinzani hawataki kubadili msimamo wao, walijaribu kuzungumza nao nje ya mkutano. Katika mazungumzo hayo, upande wa Serikali waliutaka upande wa Upinzani wakubali kufanyika serikali ya pamoja, yaani "Government of National Unity" (hii ni mara ya pili ASP kupewa shauri na wenzao ZNP/ZPPP kufanya serikali ya pamoja.) Katika serikali hiyo ya pamoja, upande wa Serikali watawapa ASP wizara tatu kati ya wizara nane na pia watawapa uwezo wa kutumia "veto" kwa jambo lolote litalotokea nao wakaliona si maslahi kwa upande wao. Yaani ASP watakuwa na madaraka sawa sawa na ZNP/ZPPP katika uendeshaji wa hiyo serikali ya pamoja. Waongozi wa AfroShirazi baada ya kuyasikia hayo, walitaka muda wa kuyazungumza na kuyazingatiya wakiwa peke yao, na waliahidi kutoa uamuzi wao siku ya pili kabla ya kuhudhuria kwenye kikao cha mkutano wa Katiba. Kwa dalili zote, walionesha kuwa wamevutika na mashauri hayo, na ilikuwa kuna tamaa kuwa watawafik. Upande wa Serikali walingojea kwa hamu na matumainio (pia na wasi wasi) kuwa shauri waliyoitoa itakubaliwa au sana watataka wazidishiwe wizara moja badala ya tatu ziwe nne, yaani wawe wao ASP na wizara nne na ZNP/ZPPP wizara nne. Wakati ulipofika siku ya pili, waongozi wa ASP wakiongozwa na Sheikh Karume walifika kwa Mawaziri. Walikataa hata kukaa kitako, Karume alisema, "Tumeyazingatia mashauri yenu. Mazuri! Lakini sisi hatutaki kushirikiana na nyinyi!" Wakazunguka wakatoka.

Kutokana na msimamo huo wa ukorofi uliopangwa, waliyokuwa wakiutumia AfroShirazi, Mwenyekiti wa mkutano huo, Waziri wa Makoloni, aliufunga mkutano bila ya kuzungumzwa lolote kukhusu maendeleo ya Katiba. Aliwashukuru wajumbe wote kwa kuhudhuria na aliwataka warejee nyumbani mpaka

22 watapoweza kuwafikiana baina yao, wakati huo Serikali ya Kiingereza itakuwa tayari kufungua tena mazungumzo ya maendeleo ya Katiba. Wajumbe wote wa upande wa Serikali (isipokuwa Sheikh Ali Muhsin) na wa upande wa Upizani, walirejea Zanzibar bila ya kuwaletea wananchi Uhuru wa nchi yao waliwokuwa wakiungojea kwa hamu kubwa. Wananchi wa Zanzibar kwa jumla walivunjika moyo na matokeo haya.

Baada ya kufuzu hayo yenye kuitwa 'mapinduzi' ya Januari 12, 1964, Katibu Mkuu wa AfroShirazi, Sheikh Thabit Kombo alisema wakati akikhutubia mkutano wa hadhara mbele ya Makao Makuu ya AfroShirazi, hapo Mapipa ya Ngozi, Kisiwandui: "Tunamshukuru Mwalimu Nyerere kwa kutuvua mtego waliyotaka kutunasa Mahizbu wakati wa mkutano wa mwanzo wa Katiba, huko Uingereza. Mahizbu walitaka kutufanyia ujanja wa kutaka tuungane pamoja katika kuendesha serikali na kwa kutaka kutimiza ujanja wao, walikiri kutupa wizara tatu katika serikali yao. Lakini mzee Karume kabla ya kusema lolote, alizungumza na Mwalimu kwa simu kumtaka shauri yake juu ya jambo hilo. Mwalimu alimwambia mzee Karume asikubali kufuata shauri hiyo ya Hizbu kwani huo ni ujanja tu wakutaka kusiwepo na upinzani. Mkitaka shauri yangu kataeni. Ndipo mzee alipokataa", alisema Thabit Kombo.

Mara nyingi utamsikia Mwalimu akisema kuwa yeye hakukhusika na lolote katika mizozo ya kisiasa ya Zanzibar. Hatujui Mwalimu anataka akhusike namna gani zaidi ya hivyo alivyokhusika (alivyo jikhusisha). Yeye Mwalimu ndiye aliyekiasisi Chama cha AfroShirazi na ni yeye aliyekuwa, "master mind" katika kuyaandaa hayo yenye kuitwa 'mapinduzi'. Wavamizi walioivamia Serikali ya halali ya Zanzibar wengi wao wameletwa Zanzibar kutoka katika nchi yake Tanganyika, na huko ndiko walikopewa mafunzo ya kutumia silaha; na hizo silaha zenyewe zilitoka huko huko kwake Tanganyika. Naiwe hakukhusika na fisadi zote hizi zilizofanyika Zanzibar kama adaivyo, bali huo ufisadi mmoja tu unatosha, nao ni wa huko kuiburura Zanzibar ndani ya huo muungano wake, muungano uhange, miezi minne tu baada ya kufuzu hayo 'mavamizi' yake. Muungano ambao leo ni zaidi ya miaka 30 na hapana hata nchi moja za jirani ziliotaka hata kuukaribia, licha kujiunga nao. Hili ni janga letu peke yetu!

BABU KUTOKA KATIKA HIZBU Muda mchache kabla ya uchaguzi wa Julai 1963, uchaguzi ambao ndio uliofuatiwa na Uhuru wa nchi, Babu akiwa ni Katibu Mtendaji wa Chama, alijitoa katika Chama. Ingelikuwa si kwa ajili ya kutaka kusafisha porojo lisemwalo na hao waliyokuwa wakijiita, "progressives" yaani wapenda maendeleo, kwa makusudi ya kusema uwongo kwa kutarajia kuwadanganya wananchi na khasa wale waliyokuwa wadogo wakati huo, basi nisinge poteza wakati kwa kueleza chochote kukhusu Babu kuacha Hizbu. Kwani kutoka Babu katika Hizbu, hakukuathiri chochote kukhusu msimamo wala maendeleo ya Chama. Kila kitu kilikwenda kama kawaida, kinyume na alivyotarajia Babu.

"Progressives" au kwa jina lengine "Makomredi" wakisema (na hata hivi sasa wapo wenyekusema kati yao) kuwa Babu alijitoa katika Chama cha Hizbu baada ya kugundua kuwa baadhi ya waongozi wenziwe wanamuendea kinyume na ati kuwa Chama kimeacha misingi yake ya kimaendeleo na kufuata mwendo wa kuyarejesha nyuma maendeleo (yaani badala ya kwenda katika mwendo wa ki"progressive" kinakwenda katika mwendo wa ki"reactionary” kupinga maendeleo). Yote hayo waliyokuwa wakiyasema na wasemayo mpaka hivi sasa hao makomredi ni maneno ya uzushi na kutaka kujitowa kimasomaso. Na kwa wakati ule walipokuwa wakitembea na bastola viunoni, yaani wakati wa "kipya kinyemi ingawa donda" na "mwenye nguvu mpishe" hapana aliyethubutu kuwatowa kombo kwahivyo wakijibwabwatia watakavyo.

DHAMIRI ZA BABU Dhamiri za Babu ulipokuwa Uhuru wa nchi unakaribia zilizidi kudhihiri, nazo zilikuwa ni kukitumilia chama kwa maslahi ya nafsi yake, ya hao aliokuwa akiwatumikia, na ya hao wachache waliokuwa nyuma yake. Mengi madogo madogo, bali yenye taathira mbaya yalikuwa yakitokea siku za karibuni kabla ya kuacha chama ambayo ukiyazingatia utafahamu mabaya aliyokuwa akiypanga, juu ya Chama kwa jumla na juu ya waongozi wenziwe wa chama khasa! Babu alidhamiriya kuwa itapopatikana Serikali ya Hizbu, iwe ni serikali yenye kufuata upande wa kushoto, yaani upande wa kikoministi, au kisoshalist. Kwa kutaka kufikilia dhamiri zake hizo, alianza mipango yake ya chini kwa chini ya kutaka patokee vurugu katika uwongozi wa chama. Vurugu hilo alipangia lianzie kwa baadhi ya waongozi wa Chama,

23 wale asiowataka kuwemo kwenye uwongozi, washindwe katika majimbo yao ya uchaguzi na wale awatakao yeye ndio wafuzu.

Kwa kutengenea mpango wake huu, natija ya kwanza itakuwa ni kutokea vurugu katika chama, khasa katika uwongozi wa chama, kwa kuingiza kutuhumiana na kutoaminiana baina ya waongozi wenyewe kwa wenyewe. Natija ya pili ya maslahi yake ni kuingiza katika uwongozi wa chama watu wake wa kutosha kumuwezesha kupitisha maoni na hukumu yake bila ya upinzani. Haya tulioyataja ni maendelezo ya njama zake ambazo kwa hakika alizianza zamani. Miongoni mwao, wakati wa mazungumzo ya mwanzo ya Uhuru yaliyofanywa huko London katika mwaka wa 1962, Babu alitumia fursa hiyo kwa kutaka kuleta balaa lake huko huko Uingereza ili paweze kuzuka kutofahamiana baina yetu wenyewe kwa wenyewe.

Kwa kuhudhuriya mazungumzo ya Uhuru huko London, Hizbu ilitengeneza mipango maalum ili baadhi ya waongozi wa Chama nawo wawepo huko London wakati wa mazungumzo hayo ya Uhuru. Miongoni mwa waliokuwepo huko ni Babu akiwa ndiye Katibu Mtendaji wa Chama, Suleiman Malik na mimi Aman Thani tukiwa ndio wenye dhamana ya Ofisi ya ZNP iliyokuwepo Cairo wakati huo. Pia walikuwepo huko London, Bwana Ali Sultan Issa, Sheikh AbdulRazak Mussa (Kwacha) na Bwana Ali Mahfoudh akiwa ndiye aliyekuwa na dhamana ya Ofisi ya ZNP Cuba na Bwana Salim Said Rasdhid Mauly ambaye ndiye aliyekuwa na dhamana ya Ofisi ya ZNP hapo London. Kwa ajili ya matengenezo fulani fulani, ujumbe huo ulitangulia kufika Uingereza kabla ya kufika Mawaziri. Waziri aliyefika mbele kabla ya wenziwe, alikuwa Dr. Ahmed AbdulRahman Idarus Baalawy. Siku moja kabla ya kufika Mawaziri wengine, Babu alitaka tukutane kwa kuzingatia mambo muhimu ya kazi zetu. Katika kuendelea na mkutano huo, Babu alieleza kuwa amepata khabari za kuaminika kuwa nyumbani Zanzibar kumeasisiwa Kamati ya watu 14. Kazi ya Kamati hiyo ni kumpa nasaha Sheikh Ali Muhsin katika uwongozi khasa katika wakati kama huu wa kukaribia kupatikana kwa Uhuru wa nchi. Aliendelea kueleza Babu kuwa, "Kamati hiyo inamtaka Sheikh Ali Muhsin ajaribu kama awezavyo kutafuta njia zitazowezesha kuwaepuka baadhi ya waongozi wa Hizbu, mimi (Babu) nikiwa ni mmoja na kila wanaye muona kuwa anazo fikra za kimaendeleo, yaani hata wewe Dr. Idarus umo katika hao wenye kutakiwa waepukwe".

Maneno hayo ya Babu yalitushangaza na kutusitusha baadhi yetu, ama wengine kati yetu walikuwa tokea mwanzo wanayajuwa. Baada ya kuyazungumza kwa urefu maneno hayo tulikubaliana tuyaakhirishe mazungumzo hayo mpaka baada ya mazungumzo ya mkutano wa Uhuru, baada ya hapo tutakaa na Sheikh Ali Muhsin pamoja na Mawaziri wote tuyazungumze. Babu aliwafiki rai hii. Baada ya kumalizika kwa mkutano, baadhi yetu tulimkumbusha Babu kukhusu kukutana na Sheikh Ali Muhsin pamoja na Mawaziri wengine juu ya masala aliyoyaeleza kabla ya mkutano wa Uhuru. Kukhusu suala hili Babu alijitia pambani za mtonga. Aliingia huku akatokea kule na mwisho aliondoka na kurejea Zanzibar kwa kukimbilia kuhudhuria mahakamani kutokana na kushitakiwa na Serikali ya kikoloni kukhusu makala aliyoyaandika katika gazeti lake (la binafsi) la ZANEWS, bila ya kufanya huo mkutano.

Miongoni mwetu tulizidi kupunguwa imani juu ya dhamiri za Babu juu ya nchi. Tokeo la pili la mipango ya makomredi ya kutaka kuleta mgawanyiko katika chama, lilifanyika wakati ambao Babu alikuwa kafungwa gerezani. Wakati huo makomredi walikuwa wakipita mitaani, vichochoroni na mabarazani kutangaza propaganda zao kuwa waongozi wa Serikali ya ZNP/ZPPP khasa Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Ali Muhsin walishirikiana na wakoloni kumfungisha Babu. Walikitangaza hayo, wakiamini kuwa umma wa Hizbu ýutasadiki udanganyifu wao na kuwaona waongozi wao wa Hizbu kuwa ni wenye nia mbaya na si wakweli. Ikiwa hali ndivyo hivyo, umma wa Hizbu utawaamini na kuonekana wao makomredi kuwa ndiwo wenye kufaa kuongoza. Walijitahidi kuitapakaza sumu hiyo Unguja na Pemba, mjini na mashamba kwa kila njia na hila. Lakini umma wa Hizbu na ZPPP haukuwa rakhisi kusadiki maneno ya sio kuwa na msingi wala ushahidi, kama hayo. Umma daima ulikuwa ukisikiliza na kuzingatia maneno na khabari zisemwazo mitaani na nyenginezo. Ulikuwa ukitumilia matawi ya chama kwa mashauriano, wakitoa rai, wakizijadili wenyewe kwa wenyewe na kuzipeleka mbele katika uwongzi wa chama. Haukuwa Umma hewalla bwana. "Ulikuwa ukiambiwa ukijiambiya"

24

KUFUNGWA GEREZANI KWA SEYYID ABDULRAHMAN BABU Serikali ya kikoloni ilikuwa daima dawamu dhidi ya misingi na msimamo wa Chama cha Hizbu, haikutokea hata mara moja kukipa uso mzuri. Kwa vile hawakupendelea kiendelee, kila wakati walikuwa wakikitafutia kila njia ya kukivuruga ili kisiweze kuwa na nguvu, na ikiyumkinika hata kitoweke kabisa. Lakini kila wakizidisha njama zao ndio umma ukizidi kuwafahamu na jitihada zao zikifeli. Babu wakati huo alikuwa ni miongoni mwa waliyokuwa hawapendiza machoni mwa wakoloni, kwa hivyo naye pia alikuwa katika mipango ya njama zao. Walipopata kipengee kutokana na makala aliyoyaandika katika gazeti lake la ZANEWS, wakoloni waliona sasa mtego wao umeweza kumnasa Babu. Pia waliona kuwa natija yake itafaa kutumika dhidi ya Hizbu. Wakoloni walimshitaki Babu kwa kosa la kuwa makala yake ni matusi ya kumtukana Mkuu wa Polisi kwa jambo la uwongo wala si kwa maslahi ya umma. Kamati Kuu ya Hizbu bali hata wananchi wengi ilifahamu wazi kuwa wakoloni wamechukua khatua hiyo ya kumshitaki Babu si kwa sababu yoyote illa ni kutaka kukidhoofisha Chama katika wakati muhimu kama huo katika juhudi za ugombozi wa nchi kutokana na ukoloni.

Kamati Kuu ya Hizbu iliamua kushirikiana na Babu katika kesi hiyo kwa hali na kwa mali, juu ya kuwa gazeti hilo la ZANEWS halikuwa gazeti la Chama bali lilikuwa la Babu binafsi. Gazeti hilo likilipiwa na Shirika la Kichina liitwalo "Hsinhua Chinese News Agency". Kutokana na mipango yake, Babu aliweza kupata wakili kutoka Uingereza aliyejitolea kumsimamia katika kesi hiyo bila ya kuchukua malipo. Wakili huyo alitaka basi alipiwe ukaaji wake katika hoteli kwa muda wa siku atazokuwepo nchini na matumizi madogo madogo. Bibi Azza Mohammed (mamewatoto wa Sheikh Ali Muhsin) alijitolea kwa niaba ya Hizbu kuzilipa gharama zote hizo. Kwa vile wakoloni walikuwa wamekwisha dhamiria kuitumia fursa hii kwa azma ya kuleta michafuko katika Chama, walitekeleza azma yao kwa kumfunga Babu gerezani kifungo cha miezi 18. Chama kilikata rufaani kwa hapo Zanzibar na baada ya kushindwa hapo, kilichukua rufaani kutoka "East African Court of Appeal" na huko pia kilishindwa na Babu aliendelea na kifungo chake kwa muda wa miezi 18, kama ilivyokwisha pangwa.

KUTOLEWA GEREZANI BABU Baada ya Babu kumaliza kifungo chake, alitolewa gerezani mnamo saa nne za usiku na ilikuwa kwa njia za siri siri. Jambo ambalo si la kawaida.

"BABU'S WEEK" Chama cha Hizbu kwa furaha ya kutolewa Katibu wake kifungoni kwa salama, kiliandaa mapokezi yake kwa sherehe kubwa kubwa. Sherehe hizo zilikuwa kwa muda wa wiki mbili, wiki moja zilifanywa Unguja na wiki ya pili zilifanywa Pemba. Kwa kusherehekea siku hio, Makao Makuu ya Chama na Matawi yake yote, Unguja na Pemba, mjini na mashamba, yalipambwa kwa mabendera na mataa ya kila rangi. Sherehe hizo zilikuwa kwa kusomwa Maulidi, kwa Dhikiri, kwa magoma na hata kwa mashindano ya ngalawa. Babu akibebwa juu ya mabega ya wananchi na huku kukiimbwa "SOTE TWAMPENDA BAABU!". "Babu's Week" (wiki ya shereha za kufunguliwa Babu) ya Unguja ilimalizika kwa Hizbu kufanya karamu kubwa katika uwanja wa Bustani ya Seyyid Khalifa Hall (sasa ati inaitwa Karume House). Baada ya hapo, Babu alikwenda Pemba na huko alifanyiwa kama alivyofanyiwa Unguja na zaidi. Wananchi wa Ziwani kwa furaha zao, walimtunukia Babu awe ni mgombea kiti cha jimbo lao la Ziwani katika uchaguzi wa 1963. Kiti hicho kilikuwa ni kiti cha hakika kwa ushindi wa Hizbu.

BABU NA FISADI YAKE YA MWISHO Babu alirejea kutoka Pemba siku ya Jumaane kiasi cha saa mbili za usiku. Usiku huo huo, alikutana na kamati ya uchaguzi ya Chama. Kamati hiyo ilimkabidhi Babu orodha ya wagombea uchaguzi wa Hizbu katika Unguja kama walivyo teuliwa na majimbo yao kwa mjini na kwa mashamba. Babu baada ya kupokea orodha huo, naye alitoa orodha wa wagombea uchaguzi wa Hizbu kwa Pemba, naye akiwa ni miongoni mwao. Kamati ilifurahikiwa na matokeo yalivyokwenda vizuri kukhusu uteuwaji wa wagombea uchaguzi, Unguja na Pemba.

Siku ya pili yake, Jumaatano, Kamati Kuu ya Hizbu ilikutana. Babu alitoa ripoti yake ya Pemba na kuiarifu Kamati Kuu kuwa yeye ameteuliwa kuwa mgombea wa kiti cha Ziwani Pemba. Kamati Kuu ilifurahikiwa na matokeo yote yaliyotokea Pemba. Baada ya kumaliza hayo, Babu alisema: "Jana usiku nilipofika tu, nilikutana na Kamati yetu ya uchaguzi nao walinikabidhi orodha wa majina ya watetezi

25

(wagombea uchaguzi) "kama walivyo teuliwa na majimbo yao hapa Unguja". Aliendelea kueleza, "Kutokana na namna kinavyoonekana Chama chetu na baadhi ya watu hapa na nje ya nchi kuwa ni Chama cha Kiarabu, nimeonelea bora safari hii tufanye mabadiliko katika kuwasimamisha watetezi wetu kwa uchaguzi huu ujao", alisema Babu. Katika kuendelea na maneno yake Babu alieleza kuwa mabadiliko hayo atakayo kuyaleta, anayaleta kwa ajili ya maslahi ya Chama. Babu alianza kwa kusema kuwa, "Safari hii, tumuondoe Sheikh Ali Muhsin katika jimbo la Malindi na tumpeleke katika jimbo la Tumbatu na aombwe Sheikh Nyakanga (aliyeteuliwa kuwa mtetezi wa jimbo hilo la Tumbatu), yeye safari hii apumzike asisimame. Jimbo la Shangani, safari hii tumuweke Sheikh Juma Aley, pahala pake (yaani jimbo la Nungwi) tumpeleke Sheikh Muhsin Abeid. Sheikh Amirali AbdulRasool, yeye aondoke Shangani aende akasimame katika jimbo la Mlandege, na Sheikh Ibuni Saleh aondoke hapo Mlandege aende akasimame katika jimbo la Kikwajuni. Jimbo la Bumbwini safari hii tulipe Chama cha FPTU., (Fedaration of Progressive Trade Unions) ( chama hichi kilitumika wakati huo kuwa ni kichakachawatoro kwa wakubwa na wengi wa wafuasi wa kilicho dhihiri baada yake kuwa ni Umma Party, yaani makomredi) wao wenyewe watamteuwa anaefaa kusimama huko. Sheikh Haji Muhammadi aombwe safari hii apumzike."

Jambo la kustaajabisha juu ya mapendekezo hayo aliyoyaleta Babu ni kuwa yeye yeye Babu baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwanzo wa 1957, ndiye alieleta mapendekezo katika Kamati Kuu ya Chama ya kutaka uwezo wa kuwateuwa wagombea wa uchaguzi uwachwe katika mikono ya Matawi na majimbo ya Hizbu wenyewe. Kamati Kuu isiwe na uwezo wa kuwateulia wagombea uchaguzi, ila iwe na uwezo wa kutoa nasaha tu pindi ikihitajika. Mpango huu ulikubalika na ukawa unatumika tokea wakati huo, hata ukaweza kuzuiya mwana kamati, Bwana Rutti Bulsara kutokuteuliwa na jimbo la Mkunazini na matokeo yake yalimpelekea Bwana Bulsara kukiacha Chama cha Hizbu. Baada ya miaka sita tu Babu huyo huyo na bila hata ya kushauriana na wenziwe na kutaka pafanywe mabadiliko ameleta mapendekezo kinyume kabisa na yale aliyoyaleta mwanzo na yakawa yamekubalika na yakawa yanatumika.

La kustaajabisha zaidi ni kuwa kufuatana na matakwa hayo ya Babu, basi ingekuwa waondolewe katika utetezi Watumbatu wawili, watu wa watu na wenye uzito mkubwa katika chama, nao ni Sheikh Haji Muhammad na Sheikh Nyakanga, na wote hawa wawili sio katika waliokuwa wakiitwa Waarabu. Jee kufanya hivyo ndio kuondosha kufikiriwa kuwa Hizbu ni chama cha Waarabu? Hapana shaka sivyo! Lakini ilivyo khasa ni kuwa matokeo ya kufanya hivyo wazee na ndugu zetu wengi Wakitumbatu wangetoka katika Hizbu, na Hizbu sio kuwa ingalilikosa jimbo la Tumbatu tu, bali ingeliweza kukosa hata majimbo mengine. Hayo ndio makusudio, na hayo yangemfurahisha mkoloni, Nyerere, Karume na yeye Babu mwenyewe. Na kumwondoa Sheikh Juma Aley mwenye asili ya kiArabu, kutoka jimbo la Nungwi na kumpeleka mjini majumba ya mawe ndio kuonesha kuwa Hizbu si chama cha Waarabu? Mipango hii yote ni mpingano wa hakika (contradictions).

Baada ya Babu kumaliza kuyataja mabadiliko yake hayo, Halmashauri Kuu ya Hizbu kwa muda wa dakika mbili mpaka tatu, ilikuwa kama imepigwa sindano ya ganzi. Kila mmoja alikuwa akimtizama mwenziwe kwani kila mmoja ilikuwa ikimpitia moyoni mwake kuwa yakifanyika mabadiliko haya, basi Hizbu lazima itashindwa katika uchaguzi huu. Khasa kwa vile wakati uliyobakia mpaka siku inayotakiwa kupeleka majina ya wagombea uchaguzi mbele ya Mrajisi, ulikuwa ni mdogo sana. Na vilevile muda wa kutoka hapo mpaka kufikilia uchaguzi wenyewe ulikuwa umebaki mdogo. Pili, vipi itawezekana baada ya kuwapa uwezo wana wa matawi na wa majimbo ya Chama wa kuwateuwa wagombea uchaguzi wao, na baada ya kukubaliwa na Kamati Kuu ikawa ghafla Kamati Kuu imegeuka na imewateuliya watu wengine kabisa tena bila ya hata ya kushauriwa. Si litazuka fujo katika Chama? Majadiliano yalikuwa makali sana siku hiyo. Babu na watu wake wawili watatu waliyokuwa daima, "sawa Babu" upande wao, na waliyobakia wote upande wa pili. Kila aliyesimama kusema, alipinga vikali mapendekezo hayo, ambayo natija yake sio hata kidogo maslahi ya chama. Babu alipoona kuwa hapana aliyemuunga mkono isipokuwa hao hao watu wake wawili, watatu, alitaka apewe ruhusa ayapitiye majimbo yote ya mjini na ya mashamba awaeleze mabadiliko ayatakayo. Na alisema anaamini kuwa wote watamkubalia mabadiliko hayo. Lakini, alitaka Kamati isimchagulie wa kufuatana nao bali yeye mwenyewe atawachagua wa kufuatana nao.

26

Hapo alisimama Sheikh Muhammed Aboud Mkandaa na alimwambia Babu, "Hichi Chama si chako wala si cha yoyote kati yetu. Sisi sote ni watumishi wa umma, kwa hivyo shauri yako itazingatiwa. Amma suala la nani utafuatana nao hilo litakuwa juu ya Kamati Kuu kulifikiria na vyovyote itavyokuwa haitokuwa uwachiwe peke yako uchague utakavyo". Maneno hayo ya Sheikh Muhammed Aboud yaliungwa mkono na wote waliokuwepo hapo. Ilipofika saa tatu za usiku bila ya kupatikana mafanikio yoyote, mmoja kati ya wana kamati alitoa shauri ya kutaka mkutano usitishwe mpaka siku ya pili. Shauri hili lilikubaliwa na wote. Vile vile ilitolewa shauri kuwa huo mkutano wa siku ya pili, ukafanywe kwenye nyumba ya Bwana Udi, huko Migombani. Shauri hiyo nayo ilikubaliwa na wote. Shauri ya tatu iliyotolewa na kukubaliwa ilikuwa wakutane Babu na Sheikh Ali Muhsin kabla ya huo mkutano wa Kamati ili wayadurusu yote hayo, kwa kuzingatia faida na khasara zake. Kisha itapokutana Kamati Kuu waweze (Babu na Sheikh Ali) kutoa ripoti ya natija ya mkutano wao.

Siku ya pili, Alkhamis, Kamati Kuu ilikutana Migombani kwa Bwana Udi. Babu alisema, "Tunasikitika kuwa hatujawahi kukutana kwa nafasi kwa sababu zimetokea dharura za lazima. Tunaomba tupewe nafasi nyengine leo tuweze kukutana na kesho Ijumaa tutaleta ripoti yetu". Ombi hilo lilikubaliwa na mkutano uliakhirishwa mpaka siku ya pili.

Siku yapili yaani Ijumaa, Kamati Kuu ilikutana Migombani na Babu alitoa ripoti kwa kusema, "Tumekutana mimi na Sheikh Ali na tumezungumza kwa urefu na kwa usafi kabisa na tumekubaliana kuwa mabadiliko niliyoyapendekeza ni mazuri lakini kwa wakati ulivyofika hivi sasa, tumeonelea bora tuakhirishe kuleta mabadiliko hayo mpaka katika uchaguzi wa siku za mbele. Jambo moja nilimuomba Sheikh Ali, naye hakulikataa lakini amenitaka nililete mbele ya kikao hiki ili liweze kupata muwafaka wa wote. Jambo lenyewe ni la kumuombea kijana wetu Sheikh AbdulRazak Musa (Kwacha), apewe kiti chenye uhakika wa ushindi, na mimi (Babu) napendelea apewe kiti cha Tumbatu". Kwa hakika Kamati Kuu ilishusha pumzi na waliona kama wameutua mzigo mkubwa uliokuwa mabegani mwao. Mwenyekiti wa mkutano huo na Naibu Rais wa chama, Maalim Zaid Mbaruk alisema, "Kabla hatujalizungumza suala hili, kwanza ningependa nimuulize Sheikh Nyakanga, kwani yeye ndiye aliyeteuliwa na watu wa Tumbatu awe mgombea wao". Sheikh Nyakanga alijibu kama hivi, "Mimi sikuingia katika Hizbu kwa ajili ya kutaka cheo cha namna yoyote. Lakini sitoweza kujibu kuwa nimekubali kumuachia kiti Sheikh AbdulRazak kwani kiti si changu mimi. Mimi kwa nafsi yangu nikotayari kukiacha lakini nikifanya hivyo hapa hapa tu, itakuwa nimewadharau wenzangu waliyonichaguwa niwe mgombea wao. Kwahivyo, shauri yangu naona bora uchaguliwe ujumbe wa watu wachache hivi leo tuondoke tukalale Tumbatu, ili tupate nafasi ya kutosha ya kuzungumza na wazee pamoja na vijana wa Tumbatu. Uamuzi utakuwa juu yao. Mimi naahidi kuwa nitasaidia kama nitavyoweza katika kuwafahamisha ndugu na watoto wangu wa Tumbatu".

Baada ya kumaliza Sheikh Nyakanga, alisimama mwana wa Kamati Sheikh Khamis wa Bumbwini ambayo ni sehemu muhimu ya jimbo la Tumbatu. Sheikh Khamis alisema, "Ndugu zangu, mimi ni Mtumbatu na ninazielewa uzuri hisia za Watumbatu wenzangu zilivyo juu ya uchaguzi huu na juu ya mgombea wao mzee Nyakanga. Kama tutavyowaeleza wenzetu wa Tumbatu, maadamu itakuwa kumuondoa mzee Nyakanga basi naapa hata ikiwa atapelekwa Zaim Ali Muhsin, Wallahi, tutakikosa kiti. Ushindani uliopo baina ya Hizbu na AfroShirazi kukhusu kiti cha Tumbatu ni mkubwa sana. Mimi natoa shauri kuwa mzee Nyakanga asibadilishwe kwa wakati huu". Hapo palikuwa kimya kwa muda. Hapana aliyeweza kusema lolote ila kila mmoja alikuwa akilichemsha bongo lake. Babu alianza kusema na alieleza, "Naona watu wote wamenyamaza kimya na hii ni ishara kuwa haya yaliyosemwa na Sheikh Khamis yanakubalika. Kwa hivyo, mimi naona hapana faida ya kupoteza wakati. Mimi naondoka na tutakutana siku ya Jumaapili asubuhi". Babu alitoka katika mkutano. Mwenyekiti wa mkutano alimnasihi Babu asiondoke bali abakie katika mkutano wapate kuyazungumza masala haya kwa upole zaidi, lakini hakufanikiwa. Babu alitoka mkutanoni na kwenda zake. Kamati Kuu ilibakia na iliendelea na kuyazingatia kwa uangalifu na utaritibu masala ya kiti cha Tumbatu na Babu kutoka katika mkutano kwa hasira. Hapana uamuzi uliyofikiliwa, Mwenyekiti Maalim Zaid Mbaruk alimtaka Sheikh Ali Muhsin ajaribu kukutana na Babu ili wazungumze kwa kutafuta maslahi ya Chama.

Siku ya Jumaapili kuanzia saa mbili za asubuhi waongozi wa Hizbu wa majimbo yote ya Unguja, wake

27 kwa waume walimiminika katika uwanja wa jumba la Bwana Udi, Migombani. Siku hiyo ya Jumaapili ilikuwa ndio siku ya kila jimbo kuthibitisha mbele ya Kamati Kuu ya Chama juu ya mgombea wao waliyemteuwa kupigania uchaguzi katika jimbo lao. Wakati ulipofika, Babu aliukhutubia umma uliyohudhuria hapo kama hivi: "Leo napenda kukuarifuni wananchi kuwa nimeamua kukiacha mkono Chama changu cha Hizbu na nitawataka radhi wananchi wa Ziwani Pemba kwa ukarimu wao wa kunitaka mimi niwe mtetezi wa jimbo lao. Mimi niliwakubalia, lakini kwa kutokana na hali zilizonitokea baadae, nasikitika kuwa nimekuwa sina budi ila kuwataka msamaha. Sababu zilizonipelekea kuamua kukiacha Chama changu ni baada ya kugundua kuwa waongozi wenzangu hawana imani na mimi hata wameweza kushirikiana na wakoloni kunifungisha gerezani kifungo cha miezi kumi na nane. Baada ya kutoka gerezani, nawaona wenzangu wameniwekea vijana wa Youth wananifuata na kunichungua kila ninalolifanya na kila ninao zungumza nao hutaka kujua nazungumza kitu gani. Kwanini yakafika hayo, hata mimi mwenyewe nashindwa kufahamu. Hivi karibuni baada ya kurejea kutoka Pemba, nilipeleka mbele ya Kamati Kuu mapendekezo kukhusu kusimamishwa kwa watetezi katika majimbo ya uchaguzi wa safari hii. Mapendekezo hayo, nimeyapeleka katika Chama kwa ajili ya maslahi ya Chama chetu. Bahati mbaya wenzangu bila kuyazingatia kwa makini, wameyapinga mapendekezo hayo. Kwa ajili ya kukhofia yasitokee mambo yatayoweza kusababisha mvutano baina yetu, niliamua kuyaweka upande mapendekezo hayo bali niliwaomba wenzangu vile vile kwa ajili ya maslahi ya Chama kuwa kiti cha Tumbatu safari hii tumsimamishe ndugu yetu Sheikh AbdulRazak Kwacha. Hata hilo nalo limepingwa kwa kutolewa kila sababu na kila hoja. Kutokana na hali kama hizo, nimeona hapana haja ya kubakia katika Chama ambacho hakimsikilizi Katibu wake na mwongozi wake. Kuanzia leo nakuageni. "Kwakherini".

Babu aliteremka na alitaka kuondoka lakini, Mwenyekiti wa jimbo la Mkunazini, Sheikh Muhammed Othman, alimuomba asubiri asiondoke. Sheikh Muhammed alisema "Tumemsikia Seyyid AbdulRahman Babu alivyotueleza lakini ilivyokuwa wengi wetu si katika Halmashauri Kuu ya Chama, basi yote hayo aliyoyaeleza Babu kwetu ni mageni. Ningependa kumuomba Zaimu Sheikh Ali Muhsin akiwa yeye ndiye mwongozi wa Chama na kwa hakika ndiye tunayemuona mwenziwe sana Babu, aje naye kutuelezea ili na sisi tupate kutoa nasaha zetu". Sheikh Ali alisimama na alisema, "Leo, ni siku ngumu sana katika maisha yangu. Kwani, haikunipitikia kuwa itaweza kutokea siku nimsikie ndugu yangu Babu akisema maneno kama hayo aliyoyasema. Kwa lipi hilo kubwa liliopo kati yetu na Babu hata tufike kushirikiana na wakoloni kumfungisha gerezani? Babu anaelewa uzuri kuwa Serikali yetu hii tuliyonayo haina uwezo wa kufanya lolote lenye maana. Na anaelewa uzuri kuwa kufungwa kwake ni miongoni mwa njama za wakoloni za kutaka kukidhoofisha Chama chetu. Sikutaraji kuwa mtu kama yeye Babu ataweza kuchezeleka akili zake kiasi kama hiki. Wakoloni siku zote wakitutafutia njia za kutufarikisha baina yetu na Babu, na kila njia wamezitumia lakini hawakuweza kufuzu. Walipopata fursa hii ya makala aliyoyaandika Babu katika gazeti lake la ZANEWS, makala amabayo wao wakoloni wameyafasiri kuwa ni ya jinai, na kumshitaki Babu binafsi, wala si Chama, lakini juu ya hivyo, Chama kimesimama pamoja naye kwa hali na mali. Linalo nistaajabisha ni kuwa Babu anavunja ile misingi aliyoijenga yeye na sote pamoja, nayo ni mwendo wa kidimokrasi. Waongozi sio wa kukata shauri, wao ni kufunza na kuongoza. Wa kukata shauri ni umma. Leo umma umeamua yeye anaudhika na anataka kukiacha Chama kwa kuwa umma haukumfuata yeye au mimi".

Baada ya kuteremka Sheikh Ali kulikuwa kimya kwa kiasi cha muda, kila mmoja alikuwa akinon'gona na mwenziwe. Hapo alisimama kijana mmoja katika waliyokuwa wakijiita, "progressive", Bwana Kadiria Mnyeji na kusema kama hivi, "Wazee wangu na ndugu zangu nakuombeni mufahamu kuwa mapendekezo haya aliyoyataka Babu kuyaleta katika kusimamishwa kwa watetezi wa uchaguzi wa safari hii ni kwa ajili ya maslahi ya Chama, kwani uchaguzi huu ni muhimu sana na inahitaji kuwapeleka watu wenye uwezo kweli kweli kwa kupambana na mkoloni ana kwa ana. Wazee wameshafanya kazi yao. Sasa ni wakati wa vijna".

Pema palikuwa hapo, Kadiria alijikuta akivutwa mashati na kuteremshwa chini bila ya mwenyewe kutaka. Hapo wazee khasa wazee wa mashamba, walianza kufungua masikio yao na kusema kuwa, "Hivyo, haya ndio makusudio yenu?" "Mnatuona sisi wazee tushakuwa hatuna tena letu jambo!" Hewa kwa wakati huo ilikuwa si nzuri hata kidogo. Kila mmoja alikuwa akichemka. Hali ilipotengenea, baadhi ya wazee walizungumza na Babu kando na kumnasihi. Wazee wa Tumbatu walifika kumwambia

28

Babu, "Tunakuomba kwa hivi sasa mwachie mzee Nyakanga asimame Tumbatu na tunakuhakikishia kuwa kiti cha Tumbatu tutakichukua. Akishaingia mzee Nyakanga katika Baraza ya Taifa kiasi ya vikao viwili mpaka vitatu, atajiuzulu na wakati huo, mlete umtakaye na tunakuahidi tutampa kura zetu kama tutavyompa mzee Nyakanga". Babu alisema nimesikia na alinyamaza kimya. Baada ya muda Babu alipanda na alisema, "Wazee wamenipa fikra zao za kunitaka nibadilishe msimamo wangu lakini nasikitika sitoweza kufanya hivyo na sasa, kwakherini". Babu aliteremka na kwenda zake na kufuatiwa na vijana wake wawili, watatu ambao hata hawakujaa gari ndogo.

Kwa kiasi cha muda umma ulifadhaika, kulikuwa kimya kabisa hata sindano ingeanguka, ingeliweza kusikilizana mshindo wake. Kila mmoja alikuwa akiona khatari ya kushindwa katika uchaguzi imetukabili. Hali ilivyokuwa hivyo, alisimama Rais wa HizbulWattan, Sheikh Vuai Kitoweo na alisema, "Ikiwa yuko mwenzetu yoyote aliingia katika Hizbu kwa ajili ya kumfuata Babu, basi Babu mumemsikia na mumemuona mbele ya macho yenu kutoka katika mkutano kwa kuwa amekiacha Chama. Basi aliyeingia katika Chama kwa kumfuata Babu, ikiwa anapenda kumfuata Babu, hazuiliwi. Ama aliyeingia kwenye Hizbu kwa kufuata siasa ya Chama na msimamo wake wa kugombania Uhuru wa nchi hii kwa ajili ya maslahi ya nchi na wananchi wake, basi Hizbu ipo, na HAY na itaendelea kuwa HAY". Kutokana na kauli hiyo ya Rais wa Hizbu, umma ulipata uhai mpya na kila mmoja alianza kufikiria umuhimu wa kusimama imara na chama khasa ilivyokuwa uchaguzi ulikuwepo machoni. Baada ya hapo mkutano uliendelea kama ilivyokuwa umepangwa kwa siku hiyo na ilikuwa kama hapakutokea lolote. Haya ndiyo ya dhahiri yaliyokuwa yametokea na kuweza kumpelekea Babu kukiacha Chama cha Hizbu. Mengineyo yote yaliyokuwa yakisemwa na yanayosemwa mpaka hivi sasa ni UZUSHI wa makusudio kwa kutaka kufikilia lengo lao maalumu hao watangazao uzushi huo. Babu hakuweza hata mara moja tangu alipotoka katika Hizbu mpaka hii leo kueleza khasa sababu za kutokea katika chama. Kama ilivyokuwa hajaweza kueleza sababu zilizomfanya kuungana na AfroShirazi kuiondowa serikali iliyochaguliwa na umma kwa kupitia uchaguzi huru.

KIPI KILICHO MPELEKEA BABU KUCHUKUA KHATUA KAMA HIZO Kama nilivyotangulia kusema, Babu alikuwa na dhamiri zake ambazo alifikiria ataweza kuzitekeleza kwa kukitumilia Chama. Alipoona kuwa kila alilojaribu kulileta, halikuweza kufuzu, ndipo alipochukua khatua kama hizo na katika wakati kama huo. Babu alikhadaika kwa maneno aliyokuwa akiambiwa na hao wafuasi wake wajiitao "progressives" wakati alipokuwepo kifungoni. Maneno waliyokuwa wakimpelekea baada ya wao kuwa wakipita wakitangaza propaganda dhidi ya uwongozi wa Hizbu, ni kuwa, "Umma wote wa Hizbu upo nyuma yako na kama utavyoamua baada ya kutoka kifungoni, ndivyo na wao watavyofuata. Ukiamua kutoka katika Chama, basi Umma utakufuata na ukiamua kubakia, nao utabakia na wewe".

Kutokana na mapokezi aliyofanyiwa Babu alipotolewa gerezani, aliona yote aliyokuwa akiambiwa na hao watu wake, yalikuwa ni mamneno ya hakika. Vilevile kulikuwepo na mipango ya chini kwa chini baina ya wenye kujiita "progressives" waliyokuwemo katika upande wa Hizbu na waliyokuwa wakijiita "progressives" upande wa AfroShirazi ya kutaka pindi wakiweza kushinda katika viti vyao vya uchaguzi waweze kushirikiana katika kuleta pendekezo litaloweza kupelekea kuanguka kwa Serikali, ili waweze kupata nafasi ya kufanya Serikali nyengine itayo kuwa na mwenendo wautakao wao, ati wa ki"progressive". Na hayo yangelimfurahisha China iliyokuwa ikimpa Babu mshahara uliokuwa kasoro kidogo na wa Mfalme. Babu akipata kutoka China kila mwezi Shs.15,000 safi na Mfalme akipata Shs. 20,000 ghafi.

Hayo yalipokuwa hayakuweza kupatikana, ndipo Babu alipojitoa katika Chama kwa kufikiria kuwa umma wa Hizbu utamfuata pamoja naye. Alipoona hayakuwa kama hivyo, ndipo alipoanzisha chama chake cha Umma Party na baadae kujiunga pamoja na wageni kama Okello na Mfaranyaki na wenziwe katika mavamizi ya nchi yake na kuiondoa Serikali ya halali iliyokuwa imechaguliwa na Umma kwa kutumia haki yao ya demokrasi ya "One Man One Vote". Alifanya hivyo akiwa bado anatarajia kuwa atachukuwa fursa hii kwa kutekeleza utumishi wake, yaani kuipeleka nchi huko kunakoitwa kwa "progressives". Hapa pia Babu alipoteza turufu yake, na hii ilikuwa ndio ya mwisho; hakuweza kutimiza utumwa wake! Kilipoingia kinyang'nyiro juu ya Zanzibar, Mwalimu Nyerere kwa uwalimu wake na kwa vile makucha yake ni makubwa zaidi, ndiye pekee aliyefuzu.

29

UCHAGUZI WA JULAI 1963 Huu ni uchaguzi wa mara ya nne kufanyika Zanzibar katika muda wa miaka sita (1957 1963). Uchaguzi huu ulifanyika baada ya muda mfupi tokea kupatikana Serikali ya Ndani (Internal Self Government) na tokea Babu kutoka katika chama cha Hizbu. Uchaguzi ulikuwa wa viti vyote 31 vya Baraza ya Taifa (National Assembly) na ulifanyika kwa usalama. Matokeo ya uchaguzi huo ilikuwa ni kupata ushindi Muungano wa Hizbu na ZPPP kwa kupata viti 18 na AfroShirazi kupata viti 13.

NYERERE ANASEMA WAKOLONI WALIPENDELEA KUIACHA SERIKALI YA ZANZIBAR MIKONONI MWA HIZBU Kweli, Waswahili wanasema, "Apendae, chongo huita kengeza". Katika uchaguzi huo wa "Mtu Mmoja Kwa Kura Moja" (One Man One Vote), katika viti 31 Muungano wa Hizbu na ZPPP ulipata viti 18 na AfroShirazi walipata viti 13. Sasa Mwalimu nani aliyepata viti vingi kuliko mwenziwe hapo hata astahiki kuendesha serikali? Au ulitaka serikali wapewe AfroShirazi kwa hivyo viti vyao 13, ndio ungeona kuwa imefanywa haki?! Mwalimu Nyerere anaelewa vizuri kuwa nidhamu za uchaguzi alizokuwa akizitumia Muingereza katika nchi alizokuwa akizitawala ni sawa na nidhamu anazotumia katika chaguzi za nchi yake. Nidhamu za Muingereza juu ya uchaguzi ni zenye kutizama mtetezi aliyepata kura nyingi zaidi kuliko mshindani wake katika lile jimbo lake la uchaguzi. Hazitizami hata chembe juu ya wingi wa kura zilizo patikana katika chama kwa jumla. Kura walizopata Labour Party katika uchaguzi uliopita ni nyingi sana kuliko kura walizopata Chama cha Conservative lakini, Labour hawakuweza kuunda serikali kwa sababu viti walivyopata Conservative ni vingi kuliko walivyopata Labour Party. Sasa mbona Labour hawasemi kuwa Malikia amewapendelea Conservative? Na hivyo, ndivyo ilivyokuwa katika chaguzi zilizofanyika Zanzibar. Wingi wa kura kwa jumla wamepata AfroShirazi ni hakika lakini hawakuweza kupata wingi wa viti. Ina maana kuwa katika baadhi ya majimbo, Hizbu na ZPPP, wameweza kukubalika na Umma kuliko walivyokubalika AfroShirazi. Na katika baadhi ya majimbo, AfroShirazi wameweza kukubalika zaidi kuliko Hizbu na ZPPP na hiyo ndiyo demokrasi ya kweli. Lakini ni majimbo mengi zaidi, (nayo ni 18) yaliyochaguwa ZNP/ZPPP kuliko yaliyochaguwa ASP (nayo ni 13).

Lenye kufaa kuzingatiwa ni kuwa chaguzi zote zilizofanywa visiwani Zanzibar, ziliendeshwa kwa njia ya demokrasi. Kila Chama kilikuwa kimeridhika na mwendo uliyokuwa ukiendeshwa na kiliridhika na matokeo ya uchaguzi. Haijapata kutokea hata mara moja kwa Chama au kwa mgombea kupeleka malalamiko yake kwa mkuu wa uchaguzi, kabla au baada ya kutolewa kwa natija ya uchaguzi. Aliyeshinda, amejua kuwa ameshinda kwa haki na aliyeshindwa, amejua kuwa ameshindwa kwa haki. Kila mtu alikuwa na ruhusa ya kushtaki, na hapana MAfro mmoja aliyeshtaki. Kinyume na nchi za jirani zetu pamoja na nchi yake yeye mwenyewe Mwalimu huko Tanganyika. Kila unapomalizika uchaguzi lazima patokee baadhi ya wagombea kulalamika na kufanya kesi juu ya matokeo ya uchaguzi. Hayo yanaonesha kuwa kuna tendeka mapendeleo namna fulani juu ya wagombea fulani. Jee, Mwalimu, umepata kusikia hayo kufanyika Zanzibar baada ya matokeo ya uchaguzi? Hayajawahi hata mara moja! Hayo hayakutokea Zanzibar kwa sababu Hizbu na ZPPP hawana uroho wa madaraka, imani yao ni kushiriki kila mwananchi katika kutumikia nchi yake, kila mmoja kwa uwezo wake. Katika uchaguzi wa 1957, Hizbu walipata kura 1/3 ya jumla, nao hawakupata hata kiti kimoja. Mbona hawakulalamika na kudai kuwa haki yao ni kupata viti viwili katika sita?

MKUTANO WA KATIBA YA UHURU. Muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Julai 1963, Serikali ya Kiingereza ilizialika pande zote mbili yaani Upande wa Serikali ya ZPPP/ZNP na Upande wa Upinzani wa AfroShirazi kuhudhuria kwenye mkutano wa mazungumzo ya Katiba ya Uhuru wa Zanzibar. Kabla ya pande mbili hizo kwenda Uingereza kwa mazungumzo hayo, Balozi wa Kiingereza wa Zanzibar Sir George Mooring, alianzisha mkutano baina ya Serikali na Upinzani hapo hapo Zanzibar kwa kurakhisisha baadhi ya mambo. Mkutano huo uliendelea kwa muda na palikuwepo mashirikiano mazuri baina ya pande zote mbili. Wakati ulipowadia, wajumbe wote wa Serikali na wa Upinzani walikwenda Uingereza na huko walizungumza kwa kufahamiana na kukubaliana katika kila kifungu bila ya kutokea pingamizi za namna yoyote. Hii ilikuwa ni ishara njema. Lakini jee hakika ya mambo ndivyo ilivyokuwa? Kwa kuvamiwa nchi mwezi tu baada ya uhuru huwenda mtu akaunganisha hili na lile akatoka na natija kuwa mipango ya kuivamia Zanzibar ilikuwa tayari kabla ya Uhuru, na ndio maana ikawa rahisi katika mkutano huu kukubaliana

30 bila ya pingamiza. Kinyume na kawaida ya viongozi wa AfroShirazi. (kama ilivyothibitisha Taarikh). Wao siku zote wakisema "zuiya"!

UHURU WA ZANZIBAR Manamo saa sita na dakika moja za usiku wa kuamkia taarikhi 10 Disemba 1963, bendera nyekundu tupu iliteremshwa kutoka kwenye mlingoti wake na Bendera ya Dola Huru ya Zanzibar yenye karafuu mbili ilipandishwa na kupepea katika mlingoti uliokuwepo kwenye ardhi ya nchi katika uwanja wa Mivinjeni (Coopers Insititute), uwanja huo hivi sasa ati unaitwa "Uwanja wa Maisara". Tafauti na koloni nyengine za Muingereza, Zanzibar haikuwepo bendera ya Kiingereza kuteremshwa, kwa sababu haikupatapo kupepea juu ya ardhi ya Zanzibar. Japokuwa ilitiwa chini ya himaya ya Kiingereza, haikuwa koloni kama vile koloni nyenginezo za Kiingereza, Zanzibar haikusita kuwa Dola kwa muda wote huo.

SHEREHE ZA UHURU Wananchi wote wakubwa na wadogo waliupokea Uhuru wa nchi yao kwa kumshukuru Mwenye Enzi Mungu na kwa furaha na bashasha. Mji ulikuwa ukin'gara kwa mapambo ya namna mbali mbali. Tamasha hizi na zile zilifanywa na wananchi kwa kufurahikia uhuru wao. Sherehe na mapambo hayakuwa Mjini tu, bali mashamba kote. Matawi ya Chama nchini kote yalisherehekea sawa na ndugu zao Mjini. Na huko Pemba nako kulifanywa sherehe kama za Unguja tangu mijini na mashamba pia. Ole wetu! vitumishi vilikuwa vimeshawekwa tayari na mabwana zao kuufisidi na kuuvuruga uhuru, bali kuivuruga Nchi na wananchi wake. Sherehe hazikuwahi kumalizika, wala majasho hayakuwahi kukauka mwilini kutokana na juhudi na mbio za kugobmea uhuru wetu, bali ghafla tulijishitukia katika msiba, tushavamiwa. Na huo ulikuwa ndio kuanzia kwa maafa ya Zanzibar na kupotea kwa kila kheri yake. u kwa kutekelezeka azma na mipango yake. Hakufuzu laa Babu walaa Karume, bali haikufuzu hata ASP!

UCHAGUZI WA JULAI 1963 Huu ni uchaguzi wa mara ya nne kufanyika Zanzibar katika muda wa miaka sita (1957 1963). Uchaguzi huu ulifanyika baada ya muda mfupi tokea kupatikana Serikali ya Ndani (Internal Self Government) na tokea Babu kutoka katika chama cha Hizbu. Uchaguzi ulikuwa wa viti vyote 31 vya Baraza ya Taifa (National Assembly) na ulifanyika kwa usalama. Matokeo ya uchaguzi huo ilikuwa ni kupata ushindi Muungano wa Hizbu na ZPPP kwa kupata viti 18 na AfroShirazi kupata viti 13.

NYERERE ANASEMA WAKOLONI WALIPENDELEA KUIACHA SERIKALI YA ZANZIBAR MIKONONI MWA HIZBU Kweli, Waswahili wanasema, "Apendae, chongo huita kengeza". Katika uchaguzi huo wa "Mtu Mmoja Kwa Kura Moja" (One Man One Vote), katika viti 31 Muungano wa Hizbu na ZPPP ulipata viti 18 na AfroShirazi walipata viti 13. Sasa Mwalimu nani aliyepata viti vingi kuliko mwenziwe hapo hata astahiki kuendesha serikali? Au ulitaka serikali wapewe AfroShirazi kwa hivyo viti vyao 13, ndio ungeona kuwa imefanywa haki?! Mwalimu Nyerere anaelewa vizuri kuwa nidhamu za uchaguzi alizokuwa akizitumia Muingereza katika nchi alizokuwa akizitawala ni sawa na nidhamu anazotumia katika chaguzi za nchi yake. Nidhamu za Muingereza juu ya uchaguzi ni zenye kutizama mtetezi aliyepata kura nyingi zaidi kuliko mshindani wake katika lile jimbo lake la uchaguzi. Hazitizami hata chembe juu ya wingi wa kura zilizo patikana katika chama kwa jumla. Kura walizopata Labour Party katika uchaguzi uliopita ni nyingi sana kuliko kura walizopata Chama cha Conservative lakini, Labour hawakuweza kuunda serikali kwa sababu viti walivyopata Conservative ni vingi kuliko walivyopata Labour Party. Sasa mbona Labour hawasemi kuwa Malikia amewapendelea Conservative? Na hivyo, ndivyo ilivyokuwa katika chaguzi zilizofanyika Zanzibar.

Wingi wa kura kwa jumla wamepata AfroShirazi ni hakika lakini hawakuweza kupata wingi wa viti. Ina maana kuwa katika baadhi ya majimbo, Hizbu na ZPPP, wameweza kukubalika na Umma kuliko walivyokubalika AfroShirazi. Na katika baadhi ya majimbo, AfroShirazi wameweza kukubalika zaidi kuliko Hizbu na ZPPP na hiyo ndiyo demokrasi ya kweli. Lakini ni majimbo mengi zaidi, (nayo ni 18) yaliyochaguwa ZNP/ZPPP kuliko yaliyochaguwa ASP (nayo ni 13).

Lenye kufaa kuzingatiwa ni kuwa chaguzi zote zilizofanywa visiwani Zanzibar, ziliendeshwa kwa njia ya

31 demokrasi. Kila Chama kilikuwa kimeridhika na mwendo uliyokuwa ukiendeshwa na kiliridhika na matokeo ya uchaguzi. Haijapata kutokea hata mara moja kwa Chama au kwa mgombea kupeleka malalamiko yake kwa mkuu wa uchaguzi, kabla au baada ya kutolewa kwa natija ya uchaguzi. Aliyeshinda, amejua kuwa ameshinda kwa haki na aliyeshindwa, amejua kuwa ameshindwa kwa haki. Kila mtu alikuwa na ruhusa ya kushtaki, na hapana MAfro mmoja aliyeshtaki. Kinyume na nchi za jirani zetu pamoja na nchi yake yeye mwenyewe Mwalimu huko Tanganyika. Kila unapomalizika uchaguzi lazima patokee baadhi ya wagombea kulalamika na kufanya kesi juu ya matokeo ya uchaguzi. Hayo yanaonesha kuwa kuna tendeka mapendeleo namna fulani juu ya wagombea fulani. Jee, Mwalimu, umepata kusikia hayo kufanyika Zanzibar baada ya matokeo ya uchaguzi? Hayajawahi hata mara moja! Hayo hayakutokea Zanzibar kwa sababu Hizbu na ZPPP hawana uroho wa madaraka, imani yao ni kushiriki kila mwananchi katika kutumikia nchi yake, kila mmoja kwa uwezo wake. Katika uchaguzi wa 1957, Hizbu walipata kura 1/3 ya jumla, nao hawakupata hata kiti kimoja. Mbona hawakulalamika na kudai kuwa haki yao ni kupata viti viwili katika sita?

MKUTANO WA KATIBA YA UHURU. Muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Julai 1963, Serikali ya Kiingereza ilizialika pande zote mbili yaani Upande wa Serikali ya ZPPP/ZNP na Upande wa Upinzani wa AfroShirazi kuhudhuria kwenye mkutano wa mazungumzo ya Katiba ya Uhuru wa Zanzibar. Kabla ya pande mbili hizo kwenda Uingereza kwa mazungumzo hayo, Balozi wa Kiingereza wa Zanzibar Sir George Mooring, alianzisha mkutano baina ya Serikali na Upinzani hapo hapo Zanzibar kwa kurakhisisha baadhi ya mambo. Mkutano huo uliendelea kwa muda na palikuwepo mashirikiano mazuri baina ya pande zote mbili. Wakati ulipowadia, wajumbe wote wa Serikali na wa Upinzani walikwenda Uingereza na huko walizungumza kwa kufahamiana na kukubaliana katika kila kifungu bila ya kutokea pingamizi za namna yoyote. Hii ilikuwa ni ishara njema. Lakini jee hakika ya mambo ndivyo ilivyokuwa? Kwa kuvamiwa nchi mwezi tu baada ya uhuru huwenda mtu akaunganisha hili na lile akatoka na natija kuwa mipango ya kuivamia Zanzibar ilikuwa tayari kabla ya Uhuru, na ndio maana ikawa rahisi katika mkutano huu kukubaliana bila ya pingamiza. Kinyume na kawaida ya viongozi wa AfroShirazi. (kama ilivyothibitisha Taarikh). Wao siku zote wakisema "zuiya"!

UHURU WA ZANZIBAR Manamo saa sita na dakika moja za usiku wa kuamkia taarikhi 10 Disemba 1963, bendera nyekundu tupu iliteremshwa kutoka kwenye mlingoti wake na Bendera ya Dola Huru ya Zanzibar yenye karafuu mbili ilipandishwa na kupepea katika mlingoti uliokuwepo kwenye ardhi ya nchi katika uwanja wa Mivinjeni (Coopers Insititute), uwanja huo hivi sasa ati unaitwa "Uwanja wa Maisara". Tafauti na koloni nyengine za Muingereza, Zanzibar haikuwepo bendera ya Kiingereza kuteremshwa, kwa sababu haikupatapo kupepea juu ya ardhi ya Zanzibar. Japokuwa ilitiwa chini ya himaya ya Kiingereza, haikuwa koloni kama vile koloni nyenginezo za Kiingereza, Zanzibar haikusita kuwa Dola kwa muda wote huo.

SHEREHE ZA UHURU Wananchi wote wakubwa na wadogo waliupokea Uhuru wa nchi yao kwa kumshukuru Mwenye Enzi Mungu na kwa furaha na bashasha. Mji ulikuwa ukin'gara kwa mapambo ya namna mbali mbali. Tamasha hizi na zile zilifanywa na wananchi kwa kufurahikia uhuru wao. Sherehe na mapambo hayakuwa Mjini tu, bali mashamba kote. Matawi ya Chama nchini kote yalisherehekea sawa na ndugu zao Mjini. Na huko Pemba nako kulifanywa sherehe kama za Unguja tangu mijini na mashamba pia.

Ole wetu! vitumishi vilikuwa vimeshawekwa tayari na mabwana zao kuufisidi na kuuvuruga uhuru, bali kuivuruga Nchi na wananchi wake. Sherehe hazikuwahi kumalizika, wala majasho hayakuwahi kukauka mwilini kutokana na juhudi na mbio za kugobmea uhuru wetu, bali ghafla tulijishitukia katika msiba, tushavamiwa. Na huo ulikuwa ndio kuanzia kwa maafa ya Zanzibar na kupotea kwa kila kheri yake.

YAITWAYO "MAPINDUZI" Mafisadi wachache kwa ajili ya maslahi ya nafsi zao hawakutahayari kuchanganyika na wageni waliyokuwepo ndani ya nchi na waliyoletwa kutoka nchi za jirani kwa makusudio khasa ya kuivamia Zanzibar na kuiondoa Serikali ya wananchi. Wananchi mafisadi hao walikubali kuongozwa na wageni,

32

John Okello aliyetoka kwao Uganda, Injin aliyetoka kwao Kenya na Mfaranyaki aliyetoka kwao Tanganyika, kuivamia nchi yao katika usiku wa manane wa kuamkia taarikh 12 Januari 1964. Wananchi, mafisadi kwa sababu ya maslahi ya nafsi zao hawakuhisi uchungu kuipoteza nchi yao, wala kuzipoteza roho za wazee wao, za ndugu zao na za marafiki zao. Kwa mujibu wa kitabu cha huyo aliyejipa ujamadari wa hayo 'mavamizi' ya Januari 12, 1964, John Okello, amesema kuwa watu waliyokufa katika 'mavamizi' hayo ni 13,000. Hii ni idadi ndogo kabisa aliyopenda kuitaja. Ukatili, ushenzi na unyama uliofanywa katika visiwa hivi vilivyokuwa na ustaarabu wa kupigiwa mfano, hauwezi hata kuhadithika. Wengi waliokuwa wanaijua Zanzibar, waliona taabu kuyaamini waliyokuwa wameyasikia yametokea Zanzibar kutokana na hayo yenye kuitwa 'mapinduzi'. Ilifika hadi, siku hiyo ya 'mavamizi' majahil na makatili hao kuwanajisi maiti wa kike. Kitendo hicho hakijapatapo kufanyika katika nchi nyingi ulimwenguni zenye ubinaadamu na ustaarabu wake. Lenye kuzidi kushangaza na kusikitisha ni kumsikia mwananchi mwenye kujulikana kuwa yeye ndiye mwongozi wa hao wenye kujiita "progressives" akasema kuwa, watu waliyouliwa katika hayo yenye kuitwa 'mapinduzi' ni 491! Oh! Mwenyewe Okello alieongoza hayo mauwaji amesema kuwa wamekufa wananchi 13,000.

Hata wangekuwa watano tu, bali ni binaadamu, ni wananchi, jee, ndio wawe wamestahiki kuuliwa kwa kuvamiwa nchi yao na wageni ambao wewe na wenzio kama wewe mumechanganyika na hao wageni katika kuifisidi nchi na wananchi wake? La kustaajbisha zaidi ila pale inapojulikana kuwa haya yote yalipangwa kabla ni kuwa kwa siku 30 tu yaaani Desemba 10 mpaka Januari 11 ilitosha kujuwa uovu wa Serikali hata ikastahiki kupinduliwa? Hata ingelikuwa ni ovu hivyo, bali njia za kuiondowa za kikatiba zilikuwepo ambazo zingaliweza kutumika, khasa na hao Wapinzani. Haikuhitaji hata kidogo kutumia nguvu. Lakini hakika khasa ni kuwa mambo yalikwisha pangwa zamani, haya ni matekelezo tu!! Sote tunakumbuka uzuri maneno ya Mwalimu aliposema, "Lau kuwa nnaweza basi ningali viburura Visiwa hivi (Zanzibar) hadi katikati ya Bahari ya Hindi" Na hivyo ndivyo afanyavyo hadi hii leo, yumo avivuta Visiwa vyetu kuelekea baharini. Tafauti iliyopo baina ya jana na leo ni kuwa leo "tugofwar" vutanikuvute baina yake na wananchi imezidi kuwa kubwa kwa vile kila siku upande wa wananchi unazidi umma na unazidi nguvu.

KUULIWA KWA MUHSIN, SULEIMAN NA AHMED Siku ya taarikhi 13 Januari 1964, siku moja baada ya hayo yenye kuitwa "mapinduzi" kufanyika, wapendao kujiita "progressives", Makomred, waliwachukua vijana watatu, Muhsin Badr, Suleiman Badr na Ahmed Suleiman kutoka katika kituo cha Raha Leo, kikiwa kimoja kati ya vituo vilivyo kuwa vimewekwa na wakuu wa mavamizi ati kwa ajili ya kuhifadhi usalama wa wananchi. Baada ya kuwaondoa hapo, waliwafunga kamba za mikono na kisha waliwafunganisha nyuma ya lori na kuwaburura kutoka Raha Leo mpaka Chukwani kiasi ya mwendo wa maili tano au sita, na huku njia nzima vijana hao walikuwa wakiteseka kwa kujipiga na mawe, kuchomwa na visiki vya mijiti, vigae na kujipiga na majiti ya njiani. Walipofika huko Chukwani walikuwa si wahai si maiti, bali walikuwa badi wakitweta. Juu ya hali kama hizo walizokuwa nazo wananchi hao katika wakati huo, midhalimu ati "progressives" walianza kwanza kuwasubu kwa kuwatukana na kwa kuwaambia maneno machafu machafu, na mwisho waliwauwa kwa kuwapiga risasi. Kisha waliwachimbia shimo na kuwafukia wote pamoja. Hayo yaliweza kujuulikana kutokana na kujisifu kwao wenyewe hao madhaalimu. Wakati utafika ikiwa watanusurika katika ulimwengu huu, kattu hawatanusurika katika ulimwengu ujao. Watalipwa kwa kila walilokuwa wamelitenda, na hivyo ndivyo itavyokuwa kwa kila mwenye kutenda mema na maovu

KIFO CHA ALI MZEE MBALIA Binaadamu kujidhulumu maisha yake mwenyewe kwa njia yoyote ni katika makosa makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yote ya dhaahiri na ya siri. Tunmweomba Mwenyezi Mungu na tunatumai kuwa atatupokelea maombi yetu na kumsamehe kiumbe chake hiki kwa makosa aliyo lazimika kuyafanya ya kujidhulumu nafsi yake.

Kutokana na mateso aliyo kuwa ameyapata kijana huyu, Ali Mzee Mbalia, alipo kuwepo katika gereza la "Kwa Ba Mkwe" (Mlango wa nyuma) aliamua kufa kuliko kuishi katika mateso. Ali Mzee alikuwa kijana mdogo mwenye kupendeza kwa sura na kwa umbile lake. Alikuwa akipendana na kijana mwenziwe wa kike na walikuwa wamesha ahadiana kuoana. Wakati wenyewe walipokuwa wakiyapanga hayo, huku

33 pembeni alitokea Mheshimiwa Mkuu wa Jeshi la Zanzibar, Brigadiya. Kwa bahati mbaya Mheshimiwa "alifol", hajijui hajitambui, kwa hicho kijitoto cha kike. Msichana huyo alikuwa hakuathirika naye, kwani alikuwa akiliona hilo ni Baba Zere tu kwake. Brigadiya alipogundua kuwa msichana anapendana na kijana mwenziwe, naye anamfanya yeye ni mpumbavu, dashere tu, alimnyakua Ali Mzee mpaka Mlango wa Nyuma kwa Ziraili Mandera, na huko aliwapa amri wamtese kijana huyo kila mateso mabaya waliyo fundishwa, na waliyo yazua wenyewe.

Ali Mzee aliteswa mateso mabaya sana hata si vizuri wala si heshima kuyataja katika maandishi. Kutokana na mateso hayo aliyo kuwa akiyapata, alitokewa na kila namna ya maradhi, na aliachwa humo humo gerezani akiteseka. Hali ilipokuwa mbaya sana, alipelekwa hospitali kuu Mnazi Mmoja na baada ya kutibiwa kwa muda, alipata afuweni, na alianza kutembea tembea kwa miguu yake. Siku Daktari alipo mwambia kuwa kesho atapata ruhusa, na ruhusa yenyewe ni kurejeshwa gerezani kwa Ba Mkwe, ndipo alipoazimia bora afe kwa kujitupa kutoka ghorofa ya tatu ya hospitali mpaka chini. Huo ndio ulikuwa mwisho wa maisha yake. Kwa maafa hayo yaliyo mtokea Ali Mzee, kijana wa kike ndio alizidi kuchongeka ukali na kutomkubali Brigadiya kabisa.

Hayo ndiyo yaliyo kuwa yakifanywa na wakuu wengi wa serikali ya mavamizi, khasa katika Awamu ya Mwanzo.

"SKOLASHIPU" ZA MISRI Kutafuta maslahi ya nchi yake, Sh. Ali Muhsin alifunga safari katika mwaka 1958 kwenda Misri kwa ajili ya kutaka msaada wa "skolashipu" kwa vijana wa Kizanzibari. Baada ya kukutana na kuzungumza na wakuu mbali mbali wa Serikali ya Misri, na mwishoe kukutana na Rais Gamal Abdel Nasser (Mungu amrehemu), aliweza kupata nafasi 40 za masomo kwa ghafla moja, na walimu kama aliowataka wende Zanzibar kwa kusomesha. Serikali ya Misri iliweka nyumba maalumu katika mtaa wa Manshiat el Bakri, mtaa aliokuwa anakaa mwenyewe Rais, kwa ajili ya wanafunzi hao. Nyumba hiyo ikiitwa "Bait Sharq Afriqiya" (Nyumba ya Afrika Mashariki), kwani Sh. Ali baada ya kupata msaada kwa Zanzibar aliwatakia pia wanafunzi wa Afrika Mashariki yote. Wanafunzi hao walitiliwa vifaa vyote, tokea vitanda, mashuka ya kutandika, mablangeti mpaka chakula na wapishi na watumishi wa nyumba. Pia waliwekewa mabibi watatu wa Kizanzibari kuwa ni waangalizi, nao ni Bi Aliya Barwani, Bi Mwalimu Riyami na Bi Saniya Mgeni. Hayo aliyataka yeye Rais kwa kusema:"Mkileta watoto wa kike, na watoto wadogo, basi walteeni mamama waangalizi kutoka kwenu, ili mdumishe tabia na nyendo za kikwenu. Hatutaki kuwafanya watoto wenu wawe Wamisiri. Huku wachukue masomo tu. Tabia ziwe za kwenu."

Kwa fitina za kina Nyerere na Francis Khamis wa Kenya serikali za Kenya na Tanganyika zilipiga marfuku kupeleka watoto Misri. Watanganyika na Wakenya wakawa hawana ruhusa kusafiri kwenda Misri kwa masomo. Serikali ya Kiingereza iliyo kuweko Zanzibar haikuweza kufanya hayo kwa uwazi, lakini ndge zote zilidai kuwa ati hazina nafasi kuwachukua hao wanafunzi. Kwa juhudi ya M.Takim aliye kwenda mpaka Addis Ababa ikapatikana mwishoe Ethiopian Air Line kuwachukua hao wanafunzi. Zama zile takriban ndege zote za kwenda nje kutoka Afrika Mashariki zilikuwa ni za mashirika ya Magharibi. Uchaguzi wa wanafunzi kwa kupewa skolahipu hizo ulifanywa na Jumuiya ya Wazee (Parents Association) kwa Unguja. Katibu wa Jumuiya hiyo alikuwa ni mwanachama wa ASP. Sh. Ali Muhsin, aliyezipigania na kuzipata "skolashipu" hizo, hakujitia hata kidogo, wala hakuwa na kauli yoyote katika uchaguzi huo. Bali yeye alipotakiwa na Serikali ya Misri awatie watoto wake watatu, aliokuwa akiwalipa mwenyewe, alikataa kata kata, kwa kuchelea asiwape mafatani wasio kuwa na adabu kuzua kuwa kafanya juhudi hizo kwa ajili ya wanawe, au jamaa zake. Basi, la Ali Muhsin wala Hizbu, hawakuwa na kauli yoyote katika kuwatia wanafunzi wawatakao kutoka kisiwa cha Unguja. Ama katika kisiwa cha Pemba, ambako Jumuiya ya Wazee ilikuwa haina nguvu, ndio Hizbu ya huko chini ya uwongozi wa marehemu Sheikh Rashid Hamadi wa Ole, ndiyo iliyo wachagua wepi wa kupata "skolashipu".

Katika baadhi ya vijana walio pelekwa Misri baada ya muda huko walirubuniwa na Ahmed Rashad aliyekuwa mtangazaji khabri katika Sauti ya Cairo, na ambaye akaritadi akawa anaunga mkono AfroShirazi, aliwafisidi hao watoto, na kuwarubuni wakatae masomo na na hata wakawa wanawavunjia heshima wakuu wa Kimisri walio jishughulisha kuwaangalia maslaha yao. Ikabidi wanafunzi hao

34 kukatiwa "skolashipu" zao. Wengine walirudi Zanzibar, na baadhi wakatokomea nchi za Kikomunisti kwa matengenezo ya Komredi Ali Sultan, mpwawe Rashad.

Hata hivyo, wengi waliendelea na masomo yao, na kila baada ya muda wengine walikuwa wakipelekwa mpaka ikawa idadi kubwa sana. Juu ya hizo "skolashipu" wazazi walio kuwa wakijiweza waliwapeleka watoto wao kwa gharama zao, na kuwalipia kuwakimu kutokana na mifuko yao wenyewe. Yalipotokea mavamizi ya Zanzibar katika mwaka 1964 Baraza la Mavamizi lilipasisha kuwakatia masomo vijana wote hao na kudai warejeshwe Zanzibar. Nyerere na Karume walitoka mguu mosi mguu pili mpaka Misri kwa ajili ya kuukomesha ule mradi wa kufadhiliwa "skolashipu" wanafunzi wa Zanzibar. Wakati huo Diria ndiye alikuwa Balozi wa Cairo. Maalim Hija Saleh alikuwa wakati huo katika Ubalozi. Wao hao walivaa njuga katika kuwasaka wanafunzi majumbani na majiani, na kuwabaka wawarejeshe Zanzibar. Waliwapata baadhi, na wengine wakaendelea na masomo yao kwa shida na taabu, mpaka wakamaliza. Ama ile nyumba ya bure iliyo wekwa kwa ajili ya wanafunzi ilibidi ifungwe kwa kuwaridhi Nyerere na Karume, na mabibi waangalizi wakatolewa. Bi Aliya kwa nafsi yake akabakia kwa miaka huko huko Misri akiwaangalia watoto waliobakia na kutazamwa na wazazi wao. Mwenyezi Mungu ndiye wa kumjazi kheri kwa wema na hisani yake. Tunatumai watoto aliowalea wa kila kabila wanamkumbuka huyo mlezi wao katika uzee wake.

Wengi miongoni mwa wanafunzi waliopata "skolashipu" walikuwa ni Waafrika, na karibu wote walikuwa ni watu wa hali ya chini, kwani kimoja katika vipimo vya ugawaji wa "skolashipu" kilikuwa ni umasikini wa wazazi; na wengi waliokatiwa masomo yao na Nyerere na Karume ni Waafrika menyu. Jee, ndiyo kheri hayo iliyoyafanya Serikali ya Kiafrika iliyo dai kuwa ati inawapigania wanyonge? Vijana hao waliyorejeshwa Zanzibar, hawakushughulikiwa kwa lolote kuhusu kuendelea na masomo yao, ila waliachwa wakizurura majiani, na mwisho wakawa kama walivyo. Huu ndio ufisadi wa nyoka kumuuma mtu siyeweza kumla!

Lenya kusikitisha ni kuwa kweli Karume alikuwa hajui thamani ya elimu kwa sababu yeye mwenyewe hakubahatika kusoma. Lakini, wakati ulipo pasishwa uamuzi huo wa kuwakatia masomo wanafunzi walikuweko Profesa Babu, Al Haji Aboud Jumbe, Komred Ali Sultan, Komred Badawi, Komred Khamis Abdulla Ameir, Komred Salim Rashid, Kanali Komred Ali Mahfoudh, Komred Kassim Hanga, Maalimu Saleh Saadala na Twala. Vipi wote hao viongozi wataalamu waliweza kuunga mkono jambo kama hilo?

Kutokana na mambo kama hayo na mengineyo mfano wa hayo, ndipo wananchi wa kweli wenye uchungu wa nchi yao na wenziwao, wanaposema kuwa waongozi wote wa serikali yenye kujiita ya "Mapinduzi" tokea wa awamu ya kwanza, hadi ya pili, hadi ya tatu, na..na...Mwenyezi Mungu anajua hapana hata mmoja aliyekuwa amesimama kwa ajili ya maslaha ya nchi, wala ya wananchi. Kila mmoja, kuanzia Rais mpaka Komisar, wote walikuwa mbioni kujitengenezea maslaha ya nafsi zao tu. Naitoshe kuwa siku ya pili tu baada ya hayo yenye kuitwa mapinduzi kufanyika katika nchi kila mheshimiwa alikimbilia kwiba motokari, na kuhamia katika majumba ya watu, mbali ya kukimbilia mabanati wa Kiarabu na wa Kihindi. Leo, baada ya kuwa wengi katika hao walio kuwa katika Awamu ya kwanza na ya pili hata na ya tatu kuwa wapo nje ndio utasikia wakisema maneno kama kwamba wao walikuwa hawakuwamo katika kufanyika hayo!

YALIYO NIFIKA NAFSI YANGU NA HAYO YENYE KUITWA "MAPINDUZI" Kiasi cha saa 12 za magharibi siku ya Jumaatatu taarikh 13 Januari 1964, siku ya pili ya hayo yenye kuitwa 'mapinduzi', mimi pamoja na mke wangu na chungu ya wananchi wenzetu wa kike na wa kiume, wakubwa na wadogo, tulikuwepo katika klabu ya wazee wa Kingazija "Comorian Club" iliyokuwepo Kisiwandui, Unguja. (klabu hiyo kwa wakati huo, wakuu wa mavamizi waliifanya kuwa ni miongoni mwa vituo vya wakimbizi). Ghafla tulisikia mlango ukigongwa kwa vishindo vikubwa na baada ya kufunguliwa, tuliwaona vijana watatu wametuingilia, wawili walikuwa wamechukua bunduki na mmoja alikuwa na bastola, huyu alikuwa ni Mzanzibari, kwa jina ni Ahmed Bushir Aboud na hao wenzake walikuwa vijana wa Kibara. Kwanza waliwachukua, Sheikh Ameir Tajo na Sheikh Ali Ahmed Riyami na baada ya muda walirejea na walinichukua mimi (Aman Thani) na Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa. Wote hao wenzangu wameshafika mbele ya haki. (Mungu awape malazi mema, Amin). Safari yetu hiyo ilimalizikia katika jumba la Raha Leo (Civic Centre) Miafuni. Jumba hilo kwa siku hizo za mavamizi,

35 lilifanywa ndio Makao Makuu ya Wavamizi. Mbele ya uwanja wa jumba hilo, tulikuta umati wa watu mkubwa sana na kila mmoja alikuwa na silaha mkononi mwake. Wengine walikuwa na mabunduki, wengine walikuwa na mapanga, mashoka, mishale, na mipinde pamoja na mikuki. Wengine walikuwa kama ni vichekesho kwani walikuwa wamejiremba marangi mwilini mwao na wamejizongeresha majani na magozi, na huku mtu mmoja huyo huyo amechukua bunduki mkono mmoja, panga mkono wa pili na upinde ameuvaa shingoni na mishale ameichomeka kiunoni.

Ndani ya hilo jumba la Raha Leo, kulikuwa kumejaa watu, wake kwa waume wakubwa kwa wadogo hata vitoto vichanga, pamoja na mama zao, hao pia walichukuliwa kutoka majumbani mwao na kuletwa hapo ati kwa usalama wao. Kitendo hichi kilithibitisha kuwa majumba yetu kuanzia wakati huo yalikuwa hayana tena usalama. Mimi pamoja na mwenzangu Mohammed Aboud Mkandaa, tulipelekwa ndani ya jumba hilo na huko tulitengwa upande. Katika upande huo tuliotengwa sisi, tuliwakuta, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani, Sheikh Mwinyi Nemshi na Sheikh Omar Mohammed aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana, "Youth Own Union".

Muda mdogo baada ya kuwekwa hapo, alikuja kijana mmoja ambaye mpaka wakati huu nilionao sijaweza kumtambua ni nani, kwani sikumbuki maisha yangu kuwa nimepata angalau kukutana naye pahala. Kijana huyo alinitaka nisimame na kiasi cha kusimama tu, alinipiga kofi la uso, niliona vimuri muri na baada ya hapo alinitesa kwa kunipiga makonde na mateke na kunipopotoa kila sehemu aliyokuwa ameipenda. Baadae aliamuru ninyanyue mikono juu na hapo alimpa amri mwenzake ambaye alikuwa na bunduki kwa kumwambia, "Muangalie huyu asiteremshe mikono yake chini mpaka nitapokuja mimi. Na ikiwa atateremsha, basi mpige risasi".

Nilibakia katika hali hiyo kwa muda mkubwa mpaka yule kijana aliyeachiwa kuniangalia, alinionea huruma na aliniachia kwa kiasi cha muda fulani kuiteremsha chini mikono yangu. Haya yote yanathibitisha kuwa misingi ya hayo mavamizi ilikuwa ni chuki na idhlali kwa wananchi. Baada ya muda walitujia, Comrade Ali Mahfoudh na Comrade Badawi Qulatain na walitutaka mimi, Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa, Sheikh Issa Mohammed Issa na Sheikh Mwinyi Nemshi tuwafuate. Walituongoza, Ali Mahfoudh akiwa mbele na Badawi akiwa nyuma na sisi tukiwa katikati mpaka nje ya jumba; na hapo tulitiwa ndani ya gari aina ya "pickup" kubwa (Lori) na tulifuatanishwa na walinzi wanane, wote wakiwa na bunduki, na wote pamoja na dereva wetu walikuwa wamelewa. Hao walinzi waliwauliza mabosi wao, "Hawa wa wapi?" Comrade Ali Mahfoudh alijibu, "Wapelekeni Kilimani".

MAAFA YA GEREZANI Tulifika katika Gereza la Kiinua Miguu, ambalo sasa linaitwa, Chuo cha Mafunzo, kiasi cha saa nne za usiku na hapo tulimkuta Comrade Hemed Hilal Barwani, ambaye yeye ndiye aliyekuwa na dhamana ya gereza hilo kwa wakati huo. Comrade Hemed Hilal alitutaka tuvue nguo zetu zote, na tulizivua na tukabaki kama tulivyotoka matumboni mwa mama zetu. Hakuweza kumwekea sitaha hata mzee wake, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani. Baada ya kwisha kusachiwa, Comrade Hemed Hilal alitoa amri tupelekwe kwenye vyumba vya "security" vya kuwekewa mahabusi. Tulipewa virago vya kulalia, (kirago ni kizulia cha usumba urefu wake kiasi cha futi nne mpaka tano na upana wake ni kiasi cha futi mbili mpaka tatu) shuka mbili za bafta na kopo la kunywia maji, uji na kunawia baada ya kwenda haja ndogo au kubwa, ndio hilo hilo. Baada ya kupewa vitu hivyo, tuliongozwa na sajin wa gereza mpaka katika hivyo vyumba. Mimi na Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa tulitiwa katika chumba kimoja na Sheikh Issa na Sheikh Mwinyi Nemshi walitiwa katika chumba kimoja. Sehemu hiyo ilikuwa na vyumba sita, kila upande vyumba vitatu na katikati ujia. Tulifungiwa kwa kufuli, lango la nje pia lilitiwa kufuli.

Baada ya kuondoka huyo sajin aliyetupeleka, tulisikia sauti ikitoka katika chumba kimoja ikiuliza, "Ni nani wenzangu mliyoletwa"? Sauti ilikuwa si ngeni kwetu lakini kwa mughma tuliyokuwa nao wakati huo, tulishindwa kuitambua. Tulimuuliza kwani wewe ni nani mwenzetu? Alitujibu, "Mimi Suleiman Said Kharusi, na chumba chengine yumo Sheikh Humoud Ali Harthi, na chumba chengine yumo Sheikh Mohammed Idi Mjasiri, na chumba cha mwisho yumo mwanangu Edi Kharusi". (Mohammed Ali Said Kharusi) Na mimi nilimjibu, "Mimi Aman Thani, na mwenzangu Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa, tumo katika chumba cha pili mkono wa kulia kutokea mlangoni". "Na wenzetu wawili, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani na Sheikh Mwinyi Nemshi, wao wametiwa katika chumba cha mwisho katika mkono huu

36 huu wa kulia." Tukiambizana kwa sauti tu si kwa kuonana. Ndani ya chumba tuliwekewa ndoo mbili. Moja ndio choo na ya pili ya maji ya kunywa. Tuliwekwa katika vyumba hivyo kwa muda wa wiki mbili bila ya kutolewa nje hata dakika moja. Ndoo za uchafu zikitolewa na wachungaji, na chakula tukiletewa na wachungaji.

Wakati huo kila sehemu ya kuwekewa wafungwa katika gereza hilo ilikuwa imejaa wananchi waliokuwa wameletwa humo ati kwa kuhifadhiwa maisha yao. Kwa jinsi umma ulivyokuwa mkubwa, Serikali ya Mavamizi iliwaachilia wafungwa wote hata waliyokuwa wamesha hukumiwa vifo, nao pia waliachiliwa huru ili ipatikane nafasi ya kuwekwa hao ati wenye kuhifadhiwa! Chumba (cell) kilichokuwa kwa kawaida wakiekwa wafungwa sita mpaka wanane, walitiwa baina ya watu 12 mpaka 16 na juu ya hivyo, bado wengine walikuwa wakilala katika vijia vya kupitia. Na mwisho lilijengwa banda kubwa la miti na makuti, na bado kulikuwa hakuna nafasi kwa jinsi ya wingi wa watu waliyotiwa gerezani. Kutokana na hali kama hiyo, serikali ya mavamizi ilifungua vizuizi vyengine vya kuwaweka wananchi. Wengine waliwekwa katika maskuli na wengine walipelekwa katika magereza ya mashamba kama Langoni na Kinu Moshi na wengine walipelekwa hata visiwani kama Kisiwa cha Makaburi "Grave Island" na Kisiwa cha "Prison Island". Baada ya muda tulitolewa ndani ya vyumba hivyo na tulichanganyishwa pamoja na wananchi wenzetu wengine. Kwa jinsi umma ulivyokuwa mkubwa na kwa ilivyokuwa hali ya usafi ni chache, maradhi ya matumbo ya kuharisha na maradhi ya macho yalikuwa yakitutokea mara kwa mara.

Katika miezi ya mwanzo, watu wetu wa nyumbani wakiruhusiwa kuja kutuona kila baada ya muda fulani, na pia tulikuwa tukiruhusiwa kuletewa chakula kutoka majumbani kwetu. Lakini hayo hayakuendelea kwa muda mkubwa, ila yote yalipigwa marufuku. Kwanza watu wa "Msalaba Mwekundu" walikuwa wakiruhusiwa kuja kutukaguwa na baadae na wao pia walipigwa marufuku. Karume na kundi lake la Baraza la Mavamizi, walikuwa kila baada ya muda waliokuwa wakikutana wenyewe, wakija gerezani kwa kuwatoa wawatakao. Mwendo ulikuwa kama hivyo mpaka kufika taarikh mosi Januari, 1965 yaani mwaka mmoja tokea kutokea hayo yenye kuitwa 'mapinduzi', wananchi wengi waliyokuwa wamewekwa magerezani na waliyokuwepo viziwizini vyengine walikuwa wamesha achiliwa huru. Wachache, na mimi nikiwa miongoni mwao ndio waliyokuwa wamebakia kiziwizini gerezani kwa "kuhifadhiwa usalama wao", kama walivyokuwa wakisema wakuu wa Serikali ya 'mavamizi'.

KUFUNGWA KIFUNGO CHA MIAKA 10 GEREZANI Taarikh 1 Januari, 1965 kiasi ya saa nne za asubuhi, Karume Raisi wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar akifuatana na wenzake wa Baraza lake la Mavamizi walikuja gerezani. Walipofika walitukuta sisi wachache tuliyokuwa tumebakia kiziwizini tumesimama kwa kungojea kwa matumanio makubwa sana ya kuachiliwa huru kama walivyo achiliwa wa kabla yetu. Alipofika mbele yetu, Karume alisema, "Leo tumekuja kuwaachilia huru wote waliyokuwa wamewekwa humu ndani kuanzia siku za mwanzo za mapinduzi". Kiasi ya kusema hivyo tu, tuliwaona baadhi ya waongozi wa Baraza la Mavamizi, wakiwemo Ibrahim Mbwana (Ibrahim Makungu), Said Natepe, Seif Bakari na Khamis Darwesh wamevutana upande na wakinon'gonezana. Baadae walimnon'goneza Karume; na hapo hapo mpira uligeuzwa kuelekea upande mwengine. Tuliona tunatolewa mmoja mmoja na kuwekwa upande mpaka tulitimia watu 25. Karume na kikosi chake waliondoka na kutuacha sisi watu 25 upande mmoja na wenzetu wengine wachache waliachwa upande wao. Baada ya muda alitujia Ofisa wa Gereza, Bwana Oliver Fernandes akifuatana na sajini (sergeant) Nyankabwa pamoja na askari wao wawili. Oliver alikuwa akitwambia na huku ameinamisha uso wake chini kwa kutuonea taabu kututizama kwa namna alivyokuwa akiona dhulma na unyonge tuliyopitishiwa ambao tokea kuanza kwake kazi hajapata kuuona wala kuusikia.

Alisema kutwambia, "Baraza la Mapinduzi, limeamua kukufungeni gerezani kifungo cha miaka 10 kwa kila mmoja wenu kuanzia hii leo Januari 1, 1965"! Kila mmoja kati yetu kwa kusikia hayo, alitokwa na kijasho mwilini mwake. Hapana hata mmoja aliyetarajia kuwa yataweza kutokea mambo kama hayo ya kufungwa bila ya kuwa na makosa na bila ya kupelekwa mbele ya mahakama. Sisi watu 25 ndio watu wa mwanzo katika taarikh ya visiwa vya Zanzibar kufungwa gerezani bila ya kutenda kosa lolote na bila ya kuhukumiwa. Ulimwengu unafaa umuulize Mwalimu Nyerere na hao wenye kujiita "progressives", kuwa huko ndio kuondoa dhulma na unyonge na kuleta usawa na demokrasi? Hao Masultani na Mamwinyi, waliwahi kutenda hata nusu ya hayo mliyoyetenda nyie katika huo utawala wenu? Tulinyolewa vipara na tulipewa nguo za kifungwa, nguo zetu, na kila kilichokuwa chetu, kilichukuliwa na kuwekwa katika

37 dhamana ya gereza. Ni shida kueleza hali zetu zilivyokuwa siku hiyo hata ikafahamika. Tulikuwa tukilia bila ya kutokwa na machozi, na tulikuwa tukitizama na ilhali tulikuwa hatuoni kitu. Tulikuwa tukisema na ilhali ilikuwa hatukijui nini tukisemacho. Mwenzetu mmoja Sheikh Mohammed Rajab (Machungwa) alipindukwa na tumbo la kuhara damu kwa uchungu wa kudhulumiwa maisha bure.

Yafuatayo ndio majina ya hao wadhulumiwa 25 tuliofungwa miaka 10 gerezani bila ya makosa na bila ya kupelekwa mbele ya mahakama:

Suleiman Sultan Malik Hassan Usi Walid Fikirini Ali Issa Ali (Mataa) Mohammed Rajab (Machungwa) Haji Hussain Ahmed Yahya Mohammed Ali Shambe Hussain Bachu Ramadhan Khamis Shariff AbdulRahman Othman Mzee Maalim Mwita Rashid Mohammed Marjeby Ali Raza Nathani (Ali Bomu) Omar Hamad (Mkame Ndume) Sheha Abdulqadir Thiney Sheha Suleiman Khamis Ali Mohammed Suleiman Wazir Ali bin Maalim Mzee Ismail Salim Said Halua Nasser Mohammed Husein Jessa Bhaloo Ali Mdungi Ahmed Abdulqadir (Qullatain) Aman Thani Fairooz

Kwa hakika siku hiyo ilikuwa ni siku ngumu sana katika maisha yetu. Tulishindwa kula na tulikesha usiku kucha bila ya kufumba jicho hata muda mdogo. Kulipokucha siku ya pili taarikh 2 Januari 1965, baada ya kupewa uji wa sembe na chembe mbili tatu za maharagwe, tulipelekwa kuonana na Mkuu wa Magereza. Wakati huo alikuwa Bwana Kilonzi. Lakini, aliyetukabili alikuwa Bwana Oliver Fernandes, msaidizi wake. Oliver alitupa Daftari kubwa lenye kuwekwa majina ya wafungwa pamoja na makosa yao na muda wa vifungo vyao. Tulipo litupia jicho, tuliyaona majina yetu yamesha andikwa pamoja na makosa yetu na mahakama yaliyotuhukumu na hakimu aliyetuhukumu na muda wa vifungo vyetu. Maelezo ya hukumu ya kufungwa kwetu huko kama yalivyoandikwa katika Daftari hilo yalikuwa kama hivi:

Kosa Letu: Kutia choko choko za kutaka kuipinduwa Serikali ya Wananchi. Hakimu Aliye tuhukumu: Mkuu wa Jeshi la Taifa. Mahakama Iliyotuhukumu: Makao Makuu ya Jeshi Muda wa Vifungo Vyetu: Miaka 10 Kila Mmoja (tangu Januari 1, 1965 mpaka Desemba 31, 1974).

Serikali gani hiyo isiyoona vibaya wala kutahayari kuweza kusema uwongo kama huo kuwasingizia raia zake, ambao hawana hata wakuwasemea. Tumefungwa bila ya kuwa na makosa yoyote na bila ya kuhukumiwa na yoyote na bila ya kupelekwa katika mahakama ya namna yoyote. Au choko choko hizo tumezifanya wapi, na nani hao tuliyowafanyia choko choko hizo wakati sote sisi tulikuwa ndani ya mikono yao tokea mwanzo wa hayo yenye kuitwa 'mapinduzi' hadi siku hiyo ya taaarikh mosi Januari, 1965 walipotufunga miaka 10 gerezani! Tulitakiwa tutie madole yetu katika hilo Daftari, na tulitia

38 kwani hatukuwa na uwezo wa kukataa. Baada ya hapo, tuliondolewa katika gereza hilo la mjini na tulipelekwa kwenye gereza la shamba, Langoni. (Langoni ni kiasi cha maili 10 kutoka mjini). Wakati wa kikoloni, mfungwa yoyote ilikuwa hafanyishwi kazi ya namna yoyote mpaka kwanza aangaliwe na Daktari mwenye ujuzi (sio muuguzaji) kukhusu siha yake. Na uamuzi wa Daktari ndio uliyokuwa ukifuatwa juu ya namna za kazi zinazomfalia mfungwa fulani kuzifanya kutokana na siha yake. Serikali ilipoingia watawala wenyekujiita, "wapigania haki za wanyonge na waleta usawa kwa wote", hapo hapo mambo yote yalibadilika ikawa wagonjwa, wazima, wadogo, wakongwe na hata walemavu, wote walifanyishwa kazi kwa kulazimishwa, tena bila ya kuangaliwa laa na daktari walaa na muuguzaji.

Kazi zilizokuwepo katika magereza ya mashamba, Langoni na Kinu Moshi zilikuwa ngumu sana zenye kuhitaji watu wenye siha kamili. Kwani, kazi zenyewe zilikuwa ni za kulima, kukata majiti makubwa kama miembe, mifenesi, kun'goa minazi na kuipangua, kubeba vigogo vya minazi na majiti mengine, kuchimba mawe na kupalilia matuta ya muhogo na konde za mipunga.

KIASI CHA KAZI ALICHOKUWA AKIFANYISHWA MFUNGWA Ikiwa kazi ni ya kupiga matuta ya muhogo, kila mfungwa alikuwa akitakiwa kupiga tuta moja unusu kwa siku, (tuta moja unusu inakuwa, tuta zima la mfungwa peke yake na tuta la pili la kushirikiana wafungwa wawili). Ukubwa wa tuta hilo ilikuwa ni kiasi cha yadi 150 urefu, yadi moja upana na kunyanyuka kwenda juu kiasi ya yadi moja. Ikiwa kazi ni ya kulima katika konde ya mpunga, kila mfungwa hupewa ngwe yake. Urefu wa ngwe ni kiasi cha yadi 150 mpaka 200 na upana kiasi cha yadi tatu. Ikiwa kazi ni za kun'goa minazi, kila mfungwa akitakiwa kwa siku ang'owe na kuipanguwa (kuikata mapande mapande) minazi miwili mpaka mitatu. Ikiwa kazi ni kuchimba mawe, kila wafungwa watatu wakitakiwa wachimbe mawe na waijaze mita yao. (mita hiyo ilikuwa na kipimo chenye urefu wa kiasi cha futi nane, upana wa futi nne na kunyanyuka kwendea juu kiasi cha futi tano. Hikima ya kuijaza hiyo mita ndiyo iliyokuwa mauti kwa wafungwa. Kwani ukitaka kuijaza kwa wakati mnaopewa kwa kufanyakazi, basi ilikuwa lazima muweze kuchimba mawe makubwa sana. Mukisha chimba mawe hayo makubwa basi lazima mutimie watu wane wakulinyanyua jiwe moja kutoka chini mpaka kumuwekea mwenzenu wa tano juu ya mabega yake, yaani mumtwike mwenzenu pandikizi ya jiwe hilo! Masafa ya kutoka panapochimbwa hayo mawe mpaka kwenye hiyo mita ni kiasi cha yadi 10. Na njia zenyewe za maweni zenye mashimo mashimo pamoja na mibigili (mibigili ni miba midogo midogo), wakati miguu chini bila ya viatu. Fikiri vipi binaadamu utakwenda maweni humo na jabali hilo mgongoni mwako, ukijikwaa ndio mauti yako au kwa uchache kupoteza mguu.

Juu ya kuwa wafungwa wadhulumiwa tukifanyishwa kazi ngumu kama hizo, kulikuwa na adabu ambazo tukipewa tunaposhindwa kukamilisha kazi tunazopewa kuzifanya kwa siku. Kutokana na ugumu wa kazi uliokuwepo mfungwa kushindwa kukamilisha kazi anayopewa kulikuwa ni jambo la kawaida. Kwahivyo, takriban kila siku baadhi ya wafungwa walikuwa wakipewa adabu kwa kuto kumaliza kwa wakati kazi zao walizokuwa wamepewa. Adabu zenyewe zilikuwa, Wafungwa wanao shindwa kumaliza kazi wanazo pewa mpaka ukafika wakati wa kusimamishwa kazi, hao wakiachwa waendelee kuzimaliza nngwe zao, wakati wenziwao waliomaliza kazi wakirejeshwa kambini na kugaiwa posho na kupumzika. Ikiwa mpaka magharibi hawaku maliza nngwe zao, basi siku hiyo, hawakiachiliwa kukoga, bali hata kujisafisha matope na majasho ya kutwa. Na pia siku hiyo wakipewa nusu ya chakula. Chakula kamili kwa kila mfungwa kwa siku ilikuwa ni wakia moja na nusu kwa chakula cha asubuhi na wakia tatu na nusu kwa chakula cha mchana. Linganisha na posho la wafungwa wakati wa kikoloni na masultani, wakati huo posha la mfungwa ilikuwa ni wakia 16, yaani ratili moja. Chakula kamili na wafungwa wakilala na njaa, seuze upewe nusu ya chakula!

Adhabu ya tatu ni kwamba wakati mwengine kwa kushindwa kumaliza kazi upewayo basi hata hiyo nusu chakula tulikuwa hatupewi. Tukilala bila ya kupewa chakula. Mimi nafsi yangu siku moja nilishindwa kumaliza kazi niliyopewa kwa sababu nilikuwa na homa, na juu ya kuwa Bwana Mganga wa gereza alinipa mapumziko, lakini mkuu wa gereza alivunja mausio ya Bwana Mganga na aliamuru nifanyishwe kazi hivyo hivyo na maradhi yangu. Matokeo yake nilipinduka wakati nilipokuwa nikilima na sikuweza kuendelea na kazi. Juu ya kuwa nalifika hadi hali hiyo, si kupewa matibabu, bali hata huruma lakini nalipewa adabu mbili kwa pamoja. Nilinyimwa kukoga, bali hata kujisafisha matope na majasho,

39 pia nalinyimwa posho, sikupewa hata robo! Na siku ya pili nilitiwa kundini kuchapa kazi kama kawaida. Hayo hayakuwa kwangu mimi tu bali yalikuwa ni mambo ya kawaida kwa kila mfungwa mwenye kuitwa wa "kisiasa". Sijui wafungwa wa aina gani au wa nchi gani au wa watawala gani au wa karne zipi waliwahi kutendewa namna hivi. Haya yametendeka katika karne ya ishirini, karne ya Uhuru, na Haki za Binaadamu na Maendeleo, yametendwa Zanzibar na Tanganyika katika utawala na hukumu ya Mwalimu Nyerere na makamo wake Sheikh Abeid Amani Karume. Waliotendewa haya ni wananchi wa Zanzibar na wa Tanganyika. Yametendwa haya na ulimwengu wakiyaona na kuyajuwa na hapana hata aliyeinua kidole, kama kwamba hawakutendewa binaadamu. Wanyama pia wanazo haki zao za kuhifadhiwa, seuze binaadamu! Mwalimu ameyatenda haya bila ya hata kuona haya au vibaya au kuchelea ulimwengu. Mwalimu haguswi na sheria, naatende apendavyo!

MAOVU WALIYOTENDEWA "WAFUNGWA WA KISIASA" Mpaka hivi sasa siwezi kusema kwa hakika kuwa matendo tuliyokuwa tukitendewa sisi wafungwa tuliyokuwa tukiitwa " wafungwa wa kisiasa" yalikuwa ni maamrisho ya Wakuu wa Serikali ya Mavamizi au yakitokana na mapendekezo ya mkuu wa magereza tu kwa chuki za kibinafsi! Lakini ni hakika kuwa mabwana wa kubwa wakijuwa yaliokuwa tukitendewa na haikutokea hata wakati mmoja kuyakanya au kuyakataza. Kwahivyo wakitaka tutendewe namna hivyo. Ilikuwa mfungwa yoyote mwenye kuitwa "mfungwa wa kisiasa", akiumwa ni marufuku kupelekwa hospitali kuu hata ikiwa Bwana Mganga wa gereza ameamua kuwa mfungwa mgonjwa huyo anahitaji kuangaliwa na daktari mkubwa. Ilikuwa kila penye kazi ngumu, wa mwanzo kupelekwa ni wafungwa wenye kuitwa "wafungwa wa kisiasa".

Lolote alilozuliwa mfungwa mwenye kuitwa "mfungwa wa kisiasa", kutoka kwa mfungwa wa kawaida, lilikuwa likiaminiwa hata wakitokea mashahidi wa kumkatalia hilo alilo singiziwa, ilikuwa hawakubaliwi. Kwa jumla, wafungwa waliokuwa wakiitwa "wafungwa wa kisiasa", walikuwa wakitendewa vibaya sana. Tukiitwa "wafungwa wa kisiasa" kwa vile Wakuu wa Serikali ya Mavamizi walijipa uwezo wa kumfunga binaadamu mwenzao kwa tuhuma yoyote bali mara nyingi hata bila ya tuhuma na bila ya kupelekwa mahakamani. Kwahivyo, yoyote afikishiwaye maafa kama hayo basi mabwana na wasaidizi wao wakimbandika mdhulumiwa huyo jina la umaarufu "mfungwa wa kisiasa". Naiwe mdhulumiwa huyo ilituhumiwa kwa kuiba n'gombe au kwa lolote la ukhalifu, madhali imeamuliwa kufungwa bila ya kupelekwa mahakamani, basi alikwisha stahiki kuwa ni "mfungwa wa kisiasa". Na hao tulikuwa wengi kuliko waliyofungwa kutokana na hayo mahakama yao ya uhange, wakihukumiwa na mahakimu wake wauza samaki wakavu na washona kofia za viuwa.

Maisha yangu na ya wenzangu kwa jumla yalifanywa kuwa mabaya sana yasiyoweza kuchukulika. Kwa kila upande tulikuwa hatuonekani kuwa ni binaadamu. Lakini hata hivyo, Mwenyezi Mungu alitupa uwezo wa kuyakabili hivyo hivyo, na kubwa zaidi alitupa subira na imani yenye nguvu sana.

KUTOLEWA GEREZANI Kila lenye mwanzo lina mwisho, na hakuna marefu yasiyo ncha na baada ya dhiki ni faraji. Wanasema wasemao: Akushutuao wewe sishutuke Yupi awezao kukwetea lake Watu wanayao Mungu ana lake

Taarikh 10 Januari 1967 ikiwa taarikh 28 Ramadhani kiasi cha saa 10 za alasiri, wafungwa wote tuliokuwa tukiitwa "wafungwa wa kisiasa" tuliyokuwepo katika gereza la Langoni tulikusanywa, na waliletwa pamoja na sisi wenzetu kutoka gereza la Kinu Moshi. Haikupita muda ila tuliyaona magari mawili ya magereza yametufikilia. Sote tulipakiwa na kupelekwa Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu (Mjini). Tulifika huko na kin'gora cha magharibi kinalia. Tulitawadha na baada ya kumaliza kusali, tulifuturu kwani sote tunamshukuru Mwenye Enzi Mungu tulikuwa tukifunga. Baada ya kumaliza kufuturu, tuliachwa kukaa katika njia ya kupitia baina ya vyumba na vyumba. Tuliachwa hapo mpaka baada ya kusali Taraweh ndipo tulitiwa vyumbani na kufungiwa ndani. Taarikh 11 Januari ikiwa taarikh 29 Ramadhani, kiasi cha saa tatu za asubuhi, Karume na kikosi chake cha Baraza la Mavamizi walifika hapo gerezani, walitukuta tumewekwa tayari, tukingojea maamuzi yao juu yetu. Upande mmoja roho zilikuwa na tamaa kuwa hwenda ikawa mkusanyo huu ni wa kuachiliwa huru, na upande wa pili roho

40 zilikuwa zikidunda dunda kwa khofu za kuwa hwenda ikiwa wengine wasiachiwe. Muradi kila mmoja alikuwa akivuta uradi moyoni mwake na kumuomba Mwenyezi Mungu atufaraji. Lakini kwa hakika tamaa za kuachiliwa sote hazikuwemo katika nyoyo zetu.

Karume alikuja moja kwa moja mpaka upande tuliowekwa na alituambia, "Leo tumekuja kwa makusudio ya kukutoeni gerezani ili mupate kwenda kusherehekea Sikukuu ya EidelFitr na Sikukuu ya Mapinduzi pamoja na aila zenu. Tumefurahi kupata ripoti ya ukaaji wenu gerezani kuwa mmekaa kwa adabu na kufuata kila amri za gereza mlizokuwa mkipewa na waliyo khusika. Kwahivyo, leo tunakuachilieni huru, na kila mmoja atapewa Shs. 1000 mpate kufurahikia Sikukuu pamoja na watoto wenu! Lakini ninakuonyeni na nakutakeni mkakae uzuri huko nje. Ikiwa mtajitia kuchanganyika na makundi ya watu wakorofi, mkaja mkakumbwa na kuletwa tena gerezani, basi adabu itayokuwa ni kifo wala si chengine. Kwakherini".

Katika kundi letu tulioachiliwa huru siku hiyo tulikuwa watu 24, mwenzetu wa 25, Mzee Maalim Mwita, yeye alitolewa gerezani kiasi cha miezi sita kabla yetu. Na wakati huo tulipoachiliwa sisi, yeye alikuwa amesha ondoka duniani. Siku hiyo ilikuwa siku kubwa sana katika taarikh ya maisha yetu. Hapana shaka ni jambo kubwa sana kwa binaadamu kurejeshewa haki yake alionyang'anywa, ikiwa ni uhuru wake basi ni kubwa mno!

Baada ya kuondoka Karume na kundi lake, tulipelekwa Victoria Gardens kwenye ofisi ya Sheikh Abdalla Musa Mfuahaya. Yeye ndiye aliyetupa hizo Shs.1000 kila mmoja wetu. Baada ya hapo, tulirejeshwa Makao ya Magereza na tulipewa nguo zetu na kubadili. Tuliagana wenyewe kwa wenyewe na kuwaaga baadhi ya wafungwa wenzetu tuliyoishi nao gerezani kwa muda. Kabla ya kutoka nje ya gereza, alitujia Mkuu wa Usalama, Hassan Mandera na alitutaka kila mmoja wetu atie saini katika waraka maalumu ulioandikwa miongoni mwa maneno, "Ikiwa nitafanya tena makosa kama haya, adabu yangu nipigwe risasi hadharani"! Kila mmoja alitia saini bila ya shida wala taabu au suala na jawabu. Tulipotoka nje ya lango la gereza, tulikuta umati wa watu, ndugu, masahibu na wananchi wenzetu wakitusubiri. Tulikumbatiana kwa furaha na huku wakitupa maneno mazuri mazuri pamoja na kutuombea madua haya na yale. Baada ya hapo kila mtu alichukuliwa na watu wake.

Nilipofika nyumbani, nilikuta nyumba imejaa watu kwani khabari za kutolewa kwetu gerezani, zilienea mji mzima. Vilio vya furaha vilianikiza majumbani mwetu na kila dakika hawa wakiingia na hawa wakitoka kwa furaha na bashasha. Kwa upande wetu siku hiyo ilikuwa siku kubwa sana kwa mengi bali, khasa kwa haya, la kwanza ni kwa kurejeshewa uhuru wa nafsi zetu, uhuru ambao tulinyang'anywa kwa muda wa siku 1095 yaani miaka mitatu na kitu tukiwa wafungwa wa Nyerere na Karume. Pili ni kuwa baada ya kuwekwa mbali na watu wetu kwa muda wote huo, bila ya kosa lolote lile illa ni kwa kudhulimiwa na kuonewa, siku hiyo ndio tumeweza kuungana tena pamoja. Jengine, tumeweza kufuturu vyakula tulivyo vitamani wenyewe na tulivyo tamaniwa na watu wetu. La nne, tumekuwa na uwezo wa kuisherehekea Sikukuu ya EidelFitr tukiwa huru pamoja na aila zetu. Tano, tumeweza kulala bila ya kufungiwa milango wala kulindwa na kuamka wakati tuliotaka, bila ya kuamshwa kwa kengele. Huo ndio utamu na fadhila ya uhuru wa binafsi, uhuru wa kuzaliwa nao kila binaadamu, bali kila kiumbe. Unyonge niliouona siku hiyo na natumai haukunifika miye tu, lazima na wenzangu umewafika hapana kuliko kule kukataliwa na watoto wangu wadogo kwa kuwa walikuwa hawanijui kwa vile hii yalikuwa ndio mara yao ya mwanzo kuniona.

Tulipo chukuliwa kuwa "wafungwa wa kisiasaa" huyo mwanangu mkubwa nilimuacha na umri wa miaka miwili unusu, na wapili alikuwa na umri wa mwaka mmoja, na watatu yeye, alikuwa bado yumo tumboni mwa mama yake. Kazaliwa baada ya hayo yenye kuitwa, mapinduzi kwa miezi mitatu. Shida nyengine nilizokuwa nikiziona baada ya kutolewa gerezani ni kuwa wananchi wengi sana walikuwa wakiishi katika maisha ya khofu, woga na ya wasi wasi mkubwa. Kila mmoja alikuwa hajuwi maafa gani atateremshiwa wakati wowote. Kila mmoja alikuwa hamuamini mwenziwe, hata ndugu kwa ndugu walikuwa hawaaminiani, bali hata mtoto na mzee wake!! Ndani ya nyumba zao wenyewe watu walikuwa wakizungumza kwa kunong'onezana tu. Fitna na hasada yalikuwa ni mambo ya kawaida katika nchi. Wananchi wengi khasa wale waliyokuwa na asili za Kiarabu, za Kihindi na za Kingazija walikuwa wakitolewa makazini bila hata ya kupewa haki zao za miaka waliyokuwa wametumikia Serikali. Haya

41 yaliwafika hata na wale waliyokuwa imani zao za kisiasa zilikuwa hapo nyuma zikikhusika na UHizbu au UZPPP. Hali za kimaisha zilivyokuwa hivyo na kila siku kuzidi kuwa mbaya wananchi wengi waliamua kuuhama wattani wao wengi wao kwa kukimbia na kuwaacha watoto na nyumba zao bila ya watizamaji wa kisharia kwa kwenda kutafuta maisha na usalama wao nchi za nje. Kwa hakika mji ulikuwa ukihuzunisha na kutilisha unyonge. Hata mgeni haikuwa taabu kutambua kuwa mji ulikuwa ndani ya msiba.

NAKIMBILIA DARESSALAAM Kutokana na hali kama hizo zilizokuwepo nchini, namiye niliamua kuikimbia nchi yangu. Taarikhi 10 Juni, 1967 niliondoka Zanzibar kwa kuhamia DaresSalaam na huko nilifikia, na nilipokelewa na ndugu yangu mpenzi Mzee Mohammed MBABA. Tuliishi pamoja kwa muda mkubwa na baada ya kupata kazi, niliondoka kwa kuhamia pahala pangu peke yangu lakini kila wakati tulikuwa pamoja kwa mashauri na kwa mazungumzo. Baada ya kupata kazi na baada ya kutamakani kidogo, nilileta aila yangu na kuishi pamoja katika maisha yetu mapya.

Ole wangu! Kumbe nimeondoka kwa wachinjaji, nimekwenda kwa wala nyama! Baada ya muda wa miezi 16, yaani tangu Juni 1967 mpaka September 1968, tokea kuishi DaresSalaam, nilisitukia ghafla mlango wa nyumba niliyokuwa nikiishi ukigongwa kwa vishindo vikubwa mnamo usiku wa manane, kiasi cha saa saba na nusu hivi. Nilipofungua mlango, waliniingilia ndani watu saba kwa jumla. Watano walikuwa wamevaa nguo za kiaskari wa polisi na walikuwa wame chukua marungu mikononi mwao na wawili, walikuwa wamevaa nguo za kiraia yaani shati na suruali. Wao walikuwa na bastola mikononi mwao. Kiasi cha kuingia ndani tu, waliniuliza, "Jina lako nani?" Niliwajibu, "Aman Thani". Mmoja katika hao wawili waliokuwa wamevaa nguo za kiraia, aliniambia kuwa, "Tokea sasa tumekukamata, na umo katika dhamana ya Polisi". Niliwauliza, "kwa kosa gani?" Nilijibiwa kuwa, "Utaambiwa utapofika Makao Makuu ya Polisi".

Niliwaomba waniruhusu kuvaa nguo kwani wakati huo nilikuwa nimevaa shuka na fulana tu. Kwanza walinikatalia na kwa kuwaomba sana, walinikubalia na walimtaka mke wangu aniletee nguo. Niliwahi kuvaa shati na suruali. Nilipokuwa nataka kuvaa soksi na viatu, askari mmoja alinizuwia na alivichukuwa yeye hivyo viatu na aliniambia, "Utavivaa utapokuwa ndani ya gari huko nje". Niliongozwa na kutolewa nje nikawaacha nyuma mke wangu na mtoto wangu mchanga wa mwaka mmoja katika nchi ya kigeni na katika nyakati za usiku kama huo. Unyonge ulioje! Nilipofika nje, nilizikuta gari mbili za polisi, na nilitiwa katika moja ya hizo. Yule askari aliyechukuwa viatu vyangu, yeye aliingia katika gari nyengine hakuingia pamoja na mimi. Nilipofika Makao Makuu ya Polisi baada ya kuandikwa jina langu nilisachiwa mwilini na nguoni. Nilipokuwa nikisachiwa nilimwambia huyo aliyekuwa akinisachi kuwa viatu na soksi zangu amechukua mmoja katika askari waliyokuja kunichukuwa kutoka nyumbani kwangu na aliniambia kuwa atanipa wakati nitapokuwepo katika gari nje, lakini sijamuona tena, kwahivyo naomba nipewe viatu vyangu.

Jawabu la huyo aliyokuwa akinisachi, lilikuwa, "Hilo mimi halinikhusu, atapokuja, atakuletea". Niliondolewa hapo na nilipelekwa katika vyumba wanavyowekwa mahabusi. Nilipofika huko, niliwakuta baadhi ya Wazanzibari wengine wameshaletwa na ilikuwa kila baada ya muda, wakiletwa wengine mpaka kulipokucha, tulitimia watu 17. Wote isipokuwa mmoja tu, walikuwa ni Wazanzibari. Huyo mmoja, yeye alikuwa ni mtu wa Tanganyika na hajawahi hata mara moja kwenda Zanzibar wala alikuwa haijui khasa. Wengi ya hao Wazanzibari waliyokamatwa usiku huo, waliondoka Zanzibar na kuishi DaresSalaam miaka mingi nyuma. Wengine zaidi ya miaka 40 walikuwa wakiishi Tanganyika na kufanyakazi huko huko kwa maisha yao yote na hata baadhi yetu hatukuwa tukiingiliana kwa lolote bali hata tulikuwa wengine hatujuani. Usiku kucha tulikuwa macho hapana hata mtu mmoja aliyekuwa angalau amesinzia. Tulikuwa tukiulizana na hapana aliyeweza kumjibu mwenziwe, kwanini tumekamatwa? Tumefanya kosa gani?

Kiasi cha saa mbili za asubuhi, alitujia Sajini mmoja pamoja na askari wake na alimwambia huyo askari wake, "Waletee hawa watu chai 'special'". Baada ya muda, tuliletewa chai katika mabirika na vikombe, maziwa, siagi na mikate. Hakika chai ilikuwa chai ya kweli, iliyokuwa imetimia kwa kila kitu. Wakati sisi tukipewa chai kama hiyo, tuliwaona mahabusi wenzetu wengine wakipewa chai kavu na maandazi

42 ya mkahawani! Tulimuuliza yule askari aliyetuletea hiyo chai, kuwa, mbona sisi tunapewa chai nzuri kama hivi na wale wenzetu wanapewa chai kavu na maandazi na ilhali sisi sote ni mahabusi? Askari alitujibu, "Kweli nyote ni mahabusi lakini nyie ni mahabusi wa kisiasa, na wale ni makriminali. Lazima iwepo tafauti kati yenu". Kwa kusikia tu neno "wa kisiasa" basi hapo hapo hiyo chai "special" ilitutumbukia nyongo, tuliiona ni "special" kweli! Hapo tena tulianza kutizamana na kila mmoja aliingiliwa na khofu moyoni mwake. Tulikuwa tukiulizana tu wenyewe kwa wenyewe, siasa hizo tumezifanya wapi au za namna gani? Mradi hatukuweza kujijibu kwa lolote.

Ilipofika saa sita na nusu mchana, tuliletewa wali wa pilau nzuri na baada ya kumaliza kula, tulichukuliwa mpaka kwenye ofisi moja na huko tulitilishwa vidole (finger prints) na baada ya hapo, tulitiwa katika gari kubwa la polisi na tulipelekwa moja kwa moja mpaka kwenye kiwanja cha ndege za kijeshi. Tulipofika kiwanjani, tulipokelewa na maofisa wawili waliyokuwa hawakuvaa nguo za kiaskari na baada ya kukaa hapo kwa muda mchache, tulitiwa katika ndege ya kijeshi ya aina ya "caribou", tukifuatanishwa na askari watatu wa polisi wote wakiwa wamechukua bastola mikononi mwao. Ndege iliruka na baada ya kiasi cha nusu saa, tuliteremka kiwanja cha ndege cha Zanzibar. Hapo, tulipokewa na askari wa magereza na tulitiwa katika gari la magereza na kupelekwa Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu.

Tulipofika gerezani, tulisachiwa kisha tuliandikwa majina yetu na baada ya hapo, tulikutana na Mkuu wa Magereza, Bwana Adam Taib naye alituambia kama hivi: "Ndugu zangu, mimi nimeambiwa nikopokeeni na nikuwekeni mpaka watapo kuja wenyewe wakubwa. Sijui lolote baada ya hapo. Kwahivyo, msiniulize lolote. Ninalo kuombeni ni kuwa mkae kwa salama mpaka mtapokutana na wenyewe, mtaweza kujua kila jambo". Mpaka tushaletwa Zanzibar, yule askari aliyechukua viatu vyangu na soksi hajafika kuniletea. Ikiwa askari waliopewa dhamana ya kuzuwia ukhalifu usifanyike katika nchi, wao ndio wevi, basi nchi hiyo itakuwa na usalama gani?! Au mwananchi atapata haki yake kutoka wapi?

MAHABUSI WADHULUMIWA WA MWALIMU NYERERE Maalim Harun Ustadh Maalim Mohammed Mattar Seyyid Hassan Sheikh Seyyid Mohammed Adnan Mzee Mohammed Mbaba AhmedRashad Ali Hashim Haji Abdalla Seyyid Hashim Abdalla Baharun AbdulLatif Binbrek Mohammed Shioni Seyyid Mohammed Mattar Mohammed Ali Abbas Ali Abdalla (Admeri) Ali Jaffer Ali Khalifa Miskiry Ali Manara (Mtu wa Tanganyika) Aman Thani Fairooz

Baada ya kumaliza kutukhutubia, Mkuu wa Magereza, aliondoka na sisi kila mmoja alipewa kirago chake pamoja na shuka mbili na kopo la kunywiya maji na ndio hilo hilo la kutumia kwa kujisafishia baada ya kwenda haja kubwa na ndogo. Tulipomalizika sote kupewa vitu hivyo, tuliongozwa mpaka kwenye vyumba vya kulala mahabusi.

Siku ya pili, waliletwa wenzetu wawili wengine, mmoja alikuwa mwanamke, Bibi Mbarawa Bakari, yeye alipelekwa katika upande wa mahabusi wa kike na mwengine alikuwa Seyyid Harun Abdalla Baharun, yeye aliletwa upande wetu. Sote kwa jumla tukawa watu 19, mmoja mwanamke na 18 wanaume. Hawa wenzetu wawili, Bibi Mbarawa na Seyyid Harun wao walikamatwa hapo hapo Zanzibar. Mpaka wakati

43 huo tulikuwa bado hatujaweza kufahamu sababu zilizopelekea kukamatwa na kuletwa gerezani. Baada ya kiasi cha mwezi mmoja tokea kuletwa gerezani, Rais Karume pamoja na kikosi chake cha 'Baraza la Mavamizi' walikuja na Karume alitukhutubia kwa kutumia maneno kama haya: "Nyinyi mmeletwa kwetu kutokana na ukorofi mnaoufanya huko DaresSalaam. Mwalimu Nyerere ametoa amri muondolewe na mrejeshwe makwenu. Mpaka sasa bado hatujaletewa ripoti yenu kamili. Tutapoipata na baada ya kuichunguza, tutatoa uamuzi wetu. Ikiwa kukuachilieni huru au kukupelekeni mbele ya mahakama. Lakini mjue kuwa mahakama yenyewe ni ya kijeshi. Ikiwa mutaonekana na kosa, basi adabu yenu itakuwa KIFO".

Baada ya kusema hivyo, alianza kututukana na kututisha kwa kutumia lugha za ukali na za vitisho na alielekeza matusi yake na vitisho vyake zaidi kwa ndugu zetu wenye asili za Kingazija kwa vile ilitokea katika hilo kundi letu, jamaa wa Kingazija walikuwa wakionekana ni wengi. Kutokana na vitisho hivyo, ndugu yetu mmoja aliingiwa na khofu hata alitokwa na haja ndogo bila ya kuweza kujizuwia. Karume na kikosi chake walipomuona katika hali hiyo, badala ya kuamrisha aondolewe kwa kusitiriwa, waliangua vicheko wakamcheka na kumfanyia istihizai. Sisi tuliinamisha nyuso zetu chini utadhani wanawari wa kizamani. Ilikuwa ni siku hiyo na pahala kama hapo, gerezani, ndipo Rais wa nchi, Abeid Amani Karume alipotoa amri ikawa ndio sheria ya kuwa Wangazija wote si raia wa Zanzibar kuanzia siku hiyo na wakati huo. Mngazija yoyote mwenye kutaka uraia wa Zanzibar basi lazima afanye maombi ya Tajnis. Hapo hapo alimtaka AlHaj Aboud Jumbe awaite waandishi wa magazeti siku ya pili na awape khabari hizo. Mzalia wa Zaire anamwambia mzalia wa Tanganyika atangaze kuwa wazalia wa Zanzibar si Wazanzibari ati kwa kuwa asili ya wazee wao ni Comoro! Hii ndiyo haki?

Jambo la kustaajabisha na kuhuzunisha ni kuwa wakati huo alipokuwa Karume akipasisha sheria hiyo ya "kifashist", hao ndugu zetu wajiitao "progressives" walikuwepo na sio kuwa walinyamaza kimya kwa kuwafik hayo, bali walifurahikia na kupigia makofi na huku wakisema, "Sawa Mzee! Sawa Mzee"! Ikiwa u"progressive" wenyewe ndio hali yake kama hiyo, basi hatujui huo u"reactionary" utakuwa hali gani! Dikteta anatoa amri, amri inakuwa sheria ya nchi, bila ya hata kushauriana na hilo gengi lake la wauwaji, isitoshe, wanaojiita "progressives" wanasherehekea!! Baada ya hapo Karume na kikosi chake waliondoka na walituacha sisi katika khofu na ya wasi wasi kwa kufikiria yepi yatayotutokea, kwani yeye ndio keshatowa ruhusa tutendewe maovu wapendavyo hao aliowaachia nafsi zetu kwao. Serikali ya 'mavamizi' haikuwa ikiendeshwa kwa njia za haki, mwendo wake ni wa kinguvunguvu na kibabababa tu. Mfunge! Mnyonge! Mchinje! Ndio sheria zilizokuwepo. Kwahivyo tulikuwa katika hali mbaya sana baada ya siku hiyo.

Kiasi cha miezi miwili kutoka siku hiyo aliyokuja Karume gerezani, natumai ilikuwa taarikh 14 Ramadhan, Disemba 1968, kiasi cha saa 12 za magharibi muda mchache kabla ya kulia kwa kin'gora, alitujia sajini wa magereza na alitutaka tuchukue futari zetu tumfuate kwani wakati huo tulikuwa tumesha letewa mapande yetu ya muhogo wa kutokosa na majani mapevu ya kisamvu. Tulichukua na tulimfuata mpaka katika uwanja wa 'kotagadi' alituambia tukae hapo. Kiasi cha muda mdogo, kin'gora kililia na tuliruhusiwa kwenda kutawadha na kusali, tulifuturu na kiasi cha kumaliza tu, taa zote za 'kotagadi' zilizimwa kumekuwa kiza totoroo! Mara lango la gereza lilifunguliwa na gari la magereza likaingia ndani kinyume nyume. Roho zilitubakuka, vinywa vilijaa mate, mradi kila mmoja hajijui, hajitambui. Muda si muda, tuliambiwa tuingie katika hiyo gari. Msafara wetu haukuwa mkubwa sana kwani ulimalizikia kwenye gereza la kwa "Ba Mkwe" au kwa jina lengine, "Mlango wa Nyuma". Wakati huo, wenzetu wawili, AhmedRashad Ali na Ali Manara, wao walikwisha achiliwa huru.

Hili gereza la "Kwa Ba Mkwe" limeanzishwa na Serikali ya Mavamizi muda mchache tu baada ya kukamata kutawala. Makusudio makubwa ya kuanzishwa gereza hilo ni la kuwatesea wananchi ili wawe na khofu wasithubutu kutoa fikra zao na maoni yao kukhusu mwendo wa serikali. Wananchi wengi sana wamepotezewa roho zao katika gereza hilo. Gereza hilo lilikuwa chini ya uangalizi wa Idara ya Usalama (Security Department) na mkubwa wa Idara hiyo alikuwa Ibrahim Makungu, na mkuu wa gereza hilo, alikuwa Hassan Reihan (Hassan Mandera) au kwa jina lengine alikuwa akijulikana "ZIRAILI" na kweli alikuwa ziraili. Kwani mtu yoyote afikae mikononi mwake basi kurejea yuhai ni miujiza. Ponapona, utamalizikia gerezani kwa kifungo cha miaka kumi baada ya kufikishiwa kila aina ya mateso.

44

Tulifika kwa "Ba Mkwe" kiasi cha saa moja unusu za usiku na tulimkuta mwenyewe Mandera na watu wake wanatusubiri. Tulianza kuandikwa majina yetu mmoja mmoja, na kila anayemaliza kuandikwa akipelekwa kwenye vyumba vya gereza hilo. Tuligawanywa katika vyumba mbali mbali. Kwa wakati huo hapana aliyeweza kujua kuwa fulani yuko katika chumba fulani au yupo pamoja na fulani. Mimi nilibahatika kutiwa chumba kimoja pamoja na Shariff Mohammed Mattar, katika chumba hicho tuliwakuta watu wane weshakuwa wenyeji zamani. Wenzetu hao walitukaribisha na mmoja kati yao, alitwita kwa majina yetu. Yeye aliweza kututambua bali sisi tulishindwa kumtambua mpaka alipotujuulisha yeye mwenyewe. Hali zao zilikuwa zikitisha kwani wote walikuwa wamejifunga matambara na magunia viunoni kuwa ndio nguo zao za kujisitiri, matumbo wazi. Manywele timtimu na yamesokotana, madevu na masharubu yameziba vinywa. Chumba kinafuka moto, chumba chenyewe ni urefu futi 10 na upana futi 10, kina dirisha moja nalo liko juu hata ukichupa huwezi kulipata. Yule mzee aliyetwita kwa majina yetu alituuliza, "Jee, mnaweza kunitambua mimi nani?" Tulimjibu laa, hatujakutambua". Alisema, "Najua kuwa hamkuweza kunitambua. Jina langu ni Abbas Othman kwa jina la umaarufu naitwa Mzee Kenyatta". Alipotutajia jina hilo la Kenyatta, hapo hapo tuliweza kumfahamu. Hakika alikuwa amebadilika sana. Mzee Kenyatta alituambia kama hivi:

"Ndugu zangu, lazima nikuelezeni kukhusu mambo yaliopo katika gereza hili. Katika gereza hili, watu hawapewi virago vya kulalia, ndio kama mnavyoona hivi tulivyo tunalala na tunakaa juu ya sakafu kavu. Kadiri ya nguo ulizokuja nazo ndizo hizo hizo utazoishi nazo kwa muda utaokuwepo katika gereza hili. Hata ukiumwa basi hupelekwi kwa daktari, ukibahatika, unaweza ukaletewa vichembe viwili vya asprin, lakini si katika kawaida. Milango ya vyumba hivi inafungwa saa ishirini na nne. Kufunguliwa kwake ni kwa muda maalumu tu, tena haifunguliwi yote kwa wakati mmoja. Ukifunguliwa mlango wa chumba kimoja, vilivyo baki vyote huwa vimefungwa mpaka warejee waliyotolewa kutoka katika chumba hicho, ndiyo kifunguliwe chengine. Yaani musiweza kukutana wa chumba hiki na chumba hiki. Nyakati zenyewe za kawaida za kufunguliwa milango ni alfajiri kiasi cha saa 11 hivi. Wakati huo ndio hutoa ndoo ya uchafu wa choo, na wakati huo ndio tunautumia kwa haraka haraka kujitia maji mwilini, bila ya sabuni; na kusugua meno kwa kidole na kutumia udongo, hata kijiti cha msuwaki huachiliwa kuwa nacho hapa.

Baada ya hapo hufunguliwa tena kiasi cha saa moja ya asubuhi kwa kwenda kuchukuwa kifunguwa kinywa. Na baada ya hapo, hufunguliwa tena kiasi cha saa tano za mchana kwa ajili ya kuzitoa nje sahani za chai ya asubuhi. Na hufunguliwa tena kiasi cha saa nane za mchana kwa ajili ya kuchukuwa chakula cha mchana. Kisha baada ya hapo hufunguliwa tena kwa mara ya mwisho kwa siku hiyo kiasi cha saa 11 za jioni kwa ajili ya kuzitoa sahani za chakula cha mchana na kwa kuchukuwa maji. Muda wa kufunguliwa na kurejeshwa ndani hauzidi dakika kumi. Si ajabu tukaona hivi sasa, ukafunguliwa mlango na akatolewa yoyote kati yetu na ikawa ndio basi tusimuone tena, au baada ya muda wautakao wenyewe ndio wakamrejesha. Akitolewa mtu ndani ya chumba huwa kwa ajili ya mambo mane ndio khasa! Imma hutolewa kwa kubadilishwa chumba au kwa kwenda kuteswa, au kwa kwenda kuuliwa, au kwa kwenda katika gereza kuu kwa kufungwa. Amma kutolewa humu kwa kuachiliwa huru, hilo ni jambo la matokeo makubwa sana."

Mzee Kenyatta alimaliza kwa kusema, "Haya niliyo kuelezeni ni mambo ya kawaida ya gereza hilii. Lakini vituko vinavyotokea katika gereza hili mara kwa mara ni vingi sana na vinaweza kututokea katika wakati wowote si mchana, si usiku. Kwa vile mpo, mtayaona wenyewe". Wakati huo, ulikuwa kiasi cha saa nne za usiku, tulitafuna vipande vyetu vya muhogo tulivyo vibakisha vikiwa ndio daku letu, na tulipiga kopo la maji kisha tulipangusa pangusa mchanga, na tulijitupa katika sakafu kavu, na kuutafuta usingizi. Wapi! Usingizi haukukubali kuja. Kucha tulizifungua TV za moyoni ikimalizika, chanal hii tukifungua nyengine; mpaka tuliposali Alfajiri jicho halikukubali kufunga hata dakika. Kiasi cha kumaliza tu kin'gora cha asubuhi cha kuingia makazini, mlango wa chumba chetu ulifunguliwa na nilimuona kijana mmoja amesimama na alikuwa akitutizama kwa uso wa kijeuri uliyo changanyika na ujinga. Kijana huyo aliuliza kwa sauti ya kijeuri kabisa, "Nani Aman Thani hapa?" Nilimjibu, "Mimi hapa". Aliuliza tena, "Wewe ndiye uliyekuwa Katibu Mkuu wa Hizbu"? Nilimwambia, "Naam, ndiye mimi". Aliniuliza tena, "Na wewe ndiye sasa Katibu Mkuu wa chama chenu cha siri cha Kiislamu huko DaresSalaam?" Nilimjibu, "Chama hicho cha siri mimi sikijui, wala sijapata kukisikia, wala mimi siye

45

Katibu Mkuu wa Chama hicho ikiwa kipo". Aliniambia, "Baada ya muda mdogo, utakijua. Wengi kama wewe walipoletwa hapa, kila walichokuwa wakiulizwa wakisema, hatujui. Lakini baada ya kukutana na vijana wa kazi, kila walilosema hawalijui, walilijuwa wenyewe. Basi na wewe baada ya muda mdogo utayajuwa yote, subiri tu". Alipomaliza kusema hivyo, aliufunga mlango kwa kijeuri. Alipoondoka huyo kijana niliwauliza wenzangu, "Huyu ndiye nani"? Mzee Abbas Kenyatta aliniambia, "Huyu anaitwa Musa Makwega. Inasemekana kuwa ni mtoto wa ndugu yake Simba Makwega".

Naam, haukupita muda ila mlango wa chumba chetu ulifunguliwa tena na safari hii alikuja kijana mwengine. Kijana huyo alikuwa amevaa chupi tu, hakuwa na nguo nyengine yoyote katika mwili wake. Alipofika alisema, "Aman Thani na atoke nje". Nilitoka na niliongozwa mpaka kwenye chumba kimoja kikubwa na huko nilimkuta Mandera na Juma Musa. Hawa wawili nilikuwa nikiwajua tokea zamani. Pia walikuwepo na wengine ambao baadae niliwajuwa majina yao. Mmoja akiitwa Ame Fidia na mwengine, Haji kwa umaarufu akiitwa Haji Kifupi, na yule aliyekuja kunichukuwa akiitwa Mzee. Haji na Mzee wote wawili walikuwa ni vijana wa Bumbwini, Unguja, na Ame Fidia alikuwa kijana wa Tumbatu, na Juma Musa alikuwa kijana wa kiUnguja katika sehemu za mashamba, sikupata kujuwa shamba gani kwao.

Katika chumba hicho, kulikuwemo meza moja kubwa na viti viwili. Juu ya meza hiyo, kulikuwepo bastola moja na pembezoni mwa ukuta, kulikuwepo na mizigo kwa mizigo ya fimbo za mipera. Chini ya hiyo meza kulikuwepo kamba ya kitani iliyokuwa nene kidogo ambayo katika ncha yake moja ilikuwa na kitanzi. Kuta za chumba hicho na sakafu yake, vyote vilikuwa vimejaa mabaka mabaka ya damu iliyokaukia. Mandera aliniambia. "Aman, mimi na wewe tunajuana zamani sana. Hatujapata kukwaana hata mara moja, bali lazima nikuambie kuwa hapa katika gereza hili, hapana udugu, wala ubaba, wala urafiki, wala hapana kujuwana. Katika gereza hili, yapo mateso ya kila namna na tuna haki ya kumtesa mtu yoyote kwa mateso ya aina yoyote, maadamu atajifanya mkaidi wa kutwambia ukweli juu ya mambo tuyatakayo kutoka kwake. Na ikiwa atatwambia ukweli, basi hatoteswa na hatokaa humu kwa muda mkubwa ila atatolewa, na kwenda zake nje na kuendelea na maisha yake. Basi nakwambia na wewe ikiwa utataka uteswe basi utateswa; ikiwa utajaribu kuuficha ukweli, sisi tunazo khabari zote, lakini tunataka tuyakinishe kutokana na vinywa vyenu wenyewe." Aliendelea kwa kusema, "Tunalolitaka utwambie, ni nini makusudio ya kuunda hicho chama chenu cha siri cha Kiislamu, na ni nani wakuu wenu wenye kukiendesha chama hicho kwa kifedha? Tunajua kuwa nyie ni wenye kutumiliwa kwa kutekeleza madhumuni ya hao wakuu wenu. Nakuahidi, ikiwa utatwambia ukweli, basi hutokaa humu hata wiki, utatolewa na utarejeshwa DaresSalaam kuendelea na maisha yako".

Hakika nilisangazwa na masuali hayo kwani licha mimi kuwemo na kutokuwemo katika chama hicho, bali hata kupata kukisikia sijapata kukisikia maisha yangu. Nilimjibu kuwa, "Mimi sikijui, wala hao wakubwa wa chama hicho ikiwa wapo, mimi siwajui". Kiasi ya kumwambia hayo tu, nilimuona Mandera amebadilika sura yake na alianza kutumia lugha za ukali na matusi na mwisho aliniambia, "Ikiwa unataka kutuonesha uhodari kwa kukataa kusema kweli, basi na sisi tutakuonesha nini tutakufanya sasa hivi. Utatuambia ukweli au vipi?" Nilimwambia, "Ikiwa unautaka ukweli, huo niliyo kwambia ndio ukweli wala sina ukweli zaidi kuliko huo", "yote haya uyasemayo miye sijui lolote juu yake". Allah Akbar! Alinipiga kibao cha ghafla, kilinitupa mpaka chini. Hapo, aliamrisha nilazwe juu ya meza, sikuwahi hata kupepesa, nilijisitukia nimesha bwagwa juu ya meza kama gunia la chumvi na nimelazwa kifudifudi. Naam, Mandera hakupoteza wakati, alianza kunicharaza kwa fimbo za mipera na huku akinitukana kwa matusi mabaya mabaya. Nilikuwa siwezi hata kufurukuta kwani hao wasaidizi wake walinidhibiti mikono na miguu, mradi nilikuwa taaban! Tokea nilikuwa nikihisi maumivu ya kupigwa mpaka mwili ulikufa ganzi nikawa sihisi chochote. Tokea nikiweza kupiga makelele na kuyayatika mpaka nilikuwa siwezi hata kuguna. Alipochoka mwenyewe, ndipo na mimi nilipopata afuweni.

Lakini, wakati huo nilikuwa chordo! Chumba chote nikikiona kinazunguka na watu nikiwaona wanazunguka. Niliachwa katika hali hiyo kiasi cha muda mdogo, kisha Mandera aliniambia niinuke kwenye meza nikae katika kiti. Nilipojaribu kujizowazowa, miguu ilishindwa kukanyaga chini kwani bakora zilifika mpaka nyayoni na pia miguu ilikuwa ikinitetemeka. Nilikamatwa huku na huku na kuwekwa juu ya kiti. Mandera aliniuliza, "Umefunga wewe leo?" (kwani siku hiyo ilikuwa Ramadhani ya kumi na tano) Nilimjibu, "Naam, nimefunga!" Aliniambia, " Basi leo, utafuturu mikwaju". Wakati huo roho ilikuwa kavu, mate yamenikauka, jasho likinitoka kila sehemu ya mwili. Matako yametutumka na

46 kupasuka pasuka. Kiti kilikuwa hakikaliki kwani kilikuwa kikinitonesha. Kwa hakika, nilikuwa katika hali mbaya sana. Baada ya Mandera kupumua kidogo, alirejea tena kuniuliza masuali yake yale yale aliyoniuliza mara ya mwanzo. Na mimi, nilimjibu kama nilivyomjibu mwanzo. Hapo, Mandera aliamrisha nitiwe ile kamba ya kitanzi na nikatiwa nayo shingoni. Baada ya kutiwa, ilichukuliwa ncha moja ikapitishwa dirishani. Dirisha hilo lilikuwa juu sana hata huyo aliyekuwa akipenyeza hiyo kamba ilimbidi apande juu ya meza kuitupia.

Wakati huo mimi nilikuwa nimekaa juu ya kiti na shingoni mwangu nimevalishwa hicho kitanzi cha kamba ya kitani. Wote walitoka nje, isipokuwa Mandera tu alibakia pamoja na mimi na kitanzi changu shingoni mwangu. Utafikiri n'gombe mkali wa kuchezwa. Wale waliyokuwa wametoka nje, kazi yao ilikuwa kuivuta ile kamba mfano wa mtu anapovuta ndoo ya maji kutoka kisimani kwa kutumia roda. Nilianza kunyanyuka, si kwa khiyari, bali kwa kule kuvutwa mpaka nilikiwacha kiti ikawa nafuata kule ninako vutwa. Mandera kazi yake ilikuwa ni kuamrisha, "Vuta! Wacha!" Akisema vuta, huvutwa na akisema wacha huachiliwa. Na ilipokuwa ikiachiwa, nilikuwa nikishindwa kujizuwia kwahivyo nikianguka kama nanga ibwatikavyo baharini. Mandera alikuwa akinipiga kwa fimbo za mipera na huku akiniambia, "Simama!". Mradi kazi ilikuwa kama hivyo, mpaka walipotaka wenyewe, waliniachia na walinitoa hicho kitanzi. Mandera alitoka nje ya hicho chumba na aliniacha mimi na hao wasaidizi wake. Juma Musa aliniambia, "Sikiliza Aman! Wacha ushupavu wako utakuja kujidhuru mwenyewe. Hapa ni pahala pabaya sana. Matokeo ya gereza hili hutoyaweza wewe, kwani ni ya khatari sana na mwisho ni kuuliwa. Basi mimi nakuomba useme kweli wa hicho chama chenu upate kujinusuru na mateso". Mimi nilinyamaza kimya sikumjibu chochote, kwani nilielewa kuwa anatumia lugha alizofundishwa katika kazi yake hii. Juma Musa alipoona hakupata chochote kwangu, na yeye alitoka katika hicho chumba na kuniacha mimi na hao wasaidizi wao wengine.

Baada ya muda, Mandera na Juma Musa walirejea katika chumba, Mandera aliwauliza hao watu wake kama nimesema chochote na Juma Musa alimwambia Mandera kuwa, "Anajifanya hodari, hataki kutwambia ukweli. Mimi nimejaribu kumnasihi, hata hakuonesha kuwa ananibali kitu". Mandera alisema, "Kwa nini hatumuuwi, kwani patakuwa kitu gani tukimuuwa? Lete ile bastola!" Kijana mmoja katika wasaidizi wake akiitwa Mzee, aliruka kuileta hiyo bastola. Mandera aliniambia, "Unaiona hii bastola, basi towa shahada kabisa. Leo utafuturu kaburini". Aliamrisha nifungwe kitambaa cha uso. Makame Fidia ndiye aliyenifunga hicho kitambaa. Nilitoa shahada. Hapo sikuweza kujuwa yalipitishwa mazingaombwe gani kwani nilisikia mlio mkubwa wa risasi lakini haikunigusa wala haikuniuwa, lakini kwa khofu nilizokuwa nazo, nilianguka mpaka chini. Nilipoanguka, niliwasikia wakicheka kwa tafrija na istihizai, na huku Mandera akisema, "Nyoo! Si unajitia uhodari wewe, mbona unaogopa kufa. Hii ya leo ni trai tu mchezo bado". Mandera aliamrisha nifunguliwe hicho kitambaa cha uso na baada ya kufunguliwa, aliniambia, "Leo tutakuachia ukapumzike na ukazidi kufikiri mpaka kesho. Utakapoletwa hapa uweumesha kata shauri juu ya kusema kweli au kuendelea na kuuficha ukweli. Lakini, nakwambia kuwa kesho ukitufanyia mchezo kama huu uliyoufanya leo, basi tutaanza kwa kukutoa kucha za vidole vya mikono, kisha tukutowe na vya miguu, na tutakupaka hina ya pili pili hoho. Sasa mrejesheni kwa wenzake. Wakati huo kin'gora cha saa nane unusu cha kutoka watu makazini kilikuwa kikilia. Mchezo ulianza tokea saa mbili za asubuhi mpaka wakati huo wa saa nane unusu ndipo ulipomalizika. Nilikuwa katika hali mbaya sana hata nilishindwa kwenda bila ya kusaidiwa kwa kukamatwa mkono utadhani mtoto mdogo anafundishwa kwenda tata.

Nilipofika katika chumba wenzangu waliponiona hali hiyo niliyokuwa wakati huo, jambo la mwanzo, walininasihi nisiendelee na saumu, na mimi nilihisi hivyo hivyo, kwani roho yangu ilikuwa kavu, midomo mikavu hata mate yalinikauka. Hapakuwepo na cha kukila kwa wakati huo, isipokuwa maji na hata kingekuwepo, basi nisingeweza kukila. Hayo maji nayo yalikuwa yakipita kwa shida. Mwili wangu ulikuwa umejaa mitutumko tutumko, na mipasuko pasuko ya bakora za Mandera hata nilikuwa na taabu kwa muda wa siku kadhaa kuweza kulala; bali hata kukaa kitako ilikuwa taabu. Ilipofika laasiri, nilipata homa kubwa sana na wenzangu walijaribu kuwaita wachungaji wa gereza hilo kwa kuwagongea mlango ili wapate kuniombea dawa. Hapana aliyekuja. Kwa bahati Mzee Kenyatta alikuwa na akiba ya vidonge vya aspirin, aliweza kunigaia vidonge viwili, si haba viliweza kidogo kunisaidia. Usiku kucha nilikesha kwa maumivu niliyokuwa nayo na kwa khofu nilizokuwa nazo kwa kufikiria hayo yaliyokuwa yakiningojea patapo kucha. Mandera nilikuwa nikimuona amenisimamia machoni mwangu. Kulipokucha

47 homa ilinizidi kwani ilikuwa kila dakika ipitayo, nilikuwa sasa hivi au khalafu nitakuja kuchukuliwa. AlHamdulillahi, nilishinda kutwa na kucha bila ya hata kuulizwa. Na ilikuwa ndio basi, hawakunichukua tena baada ya siku hiyo moja.

Tulikaa katika gereza hilo la "Kwa Ba Mkwe" tokea Disemba 1968 mpaka taarikhi 3 Mei, 1969 tulipotolewa na kupelekwa katika Makao Makuu ya Magereza. Kupelekwa kwetu huko kulikuwa kwa ajili ya kufungwa gerezani. Tulipofika 'kotagadi', ilikuwa kiasi cha saa 11 za jioni. Kila mmoja alipewa viroba vyake, na shuka moja, na kirago cha kulalia pamoja na kopo la kunywiya maji. Tulizivua nguo zetu na tulivivaa viroba vya kifungwa. (Viroba ni shati lisilokuwa na ukosi na suruali kipande, kaputura). Tulipoona tumepewa viroba vya wafungwa, kila mmoja alipigwa na msangao na machozi yalikuwa ya kimlengalenga. Tulijikaza kidume na tulikuwa tukipeyana moyo wenyewe kwa wenyewe. Waliyokuwa wakitusikitisha zaidi ni wale wenzetu waliyokuwa wazee kwa umri wao kama Seyyid Hassan Sheikh, Maalim Harun Ustaadh, na marehemu Maalim Mohammed Mattar. Wote hao walikuwa umri wao ni baina ya miaka 60 na 70 na hawakuwa na siha nzuri kutokana na maradhi waliyokuwa nayo, ya Presha, Sukari na maradhi ya ukongwe. Tuliweza kuelewa kuwa tumesha kuwa wafungwa lakini hatujui kifungo chetu ni cha muda gani. Juu ya hayo, kwa vile kuwa tumetoka katika gereza la "Kwa Ba Mkwe", tukiwa na uhay wetu. Ingawa baadhi yetu tulikutana na mateso lakini tumetoka bila ya vilema na kuwa angalau tutaweza kwenda huku na huku kuliko kukaa kitako kimoja usiku na mchana, bila ya harakati zo zote, tuliona siku hiyo kama tumeachiliwa huru.

Kabla ya kuondoka hapo 'kotagadi', tuliwaona wenzetu wengine nao wameletwa na kupewa viroba vyao. Miongoni mwao, walikuwemo, Bwana AbdulAziz Twala ambaye alikuwa Waziri katika Serikali hiyo ya Mavamizi, Bwana Jaha Ubwa, ambaye alikuwa, Mkuu wa Jimbo (Area Commissioner), Bwana Mdungi Usi, ambaye alikuwa, Katibu wa Baraza la Mji (Town Clerk), Bwana Aboud Nadhif, ambaye, alikuwa Mkuu wa Idara ya Muawana (Cooperative Society), Bwana Juma Maulid (Jimmy Ringo) ambaye alikuwa, Kamisari (Commissar). Pia miongoni mwao walikuwemo, Mzee Abbas (Kenyatta) na Ali Ngwenge, wote hao wawili ni katika wakereketwa wa AfroShirazi. Vile vile waliyoletwa kufungwa siku hiyo kutoka huko huko gerezani "Kwa Ba Mkwe", alikuwa ndugu yetu, Sheikh Saleh Ali Nasser (Saleh Master). Ndugu yetu huyu Saleh Ali Nasser (Master) ni mmoja kati ya wananchi waliyoteswa vibaya sana katika gereza hilo la "Kwa Ba Mkwe". Kwani siku hiyo tuliyoletwa Makao Makuu ya Magereza kwa kifungo, mwenzetu huyo alikuwa hata hakuweza kwenda sawa sawa kwa miguu yake.

Tulipomaliza sote tulipelekwa kwenye vyumba vya kulala mahabusi na kulipokucha baada ya kufungua vinywa kwa vipande vya muhogo mchungu wa kutokosa na uji wa sembe, tulipangwa na kunyolewa nywele mmoja mmoja kwa nyembe zilizokuwa butu kweli kweli. Kila mmoja alikuwa akichururika damu kichwani kwa kuparuzwa paruzwa. Baada ya hapo, tulipelekwa kwa Mkuu wa Magereza kwa kutia vidole vyetu katika Daftari la kuwekewa majina ya wafungwa. Kama kawaida, tuliyakuta yameandikwa yale yale ya kutia choko choko, kuhukumiwa na mkuu wa jeshi la Taifa katika mahakama ya Kijeshi. Mradi uwongo na unafiki mtupu.

Tulipofika kwa Mkuu wa Magereza, Bwana Adam Taib, ndipo tulipoambiwa kuwa tumefungwa miaka 10 kwa kila mmoja. Baada ya kuondoka hapo kwa Mkuu wa Magereza, nilimwambia Jaha Ubwa, kwa uchungu kwani ukishakuwa mfungwa huna tena unachokiogopa. Nilimwambia, Jaha, "Unaiona Serikali yako hii inavyosema uwongo hivi!? Jaji gani huyo aliyetuhukumu sisi, au mahakama gani hayo tuliyohukumiwa? Au nyinyi wenzetu, mlipelekwa?" Jaha masikini, alishindwa hata kunijibu. Alibakia akipuma tu na kunitumbulia macho. Neno alilolisema ni, "Mungu atatulipa". Yeye na wenziwe ndio hapo Mungu anawalipa kwa waliyoyatenda kuipindua nchi na kuunga mkono mauwaji ya ASP. Baada ya chakula cha mchana, tuliondolewa na kupelekwa gereza la Langoni (shamba).

MATESO YA "KWA BA MKWE" Wananchi wengi wa Unguja na Pemba wameteswa mateso mabaya mabaya katika gereza hilo la "Kwa Ba Mkwe". Wengi wamepoteza roho zao kwa mateso hayo na wengi wametoka humo na vilema katika viwiliwili vyao. Licha ya kuteswa kwa kupigwa kwa bakora bali baadhi ya wananchi wamefika kuchomwa moto wa sigireti katika tupu zao mpaka wakawachwa na madonda bila ya kupewa dawa ya namna yoyote. Wengine wamefukizwa pilipili hoho na huku wamefunikwa shuka. Wakifukizwa mpaka

48 chini ya tupu zao. Wapo waliyokuwa wameteswa kwa kumwagiwa mafuta ya petroli kisha wakawashwa moto. Wapo walion'golewa kucha za mikono na miguu na kutiwa rojo la pilipili hoho. Wapo walioteswa kwa kutiwa mpira katika tundu zao za kwendea haja kubwa na kisha wakamiminiwa maji mfano wa mtu anapopigwa bomba kabla kufanyiwa opereshini au kwa dawa fulani hospitali. Hufanyiwa hivyo, mpaka matumbo yakawajaa maji yakawa yanatokea mdomoni. Wapo walioingiliwa nyuma.

Nathubutu kusema kuwa mateso waliyokuwa wakiteswa wananchi wa Unguja na Pemba katika gereza hilo la "Kwa Ba Mkwe", hata huko Afrika ya Kusini wakati wa Rais Botha au Haiti wakati wa utawala wa Papadok, hayajawahi kufanyika kama hayo yaliyofanyika Zanzibar wakati wa Utawala wa Karume na AlHaj Aboud Jumbe. Lakini ulimwengu kwa sababu wazijuazo wenyewe, ulinyamaza kimya kama kwamba hakukuwa likitokea lolote. Lakini, ulimwengu si huu tu, utakuja ulimwengu mwengine na huko tutakutana na Hakimu mwenye kuyajuwa ya dhahiri na ya siri yaliyokuwa yametendeka. Hakimu mjuzi wa kuadhibu kama istahikivyo, bali sio Mandera, mateso ya Mandera hayawezi kulingana na hata chembe ya mchanga ya malipo ya Hakimu wa Kesho. Na tujiweke tayari, na hayo hayako mbali bali yako karibu kweli kweli. Ni kufunga pumzi tu!

MAISHA YA GEREZA LANGONI Hali ya maisha ya magereza katika wakati huo(1968) yalikuwa mabaya zaidi kuliko yale ya wakati ule wa mwanzo nilipokuwa nimefungwa (1964 1967). Shida za kila kitu zilikuwa kubwa. Chakula walichokuwa wakipewa wafungwa kilikuwa hakitoshi kulingana na ugumu wa kazi walizokuwa wakifanyishwa. Kwa jinsi ya wananchi walivyokuwa wakifungwa kwa wingi, ilifika mpaka magereza kuwa hayana nguo wala virago vya kuwapa wafungwa wepya, licha ya chakula. Wafungwa wapya walifika kupewa vipande vya magunia kuvaa viunoni na kulala juu ya upande wa gunia. Ilikuwa wanapomaliza baadhi ya wafungwa vifungo vyao, viroba vyao ndio hupewa wafungwa wengine bila ya hata kufuliwa.

Katika mwaka wa 1970 na 1971, magereza yakinuka njaa na uchafu kwani kulikuwa hakuna chakula chochote baada ya muhogo mchungu asubuhi na mchana kwa majani mapevu ya kisamvu. Wafungwa walikuwa wakikiita chakula hicho, "full suit" kwa kuwa chakula ni muhogo na kitoweo chake ni majani ya muhogo. Muhogo wenyewe ulitokea kuwa mchungu na zaidi ya mambo chumvi nayo ilikuwa imeadimika kwahivyo, mambo yalizidi kuwa magumu. Wafungwa walikuwa wakiponea makoroma ya nazi wakati wanapokuwepo katika kazi za nje, makondeni na vichakani.

Jua lilikuwa kali sana hata mito mingi na visima, vilikauka vikawa havina hata tone moja la maji. Wafungwa walikuwa wakinuka kama fungo. Mwenyezi Mungu alijaalia kisima kimoja kiliopo karibu na gereza la Langoni kilikuwa kikitoka maji. Lakini, watu wakitoka Kizimbani Sakafuni kuja kuteka maji hapo, na kisha wakiyapakia kwa mapipa na madebe katika magari ya n'gombe. Mradi dhiki ilikuwa kubwa sana. Kwa jinsi ya wafungwa walivyokuwa wengi, ulifika wakati tulikuwa tukilala wafungwa 70 mpaka 80 katika banda moja ambalo lililokusudiwa kulazwa wafungwa si zaidi ya 30 mpaka 40 kwa wingi.

Wananchi walikuwa wakifungwa ovyo bila ya makosa yoyote. Ikiwa Mheshimiwa anamtaka mke wa mtu na hampati kwa sababu wewe unamuhifadhi na kutoka ovyo ovyo, basi utasitukia unakumbwa na Mandera bila ya kulijua kosa ulilolitenda. Kwanza utawekwa katika hilo gereza lake la "Kwa Ba Mkwe" na mwisho utapelekwa katika gereza kuu kwa kifungo cha kuanzia miaka mine mpaka miaka 10! Hujahukumiwa wala hujaambiwa umefanya nini.

NYAKATI ZA KUFANYISHWA KAZI "WAFUNGWA WA SISASA" Kengele ya kuamshwa wafungwa ilikuwa ikipigwa saa 11 za alfajiri. Likifunguliwa tu banda wengine tulikuwa tukikimbilia vyooni, na wengine walikuwa wakikimbilia kuchukua kifungua kinywa. Saa 12 barabara tulikuwa tukitolewa kwenye kambi na kupelekwa sehemu za kufanyishwa kazi. Kiasi ya saa moja asubuhi tukianza kufanyishwa kazi ikiwa za kulima au za kun'goa minazi au za namna yoyote mpaka saa tisa za alaasiri ndipo inapo simamishwa kazi na kurejeshwa kambini kwa wale waliyokuwa wameweza kumaliza kazi zao. Ama kwa wale waliyokuwa hawakuweza kumaliza mpaka kufika wakati wa kusimamishwa kazi, wao walikuwa wakiachwa hapo hapo kuendelea na kazi wamalize sehemu zao.

49

Wafungwa wanaorejeshwa kambini wakiwa wamemaliza kazi zao kwa wakati, wao baada ya kula chakula na kupumzika kidogo, walikuwa wakichukuliwa tena kwa kufanyishwa kazi ndogo ndogo kama vile, kukata majani, kwenda kuokota kuni, kupalilia matuta na hata wakati mwengine kupalilia mpunga na kulima. Kazi ya wakati huo ilikuwa ikiitwa "fatiki". Ikianza saa 11 mpaka saa 12 za magharibi. Baada ya hapo ndio tukiachiliwa kiasi cha nusu saa kukoga ikiwa maji yapo.

Katika wakati wa kikoloni, wafungwa walikuwa wakifanyishwa kazi kuanzia saa moja ya asubuhi mpaka saa saba za mchana, na walikuwa hawafanyishwi kazi siku za Jumapili, wala siku za mapumziko mengine ya Serikali, wala walikuwa hawafanyishwi hiyo "FATIKI". Lakini wakati wa Serikali ya wenyewe, wenye kujiita, "waleta usawa na waondoa dhulma kwa wananchi wanyonge", ndio wakati ilipofanyika dhulma ya daraja ya juu na ndio wakati waliyokuwa wamedhulumiwa hao wanyonge. Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha DaresSalaam walipofanya maandamano na kusema bora mkoloni Mwalimu Nyerere alihamaki na kukifunga chuo hicho kwa muda! Kweli chungu.

UFUNGWA WA KARUME NI ZAIDI YA UTUMWA Mara nyingi Mwalimu Nyerere na viongozi wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar husema juu ya ubaya wa utumwa uliyokuwepo visiwani Zanzibar. Hatusemi kuwa utumwa ulikuwa ni kitu kizuri, hashaa! Kumnunua binaadamu mwenzio na kummiliki upendavyo ni jambo baya sana na wala hapana binaadamu mwema awezaye kulikubali au kulikubalisha jambo kama hilo. Kwa kufahamu ubaya na idhlali za mtu kunyimwa uhuru wake wa maumbile Zanzibar ilikuwa miongoni mwa wa mwanzoni kuharamisha utumwa. Utumwa umeondolewa rasmi Zanzibar tokea mwaka 1897, ni kiasi cha miaka 67 mpaka hapo yalipofanyika hayo 'mavamizi', katika 1964. Idadi kubwa sana ya wananchi wa Unguja na Pemba hawajui huo utumwa namna ulivyokuwa, lililokuwepo ni kusikia tu. Juu ya hivyo, iwapo tutachunguza kwa kutumia akili zetu kwa njia za insafu, na tukaweka upande chuki zetu binafsi, tutafahamu kuwa utumwa uliokuwepo katika visiwa vya Zanzibar, haukuwa wenye mateso kama ilivyokuwa katika nchi ya Kimarekani na nchi zenginezo ulimwenguni. Kwani lau ingalikuwa watumwa katika Zanzibar walikuwa wakiteswa kama wadaivyo akina Nyerere na wenziwe, basi, wakati ulipopigwa marufuku huo utumwa, asingetokea hata mmoja kukataa kuondoka katika nyumba ya huyo aliyekuwa bwana wake.

Katika kitabu "Short History of East Africa", Dr. Hollingsworth ameandika miezi mitatu baada ya kutoka sheria ya kuwa mwenye kutaka uhuru wake akabadilishe basi ni watu 120 tu waliokwenda jiandikisha. Anasema Hollingsworth, "Ni jambo la kweli kuwa watumwa wengi wakiangaliwa vizuri na bwana zao". Mpaka hivi leo wapo vilembwe vya hao waliyokuwa watumwa wanaishi pamoja na vilembwe vya hao waliyokuwa mabwana. Si kama wanaishi tu, bali wazee wao wamezaliwa katika majumba hayo na wao wenyewe wamezaliwa katika majumba hayo hayo. Na wanaishi kama ni ndugu na wajomba. Katika huo wakati wa utumwa tunavyosikia kutokana na wazee ni kuwa watumwa walikuwa wakipewa pahala pao pakulala, wakipewa chakula kizuri, wakiozwa wake na wanawake wakiozwa waume na wengine walikuwa wakiolewa na hao mabwana zao na vizazi vingalipo hadi hivi leo. Watumwa walikuwa hawafanyishwi kazi siku za Ijumaa wala siku za Sikukuu na walikuwa hawaadhibiwi kwa kupigwa labda ikiwa wamefanya makosa yaliyokuwa makubwa. Watumwa waliandikiwa mashamba na majumba na bwana zao.

Haya, natuwatizame hao watumwa wa Karume waliyokuwa wakiitwa, "wafungwa wa kisiasa", ilikuwa kabla ya kupelekwa katika mateso ya kufanyishwa kazi, kwanza walikuwa wakipelekwa kwa Mandera wakateswe kwa kila namna ya mateso. Watakao bahatika kubakia na uhai kutokana na mateso hayo ndio tena hupelekwa magerezani kwa kufanyishwa kazi ngumu zenye mateso makubwa makubwa. Watumwa hao wa Karume walikuwa wakifanyishwa kazi kutoka saa moja ya asubuhi mpaka saa 12 za magharibi na walikuwa hawapewi chakula zaidi ya muhogo na majani mapevu ya muhogo. Walikuwa hawaachiliwi kupumzika laa Ijumaa walaa Jumaapili walaa siku za Sikukuu. Wakiumwa walikuwa wakiachwa hivyo hivyo na maradhi yao mpaka wapone kwa kudra za Mwenyezi Mungu na wengine wameondoka duniani kwa kutokupata matibabu yenye kufaa. Kwa jumla watumwa wa Karume khasa tuliokuwa wakiitwa, "wafungwa wa kisiasa", tulikuwa haturuhusiwi kuja kutizamwa na watu wetu bali, hata kuwaandikia barua tulikuwa haturuhusiwi. Kwa wingi na shida ya mateso tuliyokuwa tukiyapata, katika kufanyishwa kazi, wawili kati ya kundi letu la watu 16 tuliyoletwa na Nyerere kutoka DaresSalaam walikufa gerezani. Nao ni Mzee Mohammed Mbaba na Maalim Harun Ustadh. Wote hao

50 wawili waliumwa na waliachwa wakiatilika na maradhi bila ya kupewa matibabu, ingawa Bwana Mganga wa gereza la Langoni, alitoa amri ya kutaka wapelekwe wakaonane na Daktari mkuu katika hospitali kuu ya mjini. Lakini aliyekuwa mkuu wa magereza ya Langoni na Kinu Moshi, Muhidin Khamis Kwangwati alikataa kuwapeleka na aliwaacha hapo hapo gerezani mpaka walipokuwa karibu na kukata roho, ndipo alipo waondoa na kuwapeleka kwenye kihospitali kidogo cha gereza kiliopo katika Makao Makuu ya Magereza Kiinua Miguu, na huko hawakukaa muda illa waliiaga dunia. Tuliishi katika hali kama hizo za dhiki na shida pamoja na mateso ya kila namna kwa muda wa siku 1110 yaani miaka mitatu na siku.

KUREJESHEWA UHURU WETU Taarikhi 9 Januari, 1972 katika nyakati za asubuhi, Karume pamoja na kikosi chake cha Baraza la Mavamizi walikwenda kwanza katika Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu na baada ya kuwakhutubia wafungwa huko walikuja shamba katika gereza la Langoni. Walipofika hapa Karume alitukhutubia kwa kutuambia, "Leo tumekuja kukuachilieni huru wafungwa wote na tumeamua kuyafunga magereza yote na badala yake, tutafungua Vyuo vya Mafunzo katika sehemu hizi hizi za magereza. Ingawa tokea hii leo nyote ni huru lakini mtabakia humu humu magerezani mpaka siku ya taarikhi 12 Januari, siku ya kusherehekea Mapinduzi, ndio siku mtaoachiliwa kwenda majumbani mwenu". Baada ya kumaliza kusema maneno hayo, Karume kama kawaida yake alianza kutoa porojo lake lisilo miguu wala kichwa, alipochoka mwenyewe alinyamaza, na aliondoka pamoja na kundi lake na kutuacha sisi katika hali ya furaha na kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika waliyoachiliwa huru katika wakati huo, walikuwa wafungwa wote, hawakuwa wa siasa tu peke yao hata wakhalifu nao waliachiliwa. Siku hiyo magereza yaligeuka kama viunga vya pikniki kwani baada ya kuondoka Karume na kikosi chake, tulianza kurejeshewa uhuru wetu, tulirejeshewa nguo zetu, tulikuwa huru kuzunguka huku na huku bila ya kulindwa. Usiku tulikuwa tukilala bila ya kufungiwa milango, na badala ya kwenda haja ndogo na kubwa katika ndoo na wenzio wanakuona na wanakusikia, tulikuwa tukitoka na kwenda vyooni nje ya mabanda yetu ya kulalia. Tulianza kuitwa kwa majina yetu badala ya kuitwa wafungwa kama tulivyokuwa tukiitwa kabla ya hapo. Nyoyo zilidanganyika na kuona kama yaliyokuwa yametupitia si kitu. Tulikuwa tukiziona saa hazendi kwa jinsi tulivyokuwa tukiomba siku ya taarikhi 12 ifike tupate uhuru wetu.

Saa nne za asubuhi siku ya taarikhi 12 Januari, 1972, tuliondolewa kutoka katika magereza ya Langoni na Kinu Moshi na tulipelekwa Uwanja wa Amani Chumbuni. Tulipofika huko, tuliwakuta wafungwa wenzetu waliyokuwepo kwenye makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu, wameshafika kabla yetu. Mnamo saa tisa za alasiri, uwanja wa Amani ulikuwa hauonekani kwa umayamaya wa watu. Wake kwa waume, wakubwa na wadogo, majeshi na askari polisi pamoja na wachungaji wa magereza, valantiya, pamoja na akina mama na akina baba. Wakati ulipowadia, magwaride yalipamba moto tuliwaona wa akina mama na wa akina baba wakihemkwa uwanjani na bunduki zao mabegani. Waongozi wote wa Serikali ya Mavamizi isipokuwa Rais Karume peke yake walikuwa wamevaa nguo za kijeshi hata Sheikh Thabit Kombo na Sheikh Daud Mahmoud nao walikuwa wamevaa nguo za kijeshi! Zilipomalizika hizo tafrija za magwaride, Rais Karume aliukhutubia umma uliohudhuria hapo kwa kuyataja maendeleo yaliyopatikana kutokana na hayo yenye kuitwa 'Mapinduzi'. Alipofika kusema, "Leo, tunawaachilia huru wafungwa wote na kuanzia hii leo, tunayafunga magereza yote yaliopo katika nchi na badala yake, tunafungua Vyuo vya Mafunzo", alipomaliza kusema hivyo tu, mkutano ulivunjika bila ya kuvunjwa kwa kawaida yeke.

Umma wote uliyokuwepo hapo, uliteremka uwanjani na kutujia katika sehemu tulizokuwa tumewekwa na walipotufikilia, walitukumbatia kwa furaha kubwa na huku walikuwa wakitupa stahili salama. Kufumba na kufumbua tulijiona tumeshatoka nje ya uwanja na hapo kila mmoja alichukuliwa na ndugu pamoja na masahibu na wananchi wenzetu na tulitiwa katika mamotokari na kupelekwa majumbani mwetu. Nilipo fika nyumbani nilipokelewa na ahli zangu kwa furaha na kwa hoihoi pamoja na kuvunjiwa nazi ikiwa ni "DafaalBalaa".

Kabla ya kuendelea na kuyaelezea maisha yangu baada ya kutoka katika utumwa wa Karume na Baraza lake la Mavamizi na kuwa huru pamoja na aila yangu, kwanza nitayataja yale yaliyowafika wananchi

51 wenzangu kwa kuyaona kwa macho yangu. Na yale niliyohadithiwa na waliyoyaona na waliyotendewa kwa nafsi zao kutokana na hayo yenyekuitwa, 'Mapinduzi'.

KUULIWA WANANCHI MSIKITINI Mnamo taarikhi 9 Septemba, 1964 katika kiasi cha saa tatu za usiku, mmoja katika wakuu wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, Mohammed Abdalla Kaujore, baada ya kupiga bangi zake na kunywa ulevi wake aliwaingilia wananchi waliyokuwa wakifanya ibada zao ndani ya Msikiti wa Ithinaashiri wa Kiponda na kuwauwa kwa kuwapiga marisasi bure bilashi. Watu watano waliuwawa siku hiyo. Mmoja kati ya hao alikuwa mtoto wa miaka minane akiitwa, Abbas Kassim. Wengine walikuwa, Seyyid AbdulMuttalib Hashim, Seyyid Ali Asghar, Haj AbdulHusain Tejani na Babu Haji.

Edington Kisasi akiwa miongoni wa wakuu wa hiyo Serikali ya Mavamizi na ndiye wakati huo aliyekuwa mkuu wa Polisi, alitangaza katika Radio ya Zanzibar, "Serikali inasikitishwa sana kwa kitendo kilicho fanyika katika Msikiti wa Ithinashiri, Kiponda. Na Serikali inafanya uchunguzi juu ya tokeo hilo na mara tu baada ya kupatikana matokeo ya uchunguzi huo, Serikali itachukuwa khatua za kutosha juu ya ukhalifu uliyo tendeka". Mpaka naziandika khabari hizi ndani ya hiki kijitabu, imeshapita miaka 30 tokea kutokea tokeo hilo, na hata hilo uwaji lenyewe nalo limesha kufilia mbali, na bado Serikali ya Mavamizi haijaweza kutoa natija ya hakika juu ya huo uchunguzi waliyokuwa wameusema kuwa waufanye! Katili hilo liliachiliwa likitembea kwa marefu na mapana kama kwamba halikufanya lolote,bali lilibaki katika cheo chake vilevile. (Mwizi mgema, askari mgema, na hakimu mgema. Jee mwenye mnazi atapata haki hapo?)

Bado utamsikia Mwalimu Nyerere na waongozi wake wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar na hata hao ndugu zetu wajiitao, "progressives" ati nao husema kuwa, "tumefanya Mapinduzi kwa ajili ya kuleta usawa na kuondoa dhulma zilizo kuwa zikifanywa na Masultani na Mabwanyenye!" Masultani gani hao na Mabwanyenye wepi hao waliyo wahi kuingia Misikitini au Makanisani, licha ya kuwauwa au kuwapiga waumini katika nyumba zao za Ibada, bali hata kuwazuilia kufanya Ibada zao? Hayajawahi kutokea hata mara moja katika maisha yote.

KUULIWA KWA WANANCHI WENGINE Baada ya kumalizika mavamizi hayo Jamuari, 1964 na yakatendwa yaliotendwa, tangu kwa kuuliwa na kwa kudhalilishwa kwa kila aina, haikutosha bali daima wananchi wakitishwa na kukamatwa kamatwa ovyo. Katika mwaka 1964, Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar kama kawaida yake iliwavamia na kuwakamata baadhi ya wananchi. Wananchi hao wengine walikamatwa kutoka majumbani mwao, wengine kutoka makazini mwao na wengine mabarabarani. Baada ya kuwakamata kwanza waliwapeleka kwenye kituo cha Jeshi cha Mtoni na baadae waliwaondoa, wengine walipelekwa kwenye Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu na wengine walipelekwa kwenye kituo cha Kijeshi "Army House", kilichokuweko huko Migombani.

Miongoni mwa waliokamatwa wakati huo walikuwa Mabwana hawa: (akiwemo bibi mmoja) Muhammed Salim (Jinja) Amour Zahor Said Dahoma (Kombanyongo) Mohammed Hamoud Barwani Nasser Mansour Musa Ahmed (Lashoka) Sultan Binbrek Ali Mohammed Barwani Bibi wa Unguja (Mke wa Bwana AbdulRahman Haider[ Maalesh])

Mohammed Salim Jinja, Amour Zahor, Said Kombanyongo, Mohammed Hamoud na Hamza Mohammed, wao ndiwo walioondolewa kutoka Makao Makuu ya Magereza na kupelekwa "Army House". Tokea siku hiyo waliyoondoshwa kutoka Makao Makuu ya Magereza hadi hii leo hawa jaonekana tena. Kutokana na khabari zenye kuaminika na hao wenziwao waliyokuwa pamoja wakati huo zinasema kuwa wote hao

52 yaani Mohammmed Salim Jinja, Amour Zahor, Said Kombanyongo, Mohammed Hamoud na Hamza Mohammed, wameuliwa siku moja katika sehemu ya Kama, Unguja kwa kupigwa risasi.

NAMNA WALIVYO ULIWA Kabla ya kuuliwa, kwanza walitakiwa wao pamoja na hao wenziwao, wachimbe shimo kubwa liwe ndio kaburi lao, yaani wajichimbie wenyewe kaburi lao. Baada ya kumaliza kulichimba, aliitwa kwanza, Sheikh Mohammed Salim Jinja na alitakiwa avuwe nguo zote hata chupi, na alizivua. Baada ya kuzivua, alipewa kalamu na karatasi aandike wasia ikiwa anapenda. Sheikh Mohammed alikataa kuandika. Aliambiwa afungue kinywa na baada ya kufungua, alitiwa bastola kinywani na alifyatuliwa risasi humo humo kinywani. Hapo hapo alikufa na alisukumwa ndani ya hilo shimo. Baada yake, wapili alikuwa Sheikh Amour Zahor. Yeye vilevile alitakiwa avue nguo zote, alizivua, ila yeye alikataa kuvua chupi. Yeye aliwekewa bastola juu ya kifua upande wa mkono wa kushoto na ilifyatuliwa risasi. Sheikh Amour yeye alikaiwia kidogo kufa, na alitumbukizwa shimoni akiwa bado anatweta. Mwengine, aliyefuatia kuuliwa alikuwa, Sheikh Mohammed Hamoud na baada yake alifuatia, Sheikh Said Dahoma Kombanyongo na wa mwisho alikuwa Seyyid Hamza Mohammed. Wenziwao waliyokuwa pamoja nao katika siku hiyo, walikuwa, Mabwana Nasser Mansour, Musa Ahmed (Lashoka), Ali Awadh, Awadh Salim, Idi Juma, Said Ali Hamoud AlHarthy, AbdulRahman Haider (Maalesh), Sultan Binbrek na Bibi wa Unguja. Walitakiwa wawafukie wenziwao ndani ya hilo shimo walimotumbukizwa likiwa ndio kaburi lao.

Baada ya kumaliza kuwafukia hao wenziwao, waliambiwa, "Nyie siku yenu kesho. Tutakumalizeni kama tulivyowamaliza hawa wenzenu. Leo mtarudi gerezani na kesho mtaletwa tena hapa. Tunakwambieni, hatutaki kusikia mmesema lolote katika haya yaliyopita hapa hii leo. Walirejeshwa gerezani katika hali mbaya sana kwani walikuwa kama wamerukwa na akili kwa khofu zilizowajaa kwa kushuhudia ukatili kama huo wakitendewa wenziwao. Mungu ndiye Mungu, wao walijiona ndio wenye uwezo wa kufanya kila walitakalo. Walisahau kuwa Mwenye Enzi Mungu ndiye mwenye nguvu na ndiye muweza wa kufanya atakalo. Wananchi hao waliyobakia, hawakupelekwa kwenda kumalizwa kama walivyoambiwa. Wengine kati yao, baada ya kukaa kwa muda gerezani waliachiliwa huru. Katika wao walioachiliwa walikuwa, Sheikh Ali Ahmed Riami, Sheikh Ali Mohammad Barwani, Sheikh Sultan Binbrek, Bibi wa Unguja na baadhi ya wengine waliyo kuwa pamoja nao. Waliyokuwa wamebakishwa gerezani walikuwa ni, Musa Ahmed (Lashoka), Nasser Mansour, Idi Juma, Ali Awadh, Awadh Salim, AbdulRahman Haider (Maalesh) na Said Ali Hamoud AlHarthy, wao walifungwa vifungo vya miaka 10 kwa kila mmoja. Wananchi hao, wadhulumiwa wamekaa katika magereza toka mwaka huo wa 1964 mpaka 1972 walipoachiliwa huru pamoja na wenziwao wengine.

WAFUNGWA WALIYOKUFA GEREZANI

(1) Mzee Mohammed Mbaba Mzee Mbaba alianza kuumwa mguu wa kulia, mguu huo ulikuwa haukuvimba wala haukuwa na kijaraha chochote, bali ilikuwa kila siku zikiendelea na ugonjwa ulikuwa ukimzidi kwa nguvu, na akizidi kudhoofika kiwiliwili chake. Tokea alikuwa akiweza kwenda kwa kuchechemea mpaka alikuwa hawezi kwenda bila kuchukua mkongojo. Na mwisho alishindwa kabisa hata kuunyanyua mguu huo. Kila wakati alikuwa akipata homa na kichwa kilikuwa kikimtaabisha sana. Dawa alizokuwa akipewa hapo gerezani Langoni ni, Aspirin na dawa ya kusugua (Local Liniment). Bwana Mganga wa gereza la Langoni alitoa uamuzi wake wa kutaka Mzee Mbaba apelekwe katika hospitali kuu mjini ili aweze kupata kuangaliwa zaidi na Daktari. Lakini mkuu wa Magereza ya Langoni na Kinu Moshi, Muhidini Khamis Kwangwati alikataa kufuata uamuzi huo. Mzee Mbaba aliachwa akisononeka na kuatilika hapo hapo juu ya kirago chake mpaka ilifika hadi ikiwa anataka kwenda haja ni lazima abebwe au achukuliwe kitikiti mpaka chooni. Wakati mwengine tulikuwa tukimuweka juu ya ndoo, kwani ilikuwa taabu kwake kuweza kuchutama kwenye lindi.

Alipofika hali ya kutokuweza hata kula na maji mpaka anyweshwe na kushindwa hata kusema sawa sawa, ndipo hapo, mkuu wa Magereza, Muhidini Khamisi Kwangwati, alipotoa amri ya kupelekwa Mbaba kwenye hospitali ya Makao Makuu ya Magereza Kiinua Miguu. Mzee Mbaba hakutimiza muda ila aliiaga dunia akiwa katika kifungo chake cha kudhulumiwa.

53

Tuliyoweza kuyapata baadae kukhusu sababu ya maradhi ya Mzee Mbaba ni kama haya: Mmoja miongoni mwa waliyokuwa maofisa wakuu wa Jeshi la Tanzania akiwa katika wakereketwa wa juu wa kiKomredi wakati alipokuwa na yeye kiziwizini katika gereza la Dodoma, Tanganyika kutokana na kuuliwa kwa aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, Abeid Amani Karume; alimzungumzia mahabusi mwenziwe kwa khofu alizokuwa nazo wakati huo kuwa, "Linalo niogopesha mimi ni kujatiliwa sumu katika chakula, kama alivyotiliwa Mzee Mbaba. Sumu hiyo haiuwi kwa mara moja bali inamuatilisha mtu kidogo kidogo mpaka baada ya muda ndio inapomuuwa. Sumu hii tuliletewa na baadhi ya marafiki zetu, na wa mwanzo kujaribiwa sumu hiyo alikuwa Mzee Mbaba". Hayo aliyesema kwa mdomo wake komredi huyo kutokana na khofu alizokuwa nazo. Ama kweli, mkuki kwa nguruwe, kwa binaadamu mchungu.

(2) Maalim Harun Ustadh Wakati tulipofungwa gerezani, Maalim Harun alikuwa akikurubia miaka 70 na siha yake tokea kabla ya kufungwa haikuwa nzuri kutokana na umri wake na maradhi aliyokuwa nayo, presha na ugonjwa wa miguu. Lakini kwa kuwa alikuwa akipata matibabu yaliyokuwa bora na vyakula vyenye kutengeza viwiliwili vya binadamu, na alikuwa na uhuru wake ekenda huku na huku aliweza kuishi kwa uzuri. Kwa kufungwa na kuyakosa yote hayo, na juu yake kufanyishwa kazi zisizokuwa kadiri yake kutokana na umri wake na maradhi aliyokuwa nayo, kila siku uchao alikuwa akizidi kudhoofika. Mambo yalipomzidia, alianza kukohoa na kutoka damu katika makohoo. Baadae alianza kuvimba miguu na uso na kupata shida ya kuvuta pumzi. Bwana Mganga wa gereza la Langoni, alitoa pendekezo la kutaka apelekwe Maalim Harun hospitali kuu kwa kukutana na Daktari mkuu, Muhidini Khamis Kwangwati mkuu wa gereza hilo la Langoni na Kinu Moshi kama kawaida yake alipinga na alimuacha Maalim Harun hapo hapo gerezani akiatilika na maradhi. Alipofika hali ya kuchungulia kaburi kwani alikuwa hata akisema, maneno hayatambulikani sawa sawa na kutoweza hata kujisaidia mwenyewe, ndipo hapo alipoondolewa na kupelekwa katika hicho kihospitali cha Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu. Na huko haukuchukua muda ila naye aliiaga dunia kama alivyoiyaga mwenziwe Mzee Mbaba.

(3) Idi Hassan Huyu ni kijana wa kiMakunduchi, aliwahi kuwa Inspekta wa polisi. Alipostaafu alijiunga na AfroShirazi na alikuwa miongoni mwa wakereketwa wakubwa wa AfroShirazi. Baina ya 1970 na 1971, Idi aliletwa gerezani, Langoni kwa kifungo cha miaka 10 baada ya kuwekwa katika gereza la "Kwa Ba Mkwe" kwa muda mkubwa. Alipoletwa gerezani alikuwa katika hali mbaya ya siha yake kwani kwa mujibu wa kauli yake mwenyewe alisema kuwa Mandera alimtesa sana kwa kumpiga na kwa mengineo. Idi baada ya muda mdogo tokea kufungwa, alipata maradhi ya kifua kikuu (TB). Siku moja ghafla alipokuwa anarejeshwa kutoka kufanyishwa kazi, alikohoa na kutapika mapande, mapande ya damu. Kiasi cha kwenda kuitwa Bwana Mganga kutoka kwenye 'dispensari' ya Kizimbani, alipofika alimkuta Idi zamani ameshaondoka duniani.

(4) Ramadhan Ibrahim Saadalla Huyu alikuwa mtoto wa kaka yake Saleh Saadalla aliyekuwa waziri katika Serikali ya Mavamizi Zanzibar. Ramadhan alipofungwa alikuwa na umri wa kiasi cha miaka 40 mpaka 45. Siha yake ilikuwa nzuri ingawa naye kwa mujibu wa maelezo yake, alisema kuwa aliteswa sana alipokuwa katika gereza la "Kwa Ba Mkwe". Ramadhani alisononeka kwa wakati mkubwa akiwa hapo hapo juu ya kirago chake katika gereza la Langoni. Alipofika katika sakaratilmauti, ndipo alipoondoshwa na kupelekwa huko huko kwenye hicho kihospitali cha Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu. Naye wakati wake ulipofika, aliondoka kama waliyomtangulia. Hawa ndio niliyowaona mimi tu kwa nafsi yangu wakiachwa wakiatilika na maradhi bila ya matibabu mpaka wakafa hali wanajiona. Nina hakika wapo wengine wengi waliokuwa wametendewa kama hayo wakati wakiwa ni wafungwa wa kudhulumiwa na Karume pamoja na Serikali yake.

Nashindwa kuelewa aina ya kifo cha Suleiman Amour (kwa umaarufu wake Suleiman Mpemba). Huyu ni mzaliwa wa Pemba Wingwi, na alikuwa ni mtetezi wa AfroShirazi wa kiti cha Wete Pemba akishindania kiti na Sheikh Maulid Mshangama, mtetezi wa Chama cha Hizbu. Suleiman Amour alitiwa gerezani na Karume na mpaka hii leo haikujulikana kifo chake kilikuwa ni cha namna gani. Hata katika maandishi

54 mengi yanayoandikwa na baadhi ya waandishi, na pia magazetini kukhusu waliyouwawa kwa kudhulumiwa na Karume katika magereza ya Unguja, Suleiman Amour bado halijatokeza jina lake hata mara moja. Natumai wenzangu nao watafahamu wajibu wao, wataandika na kuwataja wawajuwao wao.

WAMEULIWA VIFUNGONI

AbdulAziz Twala, Idris Abdalla Majura Wote wawili walikuwa miongoni mwa "wafungwa wa kisiasa" waliofungwa vifungo vikubwa vikubwa vya kuanzia miaka mitano hadi 10 bila ya kupelekwa mbele ya mahakama ya sheria na bila ya hata kupewa haki yoyote ya kujitetea. Wakati huo walipouliwa walikuwa wamesha vitumikia vifungo vyao kwa muda.

Mwanzoni wa mwaka 1971, Twala na Majura walitoroka kutoka gerezani, Langoni. Kwa bahati mbaya usiku wa siku hiyo hiyo waliotoroka walipatikana na walikamatwa tena na kupelekwa gerezani "Kwa Ba Mkwe". Huko waliteswa sana na baada ya kuteswa, waliuliwa wote wawili kwa kupigwa risasi. Kwa kuwa mimi (mwandishi wa kijitabu hiki) nilikuwa pamoja nao sana wakati tulipokuwa sote wafungwa wa Karume katika gereza la Langoni, Idara ya Usalama ilinichukua kutoka gereza la Langoni na nilipelekwa kwenye gereza la "Kwa Ba Mkwe" kwa kufikiria kuwa mimi ninaweza kuielewa mipango yao ya kutoroka gerezani na wapi walipokusudia kwenda. Kwa vile waliweza kuwakamata usiku huo huo, hawakuwa na haja tena na mimi. Bali hata hivyo, niliwekwa katika gereza hilo la "Kwa Ba Mkwe" kwa muda wa siku 38. (Kuwekwa katika geraza hilo kwa muda wa mwezi, hata usifanywe chochote, basi afadhali uwekwe miezi miwili katika gereza la kawaida). Nilipokuwepo katika gereza hilo la "Kwa Ba Mkwe" mmoja katika wachungaji wa gereza hilo, alinino'goneza kuwa, "Twala na Majura wameshapigwa risasi, na wote wawili wametumbukizwa katika shimo moja".

WAFUNGWA WENGINE WAULIWA Wananchi wafuatao walikuwa katika gereza la Langoni wakivitumikia vifungo vyao vya miaka kumi kumi walivyofungwa na Serikali ya Mavamizi. Jaha Ubwa Mdungi Usi Juma Maulidi (Jimmy Ringo) Khamis Masoud Aboud Nadhif Mwaka huo huo wa 1971, mwaka waliouliwa Twala na Idris Majura, kiasi cha saa moja unusu ya usiku wananchi hao wote watano walichukuliwa kutoka gerezani. Kutoka siku hiyo hadi hii leo hawajaonekana tena, na wala hawataonekana katika ulimwengu huu. Siku ya taarikh 9 Januari 1972, Karume na gengi lake la Baraza la Mavamizi walikuja gerezani Langoni kuwaachilia huru wafungwa. Katika maneno aliyoyasema mbele ya wafungwa, alisema na khasa akimkusudia ndugu yake Mdungi Usi Maalim Nngwali Usi. Maalim Nngwali wakati huo tulikuwa naye pamoja gerezani akiwa miongoni mwa wafungwa wa serikali ya mavamizi. Karume alimwambia Maalim Nngwali, "Wewe tumekufanyia kila kheri; mpaka tumekupeleka nchi za nje kusoma, lakini hukuweza kuthamini kitu ila kufuata ufisadi wa kaka yako (yaani Mdungi Usi). Haya leo kaka yako tushamuondoa duniani, utamfuata huko aliko!?" Alipokuwa akisema, "tushamuondoa duniani", Karume aliupitisha mkono wake kwenye shingo yake kuonesha kuwa ameuliwa (amekatwa roho). Ujabari ulioje huu wa Karume, kuuwa na kujisifu!!

"WAFUNGWA WA SIASA" BADO WAENDELEA KUULIWA Mnamo mwishoni mwa mwaka wa 1970, Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar kama kawaida yake iliwakamata wananchi wengi sana kwa singizio lao hilo hilo la kila siku "kutaka kuipindua Serikali ya wananchi"!! Miongoni mwa waliyokamatwa wakati huo, walikuwemo, Mabwana hawa: Salim Ahmed Busaidi Abdalla Suleiman Riyami Othman Soud Azizi Bualy Hemed Said

55

Mohammed Juma Mohammed Hamza Musa Ali Said Hamoud

Wananchi hao baada ya kukamatwa na kuwekwa kizuwizini, walipelekwa mbele ya mkutano wa hadhara uliyoandaliwa makusudi kwa ajili yao katika uwanja wa Maisara, Unguja, kati ya mwaka wa 1971. Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, kwa kutaka kudanganya Ulimwengu na wananchi wa Zanzibar, walileta katika mkutano huo bunduki na silaha nyengine ndogo ndogo kuwa ati wamekamatwa nazo wananchi hao. Pia pamoja na hizo silaha, ililetwa bendera na kusemwa kwamba bendera hio ndiyo walitaka wakamatwa hao iwe bendera ya Nchi baada ya kufuzu hayo mapinduzi yao! Hayo hayakutosha, bali Serikali ya Mavamizi, iliwatumilia baadhi ya maofisa wake wa kijeshi wengi wao wakiwamo hao wenye kujiita, "progressives" kuja kusema uwongo wa kuwahilikisha wananchi wenziwao kwa ajili ya kutafuta maslahi ya nafsi zao. Maofisa hao waongo, walisema mbele ya umma kuwa ati hao wananchi waliokamatwa walikuwa wakipanga pamoja nao mipango ya kuipindua Serikali ya wananchi. Bali wao, yaani hao maofisa waongo, walikuwa wakiripoti kwa wakubwa wao kila khatua zilizokuwa zikifanyika. Mpaka ulipofika wakati, ndipo ilipoarifiwa Idara ya Usalama na kutakiwa wafanye kazi yake. Idara ya Usalama iliwakamata wote pamoja na silaha zao ambazo ndizo hizo hapo!! Kila aliyekuwepo katika mkutano huo na kila aliyesikia hadithi hizo, ila aliyekuwa hana akili timamu au amezidiwa na chuki, aliweza kutambua kuwa yote hayo yalikuwa ni mazingaombwe ya uwongo uliyokuwa umepangwa na baadhi ya wakuu maalumu wa Serikali ya Mavamizi kwa makusudio yao maalumu.

Baada ya kusemwa uwongo huo, Karume aliwasimamisha baadhi ya hao wadhulumiwa mbele ya umma uliokuwepo hapo na aliwanazii kwa matusi, na aliwakejeli kwa kiasi alichopenda mwenyewe. Baada ya hapo, alitoa hukumu ya kuwaweka gerezani. Kazi zao alizokuwa amezitangaza mbele ya mkutano huo, zilikuwa za "Kuchunga n'gombe" huko Hanyegwa Mchana. Baada ya kuuliwa Karume, April 7, 1972 na kutawalishwa AlHaj Aboud Jumbe, wananchi hao wadhulumiwa, wote walichukuliwa kutoka magerezani na kwenda kuuliwa kwa kupigwa marisasi siku moja. Baada ya kuuliwa, wote walitumbukizwa katika shimo moja. Yale yaliyofanyika hivi karibuni huko Ruwanda si ajabu kuwa wameyaiga kwa yaliofanyika Zanzibar. Kuiga maovu ni rahisi!

Baadhi ya hao maofisa waliokubali kusema uwongo kuwazulia ndugu zao wakati huo, hivi sasa baada ya kuwa na wao yeshawafika ya kuwafika kwa matokeo ya kuuliwa Mzee Karume, ati ndio wanasema kwa sauti za majuto na za kusikitika kuwa, "Yale yote tulioyasema siku ile mbele ya mkutano ule yalikuwa ni maneno ya kupangiwa na wakubwa wetu tuyaseme, kwa hakika yote yalikuwa ni maneno ya uwongo"!! Hao ndio "progressives" wetu, wapenda maendeleo. Wametumiliwa kuivamia Serikali ya halali iliyochaguliwa na wananchi kwa uchaguzi wa kidemokrasi wa "One Man One Vote". "Progressives" hao hao ndio waliotumiliwa kwa maslahi ya nafsi zao kwa kusema uwongo uliopelekea kuuliwa kwa wananchi wenziwao bila ya kuwa na makosa yoyote. "Progressives" hao hao ndio waliotumiliwa tena, mara hii katika mipango ya kumuuwa Karume!! Si ajabu kuwa hivi sasa "progressives" hao hao wamo mbioni wakitumiliwa, wakijuwa au bila ya kujuwa, katika mipango na njama za kuleta vurugu kupitia huu "Mfumo wa Vyama Vingi" tulioletewa, bali na katika mengineyo. Watu kama hawa khatari kuwanao. Daima yafaa kuepukwa.

ALIYONIZUNGUMZIYA TWALA Mimi na Bwana AbdulAziz Twala kabla ya kuwa watumwa wa Karume na Serikali yake ya Mavamizi katika magereza yake hatukupata kuwa na maingiliano ya namna yoyote. Lakini baada ya kuishi pamoja huko utumwani, tulikuwa masahibu wakubwa kama watu tuliokuwa na maingiliano tangu zamani. Maslahi ya nchi yetu ndio yaliotukusanya pamoja. Tulikuwa kila siku baada ya kumaliza kutumwa na kumaliza kutafuna mapande yetu ya muhogo mchungu na majani mapevu ya muhogo (ati kisamvu), tulikuwa tukitafuta upenu na kukaa kwa mazungumzo. Mazungumzo yetu makubwa yalikuwa juu ya kufikiri mustakbali wa nchi yetu Zanzibar kwa kutokana na namna ya Karume alivyokuwa akiendesha nchi. Twala alikuwa na imani kubwa juu yangu hata alifika kunihadharisha na baadhi ya wenzake kama Jaha Ubwa, Mdungi Usi na Said Tumba (Said Njugu). Na wao kwa upande wao walimhadharisha yeye Twala kukhusu mimi. Walimwambia, "Tunakuona unaambatana na Aman, lakini usisahau kuwa ni

56

Mhizbu". Twala alikasirishwa na maneno hayo, na aliwafahamisha juu ya fikra zao potofu hizo. Naye alinieleza yote walioyokuwa wakimwambia.

Katika mazungumzo yetu ya kila siku, Twala alikuwa akinizungumzia mambo mengi kukhusu Serikali yao ya Mavamizi namna ilivyokuwa ikiendeshwa na Karume. Kwa hakika sitoweza kuyaeleza yote aliyo nizungumzia, lakini nitajaribu kuyaeleza japo kwa ufupi; khasa yale niyaonayo kuwa ni muhimu kwa wananchi. Khasa waliokuwa wadogo au bado hata kuzaliwa katika wakati huo, wapate kuona na kufahamu namna ya hiyo Serikali inayojitapa kuwa imeondoa dhulma, ubwanyenye na Usultani na imeleta usawa kwa wananchi. Nitaanza kwa kisa cha Othman Shariff kama alivyo nizungumzia Twala. Siongezi langu hata dogo.

YALOMFIKA OTHMAN SHARIFF Twala ameniambia kuwa tokea kuasisiwa Umoja wa Vijana wa YASU na Othman Shariff kuwa ndiye Rais wa Umoja huo, Karume alikuwa hamtizami Othman kwa jicho la rehema. Kwa vile Karume alivyojiona hakubahatika kuwa katika wasomi, na kuwa Othman alikuwa ni msomi, akifikiria kuwa siku moja Othman ataweza kuchukua uwongozi juu ya Waafrika. Na hilo, Karume alikuwa sitayari kulikubali. Twala alisema kuwa kwa kuyakinga hayo, khatua za mwanzo alizochukuwa Karume baada ya kufaulu kwa Mavamizi ya Zanzibar ni kupiga marufuku vyama vyote tokea vya kisiasa mpaka vya kijamii (Social) na vya kikabila, na YASU ikiwa moja wapo. Khatua ya pili alimuondoa Othman na kumpeleka katika nchi za nje kuwa Balozi wa Tanzania.

Twala ameniambia, katika mwaka 1966, Othman Shariff alikuja Tanzania kwa kazi za Serikali na baada ya kumaliza kazi zake DaresSalaam, alitembelea Zanzibar. Hakutimiza muda mkubwa ila ghafla tulimuona Othman ameletwa katika kikao cha mkutano wa Baraza la 'Mapinduzi'. Twala anasema kuwa Karume aliwaambia, "Nimemleta huyu fisadi mbele yenu, juu ya kumfanya Balozi wa Serikali yetu huko Marekani, bado hajatoshelezeka anataka lazima awe yeye ndiye Rais wa nchi hii. Vitimbi vyake vyote anavyovifanya vya kutaka kutuletea fujo na michafuko katika nchi yetu ili apate kuwarejesha mabwana zake, tumevipata kwa ukamilifu kabla yeye mwenyewe kufika Tanzania. Alipofika hapa vijana wa kazi walikuwa wakimuandama katika kila njia zake bila ya yeye mwenyewe kufahamu. Katika nyendo zake, vijana wa kazi wamemuona ana jishughulisha na kuvitembelea baadhi ya vituo vyetu vya kijeshi, na alikuwa akijaribu kuwatomasa tomasa baadhi ya wanajeshi wetu ili waweze kuwa upande wake hapo atapokuwa tayari kuufanya huo ufisadi wake. Vijana wa kazi walipomuona amefika kiasi hicho, walimtia mbaroni na kumleta kwangu, na mimi sasa namleta mbele yenu kwa kutaka uwamuzi wenu nini tumfanye".

Twala ameniambia kuwa wengi kati yetu tulipigwa na msangao kwani tulikuwa na hakika kuwa aliyokuwa akiyasema Karume yalikuwa maneno ya uwongo, lakini nani ataweza kuuliza au kumkaidi au kumhoji. Mwisho mwenyewe alitoa uwamuzi wake wa kumfunga gerezani Othman Shariff kifungo cha miaka kumi! Twala ameniambia kuwa, hapo hapo Karume aliwapa amri Ibrahim Makungu na Edington Kisasi wamchukue Othman Shariff kumpeleka gerezani kwa kuwa ndiyo keshahukumiwa. Twala alipokuwa akinizungumzia hayo, nilidawaa. Nilimuuliza Twala, "Kwani katika hilo Baraza lenu mlikuwa hamna haki ya kusema au kuuliza? Basi palikuwa na faida gani ya kuitana na kukutana?" Kwangu miye kuyasikiya haya hayakuwa ya ajabu kwani serikali hii kuwazuliya watu uwongo wananchi ndio misingi ya siasa yake. Huwazulia uwongo wakawafunga, wakapokonya vyoa bali hata wakawachukulia ahli zao. Huko magerezani wakawatia vilema kwa mateso na wengine wakawauwa.

Mwalimu Nyerere alipopata khabari za kufungwa Othman Shariff, Twala amesema, hakuweza kustahamili. Alijiingiza kati na alimlazimisha Karume amuachilie huru Othman. Mwalimu baada ya kumtoa Othman kifungoni, hakupendelea kumrejesha katika kazi yake ya Ubalozi, bali alimrejesha katika kazi yake ya Udaktari wa vinyama, akampeleka Iringa. Twala akasema, Karume hakupendezewa na uamuzi wa Mwalimu wa kumwachilia huru Othman. Kwa hivyo, baada ya muda, Karume alizamia mbizi na alipoibuka, aliibuka na jungu jengine jipya! Mara hii, aliwatumilia wapenzi wake wakubwa Othman Jaha Ubwa, Mdungi Usi na Said Njugu kwa kuwafanya wao ndio mashahidi juu ya mipango ya Othman ya kutaka kuipindua Serikali ya Zanzibar. Twala ameniambia, siku moja, uliitwa mkutano wa dharura wa Baraza la Mavamizi na katika mkutano huo, waliwaona wamehudhuria Jaha Ubwa, Mdungi

57

Usi na Said Njugu, ambao wote hao hawakuwa miongoni mwa Wanachama wa Baraza la Mavamizi". Karume alisema kuliambia Baraza lake, "Nimewaleta hapa hawa ndugu zenu mbele yenu baada ya kuja kwangu na kunielezea hayo waliyonielezea ambayo nitawataka wao wenyewe wakuelezeni". Alimtaka Jaha Ubwa aanze kuelezea. Jaha alisema, "Othman alipokuwepo Marekani alikuwa akituletea barua, katika baruwa zake hizo amewahi kutuandikia kukhusu mipango aliyokuwa nayo huko ya kutafuta askari wa kukodiwa kuja kuipindua Serikali ya Zanzibar. Othman alitutaka tujaribu kuzungumza na baadhi ya vijana waliyomo jeshini na tuwaweke tayari wakati utapofika waweze kuchanganyika na hao askari wa kukodiwa katika kulitekeleza jambo hilo". Jaha akaendelea kusema, "Othman Shariff alipokuja Zanzibar alitulaumu kwa kuwa hatukumjibu barua yake aliyokuwa ametuletea. Sisi tulimjibu kuwa hatukukujibu kwa sababu hatuwafiki hiyo mipango yako. Twala ameniambia kuwa Jaha amesema kuwa baada ya kumwambia Othman maneno hayo, aliwaaga na aliwaambia kuwa, "Basi msiyadhukuru tena baada ya sasa. Yasahauni." Twala ameniambia kuwa Mdungi Usi na Said Njugu wao walikuwa wakiyatilia nguvu tu hayo maneno aliyokuwa Jaha akiyasema. Mwisho Said Njugu alisema, "Tulipoona kuwa Othman hakuonesha kukubaliana na rai zetu, na kwa kukhofia tukinyamaza hwenda akaja sababisha machafuko katika nchi yetu, ndipo tulipoamua kwenda kwa Mzee na kumuhadithia yote kama hivi yalivyoelezwa hapa".

Baada ya Jaha na Said Njugu kumaliza kusema, Karume aliliambia Baraza, "Shauri yangu mimi, ningependa kuwapeleka ndugu zetu hawa kwa Mwalimu Nyerere wakamueleze kama walivyotuelezea sisi, kwani Mwalimu ameona kuwa mimi simpendi Othman. Yeye Mwalimu havijui vitimbi vya Othman kama vile ninavyo vijuwa mimi na nyinyi. Basi sijui nyinyi munaona vipi?" Twala amesema kuwa wote walikubali shauri hiyo kwani kila mwenye akili yake alifahamu kuwa hayo yote yalikuwa yamesha pangwa na hao kina Jaha Ubwa, Mdungi Usi na Said Njugu walikuwa nao wameshapangwa, na kuwa yote hayo waliyoyasema yalikuwa ni maneno ya uwongo mtupu. Lakini, kwa kuwa hapana awezaye kukaidi wala kuuliza, wote walikubali. Ikifikiriwa kuwa Mwalimu atatumia busara ayachunguwe maneno haya na Othman apate rehema. Siku ya pili yake, wote watatu walitengenezewa safari ya kwenda DaresSalaam. Haukupita muda mkubwa tokea kwenda na kurejea kwa ujumbe huo wa Karume ila Othman Shariff aliletwa Zanzibar na safari yake ilimalizikia "Kwa Ba Mkwe".

KUTESWA NA KUULIWA OTHMAN SHARIFF Kwa khabari nilizozipata kutokana na ndugu yangu Idrisa Majura tulipokuwa gerezani pamoja, aliniambia kuwa Mandera na gengi lake la watesaji, wauwaji, walimtesa sana Othman Shariff hata walimletea vijana wadogo anaowazaa wima kumnajisi, kumuingilia kwa nyuma, kwa nguvu na mwisho wakammaliza kumtoa roho kwa kumpiga, na maiti yake ikatoswa baharini. Akanyimwa haki ya kuzikwa kama binaadamu, bali hata ya kufukiwa.

Idrisa Majura ni kijana wa Kihaya amezaliwa Bukoba, Tanganyika bali amelelewa Zanzibar na Sheikh Said Komba Nyongo na amesoma katika skuli za Serikali za msingi Zanzibar. Kijana huyo baada ya Mavamizi aliondoka Zanzibar na kurejea kwao Bukoba. Alipokamatwa Othman Shariff na kurejeshwa Zanzibar, na yeye alikamatwa huko huko kwao Bukoba na aliletwa Zanzibar, walikuwa pamoja huko kwa "Ba Mkwe". Katika karasa za mbele, nitaeleza aliyotendewa yeye Idrisa wakati akiwa mfungwa wa Karume katika gereza la Langoni.

KUFUNGWA NA KUULIWA SALEH SAADALLA Chuki za Karume kwa watu waliyosoma, zilikuwa hazina mfano hata alifika katika mkutano wake mmoja wa hadhara uliyokuwepo Raha Leo, Miafuni, alisema kuwaambia wafuasi wake, "Tuwakimbiye waliyosoma kiasi cha yadi 100!!" Wengi kati ya Mawaziri wake waliyosoma walikuwa hawamo katika moyo wake. Lakini, kwa kuwa alitoka nao mbali, basi alikuwa akijilazimisha kuishi nao, mpka awapatie kisingizio, tena ndio arijojo.

Saleh Saadalla, yeye alizidi kuchukiwa na Mzee Karume kwa mawili. Kwanza kwa kuwa alikuwa msomi na la pili ni kuwa Saleh Saadalla alimuoa bibi mmoja ambaye kabla ya kuolewa na yeye, bibi huyo alikuwa wa "kimada" kwa Mzee Karume. Kwa hakika Karume alikuwa amerowa kwa bibi huyo kuliko huyo bibi alivyokuwa kwa Karume. Twala amenizungumzia kuwa siku moja katika mwaka wa 1966, Saleh Saadalla alikawia kufika katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Mavamizi. Wakati alipofika

58 mkutano ulikuwa umeshaanza. Alipotaka kukaa, Twala amesema, Mzee Karume alimwambia Saleh, "Kwanza usikae mpaka utwambie kwanini ukachelewa kuja katika mkutano mpaka wakati huu?" Saleh alimjibu kuwa, "Nimetokewa na udhuru wa kumpeleka mke wangu hospitali". Karume, alimwambia, "Kwani huna dereva wa kumpeleka? Lazima umpeleke weye?" Saleh, alimjibu, "Kutokana na hali yake ilivyo, nimeona lazima na mimi niwepo kwa Daktari, ili nipate kuzungumza naye zaidi". Karume alimwambia Saleh, "Kwani amepata maradhi gani, au maradhi ya Kaswende?" 'syphilis'. Saleh Saadalla, alimwambia Karume, "Sasa Mzee tunatukanana? Ikiwa na mimi nitakwambia wewe lugha kama hiyo, utapendezewa? Huyo ni mke wangu". Karume kwa kuambiwa maneno kama hayo, hakuweza kuchukua, alipandwa na hamaki na alichukua fimbo yake na kutaka kumpiga Saleh Saadalla. Saleh alipoona yamejiri ya kutaka kupigwa, alichomoa akiba yake kibindoni,bastola lakini kwa bahati mbaya au nzuri, haikuwa na zana zake kwa hivyo, ilitishia tu, haikuweza kufanya kazi yake.

Twala ameniambia kuwa, wakati Saleh alipochomoa bastola, kila mmoja alikuwa si hadhir. Karume, fimbo ilimdondoka. Wapendao kujipendekeza kwa bwana, walipomwona Saleh ameirejesha bastola yake kibindoni na amekaa kitako, Twala ameniambia, mambo yalikuwa hapo. Kwani walimvamia Saleh Saadalla na kwanza walikimbilia kumnya'ganya bastola. Karume alipopumua kidogo aliliambia Baraza lake, "Sitawambieni mimi kuwa humu humu katika hili Baraza letu tunao vitumishi vya wakoloni? Mumemuona nini alichotaka kukipitisha sasa hivi mbele yenu? Watu kama hawa wanafaa sisi kuwa nao pamoja?" Twala aliniambia wakati huo palizuka fujo kwani kila mmoja kwa kujipendekeza kwa Mzee, alikuwa akitoa hukumu yake kali zaidi kuliko ya mwengine. Huyu anataka Saleh apewe adabu ya kuuliwa, na huyu anataka apewe adabu ya kuteswa mpaka afe kwa mateso. Mradi, Twala amesema kuwa tulikuwa hatutambuani. Mwisho, mwenyewe Mzee alitoa hukumu yake ya kumfunga Saleh Saadalla gerezani kifungo cha miaka 10, na kutaifishwa kila kitu chake.

Alipoletwa Saleh Saadalla gerezani kwa kifungo cha miaka 10, namiye, muandishi wa hiki kijitabu, nilikuwemo gerezani nikitumikia kifungo changu cha miaka 10 nilichofungwa na Karume, na yeye Saleh Saadalla akiwa ameshiriki katika dhulma hizo. Waswahili wanasema, "Nyani akimaliza miti ya kuirukia, hurukia mabega ya bwana wake". Basi na Serikali ya Mavamizi ilipomaliza Mahizbu na maZPPP, walikulana wenyewe.

Saleh Saadalla aliletwa gerezani na Ibrahim Makungu, Edington Kisasi na Khamis Darwesh. Baada ya kunyolewa upara, alipelekwa kufanyakazi sehemu ya ushoni wa nguo za gerezani. Ulipofika wakati wa chakula, alikabidhiwa sahani yake ya mapande ya muhogo mchungu wa kutokoswa kwa maji na majani mapevu ya muhogo, kisamvu. Mheshimiwa kwa siku hiyo ya mwanzo, alishindwa kukila chakula hicho. Nakumbuka mmoja katika wafungwa wa ukhalifu wa sheria za nchi ambaye alikuwa mpishi, jina lake la umaarufu kwa gerezani, akiitwa, "HAMBA GAI" wakati alipokuwa anakusanya sahani za chakula baada ya kumaliza kula, alimwamabia Saleh Saadalla, "Mbona Mheshimiwa wewe hujala hata kidogo chakula chako?" Saleh, alimjibu, "Sina njaa! Nimekula sana asubuhi". Mfungwa huyo, Hamba Gai alimwambia Saleh Saadalla, "Sikiliza Mheshimiwa, chakula hichi unacho kiona hapa, ndicho hichi utachokila, ikiwa si leo, utakila kesho, ikiwa si kesho utakila mtondogoo, lakini mwisho wake lazima utakila maadamu umefungwa. Chakula hichi ndicho wewe pamoja na wenzio mlichokipasisha kuwa cha wafaa wafungwa kukila. Wakati huo, hukufikiria kuwa inawezekana hata wewe siku moja ukawa mfungwa; kama hivi ulivyo leo. Basi ikiwa chakula hiki ni kizuri, mbona wewe kimekushinda?"

Saleh Saadalla alikuwa taabani kwa kuambiwa maneno kama hayo na mtu ambaye wakati alipokuwa na uheshimiwa wake alikuwa hawezi hata kumkurubia licha ya kuzungumza naye. Katika nyoyo zetu mlichanganyika baina ya kuhisi kuwa anastahiki kuambiwa maneno kama hayo na baina ya kumuonea huruma, kwani machozi yalikuwa yakimlengalenga, kwa uchungu na kujiona jinsi alivyodhulumiwa, tena kudhululmiwa kwenyewe alikofanyiwa na mwenziwe waliotoka mbali pamoja. Kwa hakika wakati huo alikuwa anahitajia rehema kuliko kustahiki masusuiko, kwani alikuwa hana hila wala uwezo. Baada ya Saleh kutumikia kifungo chake kwa muda, siku moja tulipoamka na kuanza kugaiwa kazi, mwenzetu hatukumuona na ndio ikawa hatukumuona tena hadi hii leo. Kutokana na khabari zenye kuaminika tulizozipata kutoka kwa baadhi ya wachungaji wetu wa magereza zilisema kuwa Saleh Saadalla alichukuliwa na waheshimiwa wenzake mnamo pingapinga za usiku, alipelekwa Chukwani na

59 huko ndiko alikouliwa kwa kupigwa risasi na kutoswa baharini kama alivyotoswa Othman Shariff.

KARUME KUANZA KUMBADILIKIA TWALA Katika kuendelea na mazungumzo yetu baina yangu na AbdulAziz Twala, Twala aliniambia kuwa mwanzoni yeye alikuwa katika hao watoto wazuri mbele ya Mzee Karume, na ilikuwa kila alichokuwa akikitaka kwa Karume akikipata bila ya taabu yoyote. Mambo yalianza kuharibika wakati ujumbe wa Serikali ya Mavamizi ulipoalikwa Misri. Twala amesema kuwa alipokuwa akitengeneza kutoa matumizi ya safari (travelling allowances) kwa wajumbe wa safari hiyo, aliwacha kumtia katika orodha ya matumizi ya safari Bibi Fatma Karume kwa sababu Bibi Fatma alikuwa anachukuliwa na mumewe kwa matembezi tu, sio katika ujumbe rasmi. Mzee Karume, alipoona mkewe hakutengenezewa sehemu yake ya matumizi, alimuuliza Waziri wake wa Nchi kukhusu posho la mama Fatma Karume. Twala alipigiwa simu na Waziri wa Nchi, AlHaj Aboud Jumbe na alimwambia, "Mbona umesahau kuleta posho la mama Fatma Karume?" Twala alimjibu, "Laa, sikusahau lakini nimeona kuwa yeye si katika wajumbe rasmi wa safari. Lakini, ikiwa unaona na yeye anastahiki, basi nitamtengenezea". Twala amesema haukupita muda baada ya mazungumzo hayo ila alipata simu nyengine kutoka kwa Katibu wa Waziri wa Nchi kumwambia kuwa, "Unaambiwa na Mzee basi usilete posho la mama Fatma. Yeye mwenyewe atampa kutoka mfukoni mwake". Twala amesema kutokana na jawabu hilo la Mzee, alihisi kuwa amesha mtonesha Mzee kidonda; na kweli ndivyo ilivyokuwa. Kutoka wakati huo mambo yalianza kuharibika, alisema Twala. Ujumbe uliporejea Misri, Twala amesema kuwa kila alipokuwa akikutana na Mzee Karume alikuwa hampi mkabala mwema.

Jambo jengine ameniambia Twala lililozidi kutimua mavumbi lilitokea wakati mmoja alipokuwa Mwalimu Nyerere amehudhuria kikao cha Baraza la Mavamizi. Katika kikao hicho, amesema Twala, Mwalimu alilaumu kukhusu namna zilivyotumiwa fedha za kigeni kwa kununulia vitu kwa wingi kama peremendi, tofi, chakileti, ubani wa kutafuna na vyenginevyo ambavyo havikuwa na umuhimu katika maisha ya binaadamu wakati yapo mambo mengi muhimu yanayohitajia fedha za kigeni. Twala amesema kuwa Karume alivyomuona Mwalimu akilaumu kiasi hicho, alinigeukia na aliniambia, "Mheshimiwa Waziri wa Fedha, unasikia maneno hayo? Usijitumilie mapesa ovyo ovyo tu". Twala amesema, siku hiyo alishindwa kunyamaza kimya, alisema kujibu hayo, "Kweli mimi ndiye niliyempa amri Waziri wa Biashara na Viwanda, Sheikh Shaaban Soud Mponda aagizie vitu hivyo, lakini nimefanya hivyo, baada ya kupata amri kutoka katika ofisi yako ya kunitaka mimi nitowe idadi fulani ya fedha kwa kuagizia vitu hivyo kutoka Ujarumani ya Mashariki. Sasa mimi Mzee, kosa langu ni lipi hapo?" Twala ameniambia kuwa, alivyokuwa amesema hivyo, alimuona Karume amesawijika uso, na alikuwa akipuma kama n'gombe jike. Mwalimu alipoona hali haikuwa nzuri, alijaribu kuyageuza mazungumzo na kuleta maudhui nyengine. Mkutano ulipomalizika, Mwalimu aliondoka kurejea DaresSalaam. Siku ya pili yake, amesema Twala, kiasi cha kuingia katika ofisi yake, alipata simu kutoka kwa Waziri wa Nchi ya kumwambia kuwa kutakuwepo na mkutano wa dharura katika Peoples' Palace na wote wahudhurie.

Twala amesema kwa kupata khabari kama hizo tu basi nusra alikuwa atokwe na mkojo suruwalini! Alipofika kwenye mkutano, Twala amesema aliwaona baadhi ya wenzake hawakuwa na mtizamo mzuri juu yake. Kila mmoja alikuwa akimuepuka epuka. Alipoingia Mzee Karume na kwa namna alivyomuona, alisema Twala, aliona kuwa leo patakuwa na kazi hapa. Karume aliufungua mkutano kwa kusema, "Nimekwiteni kwa ghafla ili tupate kuyazungumza pamoja na kuyazingatia mazungumzo ya jana aliyoyazungumza Mwalimu Nyerere hapa, na namna mlivyomsikia Mheshimiwa Twala alivyoweza kunivua nguo na kuniacha uchi mbele ya mzee mwenzangu. Ninakuapieni kuwa jana sikuweza kupata usingizi, usiku kucha nimekaa macho nikifikiri vipi Mwalimu ataniona. Kwani mimi nilikuwa sijui kuwa amri ya kuagizia vitu hivyo nimeitoa mimi? Najuwa, lakini, ilivyokuwa maneno aliyosema Mwalimu yalikuwa na uzito, niliona bora kosa hili nimtupie mwanangu ili mimi mzee nipate kusitirika, lakini sikujuwa kuwa mwanangu ndiye ataye nifedhehesha zaidi".

Twala ameniambia kuwa hapo Karume alianza kuwatolea hadithi za watoto wa kizamani walivyokuwa na adabu mbele ya wazee wao. Karume alisema kuwa, "Wakati mwengine hutokea mzee katika baraza akatokwa na pumzi, kujamba mbele ya wazee wenziwe na ilikuwa likitokea jambo kama hilo, akitupiwa mtoto yoyote aliye kuwepo hapo, na mtoto akiwa hata yeye siye aliyefanya hivyo alikuwa hakatai, wala alikuwa hasemi chochote. Akinyamaza kimya! Baraza inapo malizika na wazee wakatawanyika, yule

60 mtoto alikuwa akipewa pesa moja au mbili akanunue kashata au chochote akipendacho kwa kuwa amewasitiri wazee wake. Na hivyo, ndivyo nilivyo tumainia kuwa mwanangu ataweza kunisitiri, lakini kanifedhehisha zaidi. Bora ningelinyamaza kimya kuliko vile nilivyokuwa nimesema". Alipokuwa akiendelea kusema hayo, Twala ameniambia, aliwaona wenzake wakitikisa tikisa vichwa kwa kuonesha wana masikitiko makubwa juu ya hayo yaliyofanyika. Baada ya Karume kumaliza kusema aliyotaka kuyasema, aliliuliza Baraza lake, "Sasa kijana kama huyu afanywe kitu gani?" Twala ameniambia kuwa, hakukutokea hata mwenzake mmoja aliyesema maneno ya kuonesha kumtakia rehema. Kila aliyekuwa anasema, akizidi kumshindilia ili Karume azidi kumuona ni mtu mbaya. Baada ya muda, Twala amesema, Mzee Karume alisema, "Leo, nakusamehe Twala. Adabu ninayokupa ni ya kukuondoa kwenye Wizara ya Fedha, kuanzia leo, kesho nakutaka ukakamate Wizara ya Afya. Kuanzia leo Wizara hii ya Fedha itakuwa chini yangu".

Twala amesema kwa kusikia hukumu hiyo, ndiyo hapo aliweza kushusha pumzi. Kwani kila alipokuwa Mzee akisema alikuwa akiyaona mauti mbele ya macho yake. Aliendelea kusema kuwa akiona wazi kuwa yale yaliowafika Othaman Shariff na Saleh Saadalla ndio hayo hayo yatakayo mfika yeye. Alisem, akijuwa kuwa ikiwa atapata rehema basi ni kumalizikia gerezani, ambako alikuwa na hakika kuwa huko hakuna mwisho mwema. Alisema, niliondoka hapo siku hiyo sina raha wala furaha.

MWISHO WA TWALA Kuondolewa AbdulAziz Twala katika Wizara ya Fedha, na kupelekwa kwenye Wizara ya Afya, ndio kulikuwa kumalizika kwake. Twala alisema kuwa alipopelekwa Wizara ya Afya, Waziri wake mdogo alikuwa Rashid Abdalla (Mamba). Twala ameniambia kuwa walikuwa na dasturi ya kukutana kila asubuhi kwa ajili ya kuzungumza juu ya kazi zao. Siku moja, amesema Twala, alimuona Rashid Abdalla amekawia kufika ofisi. Mpaka kiasi cha saa nne ndipo alipoingia na alipoingia alikwenda moja kwa moja mpaka ofisi ya Twala. Alipofika, alimwambia Twala, "Mheshimiwa, tokea sasa hivi, mimi ndiye Waziri wa Afya na wewe funga virago vyako wende nyumbani kwako. Kila kilicho chako chukuwa mwenyewe na kila cha Serikali kiwache. Hata motokari usichukuwe tena. Haya ndiyo niliyoambiwa kutoka State House, unalo suala lolote waulize wenyewe".

Twala, ameniambia kuwa hakustaajabu kwa kuambiwa maneno hayo kwani akiuelewa uzuri mwendo wa Serikali yake, lakini juu ya hivyo alitaka kuzidi kuhakikisha juu ya maneno hayo. Kwahivyo alipiga simu State House (Ikulu) na alipouliza jawabu ilikuwa, "Kama alivyokueleza Mheshimiwa Rashid Abdalla ndivyo hivyo hivyo. Pack and go"! Twala amesema kuwa, alifunga funga, na alimuachia ufunguo wa gari Waziri mpya wa Afya, na alishika njia kwenda zake nyumbani akiutwanga wa fisi. Salama wakati huo, alikuwa akikaa Mnazi Mmoja ambapo palikuwa karibu sana na hiyo iliyokuwa ofisi yake. Baada ya siku mbili tatu tokea kutolewa katika uwaziri, alijiwa nyumbani kwake na Mkuu wa Usalama Ibrahim Makungu na alimwambia, "Nimekuja kukutaka unikabidhi bastola pamoja na risasi ulizokuwa umepewa, na pia unikabidhi paspoti yako ya kidiplomasi". Twala amesema, aliingia ndani na akamkabidhi vyote hivyo. Haukupita muda baada ya hapo ila alimuona Mkuu wa Gereza la Mateso ("Kwa Ba Mkwe") Mheshimiwa Mandera amemfikilia nyumbani kwake kiasi cha saa 10 za jioni. Mandera alimwambia Twala, "Wazee wenzako wamenituma nije kukuchukuwa ili mwende mkazungumze kuhusu maombi yako ya paspoti ". Twala baada ya kunyan'ganywa paspoti ya kidiplomasi, alikwenda kuomba paspoti ya kawaida katika Idara ya Uhamiaji.

Twala ameniambia kuwa kwa kuja Mandera na kumwambia maneno hayo alihisi kuwa hakuna salama. Aliingia ndani na alimzungumzia mkewe khabari hizo. Wakati huo mama yake mzazi Twala alikuwepo nyumbani, kwani mkewe Twala alikuwa mja mzito na akitarajia kujifungua wakati wowote. Twala baada ya kumzungumzia mkewe, alitoka na kumfuata Mandera. Aliingia katika gari ya Mandera na baada ya muda mdogo, Twala amesema, alijiona amefika kwenye gereza la "Kwa Ba Mkwe". Safari yake ya kukutana na wazee wenzake ilimalizikia hapo. Twala aliniambia kuwa yeye alibahatika hakuteswa kwa namna yoyote zaidi ya kuwekwa humo bila ya kuwa na makosa yoyote. Baada ya kukaa katika gereza hilo kwa muda, Twala alifungwa kifungo cha miaka 10 gerezani kutoka taarikhi 3 Mei, 1969. Kutokana na huko kufungwa kwake, ndio tukawa pamoja na kunihadithia haya niyaelezayo katika kijitabu hiki.

61

Ilikuwa ni kawaida, kila baada ya muda wakiletwa wafungwa waliyokuwa wakiitwa, "wafungwa wa kisiasa" kutoka gereza la "Kwa Ba Mkwe". Wakati mmoja katika jumla ya wafungwa waliyoletwa, alikuwa Idrisa Majura. Idrisa na Twala wakifahamiana sana na kwa hakika walikuwa marafiki tokea walipokuwa wakijifunza uwalimu katika Chuo cha Uwalimu huko BeitelRas, Unguja. Idrisa alijiunga pamoja na sisi na tulikuwa tukikaa pamoja baada ya kumaliza kazi zetu na tulikuwa hata tukila pamoja yaani mimi, Twala na yeye Idrisa. Baada ya muda, Twala alileta shauri katika baraza yetu ya kutaka tufanye mipango ya kutoroka kutoka gerezani. Tuliizungumza kwa urefu sana mipango hiyo, na juu ya yenye kuwezakana kutendeka na yasiyowezekana kutendeka kutokana na hali ilivyokuwa wakati huo. Mimi kwa upande wangu, si kama nilikuwa na woga wa kufanya hayo, bali nilikuwa nikipinga baadhi ya mambo ambayo nikiyaona hayaingii katika mizani ya kuweza kufuzu katika mipango hiyo. Kutokana na hivyo, Twala aliniambia, "Nakuona woga wa kiHizbu umeshakuingia. Lakini nakwambia kuwa sisi hatutokubali kubakia hapa tuwe tunauliwa kidogo kidogo. Tutatoka na lolote na liwe". Tokea siku hiyo, niliwaona kidogo wakiniepuka epuka katika baadhi ya nyakati.

Siku moja asubuhi, niliwaona wote wawili wamesimama katika msitari wa wanaotaka kuonana na Bwana Mganga. Kwa hakika haikunipitikia kitu. Niliona ni mambo ya kawaida, kwani wafungwa hufanya mipango kama hiyo angalau wapate mapumziko japo madogo. Miye na wafungwa wenzangu wengine tulipelekwa makondeni kulima kwa siku ile. Tulipokuwa makondeni tukilima kiasi cha saa sita za mchana, tulisikia kipyenga cha kutukusanya pamoja. Mara niliwaona askari waliokuwa wakituchunga wakino'gonezana. Baada ya sote kuhisabiwa na kuonekana tumetimia katika hisabu yao, tuliongozwa na kurejeshwa kambini Langoni. Wakati huo tulikuwa tukifanyakazi sehemu za Kinu Moshi. Tulipofika Langoni, tuliwakuta askari wa polisi na majibwa wao, pia walikuwepo askari wa kijeshi, na Mandera naye pia alikuwepo. Roho zilitusituka na kutupiga paa! Baada ya kuhisabiwa na mchungaji mwenye dhamana ya kotagadi, tulitiwa ndani moja kwa moja, na hapo hapo tulipewa chakula, baada ya kula tulitiwa ndani ya mabanda yetu bila ya hata kwenda chooni. Kila mchungaji alikuwa ameghadhibika kuliko mwenziwe. Wapishi na baadhi ya wachungaji walituno'goneza kuwa Twala na Majura wametoroka.

Loo! Niliingiwa na jamba jamba kwa mambo mawili. Kwanza, kwa vile ilivyokuwa kila wakati tukikaa pamoja, tukizungumza pamoja, na hata tukila pamoja; basi nalihisi huenda wakubwa wakafikiri kuwa labda mimi naujuwa huo mpango wao wa kutoroka gerezani. Na ndivyo ilivyofikiriwa. Pili, nilikhofia kuwa ikiwa hawatofuzu katika mipango yao hiyo ikatokea kukamatwa, wasije kwa mateso wakafika kusema kuwa na mimi nilikuwa pamoja nao. Mradi nilikuwa si hadhir khasa kwa namna ya serikali yenyewe ilivyokuwa. Kufika kiasi cha saa moja ya usiku, niliona mlango wa banda nililokuwa nikilala umefunguliwa ghafla, na Sajin Buesha amesimama mlangoni na kusema, "Aman Thani! Toka nje na kirago chako". Roho ilinipiga paa! Niliona kishindo hicho kimeshanifika. Lakini, nilijikaza kiume, nilitoka huku nikionesha kama sina khofu ya lolote.

Nilipofika 'kotagadi', niliikuta gari ya magereza. imefunikwa turubali. Gari hii ilikuwa imekuja kutoka Makao Makuu ya Magereza pamoja na wachungaji wa magereza na ofisa wao, kijana wa kiZanzibari mwenye asili ya Kihindi, akiitwa Hassanali. Mpaka wakati huu nishakuwa ninayajuwa magereza yote na wachungaji wote, mote humo ni mwangu; si mgeni tena! Nilipofika tu, nilitiwa katika hiyo gari moja kwa moja mpaka katika vyumba vya kunyongewa (condemned cells). Huko nilimkuta kijana mdogo wa kiMakunduchi aliyekuwa mchungaji sehemu hiyo. Kijana huyo, alisikitika kwa kuniona nimeletwa katika sehemu hiyo, na neno alilolisema kwangu ni, "Inshaallah, atawajaalia waweze kutoka katika nchi hii kwa salama, na nyote mlodhulumiwa kwa kufungwa bila ya kosa lolote, Mwenyezi Mungu atakutoweni bila ya wao kupenda". Nilistaajabu kumsikia kijana mdogo kama huyo kuweza kusema maneno kama hayo, na khasa kwa vile alivyokuwa ni mfanyakazi katika serikali ya mavamizi katika wakati huo na pahala kama hapo. Langu mimi lilikuwa ni kuitikia, AMIN. Sikuwekwa sana katika sehemu hiyo, ila nilimuona Sajini wa magereza akifuatana na askari wake wawili (wachungaji) wamenitokea na walipofika tu bila ya kunambiya lolote, huyo Sajini alinitia pingu za mikono na niliongozwa kutoka hapo Makao Makuu ya Magereza hadi kwenye gereza la "Kwa Ba Mkwe", "Mlango wa Nyuma". Huko nilimkuta mwenyewe bwana Mandera akinisubiri. Mandera aliniambia kama hivi:

62

"Aman, unajua kwanini ukaletwa hapa?" Nilimjibu, "Sijui". Aliniambia, "Unajua kuwa Twala na Majura wamekimbia kutoka gerezani?" Nilimjibu, "Najua kwa kuwasikia wachungaji wetu wakizungumza hayo baada ya sisi kurejeshwa kambini". Aliniambia, "Basi umeletwa hapa, kwa ajili wewe ni wenzako sana Twala na Majura. Kwahivyo tunatumai utaweza kutwambia, wapi tutawapata. Hapana shaka wewe utaweza kuijuwa uzuri mipango yao". Nilimwambia Mandera, "Unadhani kuwa mimi napenda kuwepo gerezani? Ikiwa nikiijuwa mipango yao ya kutoroka gerezani, basi kwanini na mimi nisiwe pamoja nao? Au wewe unadhani kuwa Twala na Majura wataweza kuniamini mimi kiasi cha kuambizana siri kubwa kama hizo? Vyovyote itavyokuwa, mimi ninazo sababu za kutowaamni wao, na wao vilevile hapana shaka wanazo sababu za kutokuniamini".

Nilipokuwa nikimueleza Mandera haya, mara alikuja mmoja katika wachungaji na kunon'gona na Mandera, na hapo hapo Mandera aliondoka na alimpa amri huyo mchungaji anipeleke kwenye chumba cha mahabusi. Nilipotiwa ndani ya chumba hicho, nilimkuta mtu, kwa hakika alikuwa hayupo duniani hayuko akhera! Kwa jinsi alivyoteswa, alikuwa akikoroma tu. Uso wake wote umevimba na umepasuka pasuka na madamu yamemkaukia mwilini mwake. Alikuwa hawezi kusema, hawezi hata kutukusika. Baada ya siku tatu, usiku na mchana ndipo nilipoweza kumtambuwa, kwanza kwa kukisia tu, baadae kwa kuwauliza hao wachungaji wa gereza hilo ndipo nilipomjuwa kwa hakika. Bwana huyo tulikuwa tukijuwana kwa miaka mingi sana, kabla ya hata kuingia kwa mambo ya siasa Zanzibar. Siku za siasa, Bwana huyo, alikuwa miongoni mwa makatibu wa matawi ya Hizbu na alikuwa mpenzi wa kweli wa HizbulWattan na nchi yake. Lakini, kwa jinsi alivyoteswa katika gereza hilo, nilishindwa kumtambua mpaka nilipoambiwa. Haukuchukuwa muda mkubwa toka kuwa naye pamoja humo ndani ya chumba ila siku moja katika nyakati za asubuhi, Mwenye Enzi Mungu alichukuwa kiumbe chake, akiwa ni mwnye kudhulumiwa na serikali ya mavamizi.

Walipomuona ameshakufa, walimbeba kitikiti, mmoja amekamata mikono na wapili miguu utadhania gunia la muhogo. Binaadamu anafungwa, anateswa, anaachwa afe kisha anabebwa kama mzoga. Haya yamefanywa na wataka maendeleo na wa waondoa dhulma! Mzee huyo akiitwa Mzee Mwinyi, yeye ni mtu wa sehemu ya Shakani au Maungani. Hapo katika miaka ya nyuma akiishi mtaa wa Miembeni, Unguja. Baada ya mimi kutolewa gerezani 1972, nilisikia kuwa mzee huyo baada ya kutolewa maiti kwenye hilo gereza la "Kwa Ba Mkwe", alipelekwa hospitali kuu na waliarifiwa watu wake baada ya kuwepo hapo hospitali kwenda kumchukuwa maiti wao. Walimpeleka hospitali ionekane kwamba kafia huko! Mimi niliwekwa katika chumba hicho cha gereza la "Kwa Ba Mkwe" mpaka walipopenda wenyewe walinitoa na kunirejesha Langoni kuendelea na kifungo changu.

Kwa hakika Bwana AbdulAziz Twala alinizungumzia mambo mengi kukhusu mwendo wa Serikali yao ilivyokuwa ikiendeshwa. Mengine naona taabu hata kuyaandika. Yote alionieleza yanathibitisha tulivyokuwa tukiamini tangu awali, kuwa hakukuwa na serikali ila kilichokuwepo ni gengi la wauwaji na wanyan'ganyaji haki za watu, toka majumba, mashamba na mpaka wake, watoto na ndugu za watu. Ikiwa Raisi wa nchi alifika kuweka hashaakum, kuwadi wa kulipwa mshahara kutoka katika fedha za nchi kwa ajili ya kumletea wanawake wa kufanya nao uchafu, basi serikali hiyo, itakuwa na insafu na thamani kutoka wapi?!! Kuthibitisha kuwa wakubwa wote wa serikali hiyo walikuwa ni watu wa aina hiyo hiyo ya mkubwa wao Mzee Karume basi baada ya kufa Karume, kuwadi huyo hakupoteza kazi yake bali alitunukiwa wadhifa mkubwa na kupewa cheo cha udhamini wa Jeshi la Wanamaji katika kisiwa cha Pemba. Hivi ndivyo wanavyo tunzana na kuhifadhiana!!

MAKOMRED WAMECHANGIA MAAFA YALIOPO NCHINI Sehemu kubwa ya maafa yaliyowafika wananchi wa Unguja na Pemba na yenye kuendelea kuwafika hadi hii leo, yanatokana na mchango mkubwa kutoka kwa hao ndugu zetu wenye kujiita, "progressives", yaani makomred. Mbali ya kuchanganyika pamoja na wageni na 'mafashisti' katika kuivamia nchi na kuiondowa serikali iliyochaguliwa na wananchi wenyewe kwa kuleta hayo wenyekuyaita, "Mapinduzi", bali hata kwa yaliyofuatia baadae, ndugu zetu hao wameshiriki sana katika kuleta balaa hizo. Kuporomoka kiwango cha taalimu katika nchi na kutoweka huduma za matibabu yafaayo katika mahospitali ya serikali ni kwa sababu ya uwongozi mpotofu uliyoanzia kutokana na aliyekuwa Waziri wa wizara hizo wakati huo ambaye ni mmoja katika hao wapendao kujiita, "progressives". Yeye ndiye

63 sababu mpaka wengi kati ya walimu waliokuwa wazuri katika kazi zao, waliamua kuwacha kazi na wengine waliamua kuondoka katika nchi kwa njia za kukimbia. Hali kadhalika madaktari wajuzi, nao waliwacha kazi na kuikimbia nchi na ukorofi wa uwongozi wa Waziri huyo. Kuondolewa masomo ya dini katika maskuli na kuondolewa kusomeshwa Taarikh (Historia) ya kweli juu ya Zanzibar na Afrika Mashariki kwa jumla, yalitokea wakati wa Wizara ya Taalimu ikiwa katika mikono ya Waziri "progressive". Hata Qur'an iliachwa kusomeshwa katika maskuli ya serikali na Misahafu kuchomwa moto katika kinu cha kuchomea taka huko Saateni Zanzibar, wakati wa Waziri huyo huyo, "progressive". Badala yake vijana wetu wa kike na wa kiume walikuwa wakichezeshwa ngoma za kucheza viuno mbele ya hadhara ya watu, ngoma ambazo hazikuwa na makhusiano yoyote na utamaduni wetu wa kiZanzibari, bali ni kinyume na tabia na mila zetu. Kuanza kuvunjika kwa murwa na utamaduni wa kiZanzibari kulikwa wakati wa hayo yenye kuitwa 'mapinduuzi', na hao ndugu zetu wajiitao, "progressives" ndio waliochangia sehemu kubwa. Ilifika hadi watoto kuwaondolea adabu wazee wao majumbani, na walimu wao maskuli. Na wengine walifika kuwashitaki wazee wao kwa "Regional Commissioner" kwa kuwa ati wamezuiliwa kwenda katika michezo ya "Halaiki". Wamefanya hayo vijana wetu hao kutokana na mafunzo ya vibarazani na vichochoroni waliyokuwa wakiyapata kwa hao wenye kujiita, "progressives". Ati, ndiyo usawa na maendeleo!! Michezo ya "Halaiki" ni michezo ya kuchezeshwa umati wa watu kwa kufuata amri kama masanamu. Michezo hiyo tulifunzwa na nchi za Kikoministi, kama Korea na China. Mzee mwenzetu, Bwana Abdulla Ajmi, katika kuilani michezo hiyo alisema, "Mungu aihiliki hiyo michezo ya halaiki".

KWANINI MWALIMU NYERERE ALIKATAA KUWAPELEKA ZANZIBAR WATUHUMIWA WA KESI YA UKHAINI? Alipouliwa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, Abeid Amani Karume, Wazanzibari wengi walikamatwa na kutiwa viziwizini vya Magereza ya Zanzibar na ya Tanzania Bara. Wazanzibari waliyotuhumiwa zaidi kwa mauwaji ya Karume, walikuwa ni hao wajiitao, "progressives" au makomredi. Wao, walibakishwa viziwizini kwa muda mkubwa baada ya Wazanzibari wengine kuachiliwa huru. Baada ya muda tokea kuwekwa humo viziwizini, Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar iliwafungulia mashitaka watuhumiwa wote waliyokuwepo Zanzibar na waliyokuwepo Bara. Lakini, inasemekana kuwa Mwalimu Nyerere alikataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo katika magereza ya Tanzania Bara. Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, walipoona Mwalimu amekataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo Bara kuhudhuria katika mashitaka yao, waliendelea na mashitaka na waliwapeleka Mahakamani watuhumiwa waliyokuwepo katika magereza ya Zanzibar. Mashitaka yalichukuwa muda mkubwa, mwisho Mahakama yalitoa uwamuzi wake juu ya watuhumiwa wote wa Zanzibar na wa Bara (ambao walihukumiwa bila ya wenyewe kuhudhuria Mahakamani). Hukumu iliyotolewa na Mahakama hayo ilikuwa, wengine wapewe adabu ya vifo na wengine wafungwe gerezani kwa vifungo vya muda mbali mbali.

Miongoni mwa waliohukumiwa vifo ni huyo mkuu wao "progressives", Abdulrahman Babu. Sisemi kuwa Mahakama hayo na Mahakimu hao waliyoendesha mashitaka hayo walikuwa ni wenye kufaa au wenye ujuzi uliyokhusika na sheria, hashaa! Sote tukijuwa kuwa Mahakimu hao hawakuwa na ujuzi wowote juu ya mambo ya sheria, bali tu walikuwa na ujuzi wa kuuza samaki wakavu na kushona kofia za viuwa. Lakini, kwa vile hao wahukumiwa, wao wenyewe ni washiriki katika kuleta hiyo serikali ya mavamizi, na kwa kiasi fulani walikhusika na nyendo za seikali hiyo ambayo matokeo yake ndiyo kuwepo kwa Mahakama kama hayo na Mahakimu kama hao, kwahivyo, washitakiwa hao kuhukumiwa na Mahakimu kama hao itakuwa wanafaidika kwa matunda waliyoyapanda kwa mikono yao wenyewe. Ama wananchi wanyonge waliopata mateso kutokana na hukumu za mahakama hizo, wao ni waliyodhulumiwa. Dhulma ambazo wengi kati ya wananchi wamepitishiwa. Washitakiwa hao (wakati walipokuwa katika vyeo vyao) walikuwa wakiona kuwa vitendo hivyo vya dhulma ni ndivyo na pia wakiviunga mkono kwa maneno na hata kwa vitendo. Kwa vile dhulma haina bwana wala mwana ndio tukaamrishwa kuipiga vita kwa njia zote popote pale ilipo.

Kadhiya hii iliwasangaza wananchi wengi bali hata watu wa nje. Ilivyo ni kuwa mpaka hii leo hata miongoni mwa wakereketwa wa AfroShirazi bado hawajakitambua kitandawili kilichotolewa mpaka yakatokea hayo ya Mwalimu kukataa kuwapeleka watuhumiwa wa ki"progressive" waliyokuwepo katika Magereza ya Bara kuhudhuria kwenye mashitaka yao katika Mahakama ya Zanzibar. Kitandawili zaidi ni

64 kuwa wahukumiwa wote hao, waliohukumiwa vifo na waliohukumiwa vifungo wametolewa vizuizini na kuachiliwa huru bila ya hata rufaani. Ni nani huyo aliyekuwa na nguvu za kubatilisha hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibari?

Naiwe kama itavyokuwa, lakini, ndio imeshakuwa. Na huyo aliyekuwa na nguvu za kubatilisha hukumu iliyotolewa na Mahakama hayo, kwa nini asitumie nguvu hizo kwa kuzuwia kuweko Mahakama kama hizo, na sio kuzuwia tu, bali kuwapelekea mbele ya mahakama wote waliyokhusika na ukhalifu huo wa kuasisi mahakama kama hayo, Mahakama ya dhulma na uhange? Na badala yake kuwalipa fidia wote waliyopata kuhukumiwa katika mahakama kama hayo na wakapewa adhabu ya namna yoyote? Kwa hakika mipango na matokeo yaliyopitishwa mpaka kuuliwa kwa Mzee Karume yana kitandawili kikubwa. Kama si hivyo, Mwalimu asingekataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo katika Magereza ya Tanzania Bara na wasingeachiliwa huru baada ya muda mdogo tokea kuhukumiwa.

Mwalimu aliona ndivyo kuwapeleka Zanzibar Othman Shariff, Abdalla Kassim Hanga, Idrisa Abdalla Majura, Bibi Titi Mohammed, Kamaliza, Chipaka, (hao watatu wa mwisho ni Watanganyika) bila ya kujuulikana makosa yao au kuhukumiwa na yoyote. Nyerere huyo huyo akiwa ni mwalimu wa mipango aliona ni busara kutowapeleka hao wajiitao, "progressives" waliyokuwemo ndani ya mikono yake na waliyokuwa wakitakiwa na Serikali yake ya Mavamizi ya Zanzibar kwa kumuuwa aliiyekuwa Makamo Raisi wake Makamo Raisi wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jee, haya ni bure bure tu! Haiwezi kuwa! Lazima lipo, lakini ikiwa si leo, kesho na ikiwa si kesho, keshokutwa; bali ikiwa hata si mwaka huu, miaka ijayo. Lakini lazima siku moja ukweli utajichomoza. Vyovyote vile ilivyo lakini, Karume alikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Afike kuuliwa, na waliyo tuhumiwa kuwa ndio wauaji wamekamatwa na kuwepo katika mikono ya Serikali, kisha wakahukumiwa na pakatolewa hukumu juu ya washitakiwa hao, na baada ya hukumu wakaachiliwa huru kama kwamba hapana lililotendeka! Oh!, Kweli hayo?!! Ni hakika ingelikuwa kauliwa mwanachama tu wa ASP basi mtuhumiwa huyo angelikiona cha mtema kuni, leo kauliwa Raisi wa Nchi ndio imekuwa si chochote si lolote!

Si hayo tu yenye kuwasangaza wananchi wa Zanzibar bali yapo na mengineyo. Lishangazalo zaidi ni kuwa huyo aliyetajwa na ikakubalika kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakiendeshwa kuwa ndiye aliyekuwa mwongozi wa hayo machafuko yaliyotendeka nchini (Zanzibar) katika taarikh 7 April, 1972 na kumalizikia kwa kuuawa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar awe ameruhusiwa bila ya viziwizi vyovyote kuondoka na kurejea katika nchi wakati wowote aupendao. Si hayo tu, bali Serikali hiyo hiyo iliyomuhukumu kifo, ikawa inamualika kushiriki katika mikutano yenye kufanywa katika nchi, akiingia na kutoka maridhawa!!

SIRI HII NI KUBWA SANA!! Leo ni miaka 30 tokea kufanyika kwa hayo yenye kuitwa, "Mapinduzi" na mpaka hii leo baadhi ya waongozi wa Serikali ya Hizbu na ZPPP, hawaruhusiwi hata kuikanyaga nchi yao, Zanzibar. Na ilhali wao hawakumuuwa yoyote, licha kumuuwa Raisi wa Nchi, wala hawakunya'ganya mali ya mtu wala hawakuiba au kupoteza mali ya Nchi, hawakufanya kosa lolote dhidi ya sheria ya nchi. Ilivyo khasa ni wao ndio waliodhulumiwa tokea kuvamiwa kwa Serikali, kuuliwa watu, kufungwa magerezani, kuteswa na kubidi kutoka nchini. Isitoshe, kwa kuchukuliwa mali zao, tokea majumba mpaka mashamba ambayo wameyachuma kwa jasho lao au kwa majasho ya wazee wao. Ingalikuwa yuko mmoja katika wao aliyekuwa na kosa lolote basi Serikali ya Mavamizi ingaliwapeleka Mahakamani, lakini hakuwaona na kosa lolote, kwa hivyo waliamua kuwafanya "wafungwa wa kisiasa"na kuwaweka magerezani kwa muda wa miaka 10 bila ya kuhukumiwa. Lakini waliothibiti mahakamani kuwa walikhusika na kuuliwa kwa Rais wa Nchi na Kiongozi wa Chama cha AfroShirazi hawakuguswa, bali walitunzwa! Jee, tuseme wanaogopwa, au wanayajuwa yale yenye kuogopwa yakisemwa!

SERIKALI YA MAVAMIZI YA ZANZIBAR BADO IMO NA UBAGUZI WAKE Serikali ya mavamizi ya Zanzibar bado inaendelea katika mwendo wake wa ubaguzi. Yoyote aliyekuwa mwanachama wa ZNP/ZPPP mpaka hii leo kwao wao hana jina zuri, wala hana jema atendalo; ni mtoto wa kambo tu! Leo ni zaidi ya miaka thalathini lakini bado Mahizbu na maZPPP wanachukiza. Yote haya wanatendewa, na ilhali hiyo serikali haiwezi kuthibitisha kosa lolote juu yao. Niliyotendewa miye

65 mwenyewe (yafuatayo hapo chini) yatathibitisha ninavyosema kuwa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar bado imo kuendeleza siasa yake ya ubaguzi. Ubaguzi wa kila aina, kila upande.

NILITAKIWA NITOKE NCHINI Mimi, muandishi wa kijitabu hiki, baada ya muda wamiaka 20 toka kutoka nchini naliomba niruhusiwe kuizuru nchi yangu. Nchi nilyozaliwa mimi na wamezaliwa wazee wangu wawili. Kwa shida niliruhusiwa kwa kupewa muda wa miezi mitatu kukaa katika nchi! Kwa kupewa ruhusa hiyo, taarikhi 9 Januari, 1992 nilizuru Zanzibar na 18 Februari, 1992 nilirejea katika masikani yangu, Dubai. Baada ya miezi sita, yaani taarikh 9 Agosti, mwaka huo huo wa 1992, nilikwenda tena Zanzibar na wakati huo nilidhamiria kukaa kwa muda wa miezi mitatu kwa kuendelea na mipango ya miradi yangu ya ukulima na ufugaji niliyo kusudia kuifanya.

Niliambiwa nilipofika kiwanja cha ndege siku nilioingia nchini, kuwa ikiwa nitataka kukaa nchini kwa muda zaidi, nenda Idara ya Uhamiaji nikaombe kuongezewa muda. Baada ya mwezi mmoja, nilikwenda huko Idara ya Uhamiaji kutaka niongezwe muda wa kukaa. Nilipofika, walinizuilia paspoti yangu na kisha nikaambiwa nikaonane na "boss". Nilipelekwa mpaka kwa huyo "boss" anaeitwa Ali Daud. "boss" baada ya kunitilia mijiti hii na hii, aliniambia, "Njoo keshokutwa kwani Boss leo hayupo kenda mkutanoni DaresSalaam". Nilimuuliza huyu boss, "Kwani pana jambo gani?" Alinijibu, "boss anataka kukuona". Nilinyamaza na niliondoka. Ilipofika hiyo keshokutwa niliyoambiwa, nilifika Idara ya Uhamiaji na safari hii nilipelekwa kwa "boss" mwengine, Himid Yusuf Himid. Huyu ni kijana mdogo, Mzee wake tulikuwa tukifahamiana sana. Juu yakuwa tulikuwa na tafauti zetu kukhusu msimamo wa fikra za kisiasa, lakini tulikuwa tukihishimiana na tukisikilizana. Nilipofika ofisi ya kijana huyo Himid, aliniambia, "Mambo yako bado hayajamalizika, ikiwa utaweza, kusubiri hapo nje au unaweza kwenda na kurejea kiasi cha saa sita za mchana".

Niliporejea mnamo saa sita, aliniuliza, "Ndege ya Arabuni inaondoka hapa siku gani?" Nilimwambia, "Inategemea ndege gani uitakayo, kwani zipo ndege mbili zinazo kwenda Arabuni, na kila moja inayo siku yake na wakati wake". Aliniambia, "Hiyo unayo safiria wewe". Nilimwambia, "Inaondoka hapa kuelekea Dubai kila siku ya Jumaapili asubuhi saa tatu". Baada ya kumjibu hivyo, aliniambia, "Nifuate!" Nilimfuata mpaka ofisi nyengine na huko alimpa kijana aliyekuwa akifanyakazi sehemu hiyo pasipoti yangu na alimwambia, "Mpe muda wa kukaa Zanzibar mpaka Jumaapili tarehe 3 9 92 na muuandikie, 'Final Extension'." Nilimuuliza huyo kijana Himid, "Kwa nini yakawa yote haya kwani nimefanya jambo gani katika nchi hata ikawa nanyimwa kupewa muda zaidi, na kufika hadi kuondolewa katika nchi?" Jawabu aliyonijibu na huku anakwenda zake, "Huo ndio uwamuzi uliyofikiwa". Nilinyamaza na nilingojea pasipoti yangu nilipoipata niliondoka na kwenda kutenegeneza safari. Siku hiyo ilikuwa siku ya Ijumaa taarikhi 1 8 92. Utaona kuwa nimepewa muda wa kasoro kuliko saa 36 niondoke katika nchi yangu niliyokuwa nimezaliwa! Bila ya kuambiwa nimekosa nini. Wakati huo nilikuwa nimefuatana na mwenzangu mmoja. Yeye alihuzunishwa na uwamuzi uliyotolewa dhidi yangu na aliniuliza, "Kwa nini yakatokea yote haya?" Nilimwambia, "Usidhanie kuwa nimefanya lolote kinyume na sheria katika ukaaji wangu hapa. Sikufanya hata chembe, lakini simba ni simba hata akikonga. Akitokeza basi kila aliyepo hawachi kushituka, khasa wale wanaomjuwa tangu hapo zamanai. Kwa hivyo ndugu yangu usiwe na haja ya kutafuta lengine".

Baada ya kurejea kwangu Dubai nilianza kuyazingatiya haya niliofanyiwa, na nalikata shauri kuwaandikia wakuu wa Serikali ya Zanzibar khasa kwa vile wao wenyewe ndio walionipa ruhusu kuizuru Zanzibar. Kwa hakika sikuweza kupata jawabu lolote kwa maandishi ila nilikuwa nikisikia maneno tu, kuwa wakuu wa serikali wanasema kuwa wao hawajui lolote nililolitenda wakati nilipokuwepo nchini lakini watazidi kuchungua. Mimi kwa upande wangu nilikuwa nakwenda mbio katika kujiombea ili nipate tena kuingia Zanzibar bila ya taabu na shida yoyote. Nawashukuru shemegi zangu na baadhi ya wananchi wenzangu kwa shida walizozichukuwa za kupanda na kushuka kunitakia ruhusa, mpaka mwisho Mungu akayafungua na kukubaliwa kuingia Zanzibar tena.

Taarikhi 24 Julai, 1994 nilifika Zanzibar na baada ya kukaa kwa muda wa mwezi mmoja na siku chache niliondoka mnamo taarikhi 27 Agosti, 1994 kwa kurejea kwenye masikani yangu Dubai. Nashukuru kuwa

66 safari hii nimeingia katika nchi kwa salama na nimeachiwa kukaa mpaka nimetoka kwa salama na Inshaallah itaendelea kuwa salama daima dawamu.

NAMNA NILIVYOONDOKA KUUKIMBIA WATTANI WANGU Tokea nilipokuwepo kifungoni, nilikuwa nikipanga njia za kuondoka katika Wattani wangu, Zanzibar, nikijaaliwa kuachiliwa huru kwa salama. Baada ya kutolewa gerezani Januari 12, 1972, nilianza kutafuta pasipoti lakini nilikuwa nikihangaishwa huku na huku, mwisho niliambiwa kwa njia za kiundugu zisizokuwa rasmi kuwa, "Haitokuwa rahisi kwako kupata pasipoti kwa wakati huu". Nilipoambiwa hivyo, nilianza kutupa nyavu kila kipembe. Ilipofika taarikhi 7 Mei, 1972 (mwezi mmoja tokea kuuliwa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar) nilimuomba Mwenyezi Mungu nikifuatana na wenzangu wawili, Sheikh Mohammed Ali Abbas na mwanawe Ali Mohammed Ali Abbas.

Katika wakati huo, yaani baada ya kuuliwa Karume, usafiri wa namna yoyote ulikuwa na shida kubwa bali hata hivyo tulimuomba Mwenyezi Mungu. Ilipofika saa tatu za usiku wa taarikhi hiyo 7 Mei, tuliondoka. Kulipo pambazuka asubuhi yake, tuliingia katika moja ya bandari za kivuvi ziliopo pwani pwani ya sehemu ya bahari ya Tanganyika. Tulisali alfajiri katika msikiti wa kiambo hicho, kisha tulifungua vinywa kwa chai na maandazi katika kijikahawa kidogo kilichokuwepo hapo. Tulingojea "bas" la kuendea Tanga kwa kupitia Pangani. Kiasi cha saa mbili za asubuhi "bas" lilifika na tuliingia. Jumla yetu tulikuwa watu wane. Sisi watatu na kijana mmoja tuliyepewa na wazee atufikishe Tanga. Tulipoingia katika "bas", tulimkuta kijana wa kiZanzibari kafatana na kijana wa kiTanganyika. Kijana huyu (wa kiTanganyika) alikuwa amevaa nguo za Tanu Youth League. Huyo kijana wa kiZanzibari tulijuana tulipokuwa gerezani, Langoni. Yeye alikuwa amefungwa kwa 'kumnajisi' n'gombe. Alitulahiki kwa uzuri na tulikaa naye mpaka kufika Pangani. Tulipofika Pangani tulipokuwa tunakula chakula cha mchana, huyo kijana wa kiZanzibari alitujia kwenye meza yetu na alitwambia, "Yule mwenzangu niliyekaa naye, amewekwa sehemu hizi kuchungua watu wanaoingia kwa magendo na wenye kusafirisha karafuu kwa magendo. Alinambia kuwa ana wasiwasi juu yenu na tulipofika hapa, alitaka kukupelekeni kwenye kituo cha polisi cha hapa Pangani, mimi nimemuomba asifanye hivyo. Lakini amesema kuwa anataka kuona vitambulisho vyenu, basi nipeni nimpelekee.

Tulimwambia kuwa sisi hatuna vitambulisho vyovyote hatukuona kuwa ni muhimu kuchukuwa vitambulisho wakati tunasafiri katika nchi moja. Kijana alijitia kwenda kumjibu mwenzake. Basi alikuwa akija kwetu na akenda kwa huyo mwenziwe, yote kwa kuwa alitaka tutowe chochote tuwape. Sisi wenyewe sote watatu wakati huo rasilimali yetu ilikuwa Shs.1000. Huyo kijana wa kiTanganyika kwa alivyotwambia huyo ndugu yetu wa kiZanzibari kuwa alikuwa akitaka tumpe kwa sisi watu watatu Shs.1500. Hata kama tungetaka kutowa pesa hizo basi tungeshindwa, kwani tulikuwa hatuna. Tulianza kupatana kama tunataka kuuziana biashara tokea Pangani mpaka tukafika Tanga, mwisho twaliwapa Shs. 50 na ghasia zote zilimalizika. Tulipofika Tanga, tulipokelewa na ndugu yetu mpenzi ambaye tulijuana tulipokuwa kifungoni, Langoni. Ndugu yetu huyo, yeye alikuwa amefungwa kwa makosa ya kusafirisha karafuu kwa magendo. Yeye ni mzalia wa Tanga na ndiko alikokuwa akiishi. Baada ya kufika kwa mwenyeji wetu, yule ndugu yetu tuliyopewa atufikishe alituaga na alirejea Zanzibar. Sisi tulibakia hapo kwa kufanya mipango ya kuingia Mombasa, Kenya. Mwenyeji wetu huyo, alitupokea kwa uzuri sana na alitupa misaada tuliyokuwa tumeihitajia na hata tuliyokuwa hatukuhitajia.

Kwa kutokana na kuuliwa kwa Rais Karume, mipaka ya Tanzania na Kenya ilikuwa na ulinzi mkali sana, hata baadhi ya watu wa Idara ya Usalama kutoka Zanzibar walikuwepo katika ulinzi kwenye mpaka wa Tanzania kuingia Kenya.. Ndugu yetu huyo aliingia katika shughuli za kututafutia mipango ya kuondoka na kila njia aliyokuwa akijaribu, ilikuwa ngumu. Alifika hadi ya kutukatia vipande vya Tanu Youth League na kuwa ni Wadigo tuliyozaliwa Tanga. Yote hayakutusaidia kitu kwa jinsi ya hali ya mipakani ilivyokuwa ngumu wakati huo. Katika juhudi zake mwisho alimpata mmoja katika ndugu zake ambaye kwa kutokana na kazi zake kijana huyo, alikuwa bingwa wa njia za vichakani kutoka Tanzania kufikia Kenya. Siku moja asubuhi, alikuja yeye na huyo ndugu yake, alituzungumzia kwa kutwambia, " Mwenye Enzi Mungu akijaaliya mimi naweza kukufikisheni Mombasa, kwa njia za vichakani, lakini kwa watu waliyokuwa hawakuzowea kupita katika njia kama hizo, zinaweza kuwa ngumu kwao kwa sababu kwa hakika hakuna njia khasa, ni kupita vichakani vichakani. Aliendelea kwa kutueleza kuwa, wakati mwengine huwenda wakatokea askari wa misitu ambao kazi yao ni kulinda wanyama pori wasiwe

67 wakipigwa ovyo ovyo. Mara nyengine wakiona watu katika nyakati kama hizo, huwatia katika mashaka. Wakishapewa chochote huwa basi. Ikiwa mukotayari kuzistahamili shida hizo, basi mimi nishakubali kujitolea wala sitaki mnipe chochote. Kitacho hitajia mutowe ni nauli ya "bas" kutoka hapa mpaka hapo tutapoanzia hiyo safari yetu ya vichakani". Tulimshukuru huyo kijana kwa hayo maneno aliyotwambiya na tulimwambia, "Tutayari kwa lolote maadamu litaweza kutuondoa hapa na kutufikisha Mombasa". Kijana huyo, alisema, "Basi kesho kiasi cha saa mbili za usiku tutaondoka hapa kwa taxi kwenda kwenye kituo cha "basi" lenye kutoka DaresSalaam kuelekea Mombasa. Kwahivyo nipeni nauli ya hiyo taxi na nauli ya "basi". Tulifungua kibindo chetu na tulimpa kwa furaha na bashasha.

Siku ya pili ilipofika na wakati ulipowadia yule kijana pamoja na mwenyeji wetu walikuja. Na baada ya kuagana na huyo mwenyeji wetu, tuliingia katika "taxi" mpaka kwenye hicho kituo cha "basi". Tulipofika hapo, mwenyeji wetu alitupeleka kwenye hoteli kwa chakula cha usiku. Tulipokuwa tunakula, huyo kijana wetu wa safari alikuwa nje na kazi zake. Mara alikuja kwa vishindo na alituambia, "Twendeni zetuni, upesi upesi, wacheni chakula!". Tulisituka na tulifikiri labda "bas" limeshafika na safari tayari. Tulipotoka nje ya hoteli, kijana alisimamisha "taxi" na baada ya kuingia, alimwambia dereva, "Tupeleke Amboni". Tulikwenda moja kwa moja mpaka Amboni, tuliteremka na tulilipa nauli ya hiyo "taxi". Hapo ndipo huyo kijana alianza kutwambia kwa nini ametuondoa pale hoteli kwa haraka. Kijana alisema, "Nilipo kuwepo nje ya hoteli, niliwaona vijana watatu wa kiZanzibari wametoka na wamekaa katika viti viliopo nje ya hoteli. Vijana hao nilipata kuwaona kabla na nafikiri ni katika waliyokuwa wameletwa kuwavizia Wazanzibari wenye kupita sehemu hizi kwa kukimbia, ndipo nilipoona bora tuondoke upesi. Tutakaa hapa mpaka "bas" litapofika hapa, likifika mtawaona watu wote wanateremka na wanavuka daraja kwa miguu na "bas" litavuka tupu. Likishavuka litasimama nje ya daraja na hapo watu wataingia tena na sisi tutaingia pamoja nao. Nishafanya mipango, tutaekewa nafasi zetu". Kijana aliendelea kutuambia, "Huko mbele mtaponiona nime lisimamisha "bas" nateremka, basi na nyie teremkeni".

Ilipofika kiasi cha saa nne unusu, "bas" liliingia Amboni na lilipofika kwenye daraja watu waliteremka, na sisi tulichanganyika na abiria wenzetu tukavuka daraja kulifuatia "bas" ng'ambo ya pili ya daraja na kuendelea na safari yetu. Kiasi cha saa nane za usiku, tulimuona huyo kijana wetu amelisimamisha "bas". Tulipomuona anajitengeneza kuteremka, na sisi tuliteremka naye. Tulisimama pale kwa kiasi cha muda mdogo na kisha kijana wetu alitwambia, "Ile safari yetu niliyokuambieni, ndiyo itaanza hivi sasa, hapa ndipo pahala penyewe basi natumuombeni Mwenyezi Mungu". Wakati huo, mbaamwezi ilikuwa ikin'gaa sana. Tulianza kuingia msitu na nyika bila ya kuwa na wasiwasi wowote. Mtoto wetu Ali, wakati huo alikuwa kijana mdogo lakini, alikuwa shujaa wa kustahamili shida zote za safari hiyo. Kiasi cha saa kumi za usiku, kijana wetu alitwambia, "Munauona mwangaza wa taa zile upande wa mkono wetu wa kulia, zile ni taa za kituo cha polisi cha mpaka wa Tanzania". Baada ya mwendo wa kiasi cha saa mbili kutoka wakati huo, alitwambia kuwa, "Na taa zile mnazoziona sasa ni taa za kituo cha polisi cha mpaka wa Kenya". Baada ya kiasi cha muda, alitwambia kuwa, "Sasa hapa tulipo, tupo ndani ya ardhi ya Kenya. Ikiwa lolote litatutokea kwa hapa, tutapelekwa katika kituo cha polisi ya Kenya". Alipotwambia hivyo, tulinyanyua mikono juu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kutoka Tanzania salama na kwa kuingia Kenya. Kwani tukiamini kuwa ikiwa likitutokea lolote la bahati mbaya hapa tulipo, basi tutakuwa katika mikono ya serikali ambayo wanahishimu "Haki za Binadamu" na wanatambua Haki za Wakimbizi wa Kisiasa.

Kiasi cha saa 12 za asubuhi, tuliingia sehemu za mashamba ziliopo nje ya mji wa Mombasa na baada ya kufungua vinywa kwa chai na mahamuri katika kijikahawa cha kiamboni, tulikaa hapo kwa kusubiri "bas" la kutupeleka Mombasa mjini. Tulifika mjini Mombasa mnamo saa tano za mchana. Yule kijana wetu alipotufikisha Mombasa kwa salama, alituaga kwa kurejea Tanga. Ni taabu kuweza kueleza namna tulivyokuwa tukihisi juu ya wema wake aliyotutendea ambao lau lingetokea lolote la bahati mbaya, basi na yeye angekuwa ameyahatarisha maisha yake kwa sababu yetu sisi. Mwenyezi Mungu ndiye atayemlipa kila la kheri yeye na huyo ndugu yetu, mwenyeji wetu wa Tanga aliyekuwa ndio sababu ya kutupatia huyo ndugu yake.

Tulipofika Mombasa, kwanza tulianza kumtafuta ndugu yetu Maalim Wazir bin Ali ambaye alitangulia kuondoka Zanzibar na alikuwa akitusubiri Mombasa ili tuondoke sote pamoja kwa safari ya kuelekea Arabuni. Tulipofika hapo alipokuwa amefikia, wenyeji wake walitwambia, "Alikusubirini sana, alivyoona

68 mumekawia aliona bora atangulie. Lakini, ametuagizia kuwa mkitokea, tukupokeeni na tuwe na nyie pamoja mpaka mtapo fanikiwa kuondoka". Kwa hakika tuliona taabu kwa kutomkuta huyo mwenzetu, lakini kwa namna tulivyokuwa kwa wakati huo, hatukuwa na budi ila kukubali kubakia hapa hapa mpaka tupate safari yetu ya Arabuni. Alhamdulillahi, tunawashukuru kwani muda wote tuliokuwa kwao, walituhangaikia kwa kila yaliyokuwa ya lazima.

Baada ya kukaa hapo kwa muda wa siku kadhaa, siku moja ghafla tulipokuwa tukitembea katika barabara ya Salim Road (sasa inaitwa "Digo Road") nilikutana na shemegi yangu, Sheikh Mohammed Soud Bashir. Sote wawili tulidawaa na kupigwa na bumbuwazi. Kwa muda kila mmoja alikuwa akimuangalia mwenziwe, na mwisho tulikumbatiana kwa furaha na kwa mapenzi, na kwa kujaaliwa kukutana kama hivyo. Hapo hapo alituchukua nyumbani kwake na huko nilikutana na dada yetu mpenzi, Bi Zuweina Mohammed Rashid. Bi Zuweina naye alipigwa na msangao kwa kuniona na kwa jinsi alivyokuwa hakutarajia kuwa tutaweza kuonana kwa vile alivyosikia kuwa kamata kamata imekuwa kubwa Zanzibar kwa kuuliwa Rais Karume. Alishindwa na kujizuwia na kutokwa na machozi ya furaha. Baada ya kusalimiana na maombolezi haya na yale, tulianza kuzozana kwa suala ya kututaka tuhame huko tulikofikia na tuhamie hapo nyumbani kwao. Sisi tuliona vibaya sana kwenda kuwaambia wale wenyeji wetu kuwa, tunahama kwa sababu tumewapata jamaa zetu. Almuradi, mwisho tulikubaliana kuwa kwa ghafla tusiondoke kwa wale wenyeji wetu bali kidogo kidogo tutazungumza nao kwa njia za kuweza kufahamiana. Na ndivyo, ilivyokuwa, baada ya muda tulizungumza nao, na tuliweza kufahamiana, na tuliondoka na tukahamia kwa ndugu zetu kwa masikilizano na kwa makubaliano mazuri. Na ilikuwa kila baada ya muda tukipita kuwajuulia hali wale waliotupokea kwanza.

Siku za mwanzo tu tulipofika Mombasa, tulianza kutafuta mipango ya safari yetu ya kuelekea Dubai. Lakini, kwanza tulijisalimisha kwa Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa upande wa wakimbizi wa kisiasa, Sheikh Salim Muhasham. Sheikh Salim alitupokea uzuri na la mwanzo alitutengezea warka wa safari wa kutokea nchini (one way travelling document) kutoka Idara ya Uhamiaji ya Kenya, pia alikuwa akitusaidia kwa kila yaliyokuwa yanahitajia. Kwa kupata warka huo, ukaaji wetu wa hapo Kenya ulikuwa wa kihalali. Baada ya muda wa miezi mine tokea kufika hapo Mombasa, Mwenyezi Mungu alinijaalia kutengenekewa na mambo yangu na kuweza kuondoka Kenya mwanzo kuelekea Dubai kabla ya wenzangu wawili. (tulikubaliana kuwa mimi nitangulie). Niliondoka Kenya taarikhi 29 Septemba, 1972 kwa kupata msaada wa safari tokea tikti ya ndege mpaka pesa kidogo za matumizi kutoka katika mfuko wa Umoja wa Mataifa unao shughulikia wakimbizi wa kisiasa (UNHCR).

Kiasi cha saa mbili za usiku wa taarikh 30 Septemba, 1972 nilifika Dubai. Pamoja na miye walikuwepo wakimbizi wenzangu wengine, watoto wa Sheikh Kassim Amour Barwani na wa Sheikh Ahmed Issa Barwani. Tulipofika kiwanja cha ndege cha Dubai, tuliukuta umma wa ndugu zetu wa kiZanzibari wakitusubiri kwa hamu kutupokea. Baada ya kumaliza shughuli za Uhamiaji na Forodha hapo, tulitoka nje na huko tulianza kukumbatiana na ndugu zetu, na baada ya kuamkiana, kila mmoja kati yetu alichukuliwa na waliyokuja kumpokea. Mimi kwa usiku huo, nilipangiwa nifikie kwa ndugu yetu (aliyekuwa wakati huo ndiye Rais wa Jumuiya ya Wazanzibari "Zanzibar Asociation"), Seyyid Hashim AbdulMuttalib Hashim. Kulipokucha, yaani siku ya pili yake nilichukuliwa na ndugu yetu mwengine, Sheikh Abdalla Ali kwa majina ya umaarufu hujulikana Abdalla Baba au Abdalla Nura. Huko kwake ndiko nilikoishi kwa muda mrefu. Kila jambo langu lilikuwa hapo.

KULETA AHLI ZANGU DUBAI Tokea siku niliyofika Dubai, fikra zangu, mawazo yangu na ndoto zangu zilikuwa ni kufikiria njia za kuwaleta Dubai mke wangu na wanangu ili tuishi pamoja. Uzito haukuwa juu ya kuwapatia njia ya usafiri bali juu ya kuweza kuwaondoa Zanzibar. Baada ya mimi kutoroka katika nchi yangu, ahli zangu waliwekewa vikwazo vikubwa vya kuwazuwia kuondoka kwa njia yoyote. Wakati ulipofika, Mwenyezi Mungu aliteremsha Rehema Zake. Kama msemo wa nzi, "Ukiujuwa huu, naujuwa huu". Taarikhi 28 Disemba, 1976 ahli zangu wote tokea mke wangu mpaka watoto wangu walifika Dubai kwa kupata msaada wa Umoja wa Mataifa (UNHCR). Namshukuru Mwenyezi Mungu, hivi sasa tunaishi pamoja. Watatu kati ya watoto wangu wameshatuletea vijukuu vya kucheza nao. Namuomba Mwenyezi Mungu awakuze, kwa raha na furaha na atuletee na wengine kwa wao, na kwa waliyokuwa bado hawajajaaliwa kutuletea.

69

Hapa nimefikilia kikomo cha kuyaeleza niliyokuwa yamenikaa moyoni kuwaeleza wananchi wenzangu. Lakini khasa wale chipukizi zetu ambao kwa kutokuujuwa ukweli wa yaliotokea katika nchi yao, tangu kuanza kwa harakati za siasa na mpaka kufikishiwa tuliyofikishiwa kwa hayo yenye kuitwa mapinduzi, wakidanganywa kwa kuambiwa na kwa kusomeshwa uwongo mwingi sana. Kwahivyo, huu ndio ukweli wa mambo yalivyokuwa kwa kiasi nilichojaaliwa kukijuwa na kujaaliwa kukielezea. Kama nilivyotangulia kusema, natumai watatokea wengine baada ya kukisoma kijitabu hiki, wataingiwa na mori na kuhisi waajib wao wa kuyaandika yale wayajuwayo na ambayo sikujaaliwa kuyaandika, amma kwa kutokuyajuwa au kwa kuyasahau. Kukamilika ni Kwake Subhanahu Wataala.

MENGINEYO KWA UFUPI MWALIMU NA UISLAMU Kwa muda wa miaka mingi sana Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliweza kufuzu katika kuwalaza usingizi Waislamu wa Tanganyika na baadae wa Tanzania yote kwa jumla, yaani wa Bara na wa Visiwani, kwa kuwatumilia propaganda za Uwarabu na Utumwa. Adui yake mkubwa Nyerere sio Uwarabu bali ni Uislamu. Lau angeweza kwa siku moja, kwa ghafla moja kuuondoa Uislamu katika macho yake, basi asingekawia kufanya hivyo hata chembe. Lakini, Mwalimu kwa vile ni bingwa, wa mipango na ujanja, basi anaelewa uzuri kwamba iwapo atakuwa akiuhujumu Uislamu dhahir shahir, wakati ambapo idadi ya Waislamu Tanzania ni wengi kuliko waliokuwa sio Waislamu, (wanakaribia sabini katika mia {70%} ya wananchi wote) basi hatofuzu juu ya lengo lake la kuwakandamiza Waislamu. Kwahivyo ndio daima dawamu anatumia ubingwa wake kwa kuelekea kwenye lengo lao. Waislamu wa Tanganyika ndio waliyompa Nyerere umbele kwa vile walikuwa na niya safi ya kutaka maendeleo ya nchi yao. Haikuwapitikia hata chembe kuwa wanachukua silaha na kumpa adui aitumie kwa kuwauwa wenyewe. Mara tu baada ya Nyerere kupata nguvu za kisirikali, alianza polepole kuwaweka upande waongozi wote wa Kiislamu. Alimuanza Sheikh Suleiman Takadiri kisha alimpikia jungu Cheif Said Abdalla Fundikira. Baada ya hapo aliwaandama Sheikh Said Tewa, Sheikh Zubeir Mtemvu, Sheikh Ali Mwinyi Tambwe, Bibi Titi Mohammed na wengineo wengi. Hawa wanatosha kuwataja miongoni mwa waongozi wazalendo wa TANU na serikali yake ambao Mwalimu amewafikishia aliyowafikishia, akiamini kuwa hawa sio katika yeye; damu yao mbali na damu yake. Hawa ni watu wa kauli moja sio kumi na moja!

Kila walivyozidi kubanwa Waislamu katika kila kipembe, tokea katika Taalimu ya Juu mpaka katika nafasi za daraja ya juu, serikalini, viwandani na kote, ndivyo walivyozidi kupewa fursa hizo wananchi wenzao wasiokuwa Waislamu. Kwa kufikishwa wao (wasio kuwa Waislamu kwa wingi zaidi) katika fursa zenye maana na uzito inampelekea mtu asiyeijuwa hali ya nchi ilivyo kwa hakika, akadhania kuwa Waislamu katika Tanzania ni kidogo, kinyume na hakika ilivyo. Wakati wowote Mwalimu Nyerere anapoutaja Uwarabu, makusudio yake ya ndani ni Uislamu. Kwa bahati mbaya, kiasi cha wakati kwa kutokufahamu kuwa mwenziwao anaikusudia Dini yao kwa kutumilia mwavuli wa Uwarabu na Utumwa aliweza kuwafanya Waislamu wenyewe wakawa wanampigia makofi na vigelegele anaposema hivyo.

Wakati Tanganyika ilipopata Uhuru, taarikh 9 Disemba, 1961 Makanisa yalitengeneza beji maalumu zilizokuwa zimeandikwa, "Maria Mtakatifu, Ubariki Uhuru wa Tanganyika". Beji hizo zilivaliwa na Wakristo na baadhi ya Waislamu wengi wa Tanganyika, na hata baadhi ya Waislamu wa Zanzibar (waliyokuwa wafuasi wa Chama cha AfroShirazi). Kama nilivyo tangulia kusema, Tanganyika Waislamu ni wengi kuliko Wakristo, lakini katika sherehe ya siku ya kuupokea Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Muingereza hiyo 9 Disemba, 1961 kwanza alipanda Kasisi wa Kikristo kuutakia kheri na baraka Uhuru wa Tanganyika, baadae ndio alipanda Sheikh wa Kiislamu. Yoyote aliyeyaona hayo, bila ya shaka aliondoka na fikra kuwa Wakristo ndio wananchi wengi katika Tanganyika. Bali wengine hata wamefika kuamini, na wengine bado mpaka hivi sasa wanaamini kuwa Tangaynika ni nchi ya kiKristo na hali ya kuwa sivyo hivyo hata kidogo. Isitoshe, kutokana na mazingara ya Nyerere wakati wa utawala wake, bali hata baada ya kustaafu kwake (kunakoitwa kustaafu, ilivyo khasa ni kupanga na kuamrisha mambo yote muhimu ya uwendeshaji wa nchi akiwa nyuma ya pazia), bado inaonekana kuwa Ukristo (nakusudia dini, sio watu) una nguvu za juu kwa sababu ndio wenye wafuasi wananchi wengi zaidi. Ikafichika hakika kuwa sababu ni nguvu za Dola ambazo ndizo zinazoupa huo Ukristo umbele, utukufu na umuhimu na kuwanyima nafasi sawa wananchi wengine kwa sababu ya imani yao ya dini, ni Waislamu!

70

Nyerere miongoni mwa mipango yake yakutaka kuudhofisha Uislamu, ameleta jambo ambalo kwa kutofahamu vitimbi na ujanja wake, hata Waislamu wenyewe nao wamelikubali. Ameleta nyimbo yakuwa "SERIKALI YA TANZANIA HAINA DINI". Hii ni fimbo, fimbo ambayo amekusudiya kuwapigia Waisilamu wasiweze kufurukuta katika maendeleo yao. Bali zaidi wasiweze kuendeleza Dini yao katika nyanja mbali mbali kama vile, kushirikiana na Waislamu wenziwao wa sehemu zenginezo za ulimwengu, wasiweze kujiuunga na Vyama vya Kiislamu viliopo katika ulimwengu, bali hata vya hapa hapa Afrika Mashariki. Fimbo hiyo iwazuwiye Waislamu wasiweze kutafuta na kutekeleza mipango ya maendeleo yao khasa, bali na ya wananchi wenzao kwa jumla, kama vile kuasisi na kuendesha vyuo vya taalimu ya Kiisilamu na vya masomo mengineyo, huduma za utibabu, mipango ya maisha na mengineo mfano wa hayo. Mfano mzuri wa kila Muisilamu kuuzingatia juu ya mbinu za Mwalimu katika kuupiga vita Uislamu ni huu uliyotokea hivi karibuni (katika robo ya mwisho ya 1993) wa Serikali ya Zanzibar kutaka kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu "Organization of Islamic Conference" (OIC). Nyerere kwa chuki zake za Uislamu, alishindwa kuficha kucha zake juu ya suala hili, alimwambia Raisi wa Zanzibar, Sheikh Salmin Amour achaguwe baina ya Uraisi, muungano au OIC. Na jengine ni la kuvunjwa East African Muslim Welfare Society, na pia la kuvunjwa African Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT).

Yote haya yamefanyika katika utawala wa Nyerere, bali lenye kuhuzunisha ni kuwa mote humo aliwatumilia ndugu zetu wanaovaa kanzu kumfanyia kazi yake chafu hiyo. Yeye daima hagusi matope! Tangu katika siasa mpaka katika dini (yote ni dini, hakuna tafauti baina ya dini na siasa au siasa na dini). Mreno wakati fulani alitawala Zanzibar na baadae alikuja Muingereza kwa njia za ujanja kuwa anaihami Zanzibar, bali ni kuitawala. Jarumani alitawala Tanganyika na baadae alikuja Muingereza, wote hao ni Wakristo wakubwa lakini hata mara moja hawajawahi kuingilia katika mambo ya Dini kwa kutaka kubadilisha nyendo za kidini bali hata za kimila za watu katika nchi hizo. Waisilamu walikuwa wakiowana na wakirithiana kwa kufuata mafunzo na sharia ya Dini yao na Wakristo hali kadhalika bali hata Mapagani (watu wasokuwa na dini yeyote) nao walikuwa wakiachiliwa kutumia njia zao za kuowana na kurithiana. Lakini alipoingia Mwalimu alisema, amma miye au Uislamu, lakini Waislamu watakiona kilichomtoa kanga manyoa. Lakini wapi! Mwenyezi Mungu hasimami naye.

Mbinu kubwa iliyochukuliwa kuuvunja nguvu Uislamu katika Tanzania ni huo mtindo wa kunyang'anya mali ya watu kudai ati ni "kutaifisha". Kwa kitendo hicho si kama Umma mzima wa Kiislamu umefilisiwa, bali hata misikiti na madarasa na mayatima. Mashamba ya Saidi na Abdulla amepewa Petro na Paulo na Edington. Juu ya wakfu za Misikiti yamejengwa makanisa. Wakfu za misikiti zimeporwa, lakini wakfu za Makanisa ziko Ulaya na Amerika katika Mabenki zikichuma riba, na katika mashirika makubwa makubwa zikipata faida. Na Waafrika Waislamu kwa ujinga wao wanasherehekea; "Mali ya Umma" "Mali ya Umma!" Haya ni mali ya Paulo na Patro na Juliasi. Na hivi sasa bila ya kificho wanapewa Mataliana. Hao ndio bwana zetu wapya. Wao watasaidia kujenga makanisa kwa fedha za fisadi. Pandu na Jecha wako wapi hapo? Hata hayo yaliokuwa yakiambiwa makombo sasa hayapatikani. Bali hawana ruhusa hata ya kuteka maji au kupita katika ardhi zao wenyewe, za nchi yao, walizopewa hao mabwana wapya! Huyo ndiye Mwalimu na Maendeleo, Ujamaa na Kujitegemea. Huyo ndiye Mwalimu akitekeleza ahadi yake "Amma miye au Uislamu". Wananchi wanapomuona kiongozi yumo kujaribu kuuzuwiya wakati na maji yasijae, basi ni wajibu wao kuchunguwa uzima wa akili ya kiongozi huyo na faida na khasara kwa nchi kutokana na ya hayo ayatendayo.

MWALIMU NA UTUMWA Hili ni jambo la pili ambalo Mwalimu hulitumia katika njama zake za kuupiga vita Uislamu khasa anapokuwa anazungumzia kukhusu Zanzibar na Uwarabu. Mwalimu akizungumza juu ya utumwa lazima auwambatanishe na Uwarabu na Usultani na Zanzibar, kama kwamba jambo hilo halikufanyika popote ulimwenguni isipokuwa Zanzibar tu, na hapana waliyofanya ovu hilo ispokuwa Waarabu tu. Kama inavyojulikana na kufahamika na kila mtu wa kawaida kuwa biashara ya utumwa, zama hizo ilikuwa ni biashara iliyokuwa ikifanywa na ulimwengu wote. Waarabu, Wazungu, Waafrika, Wahindi na makabila yote na wafuasi wa dini zote walikuwa wakifanya biashara hiyo ya kuuza na kununua binaadamu wenziwao. Na iwapo utalinganisha kwa kuangaliya wafuasi wa dini mbali mbali utaona kuwa Wakristo ndio waliyokuwa katika msitari wa mbele kabisa katika kufanya biashara hiyo. Afrika ikitoka bidhaa

71 hiyo, na kwa Wazungu huko Amerika na koloni zao nyengine ikichukuliwa kwa kuendesha mashamba yao na kazi ngumu nyenginezo katika miradi yao mbali mbali.

Watu weusi wote waliyoko Amerika walifikaje huko? Ikiwa hawakupelekwa huko na Wazungu baada ya kununuliwa, Wazungu hao ni wa dini gani ikiwa si Wakristo, au Wazungu hao walikuwa ni Waisilamu!? Mwalimu ameudanganya na ameuchezea Umma wa Waisilamu wa Tanzania kwa muda mkubwa, lakini Alhamdulillahi, Umma wa Kiisilamu uliopo leo Tanzania, umeshamtambua uzuri Mwalimu, kama walivyokwisha tambuwa kuwa Mwalimu anapo taja Uwarabu makusudio yake khasa ni Uislamu na kwa hivyo, Waisilamu wamesha fumbua macho. Katu hawatokubali tena kuzugwa. Hawatokubali kuzugwa na kudanganywa mpaka wakafika kuuwana wenyewe kwa wenyewe kama walivyofanya katika mwaka 1964 huko Zanzibar. Kwa udanganyifu wananchi wa Zanzibar waliambiwa wanaondowa Usultani na Uwarabu, kisha wakauliwa wangapi waliokuwa si Waarabu na wala hawana makhusiano yoyote na Usultani, lakini walikuwa Waumini. Wangapi waliouliwa baada ya hayo mavamizi (miongoni mwa niliowataja mwanzo) sio Waarabu, Othman Sharif, Mdungi Usi, Jaha Ubwa, Saleh Saadallah, Abdulla Kassim Hanga, na wengine wengineo. Wangapi miongoni mwa hao wenye kuitwa Waarabu japo kuwa wamefanya maovu katika hiyo hiyo serikali ya mavamizi hawakuguswa, bali walihifadhiwa na kutunzwa.

Jambo muhimu la kuzingatiwa kukhusu suala hilo la utumwa, na sio kuwa Mwalimu hayajui hayo, laa, anayajuwa vizuri lakini, kwa sababu azijuwazo mwenyewe hataki kuyataja hayo. Jambo la kuzingatiwa ni kuwa katika mwaka 1822, Seyyid Said Bin Sultan aliyekuwa Mfalme wa Oman na Zanzibar wakati huo, alipiga marufuku biashara ya utumwa baina ya mamlaka zake zote na nchi za Kizungu. Na katika mwaka 1845, alizuwiya kabisa kusafirishwa watumwa kutoka Afrika Mashariki kupelekwa Oman. Katika mwaka 1872, Seyyid Barghash aliyekuwa Sultan wa Zanzibar wakati huo, na yeye vile vile alipiga marufuku kabisa biashara ya utumwa. Madola ya nchi za magharibi (ambao ni Wakristo) walitangaza kuzuwia biashara ya utumwa dunia nzima baada ya hicho kinachoitwa "Brussels Act of 1890". Utaona kuwa biashara ya utumwa imepigwa marufuku ulimwenguni na hao wazungu baada ya miaka 18 tokea kupigwa marufuku biashara hiyo huko Zanzibar.

Katika mwaka wa 1897 Mfalme Seyyid Hamoud, yeye aliondowa kabisa utumwa katika Zanzibar na tokea wakati huo hadi hii leo haukuwepo tena utumwa Zanzibar. Katika Kenya, Waingereza wao walipiga marufuku biashara ya utumwa katika mwaka 1912. Ni kitambo cha miaka 15 tokea Zanzibar kuundoa utumwa kabisa nchini. Ama katika Tanganyika, Majarumani, wao waliendelea na utumwa mpaka wakati waliposhindwa katika vita mnamo mwaka 1918. Waingereza ambao ndio waliyowashinda Majarumani katika vita hivyo, wao waliendeleza utumwa katika Tanganyika mpaka mwaka 1920 ndipo walipouzuwia kabisa. Kwahivyo, utaona kuwa utumwa uliendelea kuwepoTanganyika kwa muda wa miaka 23 baada ya kuondolewa kabisa Zanzibar. Je Mwalimu, wapi panafaa kuitwa penye "Kitovu cha Utumwa".

Utumwa uliyokuwepo na ambao ni mbaya zaidi kuliko hata huo utumwa uliyokuwepo miaka hiyo, ni huu utumwa uliyoletwa na Nyerere pamoja na Karume. Utumwa wa kuwafunga Wazanzibari (bali pia Watanganyika) katika magereza bila ya kuwa na makosa ya namna yoyote na bila ya kuwapeleka katika mahakamani. Baada ya kuwafunga kidhulma namna hivyo tena wakaongezewa dhulma nyengine kwa kufanyishwa kazi ngumu kuanzia saa moja ya asubuhi mpaka saa 12 za magharibi. Na wengine wakawekwa katika magereza maalumu ya kuwatesea wananchi bila ya kuwapa chakula, na kwa kuwapiga na kwa mateso ya namna nyengine ambayo mengine hata kuyasema ni uchafu. Huo ndio utumwa uliyokuwepo Zanzibar wakati wa ufalme wa Karume na AlHaj Aboud Jumbe Mwinyi. Kwa vile Mwalimu Nyerere ndiye aliyekuwa Rais wa Tanzania, basi ni yeye anayekhusika moja kwa moja na utumwa huo uliyokuwepo Zanzibar. Mbona utumwa huo, Mwalimu hatukusikii kuutaja? Bali hata hao wanaokusaidia kusema, haya yako hawayasemi!!

POROJO LA MITAANI Baada ya kufuzu kwa hayo yenye kuitwa, "Mapinduzi", uwongo mwingi sana ulikuwa ukivumishwa dhidi ya Serikali ya Hizbu na ZPPP kwa makusudio ya kutaka kuondoa imani za wananchi juu ya waongozi wao. Wazushi walijaribu kuupanga uwongo wao hata ilifika hadi ya baadhi ya wananchi kwa

72 kutoufahamu ukweli na wakati mwengine kwa imani dhaifu kukaribia kuyaamini hayo yaliyokuwa yakivumishwa, na wengine waliyaamini.

Porojo kubwa lililokuwa likisemwa na hao wazushi, ni kuwa waongozi wa Serikali ya Hizbu na ZPPP walikataa msaada wa ulinzi waliyopewa na Serikali ya Kingereza. Na wengine wakisema Serikali ya Jamhuri ya Misri ilitaka kuwapa msaada wa kijeshi kwa ajili ya ulinzi wa nchi lakini, waongozi wa Serikali ya Hizbu na ZPPP walikataa msaada huo na badala yake waliomba wapewe wapiga vinanda na wachezaji nachi wa kiMisri!! Na wengine wakisema kuwa Ali Muhsin alikubaliana na Karume kwa siri katika mipango ya kufanywa mapinduzi ili ipate kuondolewa Mfalme. Nasema kuwa yote hayo yaliokuwa yakisemwa au ikiwa yanasemwa mpaka hivi sasa, basi yote hayo ni maneno ya uwongo tena uwongo mkubwa. Serikali ya Kiingereza wao ndio waliyokataa kuandikiana mkataba wa kuisaidia Zanzibar katika kuweka usalama, kwa kudai kuwa wakishatoka hawataki jukumu lolote. Hayo walikataliwa Mawaziri bali alikataliwa hata Mfalme. Serikali ya Kiingereza (kwa sababu zao ambazo zimedhihirika baadae) haikutaka kuipa msaada wowote wa ulinzi Serikali ya Zanzibar juu ya kuwa Uingereza hiyo hiyo ilifanya mikataba wa misaada ya kijeshi pamoja na Kenya, Uganda na Tanganyika. Muingereza ameitawala Zanzibar (kwa kutumia ujanja wake wa kuwa akiihami) kwa mafahamiano na usalama, kwa muda wa miaka 73 (1890 1963). Muingereza huyo huyo mwezi mmoja tu tokea kuondoa himaya yake, kwa ridhaa na bila ya hata mmoj kati yao (hao watawala) kuguswa au kusukumwa, amekataa kuipa msaada nchi na serikali ambayo ameishi nayo muda wote huo. Tafauti ni kuwa serikali hiyo ilipovamiwa na kuhitajia msaada ilikuwa huru, ikiongozwa na Hizbu na ZPPP.

Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje walimkabili Balozi wa Kiingereza, Mr. Crostwaith, aliyekuwepo Zanzibar siku hiyo yaliyofanywa hayo yenye kuitwa "Mapinduzi", kumtaka msaada wa kijeshi uje kuzuia fujo lililokuwa likifanywa na wageni waliyoletwa kwa makusudi ya kuivamia nchi. Bwana Balozi huyo alikataa ombi la Serikali ya Zanzibar, Serikali ambayo imechaguliwa kwa voti za wananchi. Alikataa kwa kutumia mipango ya kusema kuwa, "Leo ni Jumaapili, haitokuwa rahisi kuweza kuipata Serikali ya Kiingereza!" Jee ndio ifahamike kuwa Jumaapili, Serikali yote ya Kiingereza huwa imelala au imekwenda vua samaki!? Mbona taarikh 20 Januari, 1964 siku nane tu tokea kufanyika mavamizi Zanzibar, Jeshi la Tanganyika lilipofanya majaribio ya mapinduzi, Serikali hiyo hiyo ya Kiingereza kwa muda mchache sana waliweza kulipeleka jeshi lao na kuzuwia ghasia pamoja na kumrejesha Nyerere na uraisi wake? Nyerere ambaye kwa matokeo ya ghasia hizo alikuwa ameshakimbia na kujificha kwa kuyanusuru maisha yake. Sababu kubwa na khasa ni kuwa sisi hatukuonekana katika fikra na mipango yao kuwa ni "watoto wazuri", bali Mwalimu ni "mtoto wa nyumbani". Hayana shaka haya!

Kukhusu msaada wa ulinzi kutoka Serikali ya Misri, kuwa Serikali ya Hizbu na ZPPP ilikataa, na hilo pia si kweli. Jambo hilo la ulinzi kutoka katika Serikali ya Misri lilizungumzwa kwa urefu baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Misri. Kwa natija ya mazungumzo hayo khatua mbali mbali ilikuwa zichukuliwe kufuatana na utaratibu na njia za kisirikali. Kwa kutokana na kupenya kwa mipango hiyo na kuwafikia "wakuu wa ulimwengu" ndipo walipo mtumilia kibaraka wao naye akawatumilia vibaraka vyake kuharakisha mbio mbio kuivamia Zanzibar na kuiondoa Serikali ya halali iliyokuwa imechaguliwa na wananchi wenyewe kwa uchaguzi wa halali na wa kidemokrasi wa "One Man One Vote". Suala la waimbaji na wachezaji halikukhusika na ulinzi wa nchi, hayo ni mambo mawili mbali mbali. Ama suala la Ali Muhsin kuwa alikubaliana na Karume kufanya mapinduzi kwa sababu ya kumuondoa Mfalme, hayo sio kama ni maneno ya uwongo tu, bali ni maneno ya ujinga. Na kufika hadi mtu kusema maneno kama hayo, ima amepungukiwa na akili au kwa ajili ya kutokuifahamu katiba ya nchi ilivyokuwa kukhusu suala la kuwepo au kutokuwepo kwa ufalme katika Zanzibar.

Jambo la kushangaza ni haya maneno yao yenye kugongana, nayo ni kuwa huku inasemwa Ali Muhsin na serikali yao ya ZPPP/ZNP ni ya Kisultani na huku kunasemwa kuwa Ali Muhsin alishirikiana na Karume kumuondoa Mfalme. Lakini Karume baada ya kufuzu kwa 'mapinduzi' alimgeukia Ali Muhsin na badala ya kushirikiana naye katika kuendesha Serikali, amemtia gerezani! Sasa, tushike wapi? Upande mmoja Ali Muhsin anaambiwa ni mtu mwenye kupenda utawala wa kiSultani na vyama vya Hizbu na ZPPP na serikali yao vilikuwa vya kiSultani. Na upande mwengine kunasemwa kuwa, Ali Muhsin alishirikiana na Karume katika mipango ya kumuondoa Sultani. Sasa tunaemewa hatujui tumuhukumu vipi Ali Muhsin huyu, kuwa akiupenda uSultani au alikuwa hautaki uSultani. Ilivyokuwa maneno haya yanagongana

73 wenyewe kwa wenyewe hadi hii, ni dalili wazi kuwa ni maneno yasiokuwa na msingi wala ukweli. Ni porojo la mikahawani. Inataka ifahamike kuwa Ufalme wa Zanzibar ulikuwa ni Ufalme wa Katiba na Mfalme wenyewe naye alikuwa Mfalme wa Katiba. Ni maarufu kua chama cha AfroShirazi hakimtaki Mfalme. Basi ingekuwa na serikali ya kina Ali Muhsin nayo haimpendi Mfalme nini cha kuzuia Baraza ya Taifa isipasishe kwa pamoja kumuondoa Mfalme kwa kura.

Ama hao wasemao kuwa Karume alimpa Ali Muhsin uwaziri katika Serikali yake yenye kuitwa ya "Mapinduzi", hao tena pahala pao pa kufaa kuishi ni katika hospitali ya wendawazimu, (Kidongo Chekundu kwa Zanzibar). Ikiwa kupewa cheo cha uwaziri ni tunza ya kushirikiana na Karume katika mauwaji ya wananchi na kumuondowa Mfalme, kisha kuyaita mauwaji hayo "mapinduzi", basi vyema, natuikubali, fikra hiyo. Kwahivyo basi, ni Babu na wenziwe ndiye aliyeshirikiana na Karume katika kumuondoa Mfalme sio Ali Muhsin, kwani ni yeye Babu ambaye baada ya kufuzu hayo 'mavamizi' alifanywa Waziri wa Mambo ya Nje! Mambo sio hayo tu, wapo vilevile wenye kusema kuwa Ali Muhsin aliambiwa AfroShirazi na Makomredi wanapanga kuipindua Serikali lakini Ali Muhsin amedharau na amejibu, "Kwani Serikali ni kisahani cha chai?" Ukiuliza ni nani huyo aliyekwenda kwa Ali Muhsin kumwambiya maneno hayo na akajibiwa hivyo, kila aulizwae, jawabu ni hilo hilo kuwa, "Mimi nimewasikia watu wakisema". Na katika suala hili, wengine utawasikia wanasema aliyekuwa amesema hivyo, Ali Muhsin, na wengine husema Juma Aley na wengine, Dr. Idarus Baalawy, mradi kila apendaye kuvurumisha uwongo wake, huuvurumisha bila ya kiwewe chochote!

Sheikh. Ali Muhsin alikuwa ni mwongozi wa chama na uwongozi wenyewe sio kuwa ulikuwa kwa kuchaguliwa kuwa awe mwongozi, laa, uwongozi wake ulitokana na mapenzi tu ya umma wa Hizbu wenyewe mpaka kufika kumwita "Zaim", yaani kwa Kiswahili, Mwongozi. Hata hivyo, Ali Muhsin hakuwa mwongozi wa Serikali, bali alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Mwongozi wa Serikali alikuwa Sheikh Mohammed Shamte Hamad. Usalama na Ulinzi ulikuwa chini ya Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Sheikh Salim Kombo. Waziri Msaidizi wa Mambo ya Ndani ni Sheikh Rashid Hamad. Kwahivyo, Ali Muhsin hakukhusika na kazi ya Ulinzi na Usalama wa nchi wakati huo.

Waziri Mkuu Sheikh Mohammed Shamte mara tu baada ya kupata khabari za kuwa maAfro na maKomredi wanajitayarisha kufanya michafuko kama yaliyofanywa Juni, 1961 hapo hapo alichukuwa khatua za kiserikali. Aliwaita wakuu wa Polisi na wakuu wa Idara ya Usalama ambao ndiwo waliyokuwa wamekhusika na usalma na ulinzi wa nchi na kuzungumza nao khabari zilizokuwepo nchini. Wakuu hao walimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa wanazo khabari hizo, nao wamesha jitayarisha kukabiliana na michafuko ya namna yoyote ikiwa itatokea maadamu haitokuwa yenye kutoka nje ya nchi. Kwa mwenendo wa Serikali za kidemokrasi, Waziri Mkuu kwa khatuwa hiyo aliyochukuwa amekuwa ametekeleza wajibu wake, yaliyobakia ni juu ya waliyokhusika na utekelezaji.

Ikiwa palifanywa dharau zozote katika masala haya hata yakatokea yaliotokea, na ikiwa kunastahiki lawama, na iwapo kulaumu kuna faida, basi lawama hizo ni kwa waliyokuwa wamekhusika na utekelezaji juu ya ulinzi wa nchi, si kwa Waziri Mkuu, wala kwa Mawaziri wake. Wao, walikuwa ni watungaji na wapangaji wa sheria na siasa ya nchi, kwa kufuatana na misingi na katiba ya nchi, hawakuwa watekelezaji, watekelezaji walikuwa wengine. Demokrasi hairuhusu "kuvaa kofia mbili" katika uendeshaji wa mambo ya nchi, yaani kofia ya utungaji wa sheria na kofia ya utekelezaji wa sheria. Ikiwa lawama ni kuwa kina Ali Muhsin walihishimu demokrasi, basi hilo ni suala la kuzingatiwa na kudurusiwa kwa namna yake.

Ukweli (lakini iwe ni ukweli) inafaa usemwe, lakini si kwa ajili ya kulaumiana tu, kwani huu si wakati wa kulaumiana, huu ni wakati wa kushirikiana katika kutafuta njia za busara, za usalama na za siasa katika kuijenga nchi yetu kwa kutokana na majaraha ya mitarimbo ilyopigwa katika kila sehemu yake ya maendeleo. Tusikae tukiomboleza tukililia maziwa yaliokwisha mwagika na wakati unatupita na madhara yanazidi kila leo, bali kila saa na kila dakika. Wajibu wetu tuwe kitu kimoja tuiokowe nchi yetu, kwa munufaa ya vizazi vyetu. Jukumu liko juu ya mabega ya kila mmoja wetu, na sote ni wenye kuhesabiwa kwa masuliya haya mbele ya Mwenye Enzi Mungu kama tutavyokuwa daima tunahisabiwa na vizazi vyetu.

74

DEMOKRASI YA VYAMA VINGI (MULTIPARTY DEMOCRACY) Kulazimika kuundwa vyama vingi vitavyokuwa vinazozana sio makusudio khasa ya kuwepo kwa Multi Party Democracy. Na mtindo wa wachache kutawala wengi au wengi kutawala wachache sio makusudio khasa ya demokrasi ya kweli. Linalo takikana ni kuondolewa mwendo wa kupigwa marufuku uasisiji wa vyama baada ya kuwepo hicho kimoja tu cha watawala. Miongoni mwa Haki za Binaadamu ni kuwa wananchi wanayo haki ya kuweza kuasisi au kujiunga au kutokujiunga na chama chochote. Lililokuwa kinyume na Haki za Binaadamu ni kuwanyima wananchi haki zao za kiwananchi kwa kutojiunga kwao na chama tawala.

Hakika hata ikiwa mwananchi mmoja tu itafika kuwa hana haki sawa na mwananchi mwenziwe katika nchi yake kwa sababu hayumo katika chama tawala au kwa sababu yumo katika chama chengine (sio chama tawala), au kwa rangi yake au kabila yake au asili yake au kwa dini yake basi hapo misingi ya kidimokrasi haikutekelezeka. Kinyume cha hivyo ndiyo demokrasi ya kweli. Demokrasi ya chama kimoja kama ilivyokuwa (au ilivyo hadi hii leo, kwani hivyo vyama vyengine bado havina kauli yeyote) katika Tanganyika na Zanzibar hiyo si demokrasi hata kidogo. Bali ni utawala wa wachache kuwatawala wengi uitwao, "OLIGARCHY". Wenyewe viongozi wa CCM wanadai kuwa chama chao kina wanachama milioni mbili, katika wananchi milioni 26! Naiwe madai hayo ni kweli, lakini basi, hao milioni mbili wenyewe hawana kauli yoyote yenye kusikilizwa , lao wao ni kufuata tu na kuitikia, "Ndivyo Mzee". Kwa hakika ni udikteta wa mtu mmoja ambao huitwa, "AUTOCRACY". Lakini vilevile, sio maana ya demokrasi kuwa ni utawala wa waliyo wengi kuwadhili au kuwatawala waliyo wachache. Demokrasi ya kweli ni utawala wa wananchi, uliochaguliwa na wananchi, kwa maslahi ya wananchi. Kila mwananchi awe na haki sawa na mwenziwe, sauti yake inasikilizwa na inazingatiwa katika uendeshaji wa nchi yake. Bali hata ambao si wananchi nao wana haki zao katika demokrasi ya nchi.

VIPI KUIFIKILIA DEMOKRASI Mipango mizuri ya kuweza kupatikana kwa demokrasi yenye kukubalika ni kufuata mipango ya Proportional Representation. Yaani kuchaguliwa kwa mujibu wa idadi ya kura. Kwa mpango kama huo, hata vyama vidogo vidogo vitaweza kuwa na wajumbe wao katika Baraza ya Taifa (Bunge). Na kwa njia kama hizo, sauti za wachache nazo pia zitaweza kusikilizana katika mwendo wa uendeshaji wa Serikali ya nchi yao. Hapana shaka waliyokuwa wengi, sauti zao nazo zitakuwa nyingi, lakini na waliyokuwa wachache, haitowezakana kuwaziba vinywa kabisa. Na amuwo litalokuwa na uzito itakuwa ni amuwo la Parliament (Bunge), wala sio la Rais.

Mwendo kama huo, "Parliamentary Propotional Representation" unatumiwa na nchi nyingi ulimwenguni, miongoni mwao ni Sweden, Denmark, Norway, Belgium, Holland, Austria, Switzerland, Ujarumani. Kwa mujibu wa Katiba za nchi hizo, Rais au Mfalme wa nchi huwa hana madaraka ya kuendesha serikali bali huwa na cheo cha heshima tu. Madaraka huwepo juu ya Bunge kwa wasta wa Waziri Mkuu ambaye anakuwa chini ya hilo Bunge au Baraza la Wawakilishi. Mwendo huu unafaa sana kwa nchi zilizokuwa ndio kwanza zinajigomboa kutokana na udikteta wa Serikali ya chama kimoja au ya mtu mmoja, au inayotoka katika ukoloni. Bali mwenendo huu unafaa zaidi kwa nchi zilizokuwa bado zinazo mabakio ya khitilafu za kikabila au kitaifa au kidini, au zilizomo katika mvutano wa vyama vya kisiasa ambavyo bado havijaweza kuhishimu demokrasi na kuhishimu natija ya chaguzi huru. Muhimu zaidi ni kuwa mwenendo wa aina hii utasaidia katika kuepusha uroho wa madaraka, kama utavyoleta kushirikisha umma wote (kupitia wawakilishi wao) katika dhamana ya "kutenda na kuhesabiwa".

Sisi wananchi wa Zanzibar tumetafunwa na nyoka, basi lazima tuwe na khofu hata tukiuona un'gongo. Tufanye kila tuliwezalo katika kujiepusha na bughdha za zamani. Wenzetu wa nchi za kiMagharibi mpaka hivi leo hawajasahau kuwa Unazi na Ukoministi ndiyo uliyokuwa adui yao mkubwa. Basi na sisi tusisahau kuwa, Ugozi, Ukabila na Unvensiremosi na Saguru kuwa ndivyo vilivyotuhilikisha. Kwa yaliotupata kutokana na maradhi hayo ni wajibu wetu tufanye mwisho wa uwezo wetu tujikinge na maradhi hayo. "Mumini Hatafunwi na Nyoka Pango Moja Mara Mbili"

75

SHUKRANI Nachukua fursa hii kupitia katika kijitabu hichi kwa kuwashukuru wote waliyosimama pamoja na mimi na wenzangu kwa kutufanyia kila misaada mikubwa na midogo katika kuturakhisishiya mipango ya usafiri wetu tokea kutoka Zanzibar hadi kufika Mombasa na kutoka Mombasa hadi kufika Dubai. Kwa ajili ya sababu fulani fulani, sina budi na kujizuwia kuyataja baadhi ya majina ya wafadhili wetu khasa kwa wale waliyokuwa wamejitolea katika kutupatia chombo cha kutuvusha kutoka Zanzibar hadi kutufikisha katika sehemu fulani za pwani ya Tanganyika. Na zaidi kwa kutupa mwenzao, wa damu yao, kufuatana na sisi katika njia za khatari kama hizo. Vile vile silitaji jina la ndugu yetu mpenzi aliyetupokea tulipofika Tanga, na kutuweka katika nyumba yake pamoja na kutukhudumia kwa kila la lazima kwa binadamu. Pia nalizuia jina la kijana wetu aliye jihatarisha maisha yake katika kutusaidia kwa kutupitisha katika njia za siri za misituni mpaka akatufikisha Mombasa salama usalmini. Kwa wale ifaayo kuwataja, kwa nafsi yangu na kwa niaba ya wenzangu tuliofuatana katika safari hiyo, nitaanza kwa kumshukuru Sheikh Mohammed Soud Bin Ali Bin Bashir pamoja na ukoo wote wa Sheikh Soud Bin Ali Bin Bashir wa Mombasa, Kenya. Ukoo huu ndio uliyotupokea hapo Mombasa na ndio uliyotushughulikia kwa kila jambo letu. Kwa muda wote, tuliyoishi pamoja na ukoo huo, haijapata kutokea hata mara moja kuhisi kuwa zipo khitilafu zozote za kasoro katika kuishi na sisi. Si kwa kuandika wala si kwa kutamka bali sitoweza hata kidogo kufikilia kiwango cha kuweza kutoa shukurani zangu juu ya ukoo huo hata zikaweza kufikilia thamani inayo wastahikia. Naelewa uzuri kuwa wao wenyewe hawatopenda kutajwa kwa kushukuriwa kutokana na kheri walizotufanyia lakini nawaomba wanisamehe kwani si rahisi kuweza kujizuwia na kuwataja. Namuomba Mwenyezi Mungu aupe ukoo huo kila mafanikio hapa duniani na kesho Akhera Amin.

Vilevile ni fakhari yangu kumshukuru mzee wangu mahabub, Sheikh. Nasser Bin Salim AlRiyami. Mzee wetu huyu aliacha kila raha na kazi zake na kujitolea kwa nafsi yake na chake kwa kuwatumikia wananchi wenzake waliyokuwa wakifika Mombasa katika mipango yao ya kwenda Arabuni. Nathubutu kusema kuwa, lau kama si juhudi zake, basi mambo mengi kukhusu mipango ya safari ya kuelekea Arabuni, yasingeweza kutekelezeka kwa urahisi. Mwengine mwenye kusitahiki shukurani zangu, bali zetu, ni Sheikh Salim Muhasham. Bwana Muhasham ndiye aliyekuwa mjumbe rasmi wa Umoja wa Mataifa katika sehemu yenye kushughulikia wakimbizi wa kisiasa. Mbali yakuwa alikuwa akitekeleza kazi yake, bali alikuwa akifanya zaidi ya kazi yake katika kuwasaidia ndugu zake waliyokuwa wakikimbia Zanzibar katika wakati huo.

Shukurani zangu hazitoweza kukamilia ikiwa sikumfikishia Bibi Sharifa Ahmed AlBusaidy. Bibi huyu alijitolea kwa wakati wake, usiku na mchana, kuwatumikia wananchi wenzake waliyokuwa wamefika kwake bila ya kutizama huyu nani na huyu nani, au kuwa anamjuwa au hamjuwi. Kila msaada aliyoweza kusaidia tokea wa fedha mpaka wa utumishi alisaidia kwa furaha na bashasha. Namuomba Mwenyezi Mungu awape wote hao kila ya kheri duniani na Akhera. Amin. Na mwisho, bali sio mwisho kabisa; napenda kuishukuru Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Wazanzibari ya Dubai iliyokuwepo wakati huo, yaani kina Seyyid Hashim AbdulMuttalib Hashim pamoja na Kamiti yake yote, kwa mapokezi na misaada mema waliyokuwa wakiwapa nduguzao wakimbizi wakati walipokuwa wakifika Dubai. Nitakuwa mwizi wa ihsani ikiwa nitawacha kumshukuru ndugu yangu Seyyid Mohammed AbdulMuttalib Hashim kwa juhudi zake za kuniombea na kupatia pasipoti ya Dubai na baadae ya United Arab Emirates.

Na kwa kufikia kikomo cha shukurani zangu napenda kuzifikisha kwa ndugu yangu mpenzi Sheikh Abdalla Ali, maarufu Abdalla Baba au Abdalla Nura, pamoja na aila yake yote kwa mapokezi yao na kwa wema wao waliyonitendea nilipofika Dubai. Kwani wao ndio waliyonipokea na kukaa na mimi nyumbani kwao mpaka Mwenyezi Mungu aliponiwezesha na mimi kupata pahala pangu. Namuomba Mwenyezi Mungu awape wao na vizazi vyao kila la kheri hapa Duniani na kesho Akhera, Amin. Vilevile shukrani zangu za dhati kwa wote waliosaidia tangu kwa kunishajiisha zaidi katika kukiandika kijitabu hichi na wengine wote waliosaidia kwa njia mbali mbali mpaka Mwenye Enzi Mungu akajaaliya kijtabu hiki kikaweza kutoka. Mwenye Enzi Mungu ajaaliye, kisomwe, kifahamike na ipatikane faida. KWA KUFANYA KAZI KWA NIA MOJA INSHALLAH TUTAFUZU

76