Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Wizara Ya Ujenzi Na Uchukuzi
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI HOTUBA YA WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI, MHESHIMIWA MHANDISI DKT. LEONARD MADARAKA CHAMURIHO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2021/22 DODOMA MEI, 2021 HOTUBA YA WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI, MHESHIMIWA MHANDISI DKT. LEONARD MADARAKA CHAMURIHO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2021/22 A. UTANGULIZI 1. Mheshimiwa Spika, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuchambua Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2020/21. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/22. 2. Mheshimiwa Spika, nianze kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa afya njema na uzima aliotujaalia. 3. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii, kwa masikitiko makubwa, kuungana na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kutoa pole kwako wewe binafsi, Bunge lako Tukufu na watanzania wote kwa ujumla kufuatia kifo cha mpendwa wetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichotokea tarehe 17 Machi, 2021. Hakika tutamkumbuka shujaa huyu wa Afrika kwa uzalendo, ujasiri, vita dhidi ya ufisadi na uongozi 3 wake mahiri ulioacha alama kubwa kwa Taifa letu na Afrika kwa ujumla.
[Show full text]