MKUTANO WA KUMI NA MBILI Kikao Ch
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE ________________ MKUTANO WA KUMI NA MBILI Kikao cha Hamsini na Moja – Tarehe 22 Agosti, 2008 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA UCHUMI (MHE. OMAR YUSSUF MZEE): Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Fedha na Uchumi kwa Mwaka wa fedha 2008/2009. MHE. DR. ABDALLAH O. KIGODA - MWENYEKITI WA KAMATI YA FEDHA NA UCHUMI: Taarifa ya Kamati ya Fedha na Uchumi kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha uliopita, pamoja na maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2008/2009. MHE. FATMA ABDULHABIB FEREJI – MSEMAJI WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI: Taarifa ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha uliopita, pamoja na maoni ya Upinzani kuhusu makadirio ya matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2008/2009. MASWALI NA MAJIBU Na. 447 1 Mgao wa rasilimali fedha na vyandarua MHE. JOHN P. LWANJI aliuliza:- Kwa kuwa takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa, Mkoa wa Singida ni wa mwisho kwa pato la mtu kwa mwaka (per capital income) nchini:- (a)Je, ni vigezo gani vilitumika kwenye kugawanya fedha za MCC za Mheshimiwa Rais George W. Bush takriban shilingi bilioni 700 na kuacha Mkoa wa Singida usipate hata senti moja wakati lengo la fedha hizo ni kupunguza makali ya umaskini? (b)Je, Mkoa wa Singida ulipata mgao gani kati ya vyandarua milioni tano vilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Bush? (c)Je, kwenye mgao huo wa rasilimali fedha na vyandarua, mikoa kwa ujumla ilihusishwa vipi kabla ya kufikiwa kwa maamuzi yaliyotolewa na kwamba, Mkoa wa Singida usipate na mikoa mingine maskini ipate mgao huo? MWONGOZO WA SPIKA MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO: Mwongozo wa Spika? SPIKA: Mwongozo wa Spika, Mheshimiwa William Shellukindo. MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO: Mheshimiwa Spika, naomba mwongozo wako kwa sababu swali hili halielekei kama ni la Afya? SPIKA: Swali hili lina? MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO: Halielekei kama ni la Afya hili, linazungumzia pato la taifa. SPIKA: Wajibu wa Serikali ni kujipanga kujibu maswali. Sasa nitaona walivyojipanga, nadhani kama wamepanga wao kwamba lijibiwe na Wizara ya Afya kwa sababu linahusu vyandarua. Nadhani vyandarua hivi ni vya mbu, kuzuia mbu, siyo vyandarua vya urembo na mambo mengine kama ya MCC fedha zilizo kwenye Sekta ya Afya. Nadhani tuwaachie Serikali tu watusaidie. Ndiyo, sawa sawa. Nafahamishwa hapa, utaratibu ni kwamba sisi tunapeleka kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu anajua namna ya kupanga miongoni mwa Waziri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya. 2 NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Paul Lwanji, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Katika mwaka 2008 kutakuwa na kampeni ya kugawa vyandarua kwa watoto wote walio katika umri chini ya miaka 5. Katika kampeni hiyo mikoa yote ya Tanzania Bara itahusika, ukiwemo mkoa wa Singida. Hakuna Wilaya, Kata wala Kijiji ambacho hakitakuwa kwenye mpango huo wa kupata vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu. (b) Mheshimiwa Spika, fedha zitakazotumika katika kampeni hii ya vyandarua zimechangiwa kutoka maeneo makuu matatu ambayo ni Benki ya Dunia (World Bank) asilimia 38%. Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria yaani Global Fund asilimia 58%, pamoja na mfuko wa Rais Bush wa Marekani wa kupambana na ugonjwa wa malaria, (PMI) asilimia 5%. Jumla ya vyandarua milioni 7.2 vinatarajiwa kusambazwa katika kampeni hii, ili kuhakikisha kuwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano, wanapata vyandarua bora ili kujikinga na ugonjwa wa malaria ambao unahatarisha zaidi maisha yao. (c) Mheshimiwa Spika, Mikoa yote kwa ujumla inahusika katika kampeni hii na imehusishwa kutambua idadi ya watoto chini ya miaka mitano na hakuna mkoa ulioachwa ukiwemo Mkoa wa Singida. MHE. JOHN P. LWANJI: Ahsante Mheshimiwa Spika. Swali hili nililiwasilisha muda mrefu na nilitarajia kwamba lingapata majibu ya kina kwa sababu awali tuliambiwa kwamba malengo ya mfuko huu ilikuwa ni kwenda kuhuishia barabara zetu, mambo ya miundombinu, umeme pamoja na afya kwa maana ya UKIMWI na vyandarua. Lakini ninaona Serikali imetoa jibu kwa ajili ya swali namba (b). (a) na (c) limeachwa kabisa. Sasa ningelipenda kujua Mkoa wa Singida umepata nini kwa sababu Mkoa wa Singida barabara zake za ndani ni mbaya sana na hasa hii barabara ya kutoka Itigi, Chunya mpaka Mbeya pamoja na barabara hii ya kutoka Manyoni Kiheka na kwenda mpaka Isanza. Sasa ningelipenda nipate majibu ya uhakika kwamba sisi tunaishia vyandarua tu? Halafu utaratibu huu uliotumika katika kujibu swali je, hii si ni njia ya kukwepa maswali ya msingi? Naomba majibu. 3 SPIKA: Hakuna linalokwepwa hapa. Msisitizo wako wewe Mheshimiwa katika swali lako ni vyandarua si yako hapa, yako (b) na (c). Kwa hiyo hakuna kilichokwepwa hapa. Hii pia iwasaidieni namna ya kuuliza swali, ukiweka msisitizo kwenye jambo, hilo ndilo litachukuliwa. Sasa (b) na (c) yote ni vyandarua. Ni (a) tu ndiyo umesema juu ya Singida sipati hata senti moja. Sasa Mheshimiwa Waziri wa Afya kwa majibu. WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Spika, naomba niongeze majibu kufuatana na swali la Mheshimiwa Lwanji, ningependa Bunge lielewe kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekuwa na uhusiano na juhudi za Rais Bush kabla hata waliposaini MCC alipokuja hapa nchini na MCC aliyoizungumzia Mheshimiwa Lwanji kusema kweli inakwenda kwenye barabara, maji na vitu kama hivyo, sisi tuna uhusiano na Mfuko wake unaitwa Presidential Malaria Initiative ambao ulikuwepo kabla ya MCC. Kwa hiyo, ningemshauri Mheshimiwa Lwanji aulize swali kuhusu MCC itakwenda kwenye Wizara ambayo inahusika ambayo sisi nadhani hatupati senti hata moja. Ahsante sana. Na. 448 Hospitali ya Wilaya ya Muheza MHE. NURU AWADHI BAFADHILI aliuliza:- Kwa kuwa Wilaya ya Muheza haina hospitali ya Wilaya, bali inategemea huduma kutoka hospitali Teule ya Mission:- Je, ni lini Serikali itaiangalia kwa jicho la huruma Wilaya hiyo ili kuwa na hospitali ya Serikali? NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadhi Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kabla na baada ya uhuru, Serikali imekuwa ikishirikiana na taasisi za dini na zisizo za kidini kutoa huduma za afya. Kwa kuzingatia misingi ya ushirikiano huo Serikali haikuona ulazima wa kujenga hospitali nyingine katika maeneo ambayo tayari kulikuwa na hospitali za taasisi au mashirika ya dini. Hospitali hizo zimepewa hadhi katika maeneo husika kulingana na mfumo wa utoaji wa afya nchini. Serikali huingia makubaliano na wenye hospitali hizo ili kutoa huduma kwa niaba ya Serikali katika maeneo yao. Hivi sasa Serikali inatumia hospitali 23 kama hospitali 4 teule za Wilaya ikiwemo hospitali ya Muheza, Hospitali moja kama Hospitali Teule ya Mkoa (Dar es Salaam) na Hospitali mbili za Rufaa (KCMC na Bugando). Hali hii inaboresha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi inayopewa umuhimu mkubwa sasa ulimwenguni pote. Jukumu la Serikali kwa hospitali hizi ni kutoa fedha zote zinazohitajika kuendesha hospitali. Hii ni pamoja na mishahara, dawa, vifaa na fedha kwa matumizi mengine ya kila siku. Halmashauri za Wilaya zina jukumu la kusimamia huduma katika hospitali Teule za Wilaya/Halmashauri. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inazihudumia hospitali teule za Wilaya kama hospitali za Serikali na kwa kuwa utaratibu uliopo Wilaya moja haiwezi kuwa na hospitali mbili za Wilaya, tunadhani haitakuwa vema kujengwa hospitali nyingine ya Wilaya ya Muheza kwa sasa. Naomba kutumia fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kuhimiza ushirikiano huu, hasa sasa ambapo Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM). Katika Kijiji ambapo tayari kuna Zahanati ya Shirika la Dini au binafsi kusiwe na haja ya Halmashauri kujenga Zahanati nyingine na vile vile vituo vya afya. Halmashauri ifanye makubaliano na wamiliki wa vituo hivyo ili vitoe huduma kwa niaba ya Halmashauri. Wizara imeandaa utaratibu wa makubaliano hayo yaani (Service Agreement). MHE. NURU AWADHI BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake aliyonipa. Lakini ingawaje tunatakiwa kuwa kwenye hospitali teule kusiwe na vituo vya afya. Kwa kuwa katika Wilaya ya Muheza, Wilaya imepanuka sana, watu ni wengi na katika hospitali teule ya Muheza wanakuwa wanarundikana kiasi cha kuwa huduma inakuwa ni ndogo. Je, Serikali inafikiriaje kutumia majengo ya zamani yaliyokuwa hospitali ya Mbaramu kufanya ni kama ni kituo cha afya cha Muheza. (Makofi) NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Spika, kwanza niweke kumbukumbu vizuri katika Hansard nimesema, sikusema kwamba mahali pana hospitali teule pasiwe na vituo vya afya. Nimesema mahali ambapo pana hospitali teule au vituo vya afya basi isirudie sehemu ile itafutwe sehemu nyingine kujengwa. Nilitaka niliseme hilo kuweka kumbukumbu vizuri. Mheshimiwa Spika, ni kweli nakubaliana kwamba hospitali teule inafurika kwa sababu haina hospitali anayoidai Mheshimiwa Mbunge, lakini vile vile vituo vya afya pale ni vichache. Mheshimiwa tumekuwa tunawasiliana na Halmashauri na vile vile tunazungumza na Wabunge kwamba jukumu la kujenga vituo vya afya ni jukumu la Halmashauri husika. Lakini vile vile hakutakuwa na tatizo kama Halmashauri yenyewe itaona ile hospitali iliyokuwa ya zamani Mbaramo