20 Aprili, 2012 1 Bunge La Tanzania
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) 20 APRILI, 2012 BUNGE LA TANZANIA ________________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA SABA Kikao cha Tisa – Tarehe 20 Aprili, 2012 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- MHE. MARTHA M. MLATA (K.N.Y. MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA ZA JAMII): Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA MAENDELEO YA JAMII: Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MHE. IGNAS A. MALOCHA (K.N.Y. MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA SHERIA NDOGO): Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI: Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MHE. JADDY SIMAI JADDY (K.N.Y. MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA): Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY (K.N.Y. MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE VIWANDA NA BIASHARA): Taarifa ya Kamati ya Bunge 1 20 APRILI, 2012 ya Viwanda na Biashara ya Bunge Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA: Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Kuhusu Utekelezaji wa Shughuli zake kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, maswali, tunaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu. Atakayeuliza swali la kwanza ni Mheshimiwa Amos Gabriel Makalla. Na. 106 Mgogoro wa Ardhi Kinyenze MHE. AMOS G. MAKALLA aliuliza:- (a) Je, Serikali inashughulikiaje mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji na Kitongoji cha Kinyenze kilichopo Kipera unaohusu uhalali wa umiliki, mipaka na unyanyasaji mbalimbali? (b) Kwa nini kuna tofauti ya ramani ya sasa na ya awali ya mwaka 1950 kuhusiana na mipaka? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amos Gabriel Makalla, Mbunge wa Mvomero, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Serikali inatambua kuwepo kwa mgogoro wa ardhi baina ya mwekezaji na wakazi wa Kitongoji cha Kinyenze kilichopo Kipera katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero. Mgogoro huo wa ardhi unahusu shamba Na.296 lenye ukubwa wa hekta 97.7 lililopo katika Kijiji cha Kipera. Shamba hili linamilikiwa na Badrudin Dharams Walji wa Morogoro tangu mwaka 1959 bila Hati. Upimaji wa shamba hilo ulifanyika mwaka 2 20 APRILI, 2012 1997 na kupewa Hati ya kumiliki Na.48836 ya miaka 99 tangu tarehe 1 Oktoba, 1997. Mheshimiwa Spika, baada ya mmiliki wa kwanza wa shamba hili kufariki mwaka, 2008 warithi wa mmiliki huyu walihamisha miliki ya shamba hilo kutoka kwa Badrudin Dharams Walji kwenda kwa Tanbreed Poultry Limited wa Morogoro. Mgogoro huu ulijitokeza baada ya eneo hilo kupimwa na mwekezaji kufunga njia zote zilizokuwa zinakatiza ndani ya shamba hili ikiwemo kuwaondoa baadhi ya wananchi waliokuwa wakilima ndani ya shamba hilo. Lalamiko lingine limekuwa ni baadhi ya wananchi kulalamikia mipaka ya shamba la mwekezaji huyo ambalo lilimeza maeneo yao waliyokuwa wakiyalima kwa muda mrefu. Mheshimiwa Spika, Halmashauri imeshughulikia mgogoro huu kwa kuwakutanisha mwekezaji na wananchi ambapo maazimio yaliyofikiwa ni kufanyika kwa uhakiki wa mipaka ya shamba hilo ili kundoa utata uliyopo na mwekezaji kuridhia pendekezo la kufunguliwa kwa njia inayokatiza katika shamba hilo. (b) Mheshimiwa Spika, shamba hili halikuwahi kupimwa kutoka mwaka 1959 hadi mwaka 1997 lilipopimwa na kupatiwa ramani Na. E/357/2 iliyoidhinishwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi. Kwa maelezo hayo eneo hilo halijawahi kuwa na ramani mbili tofauti. MHE. AMOS G. MAKALLA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo hayajatoa matumaini sana juu ya tatizo hili, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali inakiri hapa kwamba vipo vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kufunga njia na kuwanyanyasa wananchi walioko katika eneo hilo vinavyofanywa na huyu Tanbreed Poultry Limited na kusababisha sasa kuweza kuwepo na umwagikaji wa damu; Serikali inatamka nini sasa kuharakisha suala hili kuona kwamba tatizo hili linamalizwa kuwepo kwa usalama na wananchi wapate haki yao na mwekezaji apate haki yake? Pili; kwa kuwa Serikali inakiri kwamba shamba hili halijawahi kupimwa toka mwaka 1959, limekuja kupimwa mwaka 1997; na wananchi wa eneo hilo, nimeenda mara mbili, wanalalamika kwamba eneo lao limemegwa na hata uhalali wa kumiliki huyu Badru unakuwa wa mashaka kwani halikuwahi kupimwa. 3 20 APRILI, 2012 Je, kwa nini mimi na wananchi wangu tusiamini kwamba ramani iliyoko sasa imechakachuliwa, siyo kama ile ya awali ambayo wananchi walikuwa na haki na eneo hili? SPIKA: Asante sana. Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu. Naomba maswali yenu ya nyongeza yawe mafupi na majibu ya nyongeza yawe mafupi. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa mimi nataka niliweke vizuri hapa, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Amos Makalla kwamba sisi kama ofisi tuko tayari pia kushirikiana na yeye. Tumelifuatilia jambo hili kwa karibu sana na nimeeleza hapa mambo yaliyojitokeza hapa. Mheshimiwa Spika, mimi ninachoweza kushauri kwa hatua hii tuliyofikia sasa hivi, iko haja ya Mheshimiwa Mbunge pamoja na Halmashauri, kwa sababu wameanza mazungumzo haya, na wanazungumza vizuri na ninavyoona mazungumzo na maelezo niliyopata yanavyotiririka, mimi naona muafaka unaweza ukapatikana katika hali ya amani kabisa bila kuingiza mgogoro wa aina yoyote ile. Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi hawa walizoea kulima pale, lakini sasa baada ya umilikaji huu ambao nimeuzungumzia, mmilikaji akaenda akafunga njia na akafunga eneo lote lile. Kwa hiyo, wale watoto wa shule waliokuwa wanapita katika eneo lile, hawawezi kupita tena. Nadhani ndhicho hiki Mheshimiwa Amos Makalla anachokitafsiri kama ni kunyanyaswa. Pia watu waliokuwa wanalima katika eneo lile nao wamezuiwa katika sehemu fulani ya hilo eneo wamezuia. Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka niseme tu kwamba tuko tayari sisi kusaidiana na Mheshimiwa Amos Makalla pamoja na Halmashauri kuhakikisha kwamba tatizo hili linaondoka. Sasa hili la kupimwa eneo kwamba limepimwa vibaya, halikukaa... ndicho ninachojibu hapa na Mkurugenzi nimemwagiza pamoja na wenzake na Wapima wote waende wakahakiki. Swali lilikuwa linaulizwa kwamba kuna ramani mbili, nimethibitishiwa kwamba pale hakuna ramani mbili. 4 20 APRILI, 2012 Lakini hiki anachosema Mheshimiwa Mbunge, tunakubaliana naye na tumeagiza Halmashauri pamoja Wapima waende wakapime pale ili kuhakikisha kwamba kilichopo katika ramani ndicho kilichoko katika ardhi. Hayo ndiyo ambayo naweza nikashauri kwa sasa hivi. (Makofi) MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Suala la migogoro ya ardhi limejikita sana ndani ya Mkoa wa Morogoro, hata hivi nina document nimeletewa kutoka Kijiji cha Mkangawaro kule Mgeta ambapo Wenyeviti wa Vijiji wameshiriki sana kuuza ardhi ya wananchi bila ridhaa ya wanavijiji wenyewe; na limejikita Wilaya zote Mkoa wa Morogoro. Je, Waziri sasa yuko tayari nikimletea orodha ya maeneo yote yenye migogoro ndani ya Mkoa wa Morogoro Wilaya mbalimbali na kuishughulikia haraka bila kupoteza muda ili wananchi wapate maendeleo yao? (Makofi) SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu kwa kifupi. Naomba maswali yawe mafupi kusudi tuweze kuwa na watu wengi wanaochangia. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, kama yeye anavyo vielelezo na kama anavyoeleza, Morogoro nimefika kule. Tunamwomba atuletee halafu tutashughulikia. MHE. MOSES J. MACHALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Hivi karibuni kulikuwa na mgogoro wa ardhi katika mapori ya Kagera Nkanda kule pamoja na Vijiji vya Mvinza ambapo mgogoro huu tuliweza kuushughulikia na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Moja ya mambo ambayo tulikubaliana ilikuwa ni pamoja na kuweza kuwashughulikia watumishi wa Idara ya Maliasili na Mazingira ambao waliwaacha wananchi wa Wilaya ya Kasulu kuendelea kwenda kulima katika mapori hayo. Lakini mpaka leo hii watu hao hawajaweza kuchukuliwa hatua. Naomba kuuliza. Je, Serikali iko tayari kuweza kuwawajibisha wale maafisa wa Maliasili ambao waliwaacha wakulima kwenda kulima kwenye maeneo ya Hifadhi kwa mujibu wa Serikali na hivyo kuweza kuondolewa katika maeneo yale bila kufuata utaratibu? 5 20 APRILI, 2012 WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikubaliana kwamba uchunguzi ufanyike na hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wale ambao wataonekana wamefanya makosa. Watumishi walioko kwenye Halmashauri wako kwenye mamlaka ya nidhamu ya Halmashauri kama ambavyo jana ilielezwa kwamba ukiachia Mkurugenzi, watumishi wengine wote wanasimamia tu sekta lakini mamlaka yao ya nidhamu ni pale pale kwenye Halmashauri. Walioko kwenye sekretarieti ya Mkoa, mamlaka yao ya nidhamu iko kule kule Mkoani. Tumekwishakutoa maelekezo ya kitalaam sisi kama Wizara kueleza ni namna gani wanapaswa kufanya kazi zao na tayari tumekwishakuwasiliana na Mkoa kwamba taratibu za nidhamu kwa pale ambapo watakuwa wamekosea, zifuatwe na zichukuliwe haraka. Na. 107 Wajibu wa Wenyeviti wa