MKUTANO WA PILI Kikao Cha Nane – Tarehe 11 Februari, 2021 (Bung
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA PILI Kikao cha Nane – Tarehe 11 Februari, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunaweza kukaa. Katibu. NDG. STEPHEN KAGAIGAI - KATIBU WA BUNGE: KIAPO CHA UAMINIFU SPIKA: Kiapo cha Uaminifu NDG. BAKARI KISHOMA – KATIBU MEZANI: Waheshimiwa Wabunge, wafuatao waliapa Kiapo cha Uaminifu 1. Mhe. Ameir Abdalla Ameir 2. Mhe. Bakar Hamad Bakar 3. Mhe. Bahati Khamis Kombo 4. Mhe. Mwantatu Mbarak Khamis 5. Mhe. Suleiman Haroub Suleiman SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kama mlivyoona kwenye Order Paper tumekuwa na zoezi la Kiapo cha Uaminifu baada ya jana kupokea Waraka kutoka kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) kwamba wenzetu hawa Waheshimiwa ambao tumewaapisha hivi punde ndiyo wamechaguliwa kutoka katika Baraza la Wawakilishi kama Katiba yetu inavyotaka. Waheshimiwa Wabunge, Katiba yetu inasema Wajumbe watano wa Baraza la Wawakilishi watajiunga na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, takwa hilo la Katiba limekwishatekelezwa, sasa nafasi zilizobaki ni zile tu za Mheshimiwa Rais kuzijaziliza kadri atakavyoona inafaa. Sasa Bunge linazidi kukamilika katika kuliunda kwake kwa maana ya wajumbe. Katibu. NDG. STEPHEN KAGAIGAI - KATIBU WA BUNGE: MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Maswali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, karibu sana. (Makofi) Muuliza swali la kwanza atakuwa Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kumi zinazozungumzwa sana Barani Afrika. Ni lugha ya pili kwa kuzungumzwa na watu wengi Barani Afrika na pia ni kati ya lugha kumi zinazozungumzwa sana duniani. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Kiswahili kinakuwa bidhaa hasa wakati wa kuchangia diplomasia ya uchumi na kuwa fursa ya ajira kwa Watanzania? (Makofi) SPIKA: Majibu ya swali hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu, tafadhali. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye leo ametupa uhai wa kukutana hapa na kuendelea na shughuli zetu za Bunge. Mheshimiwa Spika, pili, niungane nawe kuwakaribisha Waheshimiwa Wabunge wenzetu kutoka Baraza la 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Wawakilishi kuungana nasi kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibuni sana, tutawapa ushirikiano wa hali ya juu na kwa kweli mtasaidia sana kuchangia yale muhimu na kuishauri Serikali na sisi Serikali tupo tayari kupokea ushauri wenu. (Makofi) Mheshimiwa Spika, naomba nianze kujibu swali la Mheshimiwa Baba Askofu Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kiswahili sasa kimepata nafasi kubwa ya kuzungumzwa kwenye mataifa mengi duniani na wala siyo kuzungumzwa tu pia hata matumizi yake yameongezeka. Tumeanza kuona nchi mbalimbali kubwa duniani zikiandaa vipindi vya Kiswahili kwenye redio na kwenye magazeti yao. Hii ni ishara kwamba Kiswahili chetu sasa kinakua duniani kote. Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kutengeneza fursa hata kwa Watanzania ambao ndiyo wenye Kiswahili? Kiswahili hiki hapa nchini kinazungumzwa na makabila yetu karibu yote na ndiyo lugha ambayo inatuunganisha Watanzania. Tumeanza kusambaza Kiswahili hiki kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki, tumeona nchi zote za Afrika Mashariki zinazungumza lugha hii. Wote ni mashahidi tumeona jitihada ambazo zimefanywa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kusambaza Kiswahili kwenye Nchi za Ukanda wa Kusini (SADC) pale ambapo amekutana na Marais mbalimbali kuwahamasisha na sasa tumeona Kiswahili kimeanza kufundishwa kwenye nchi zao, kwa hiyo, Kiswahili kinazidi kupanuka. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, Kiswahili nacho kinaenda mbali zaidi, utaona Ujerumani, Marekani, Uingereza na Mataifa mengine makubwa yanaendelea kutumia Kiswahili. Sisi kama Serikali tumeweza kuwasiliana kupitia Balozi zetu, kila Balozi tumeiagiza kwenye nchi ambazo Balozi yupo kuanzisha kituo cha kujifunzia Kiswahili. Malengo yetu ni kupanua matumizi ya lugha ya Kiswahili. (Makofi) 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, tunapowafikishia Mabalozi na kufungua vituo na kuwafanya wananchi wa nchi husika kujifunza Kiswahili hapo sasa tumeingiza kwenye diplomasia ya Kiswahili. Kwa kuwa sasa Kiswahili kinapendwa duniani kote na kinazungumzwa na nchi nyingi sisi Watanzania sasa tuna fursa ya kuwa walimu wazuri kwenye nchi hizo kwenye vituo vyetu vya kufundisha Kiswahili. (Makofi) Mheshimiwa Spika, tunapokwenda kuwa walimu kwenye nchi hizo tayari tunafungua fursa za kiuchumi kwa kuajiri Watanzania kwenda kufanya kazi kwenye nchi hizo. Watanzania wakishapata ajira tunajua kodi kidogo inarudi nchini na tunaboresha uchumi wetu wa ndani. Kwa hiyo, tutatumia diplomasia hii kukuza uchumi wa ndani na hasa kwa kutoa fursa ya Watanzania kuajiriwa kwenye maeneo hayo kuendeleza kuboresha Kiswahili. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi) SPIKA: Ahsante sana. Swali linalofuata linatoka kwa Mheshimiwa Neema Kishiki Lugangira, uliza swali lako, kifupi tafadhali. MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, swali langu ni kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la masoko ya mazao yetu hata kama tunazalisha kwa ubora wa juu. Je, Serikali iko tayari kupeleka wataalam wake nje ya nchi na hasa kwenye nchi ambazo zimefanikiwa ili kujifunza namna bora ya usimamizi wa masoko yetu? Ahsante. SPIKA: Majibu ya swali hilo, Mheshimiwa Waziri Mkuu. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lugangira, Mbunge wa Mkoa wa Kagera, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, suala la kutafuta masoko kwenye mazao yetu lakini pia Mheshimiwa Mbunge anataka kujua 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) mpango wa Serikali wa kuwapeleka wataalam wetu nje ya nchi kujifunza kutafuta masoko. Sina uhakika sana kama alikuwa anataka kusisitiza kuwepo kwa masoko au suala ni kupeleka wataalam kujifunza masoko. Hata hivyo, Serikali yetu inatambua na inao mkakati ambao sasa tunaendelea nao wa kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara. Kwenye mazao yote ya biashara tumeendelea kuboresha kupata masoko ya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwapatia nafasi nzuri wakulima wetu kuuza mazao yao vizuri. Mheshimiwa Spika, lakini pia inapoingia kwenye utaalam wa kutafuta masoko muhimu zaidi ni kujua kama mazao tunayozalisha tuna masoko huko nje? Tunachokifanya sasa kila zao kupitia Balozi hizi nazo tunazitumia kutangaza mazao tuliyonayo ndani ya nchi ili tuweze kuyauza kwenye nchi wanazotumia mazao hayo. Zoezi hili linaendelea na tunapata wateja wengi kuja kununua mazao yetu na hali hiyo imesababisha masoko yetu kuimarika. Mheshimiwa Spika, muhimu kwetu sisi ni kutafuta mfumo mzuri unaowezesha mazao haya kujulikana na kuyauza na tupate bei nzuri. Kama ambavyo sasa ndani ya nchi tumeweka Mfumo wa Stakabali Ghalani ambao unakusanya mazao pamoja na kuwaalika wanunuzi kila mmoja anatamka atanunua zao hilo kwa shilingi ngapi kwa kilo, yule mwenye bei ya juu ndiye ambaye tunampa fursa ya kununua. Kwa hiyo, huo ni mfumo wa uuzaji wa mazao yetu ambao tumeuandaa na tutapata bei nzuri. (Makofi) Mheshimiwa Spika, lakini pia Serikali tunao mpango wa kutafuta masoko kwenye nchi ambazo zinazohitaji mazao hayo. Juzi hapa nilikuwa na Wabunge wa Mkoa wa Rukwa wakiomba Serikali iwasaidie kutafuta masoko ya mazao yanayolimwa Mkoani Rukwa kwa nchi za Zambia, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo, kazi ambayo Serikali inafanya sasa ni kuwasiliana na nchi ambazo ni walaji wa mazao haya ili kuhakikishia kuwa mazao haya yanapolimwa na kuvunwa tunayapeleka kwenye nchi husika. Hiyo ni njia pia ya kupata soko zuri la mazao yetu. 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, pia Serikali kwa sasa tunaendelea kujenga masoko ya kimkakati, masoko ya kikanda, ambayo tunayajenga pembezoni mwa nchi yetu ili kukaribisha ndugu zetu walioko jirani kuja kununua. Miezi mitatu iliyopita nilikuwa Mkoani Kilimanjaro, nimekwenda pale Horohoro, tunajenga soko kubwa sana ambalo pia wananchi wa maeneo hayo wakizalisha mazao yatawekwa hapo, wa nchi jirani wote watakuja hapo. Kwa hiyo tunawapunguzia ugumu wa kuingia mpaka huku ndani kutafuta mazao hayo badala yake tunawa-allocate kwenye masoko yale. Mheshimiwa Spika, mwezi mmoja uliopita pia nilikuwa Mkoani Kigoma kule Kagunga. Tumejenga soko zuri sana. Kwa hiyo tunawakaribisha ndugu zetu wa Burundi na Rwanda kuja kununua pale. (Makofi) Mheshimiwa Spika, tunajenga soko lingine kubwa sana Mkoani Kagera pale Nyakanazi. Lengo letu wale wote kutoka Kongo, Rwanda watakuja pale Nyakanazi kwenye soko letu lile la zaidi ya bilioni 3.5 ili wapate bidhaa. Kwa hiyo muhimu kwetu sisi ni kuweka mkakati wa namna gani mazao yetu yaliyoboreshwa yaweze kupata thamani kubwa kwa lengo la kumfanya mkulima aweze kupata tija kwa kazi ya kilimo anayoifanya. Kwa hiyo Serikali inaendelea na maboresho haya, Waheshimiwa Wabunge kama mna mawazo mengine ya kuboresha masoko, tunawakaribisha ili Serikali iweze kuimarisha upatikanaji wa mazao haya na iweze kuuza mazao haya kwa bei nzuri sana. Ahsante sana. (Makofi) SPIKA: Mheshimiwa Stella Simon Fiyao kutoka CHADEMA. Hayupo; Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali lifuatalo:- Mheshimiwa Spika, kwa vile Serikali iliona umuhimu wa kuwafikishia wananchi kule vijijini umeme kwa gharama nafuu, kwa hivyo wakaweka utaratibu wa kuunganishia nyumba umeme