MKUTANO WA PILI Kikao Cha Nne – Tarehe 5 Februari, 2021 (Bunge
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA PILI Kikao cha Nne – Tarehe 5 Februari, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. ASIA MINJA – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, maswali tutaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini sasa aulize swali lake. Kwa niaba yake Mheshimiwa Innocent Bilakwate. Na. 42 Ujenzi wa Vituo vya Afya kwa Nguvu za Wananchi MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. ALMAS A. MAIGE) aliuliza:- Wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wamejitolea kujenga Vituo vya Afya katika Kata za llolangulu, Mabama, Shitagena na Usagari katika Kijiji cha Migungumalo:- Je, Serikali ipo tayari kuanza kuchangia miradi hiyo? 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa wananchi katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini. Hivyo, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuchangia nguvu hizo za wananchi katika kukamilishaji vituo hivyo ili vianze kutoa huduma kwa wananchi. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ukarabati na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo kukamilisha maboma ya majengo ya kutolea huduma za afya yaliyojengwa na wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo ujenzi wake ulisimama kwa kukosa fedha.
[Show full text]