Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MKUTANO WA TANO ___________________ Kikao cha Saba – Tarehe 16 Novemba, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Jenista J. Mhagama) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 84 Hali Mbaya ya Hospitali ya Wilaya – Mbozi MHE. GODFREY W. ZAMBI aliuliza:- Majengo ya Hospitali ya Wilaya Mbozi – Vwawa yako kwenye hali mbaya na wodi za kulaza wagonjwa hazitoshelezi hali inayosababisha msongamano katika wodi chache zilizopo:- Je, Serikali itayakarabati lini majengo ya zamani na kujenga mengine kwa ajili ya kulaza wagonjwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey W. Zambi, Mbunge wa Mbozi Mashariki, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ya Vwawa ilipandishwa hadhi kutoka kituo cha afya mwaka 2002 kwa kuongezewa majengo yafuatayo Wodi ya Mama wajawazito1, wodi 1 ya wanaume, pediatric ward 1, Chumba cha kusubiria mama wajawazito kimoja, chumba cha upasuaji, jengo la mapokezi, isolation ward, jengo la kliniki (RCH), jengo la utawala, chumba cha kuhifadhia maiti, jengo la kufulia nguo, jengo la upasuaji mkubwa na chumba cha X–ray. Aidha, ni kweli kuwa baadhi ya majengo ya hospitali hiyo yameharibika kiasi cha kuhitaji kukarabatiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012 Halmashauri imepanga kutumia shilingi 40,000,000 kwa ajili ya kukarabati jengo la upasuaji, shilingi 28,292,648 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la utawala na shilingi 18,968,672 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la wodi ya wazazi (Maternity Ward).
[Show full text]