Hii Ni Nakala Ya Mtandao (Online Document)
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Arobaini na Mbili – Tarehe 14 Agosti, 2006 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI: Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. MUSTAFA H. MKULLO): Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2006/2007. MWENYEKITI WA KAMATI YA FEDHA NA UCHUMI: Maoni ya Kamati ya Fedha Kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha Uliopita, Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2006/2007. SPIKA: Ahsante sana Mwenyekiti, kwa taarifa ya wageni wetu huyo ni Dr. Abdallah Omar Kigoda, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi. Oh leo naona mambo ni mazito kidogo wanakuja wazito watupu. MHE. HAMAD RASHID MOHAMED - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI –WIZARA YA FEDHA, MIPANGO NA UWEZESHAJI: Maoni ya Kambi ya Upinzani Kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha Uliopita, Pamoja na Maoni Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2006/2007. SPIKA: Kwa taarifa ya wageni pia aliyewasilisha taarifa sasa hivi ni Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ndani ya Bunge. (Makofi) MASWALI NA MAJIBU Na. 395 1 Uharibifu wa Mazingira na Kampuni ya Placer Dome MHE ALI KHAMIS SEIF (K.n.y. MHE. CHACHA Z. WANGWE) aliuliza:- Kwa kuwa, Kampuni ya Placer Dome ina mwaga maji na takataka zenye sumu aina ya cynide na mercury kwenye mto Tigithe, ambapo wananchi wa maeneo hayo wanayatumia maji ya Mto huu kwa shughuli mbalimbali na tayari watu kadhaa na mifugo imeathirika na kemikali hizo:- (a) Je, Serikali inaweza kufanya Environmental Impact Assessment ya mgodi huo ili kuwanusuru watumiaji wa maji ya Mto huo kutokana na kemikali hizo? (b) Kwa kuwa, Mto Tigithe humwaga maji yake kwenye Mto Mara na Mto Mara humwaga maji yake Ziwa Victoria. Je, Serikali haioni kwamba, samaki wanaovuliwa ziwani hawafai kwa matumizi ya binadamu kutokana na kemikali hizo na itafanyaje? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MAZINGIRA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Wangwe, Mbunge wa Tarime, lenye sehemu (a) na (b) napenda kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Mgodi wa Dhahabu wa Placer Dome huko katika eneo la Gokoni Nyabigena karibu na Mto Tigithe, Wilaya ya Tarime. Shughuli inayofanyika katika eneo la Gokona ni uchimbaji udongo (Malighafi) ambao husafirishwa Nyabirama umbali wa kilomita saba. Eneo hili ni kilomita 100 Mashariki ya Ziwa Victoria. Mheshimiwa Spika, cyanide kemikali ambayo kiasi chake kikiwa kikubwa katika mchanganyiko wa vimilika huwa ni sumu kali hutumia viwandani katika kutengeneza dawa za kuulia wadudu, plastiki, rangi, nailoni na katika uchimbaji wa madini. Kiasi kidogo cha cyanide upatikana kiasilia katika vyakula kama vile mihogo, ulezi, kabeji na mchicha. Hata hivyo hakuna matatizo ya muda mrefu ya kiafya kuwepo na kiasi hiki kidogo cha cyanide. Mheshimiwa Spika, Placer Dome hutumika sana katika uchenguaji wa dhahabu (Gold Processing) uchenguaji hufanyika Nyabirama na mabaki ya uchafu wa uchenguaji yenye cyanide huwekwa kwenye kwenye bwawa maalum (tailing storage facility) ili kudhibiti uvujaji unaoweza kuathiri mazingira, maji yenye kiasi kidogo ya cyanide yanayotokana na uchafu huo nayo huhifadhiwa katika bwawa maalum kabla ya kurejeleshwa kiwandani. Bwawa limewekewa kinga madhubuti. Uangalizi wa kila mara (Environmental Monitoring) hufanywa ili kudhitibi uvujaji wa aina yoyote ile unaoweza kupenya chini kwa chini hadi Mto Tigithe au Mto Mara. Kampuni ina maabara ambayo inafanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali ili hatua za haraka zichukuliwe endapo panatokea matatizo. Uchunguzi wa muda mrefu wa 2 sampuli kutoka Mto Mara na Mto Tigithe umeonyesha hakuna dalili za kuwepo kwa chembe chembe (traces) za ‘cyanide’. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wangwe, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment) ya mgogi wa Placer Dome ilifanyika mwaka 2000 kabla ya kuanza rasmi shughuli za uzalishaji na iliwasilishwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wizara ya Nishati na Madini. Ripoti na Mpango wa Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Plan) ilijadiliwa na kukubaliwa na wadau wote toka sekta husika. Mwaka 2002 NEMC ilishauri Kampuni ya Placer Dome kufanya uchunguzi wa kina ili kubainisha athari kwa mazingira, wafanyakazi, na jamii inayozunguka mgodi, zinazoweza kutokea kutokana na shughuli za uchimbaji. Matokeo ya uchunguzi huo yaliiwezesha Kampuni hiyo kuboresha Mpango wa Usimamizi wa Mazingira (EMP) ya kutengeneza Mpango wa Nyongeza uliozingatia ushauri huo. Mwaka huo huo ulifanyika utafiti ili kujua hali ya viumbe hai katika Mto Mara na Mto Tigithe. Matokeo ya utafiti huo hayakubainisha madhara yanayotokana na shughuli za uchimbaji yanayohatarisha maisha ya viumbe hai katika mito hiyo. Hata hivyo Serikali inawataka wenye migodi kwa kushirikiana na wataalamu toka NEMC na Wizara ya Nishati na Madini, kuendelea kufanya Ukaguzi wa Mazingira environment audit na kubaini kama kuna athari zote, ili hatua za haraka zichukuliwe inapobidi. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mgodi wa Placer Dome hautumii zebaki (mercury) katika uchenguaji wa dhahabu hakuna uwezekano wa kuwepo kemikali hiyo katika maji taka yanayotokana na shughuli za mgodi huo. (b) Mheshimiwa Spika, mwaka 2005 kupitia Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria kwa kushirikiana na Shirika Lisilo la Kiserikali la Kimataifa la Hifadhi ya Mazingira na Wanyamapori na Kampuni ya Placer Dome ilifanya utafiti wa hali ya samaki katika Ziwa Victoria na Mto Mara. Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa vipimo vya ubora wa samaki wa Ziwa Victoria kwa matumizi ya binadamu vipo juu ya viwango vya Kimataifa. Aidha, maabara za kisasa zilizo kwenye viwanda vya minofu na Taasisi za Kiserikali zinatumika kupima ubora wa minofu ya samaki. Kwa kuzingatia hayo samaki wanaovuliwa toka Ziwa Victoria huuzwa kwenye masoko ya Ulaya ambako viwango vya ubora vinapewa kipaumbele. Hakuna malalamiko toka kwenye masoko ya ndani na nje ya Tanzania ndiyo maana uuzaji wa minofu ya samaki nje ya nchi bado unaendelea. 3 Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo haya, napenda kuwahakikishia wananchi wanunuzi wa samaki kutoka nje ya Tanzania vile vile napenda kumhakikishia huyo Bwana Hubert Sauper kwamba samaki wanaovuliwa toka Ziwa Victoria ni salama kabisa hawana chembechembe cha aina yoyote zenye kuhatarisha afya ya binadamu. MHE. ALI KHAMIS SEIF: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa sababu Mheshimiwa waziri amekiri kuwa cyanide kwa kiwango kikubwa inaweza ikaleta athari. Na amekiri kuwa huko kunakochimbwa madini ni kuwa kuna hifadhi ya cyanide katika mabwawa. Je, Mheshimiwa Waziri hakuna njia nyingine ya kuhifadhi cyanide isipokuwa kuwekwa katika bwawa? SPIKA: Halikusikika Mheshimiwa Mbunge. Ebu tafadhali rudia swali. MHE. ALI KHAMIS SEIF: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekiri kuwa iko cyanide ambayo inatumiwa kwa kuhifadhia dhahabu. Na amekiri kuwa cyanide inahifadhiwa katika mabwawa na cyanide ikiwa nyingi inakuwa ni sumu, je, hakuna njia nyingine ya kuhifadhi cyanide isipokuwa katika mabwawa? SPIKA: Yaani Waziri cyanide lazima itupwe kwenye mabwawa tu hakuna njia nyingine ya kuweza kuyatokomeza? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, cyanide ni kemikali ambayo kiasilia inakuwa na carbon na nitrate. Kuweza kuharibika haraka yaani ikapoteza nguvu yake ya kemikali kwa kukutana na mionzi ya jua ndiyo maana huwekwa kwenye mabwawa ambayo moja kwa moja inakutana na mionzi ya jua na kuharibika. WAZIRI WA KAZI, AJIRA NA MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Spika, kuweka cyanide kwenye mabwawa ni katika hatua muhimu ya detoxification yaani kuifanya cyanide isiwe nafuu. Mheshimiwa Spika, cyanide ni madini ambayo ni sumu sana na yakiwepo katika kiwango kidogo sana yanaweza kuleta maafa. Kwa hivi kiasi ambacho kinakuwa pale kikiingia kwenye ziwa na kuwa detoxified hakina madhara yoyote. (Makofi) Na. 396 Uchafuzi wa Mazingira MHE. RIZIKI OMAR JUMA (K.n.y.MHE. SUSAN A. J. LYIMO) aliuliza:- Kwa kuwa, mazingira ni suala mtambuka na kwamba, Serikali imejitahidi sana kudhibiti hali ya uchafu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuongeza ushuru kwenye mifuko ya plastiki lakini pamoja na juhudi hizo bado mifuko ya plastiki maarufu kama 4 Rambo inaendelea kuzagaa kwenye sehemu nyingi hasa za mijini na kuhatarisha afya za watu na wanyama wachungwao:- (a) Kwa kuwa, historia inaonyesha kuwa, mifuko hiyo haikuwepo katika miaka ya nyuma na badala yake ilitumika mifuko ya karatasi za khaki na magazeti. Je, Serikali haioni hoja ya kuzuia kabisa mifuko ya Rambo isitumike tena hapa nchini na kurudia utaratibu wa nyuma? (b) Kama Serikali haiwezi kuzuia bidhaa hizo za plastiki, kwa nini isinunue kinu ili mifuko hiyo pamoja na bidhaa za aina hiyo zifanyiwe recycling? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MAZINGIRA alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mwezi April 2006 Serikali ilitoa tamko la kupiga marufuku utengenezaji, uagizaji, ununuzi na matumizi ya mifuko ya plastiki laini na ile ya kufungia maji na maji ya matunda. Serikali imeongeza kodi kwenye mifuko mingine ya plastiki kwa asilimia 120. Aidha, Shirika la Viwango liko katika hatua za mwisho katika kuweka viwango vya plastiki vinavyokubalika