MKUTANO WA SABA Kikao Cha Tisa – Tarehe 19 Aprili, 2017 (Bun
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA SABA Kikao cha Tisa – Tarehe 19 Aprili, 2017 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Tukae Waheshimiwa Wabunge. Katibu. NDG. RAMADHAN ISSA ABDALLAH - KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tutaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, sasa aulize swali lake. Na. 70 Maombi ya Halmashauri ya Busekelo kuwa Wilaya MHE. FREDY A. MWAKIBETE Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itayakubali maombi ya wananchi wa Halmashauri ya Busokelo ya kuifanya Halmashauri hiyo iwe Wilaya? 1 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali GN Namba 286 ya tarehe 9 Septemba, 2011 ikiwa ni sehemu ya Wilaya ya Rungwe kwa lengo la kusogeza karibu huduma zilizokuwa zikitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe. Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo ya kuifanya Halmashauri ya Busokelo kuwa Wilaya yaliwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) iliyokutana tarehe 4 Julai, 2013. Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Mkoa kupitia maombi hayo ili kujiridhisha kama Halmashauri hiyo inakidhi vigezo kuwa Wilaya kamili. Mheshimiwa Naibu Spika, Sekretarieti ya Mkoa ilifanya tathmini ya maombi ya wananchi wa Busokelo ya kuwa Wilaya kamili kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua nia njema na juhudi kubwa ya Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa kuzingatia taarifa ya tathmini iliyofanywa na Sekretarieti ya Mkoa, hususan katika idadi ya watu, ukubwa wa eneo pamoja na kuwepo kwa tarafa moja pekee, imesababisha kutokidhi vigezo vya uanzishwaji wa Wilaya ya kiutawala ya Busokelo. MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali kwamba Halmashauri ya Busokelo haijakidhi vigezo vya kuwa Wilaya, nina maswali mawili kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. 2 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo vigezo anavyosema haijakidhi sijui ni vipi kwa sababu vigezo ambavyo vinazingatiwa, hasa ni idadi ya watu pamoja na jiografia ya eneo husika, kwetu kwa sababu hii tathmini ilishafanyika tangu miaka 2013 na sasa hivi ni 2017. Hauoni kwamba kuna umuhimu sasa wa kuanzisha hiyo Halmashauri ya Busokelo iwe inaitwa Wilaya ya Busokelo badala ya sasa ilivyo? Swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Wilaya pamoja na DAS wanafanya kazi nzuri katika Wilaya ya Rungwe, kwa bahati mbaya kwa sababu ya jiografia ya Rungwe ilivyo kuna zaidi ya kata 40 na huyu Mkuu wa Wilaya hawezi kusimamia ama kufuatilia zote kwa wakati mmoja kufuatana na jiografia ilivyo. Je, hauoni pia ni miongoni mwa sababu ambayo inaweza ikasababisha ianzishwe Wilaya ya Busokelo na hivyo iweze kuanzishwa haraka iwezekanavyo? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hayo majibu na mimi nayasikiliza kwa makini hapa. (Kicheko) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa sababu specification inataka angalau eneo hilo liwe na eneo lisilopungua kilometa za mraba 5,000 nwakati pale kiuhalisia ziko kilometa za mraba 969. Kwa hiyo, hii ilikuwa ni kigezo kimojawapo ambacho kimesababisha isiweze ku-qualify. Kipindi kile idadi ya watu kwa muongozo inatakiwa watu wasiopungua 250,000 lakini katika kipindi kile tathmini ilivyofanyika kulikuwa na watu takribani 96,348. Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu muda mrefu sasa hivi umeshapita kutoka kipindi kile mpaka sasa hivi hii tathmini ukiiangalia huenda population imeongezeka, lakini vilevile hata ukiangalia suala zima la tarafa, vigezo lazima angalao kuwe na tarafa tatu pale ukiangalia ni tarafa moja. Ninafahamu kwamba mlikuwa na juhudi ya kuitenga ile Tarafa moja mpate tarafa nyingine tatu, hii nilidhani kwa sababu Mbunge mnafahamu kama ulivyosema mna kata 3 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) zipatazo 40, mnaweza mkakaa kwa pamoja sasa na RCC yenu kuangalia mnaweza kuishauri vizuri nini cha kufanya. Baadae ikionekana vigezo hivi sasa vimekaa vizuri basi Serikali itaona nini cha kufanya na jinsi gani ya kupata eneo hili kuwa eneo la kiutawala la Kiwilaya. Mheshimiwa Naibu Spika, suala kwamba Mkuu wa Wilaya ya Busokelo anahudumia eneo kubwa sana, kwa hiyo kuna haja ya kuona hili jambo sasa ikiwezekana Wilaya ile sasa Busokelo iwe Wilaya kamili. Kama nilivyosema pale awali ni kwamba hivi sasa ninyi angalieni jinsi ya kufanya. Nafahamu kwamba ni kweli Mkuu wa Wilaya ya Rungwe anafanya kazi kubwa sana, nilikuwa nae pale site siku ile tulipopata lile tatizo, kweli ni miongoni mwa Wakuu wa Wilaya ambao wanajituma sana katika kazi yake. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile wote kama Viongozi Wakubwa na Mheshimiwa Naibu Spika uko hapa, nadhani mtaliangalia kwa uzito wenu kwa jinsi gani mtafanya, kama Busokelo, kama Rungwe kwa wakati mmoja ni jinsi gani hata mtafanya mipaka yenu na kila kitu. Lengo kubwa ni kupeleka huduma kwa wananchi na Serikali mkiona kwamba mmekidhi vigezo hivyo, haitasita kufanya maamuzi sahihi. MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo yaliyopo huko Busokelo yapo pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Katika Wilaya ya Manyoni kuna Halmashauri ya Manyoni na Hamashauri ya Itigi; Halmashauri ya Itigi square kilometer zinakidhi na maombi yamekuwa yakipelekwa kila mara na toka mwaka 1980 Serikali imekuwa ikiwaahidi wananchi wa Itigi kwamba watapatiwa Wilaya kamili. Je, sasa ni lini Serikali itaipa Halmashauri ya Itigi kuwa Wilaya kamili? 4 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukiangalia Manyoni, lazima tufahamu juhudi kubwa ya Serikali iliyofanya pale, mwanzo ile yote ilikuwa inaitwa Wilaya na Halmashauri ya Manyoni. Hapa katikati ndiyo tukapata Halmashauri mpya ya Itigi na wewe Mheshimiwa Mbunge unafahamu hata suala zima la upelekaji wa fedha ndiyo kwanza tumepeleka kwa ajili ya kujenga miundombinu ya Halmashauri ile. Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ninafahamu kwamba, siku ile nilikuwa na Mkuu wa Wilaya pale na alisikitika katika hilo alisema kwamba mafuta anayoyatumia ni kwamba, akiamua kuzunguka eneo lake matufa yanaisha kwa sababu Manyoni ukijumlisha na Itigi ni eneo kubwa sana. Naomba niseme japokuwa maombi hayo inawezekana mwanzo yalikuja yalidondoka kwa sababu yalishindwa kupata sifa, hizo sifa sasa hivi zikikamilika basi naomba mfanye ile michakato ya kisheria kama inavyokusudiwa kuanzia katika ngazi za Ward DC, Baraza la Madiwani, DCC, RCC na ikifika katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Waziri wangu yuko hapa, hawezi kushindwa kufanya maamuzi sahihi kwa kadri anavyoona jambo hilo linafaa kwa maslahi mapana ya wananchi wa Itigi. MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda yenye majimbo ya Mwibara na Bunda ni majimbo mawili ambayo hayapakani. Jimbo la Bunda liko kwingine na Jimbo la Mwibara liko kwingine, lakini ndiyo yanaunda Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo hili tulishampelekea Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, na kwa kuwa Mwibara iliwahi kuwa Jimbo tangu mwaka 1974, lakini tulishapeleka TAMISEMI iwe Wilaya mpaka leo vigezo ilishatimiza lakini hatupatiwi. 5 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini wana- Mwibara juu ya jambo hili ambalo ni changamoto ya miaka mingi? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, wasiofahamu hili Jimbo la Mheshimiwa Kangi Lugola ni sawasawa kama unazungumza kama lile bakuli halafu katikati kuna kile kisahani. Katikati ya kisahani pale unapata Jimbo la Dada yangu Mheshimiwa Ester Bulaya, Jimbo la Bunda Mjini. Ukienda huku utakuta Jimbo la ndugu yangu Mheshimiwa Boniphace Getere na huku unakuta Jimbo la Mwibara, kwa hiyo anachozungumza ni kweli. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine tunapoenda kufanya maamuzi ya mgawanyo wa haya maeneo wakati mwingine hatuweki mipaka sahihi. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pale hata ukiangalia ni kama yai, katikati kiini cha yai ndiyo Jimbo la Mheshimiwa Ester Bulaya hata ninaamini inawezekana ukatokea ugomvi mkubwa wa wapi Halmashauri ya Jimbo hilo itajengwa inawezekana ni kutokana na huko mwanzo maamuzi yetu hayakuwa sahihi. Inawezekana ilikuwa ni mihemko ya kisiasa ya kugawanya, jinsi gani tugawanye, hatukufanya maamuzi sahihi. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba hili kweli ni changamoto kubwa. Kama Mheshimiwa Kangi Lugola nafahamu kweli changamoto yako ni kubwa na nimefika mpaka kule ziwani siku ile nilivyofika, nimechanginyikiwa kweli Jimbo lako lilivyo. Basi mtajadiliana kwa pamoja kule katika vikao vyenu kuangalia nini cha kufanya. Jukumu letu kubwa Serikali ni kuona jinsi gani tutafanya ili wananchi waweze kupata huduma. Hivi sasa ninaamini wewe na Mbunge mwenzako ni lazima mkae vizuri la sivyo inawezekana mkapishana wapi Makao Makuu yenu itaenda kujengwa kwa maslahi mapana ya maeneo yenu. Ahsante sana. 6 NAKALA YA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ryoba Chacha swali fupi tafadhali. MHE.