Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________ MAJADILIANO YA BUNGE ______ MKUTANO WA KUMI NA MBILI Kikao cha Thelathini na Mbili - Tarehe 25 Julai, 2003 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) DUA Spika (Mhe. Pius Msekwa) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara kwa Mwaka 2003/2004. MHE. SALOME J. MBATIA (k.n.y. MHE. WILLIAM H. SHELLUKINDO - MWENYEKITI WA KAMATI YA UWEKEZAJI NA BIASHARA): Taarifa ya Kamati ya Uwekezaji na Biashara kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara katika mwaka uliopita pamoja na maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2003/2004. MASWALI NA MAJIBU Na. 309 Barabara ya Kigarama, Bugomora hadi Murongo MHE. BENEDICTO M. MUTUNGIREHI aliuliza:- Kwa kuwa katika Mkutano wa Bunge wa Bajeti ya Mwaka 2001/2002 Serikali iliahidi kuifanyia matengenezo barabara ya Kigarama - Bugomora hadi Murongo; na kwa kuwa hadi kufikia sasa barabara hiyo bado haijafanyiwa matengenezo na imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa maeneo inakopitia:- (a) Je, Serikali kwa kutotimiza ahadi yake inawaambia nini wananchi wa Kata ya Mabira, Bugomora na Murongo inakopitia barabara hiyo ambao wamekata tamaa kwa ahadi isiyotekelezwa? (b) Je, sasa Serikali inaahidi kuitengeneza lini barabara hiyo? (c) Je, Serikali itatengeneza lini barabara ya Kakanja, Nyakirigita, Kikuku hadi Kitwe ambayo haijawahi kutengenezwa tangu miaka 30 iliyopita? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- 1 Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benedicto Mutungirehi, Mbunge wa Kyerwa, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Serikali iliahidi kuifanyia matengenezo barabara hiyo kwa awamu mbili kwa kuanzia kilomita 40 kupitia Mradi wa Uwiano na Maendeleo Vijijini (KDRDP) na Mfuko wa Barabara za Serikali za Mitaa (LGRF). Lakini Mhisani wa Mradi huo wa Uwiano wa Maendeleo Vijijini kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2002 alifuta Bajeti ya matengenezo ya barabara (Road Rehabilitation) kwa kutenga Bajeti ndogo kwa ajili ya kujenga madaraja ya mbao na makalvati tu. Pamoja na fedha za Mfuko wa Barabara kuwa ndogo na kushindwa kukidhi matengenezo ya barabara hiyo, katika mwaka 2002/2003 Halmashauri ya Wilaya kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ilipanga kufanya matengenezo ya kawaida ya kilometa 40 na matengenezo ya sehemu korofi kilometa 29 ili kupunguza usumbufu uliopo kwa wananchi wa maeneo hayo wakati wa kusafiri/kusafirisha mazao yao kwa nyakati za mvua pamoja na kiangazi. (b) Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2003 jumla ya kilometa 13.4 za barabara kutoka Murongo hadi Nyamiyaga imetengenezwa kwa gharama ya shilingi 21,015,800/=. Kazi ya kuitengeneza barabara hii itaendelea kufanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. (c) Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Karagwe iliahidiwa kutengenezewa barabara zenye urefu wa kilomita 97.9 na Mradi wa kusimamia Kilimo na Mazingira Mkoani Kagera (KAEMP) ambazo ni Kihanga - Rwambaizi, Nyakagoyagoye - Rwabere, Chabalisa - Kayungu, Kayungu - Kandegesho, Kakanja - Kikukuru - Kitwe, Kyerwa – Kagenyi. (vii) Rugu - Ruhita na Rwabitembe - Kibwera. Mheshimiwa Spika, mpango huo wote uliotajwa hapo juu nao haukuweza kutekelezwa kutokana na gharama za matengenezo ya barabara hizo kuwa kubwa. Lakini mradi wa kusimamia Kilimo na Mazingira Mkoani Kagera (KAEMP) ulitenga kiasi kidogo cha fedha ambazo wameamua kutengeneza barabara ya Nyakagoyagoye - Rwabere kilometa 25.2. Pamoja na matatizo hayo Halmashauri ya Karagwe ina mpango wa kuifanyia matengenezo barabara hiyo aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge kwa awamu kwa kutumia fedha toka Mfuko wa Barabara wa Serikali za Mitaa. MHE. BENEDICTO M. MUTUNGIREHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, amekiri kwamba hela za Mhisani zimepungua; na katika swali (c) amekiri kwamba hela zilizotengwa na KAEMP zilipungua kama alivyokwishakujibu hapa; je, sasa Serikali kwa sababu imetambua hilo na vyanzo vya mapato vya Halmashauri navyo vimepungua, ina mpango gani sasa wa kutafuta katika vyanzo vingine ili iweze kuhakikisha kwamba barabara hizo ambazo hazijatengenezwa kwa miaka 30 sasa zinatengenezwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, mipango yote niliyoieleza ilikuwa ni juhudi za Serikali katika kujaribu kuboresha mawasiliano ya barabara katika eneo hili. Kwa hiyo, ninachoweza kumwahidi tu ni kwamba Ofisi yangu bado inaendelea kushirikiana na Halmashauri yake ili kujaribu kutafuta mbinu nyingine za kuiwezesha barabara hiyo, kuweza kupata mfadhili. Lakini vile vile tumekubali kwamba katika mipango inayokuja, tutajaribu kuzungumza na Halmashauri hiyo ili tuone ni kiasi gani tunaweza pengine tukarekebisha programu ili kuwezesha fedha zaidi kidogo kupatikana. Na. 310 Sheria ya Kodi ya Majengo 2 MHE. RAYNALD A. MROPE aliuliza:- Kwa kuwa Serikali imeanzisha sheria ya Kodi ya Majengo chini ya Sheria ya Mamlaka za Miji Na. 2 ya Mwaka 1983; na kwa kuwa Mamlaka za Miji zimeweka Kodi za Majengo yaliyothaminiwa Mijini; na kwa kuwa lengo la Sheria hiyo ni kuendeleza Miji hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, majengo yanayohusika na maendeleo ya jamii na kadhalika:- (a) Je, ni kiasi gani cha fedha kimekusanywa kupitia kodi hiyo tangu mwaka 1995; na ni kiasi gani kinatumika kujengea barabara Mijini ama kuendeleza vitongoji vya Miji? (b) Kwa kuwa ipo haki ya kimsingi isemayo hakuna haki ya kutoza kodi bila uwakilishi au kuonyesha maendeleo yake yaani No taxation without representation; je, ni sababu zipi zinazoifanya Serikali kuwatoza wananchi kodi ambazo haziwajengei miundombinu ya barabara kama ilivyo katika vitongoji vya Mbezi Beach, Tegeta, Mikocheni, Mjini Dar es Salaam na Vitongoji vya Miji mingi nchini? (c) Je, ni lini Serikali itafuta Sheria kama hiyo ili kuondoa migogoro katika ukadiriaji na ulipaji na badala yake kuleta Sheria ya mipango itakayowanufaisha walipaji wenyewe na kuleta ufanisi katika maeneo yao? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raynald Mrope, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kuwa Halmashauri za Manispaa 11 zilizopo chini ya Programu ya Uimarishaji Huduma Mijini zilikusanya kiasi cha shilingi 13,417,020,000/= kati ya mwaka 1995 hadi mwaka 2002 kutokana na kodi ya majengo. Fedha hizo zilitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara za Halmashauri. Kwa mfano, katika ujenzi wa barabara iendayo Chuo cha Usafirishaji, Halmashauri ya Kinondoni ilichangia shilingi milioni 36 milioni, Manispaa ya Moshi ilitumia shilingi milioni 25 kusawazisha barabara za Mitaa ya Kibororoni, Majengo na Pasua. Aidha, kutokana na mchango wa Halmashauri ya Manispaa ya Tanga programu ya barabara za lami iliongezeka kutoka kilometa 12 hadi kilometa 18. (b) Mheshimiwa Spika, madhumuni ya kutoza kodi ni kuziwezesha Serikali za Mitaa kutoa huduma kwa wananchi na kuendesha shughuli zake za kila siku. Hivyo, Halmashauri zote nchini hutoza kodi na kutumia kwa maendeleo ya wananchi. Aidha, matumizi ya fedha zinazotokana na kodi au ruzuku ya Serikali inategemea na vipaumbele vya Halmashauri husika ambako Waheshimiwa Wabunge ni Madiwani. Hata hivyo, ukweli ni kwamba kodi inayotozwa haitoshelezi kukamilisha mahitaji yaliyopo katika Halmashauri husika japokuwa yapo maendeleo yaliyotokana na kodi zinazotozwa na Halmashauri hapa nchini kama nilivyoelezea hapo juu. (c) Kwa sasa Serikali haina mpango wowote wa kufuta kodi ya majengo kwa kuwa imeonekana ndiyo kodi pekee inayoweza kukusanywa kirahisi bila kuleta kero kwa watu walio wengi. Wakati wote kodi hutozwa kwa kuzingatia mahitaji ya kimaendeleo ya wananchi na si vinginevyo. MHE. RAYNALD A. MROPE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri huyu ni hodari sana wa kujibu vizuri maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Lakini kwa swali hili leo naona hakufanya uchunguzi wa kutosha kwani angekuwa amegundua adha, unyanyasaji na ubabe wanaopambana nao wananchi katika ukadiriaji holela usio na kanuni wala taratibu; je, Serikali haioni kuwa hii ni kero kubwa kama ilivyokuwa kodi ya maendeleo na hivyo ifutwe? (Kicheko/Makofi) 3 Mheshimiwa Spika, pili, sehemu nyingi duniani kodi ya majengo ni maalum yaani specific kwa ajili ya kujenga miundombinu kama barabara, maji, kuzoa taka na kadhalika; je, kuna maana gani kuwatoza wananchi kodi ya majengo katika mitaa yenye mashimo, mabwawa, uchafu uliokithiri ama maeneo ambayo hayakupimwa? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza, namshukuru kwa kauli yake nzuri kwamba najitahidi kujibu vizuri pamoja na kujaribu kuniponda katika jibu nililolitoa leo. (Kicheko/Makofi) Mheshimiwa Spika, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Raynald Mrope, kwamba kodi hii ni kodi ambayo inatozwa kutokana na Sheria ambayo imetungwa na Bunge hili. Taratibu zake za namna ya kufanya assessment ya majengo ziko very clear na kwa kweli wala hazina hali ya kudhani kwamba hakuna uwazi katika assessment ya majengo hayo na ndiyo maana nimesema kwa sehemu kubwa ndiyo kodi tunayodhani haina kero kubwa kama zilivyokuwa kodi nyingine. Kwa hiyo, bado tutaendelea na kodi hiyo. Mheshimiwa Spika, lakini pili, Mheshimiwa Raynald Mrope, anasema katika nchi nyingine