HOTUBA FUPI YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA HAFLA YA UCHANGISHAJI FEDHA KWA AJILI YA UJENZI WA KITUO CHA WANAFUNZI, CHUO KIKUU CHA , UKUMBI WA MIKUTANO WA MLIMANI CITY, TAREHE 18 OKTOBA, 2011

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad;

Waheshimiwa Mawaziri Wakuu wastaafu: Mhe. Jaji Joseph Warioba, Mhe. Cleaopa Msuya, Mhe. Dk. , Mhe. John Samwel Malecela, Mhe. na Mheshimiwa ;

Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri;

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Fulgence Kazaura;

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala;

Waheshimiwa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

Wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

Nianze kwa kuwashukuru waandaji wa shughuli hii ya kihistoria ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kazi nzuri waliyoifanya. Shughuli imefana sana. Ukumbi umejaa. Nafurahi kwamba mmefanikiwa. Nawashukuru kwa heshima hii kubwa ya kunikutanisha na wanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (wana-kaya wenzangu) katika shughuli hii adhimu.

Aidha, nawapongeza viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kubuni mradi huu muhimu na hasa kwa uamuzi wa busara wa kuwashirikisha wana-kaya ya Chuo hiki na Watanzania wengineo wakereketwa wa elimu. Hii ni mara ya kwanza kwa wahitimu wa Chuo Kikuu chetu kikongwe kuliko vyote nchini kukutana kwa shughuli ya uchangiaji wa maendeleo ya taasisi yao iliyowapatia ufunguo mkubwa wa maisha, elimu ya juu.

Aghalabu, tumezoea utaratibu kama huu ukitumika kwa shule za sekondari na hata za msingi. Nafurahi kuona kwamba busara imewaongoza kutumia maarifa hayo ili sisi tulio wahitimu na wafanyakazi wa Chuo hiki tuchangie katika maendeleo yake. Nafurahi pia kwamba mkusanyiko huu umetupa fursa ya kukutana watu ambao tulipotezana miaka mingi. Tunawashukuru sana.

Ndugu Zangu; Wana-Kaya Wenzangu;

Bila ya shaka tunatambua juhudi kubwa zilizofanywa na viongozi wetu waasisi wa taifa, hususan Baba wa Taifa na viongozi wenzake wa Chama cha TANU kabla na baada ya mwaka 1961 na baadae Muungano wa mwaka 1964 za kuendeleza elimu ya juu hapa nchini. Mtakumbuka pia kwamba uamuzi wa busara na wa kishujuaa uliofanywa na Chama cha TANU wa kukabidhi jengo lake ililolijenga kwa nia ya kuwa Makao Makuu yake pale Lumumba ili litumike kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baadaye mwaka 1964 ujenzi ulipokamilika wa majengo katika makao rasmi, ambako kwa sasa panajulikana kama Mlimani, ndipo Chuo kilipohama kutoka mtaa wa Lumumba.

Juhudi hizo zimeleta mafanikio makubwa. Chuo Kikuu kilichoanza na Kitivo kimoja cha Sheria chenye wanafunzi 13 leo kinazo takriban fani zote kuu za kitaaluma na wanafunzi wapatao 16,000. Kwa sasa Vyuo Vikuu nchini vimeongezeka na kufikia 35 vyenye wanafunzi 135,367. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimezaa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine mwaka 1984 na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Muhimbili mwaka 2007. Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia kilikilea kilichokuwa Chuo cha Ardhi hadi kuwa Chuo Kikuu kamili mwaka 2007.

Ndugu zangu, maendeleo makubwa yaliyopatikana na hasa upanuzi mkubwa uliotokea muongo mmoja uliopita katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vimeibua mahitaji mengi mapya. Mengine yamegeuka kuwa changamoto za maendeleo hapo chuoni. Kwa upande mmoja kumekuwepo na mahitaji ya kuboresha mitaala pamoja na ya upatikanaji wa vifaa na kuwa na njia na mbinu bora za kufundishia ili chuo kipate wahitimu watakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya nchi ya wakati wa sasa na miaka ijayo kulingana na mazingira ya dunia tunayoishi yanavyonyumbulika. Aidha, kuna mahitaji yahusuyo kuboresha mazingira ya maisha ya wanafunzi chuoni kuhusu malazi, hali pa kuishi, kujisomea, kupumzikia na kujipatia huduma mbalimbali kama vile chakula, burudani na mengineyo.

Ongezeko kubwa na la haraka la udahili katika Chuo Kikuu katika miaka ya hivi karibuni limefanya mahitaji yahusuyo mazingira ya maisha ya wanafunzi kuwa changamoto kubwa. Kwa upande wa malazi, chuo hakijaweza kuwapatia wanafunzi wote nafasi ya kulala hapo chuoni hivyo kulazimika kujenga hosteli nje ya Chuo huko Mabibo na kununua hosteli ya NBC Ubungo na nyumba za CRDB Kijitonyama. Hata hivyo, bado wapo wanafunzi wengine ambao wamekosa nafasi hata kwenye hosteli hizo na kulazimika kujitafutia wenyewe malazi ya kupanga. Chuo na Serikali wanaendelea kushughulikia suala la kuwapatia wanafunzi malazi mazuri ili wasilazimike kupanga mitaani.

Kwa wale wanaoishi nje ya Chuo wanapokuwepo Chuoni kwa masomo, wanahitaji mahali pa kujisomea, mahali pa kupumzika wanaposubiri vipindi au mahali pa kuzungumza na wenzao au wageni wao wanapowatembelea. Hivi sasa wanazagaa zagaa tu chini ya miti au kwenye corridors. Kwa kweli wanapata taabu hasa wakati wa jua kali na mvua. Wanahitaji mahali pa kupata huduma ya internet - hakuna, wanahitaji mahali pa kupata vinywaji, vitafunio au hata na chakula.

Kuwepo kwa Kituo cha Wanafunzi kutakidhi mahitaji haya muhimu kwa wanafunzi wetu. Kwa kiasi kikubwa adha wanazopata wanafunzi zitapungua hasa kwa wale wanaoishi njie ya Chuo na hata wale wanaoishi Chuoni. Hivyo basi, kupatikana kwake kutaboresha sana mazingira na maisha ya wanafunzi Chuoni.

Kituo hiki si cha ajabu kujengwa duniani. Wale wenzetu mliopata fursa ya kusoma nje au kutembelea vyuo vikuu vya nchi nyingine mtakuwa mnafahamu kwamba ni jambo la kawaida kwa Vyuo kuwa na vituo vya namna hii. Kwa Chuo Kikuu kikubwa na chenye hadhi na historia iliyotukuka kama UDSM kuwa na Kituo cha Wanafunzi ni jambo ambalo lililotakiwa kuwepo miaka mingi nyuma. Tumechelewa nalo.

Naamini sasa wakati umefika kwa Chuo chetu kuwa na kituo cha namna hii ili vijana wetu wanufaike. Wapate huduma nzuri ili wafanye vizuri katika masomo yao na taifa lipate wataalamu walio bora.

Kama tulivyoelezwa, tayari jitihada kubwa imefanyika kufanikisha mradi huu. Wenyewe wanajumuiya ya Chuo wameonesha mfano wa kujitoa, na wamejitoa kweli kweli. Watu wengine, wakiwemo wadau na wahitimu walioko nchini Uganda, pia wameshirikishwa. Tumeambiwa kwamba leo ndiyo zamu yetu sisi wana wa kaya hii na marafiki zetu wa karibu. Ni matumaini yangu kwamba sote tuko tayari kutekeleza wajibu wetu na kuchangia tuwezavyo.

Nawashukuru sana kwa kujitokeza na karibuni sana.