Hotuba Ya Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE SHEREHE ZA KUADHIMISHA MIAKA 45 YA UHURU WA TANZANIA BARA, UWANJA WA TAIFA, DAR ES SALAAM, TAREHE 09 DESEMBA, 2006 Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda; Mheshimiwa Levy Mwanawasa, Rais wa Jamhuri ya Zambia; Mheshimiwa Mwai Kibaki, Rais wa Jamhuri ya Kenya; Mheshimiwa Armando Guebuza, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji; Mheshimiwa Dkt. Bingu wa Mutharika, Rais wa Jamhuri ya Malawi; Mheshimiwa Ahmed Abdullah Mohamed Sambi, Rais wa Comoro; Mheshimiwa Pakalitha Mosisili, Waziri Mkuu wa Lesotho; Mheshimiwa Marine Barampama, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Aman Abeid Karume, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ; Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; Mheshimiwa Samuel Sitta, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Barnabas Samatta, Jaji Mkuu wa Tanzania; Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili; Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu; Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu; Mheshimiwa Mama Maria Nyerere; Mheshimiwa Mama Fatma Karume; Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge; Waheshimiwa Mabalozi; Waheshimiwa Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Vyama vya Siasa; Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana. Ndugu Wananchi; Leo ni siku ya aina yake katika historia ya nchi yetu. Ni siku ambayo miaka 45 iliyopita tulikata minyororo ya ukoloni. Tarehe kama ya leo, mwaka 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alituongoza wananchi wa Tanganyika, wakati ule, katika kuupokea uhuru wetu na wa nchi yetu. Ni siku ambayo aibu ya takriban miaka 77 ya kutawaliwa na wageni ilikoma. Yaani tulitawaliwa na Waingereza kwa miaka 43 (1918 – 1961) na kabla yao miaka 34 (1884 – 1918) ya ukoloni wa Ujerumani. Ndiyo siku lilipozaliwa taifa huru la watu wa Tanganyika, ambayo sasa ni Tanzania Bara kufuatia kuungana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Aprili 26, 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndugu zangu; Wananchi Wenzangu; Leo ni siku ambayo kila Mtanzania popote alipo, ndani na nje ya nchi yetu, anayo kila sababu ya kufurahi na kusherehekea. Natambua kwamba zaidi ya theluthi mbili ya Watanzania tuliopo sasa hawakuwepo wakati ule. Wakati ule nchi yetu ilikuwa na watu milioni 9 tu ukilinganisha na sasa ambapo tuko watu milioni 36. Hata hivyo, wote tunawajibika kusherehekea siku ile kwa sababu ndiyo siku ya ukombozi wetu sote, kwani kama uhuru usingepatikana siku ile huenda hata leo tungekuwa kwenye harakati za kupigania uhuru. Ndugu Wananchi; Katika kusherehekea siku hii kubwa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwanza kwa kutuweka hai na kutufikisha salama siku ya leo. Pili, kwa kuiangazia nuru njema nchi yetu, kuilinda na kuiwezesha kuwa na amani, umoja, upendo na mshikamano thabiti kwa kipindi chote cha miaka 45 ya uhuru wetu. Wakati tunaadhimisha miaka 45 ya Uhuru wa Tanganyika, ni siku pia ya kusherehekea na kuwakumbuka wazee wetu waliojitolea muhanga kupambana na mkoloni mpaka akasalimu amri na kuondoka. Wengi wa wazee wetu hao akiwemo jemadari mkuu wa mapambano hayo Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere wameshatangulia mbele ya haki. Lakini, wapo pia wengi kiasi ambao bado wako hai na baadhi yao tunao hapa leo. Naomba nitambue kuwepo kwa Chifu Patrick Kunambi, Mzee Ally Sykes, Mzee C. Milinga na Mzee Suleiman Kitwara ambao pamoja na wenzao 12 chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere walianzisha Chama cha Ukombozi cha TANU tarehe 07 Julai, 1954. Uamuzi wao wa busara na moyo wao wa ushujaa na ujasiri wa kuongoza harakati za kupigania uhuru na ukombozi wa Tanganyika ndiyo uliozaa Tanganyika huru. Kwa kweli leo ni siku yao ya kuwakumbuka na kuwashukuru kwa wema mkubwa walioifanyia nchi yetu na sisi watu wake. Wakati tukiwakumbuka na kuwashukuru waasisi wa Chama cha Tanu tunafanya hivyo pia kwa wazee wote wengi waliojiunga nao katika harakati hizo. Wengi hawako nasi duniani, tunawatakia mapumziko mema. Lakini wapo wengi tunao miongoni mwetu na bahati nzuri baadhi yao tunao hapa leo wakiongozwa na Simba wa Vita mzee wetu Rashid Mfaume Kawawa. Nyote tunawashukuru sana. Katika siku ya leo, tunapowakumbuka wazee wetu waliojitolea muhanga kwa ajili ya uhuru na ukombozi wa nchi yetu, pia tunawakumbuka wale wote walioanzisha harakati za kuukataa ukoloni hata kabla ya kuzaliwa kwa Chama cha TANU. Natambua juhudi za mashujaa wa vita vya Maji Maji kuanzia Kilwa hadi Songea, mashujaa wa Kihehe na Kichaga na wengineo wengi. Katika kukataa kutawaliwa baadhi yao walipoteza maisha. Wao ndio waliopanda mbegu ya awali iliyokuja kuchipua katika TANU na kuzaa tunda tunalolisherehekea leo. Ndugu Wananchi; Wakati tukisherehekea miaka 45 ya Uhuru wa nchi yetu, ni siku pia ya kutafakari tulikotoka, tulipo sasa na kuangalia mbele tuendako. Ni dhahiri kabisa kwamba ukilinganisha tulipo sasa na kule tulikotoka miaka 45 iliyopita tumepiga hatua kubwa sana. Katika nyanja zote za maisha ya mwananchi wa Tanzania Bara tumepata maendeleo makubwa ukilinganisha na pale alipotuacha mkoloni. Tumefaulu. Umoja wa Kitaifa Ndugu Wananchi wenzangu; Kwa sababu ya sera yake ya “wagawe uwatawale” (divide and rule) mkoloni alituacha wananchi wa Tanganyika wakati ule tukiwa tumegawanyika kwa makundi makundi. Mkoloni alituacha tukiwa tumegawanyika kwa makabila yetu, kwa dini zetu na kwa rangi zetu. Kila kabila na chifu wake, mtemi wake au mtawala wake wa jadi lilikuwa ni taifa pekee. Watu walitambuana, kushirikiana na kusaidiana kwa dini zao au kwa rangi zao na makabila yao. Hata kwa watu wa kabila moja walibaguana kwa maeneo watokako. Kadhalika watu waliishi na huduma zilitolewa kwa misingi ya rangi zao. Miji ikawa na mitaa ya Uzunguni, Uhindini na Uswahilini. Hivyo hata huduma za elimu, afya, maduka, burudani, uchumi na hata makaburi yaligawanywa hivyo hivyo. Lakini baya zaidi hata thamani ya utu wao ilipewa daraja kwa misingi ya rangi ya ngozi zao ambapo mtu Mweusi alikuwa na daraja la chini, Muasia la kati na Mzungu ndiyo mbora wa wote. Mswahili alikuwa haruhusiwi kupanda ndege bila kudhaminiwa na Mzungu, au Muhindi au Mwarabu kwani kwa ushamba wake eti anaweza kutapika akachafua ndege au hata kufanya vurugu angani kwa hofu zake. Hata bia Mwafrika alikuwa haruhusiwi kunywa maana stahili yake ni dengerua na inapouzwa panaitwa Mwafrika Bar au Pombe shop. Uchumi nao ulikuwa mikononi mwa Wazungu na Waasia. Biashara ndogo ndogo zilikuwa mikononi mwa Waarabu na Mwafrika alikuwa mtumishi wa wote hao. Ni kibarua anayelipwa ujira mdogo sana na muda mwingi kuambulia matusi na hata makofi. Hiyo ndugu zangu ndiyo sura ya maisha ya wananchi wa Tanganyika wakati tunapata uhuru. Nchi yetu haikuwa taifa moja la watu wamoja, wanaoishi pamoja na kushirikiana. Lilikuwa ni taifa la mkusanyiko wa watu ambao kila mmoja na lwake. Watu wanadharauliwa na kunyanyaswa chini ya utawala wa mkoloni Mwingereza. Uhuru ulimkomboa Mwafrika wa Tanganyika dhidi ya manyanyaso na ulimrejeshea heshima yake na utu wake ulioporwa na wakoloni. Katika mazingira hayo basi kazi ya kwanza iliyofanywa na Serikali ya Tanganyika huru ilikuwa kumjenga mwananchi ajiamini kuwa yuko huru. Pili, kujenga taifa la watu wamoja, wanaoishi kwa upendo na ushirikiano kama taifa. Hii ilikuwa ndiyo changamoto kubwa ya kwanza ya Serikali ya Tanganyika huru. Chini ya uongozi mahiri na shupavu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kazi ya kujenga taifa moja ilifanyika kwa ufanisi wa hali ya juu. Ukabila, udini, ubaguzi wa rangi na ubaguzi kwa mujibu wa maeneo vilizikwa. Watu walikuwa hawatangulizi dini, kabila, rangi au eneo atokalo kama sharti la kuishi au kushirikiana na mwenzake. Ndugu Wananchi; Lakini, katika kujenga umoja, Mwalimu Nyerere aliisogeza Tanganyika hatua moja zaidi. Kwa kushirikiana na mwana mapinduzi shupavu, Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar waliunganisha nchi zao mbili huru na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Leo tunaposherehekea miaka 45 ya Uhuru wa Tanganyika tunasherekea nchi ambayo imefanikiwa kujenga umoja miongoni mwa watu wake na miongoni mwao na ndugu zao wa nchi huru ya Zanzibar. Bahati nzuri, bado misingi ya umoja wa wananchi na taifa letu ni imara pamoja na misukosuko ya hapa na pale ambayo imekuwa inatokea katika vipindi na nyakati mbalimbali. Muungano ni imara na inshallah Mwenyezi Mungu atatujalia utapanda daraja na kuwa Shirikisho la Afrika Mashariki. Bado udini, ukabila, ubaguzi wa rangi au wa eneo ni mambo yanayopingwa na kukataliwa na Watanzania walio wengi. Bado ni misingi inayoongoza maadili ya utaifa na mahusiano baina ya watu wa nchi yetu. Ndugu Wananchi; Wahenga wamesema usione vinaelea vimeundwa. Waundaji wa umoja na mshikamano wa watu wa nchi yetu si wengine bali ni sisi wananchi wenyewe, chini ya uongozi bora wa viongozi wa nchi yetu na serikali zetu mbili tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Misingi mizuri na imara ya umoja waliyoiweka na kuzingatiwa na viongozi wa awamu zote zilizofuatia kwa upande wa Muungano na Zanzibar, ndiyo iliyoiwezesha nchi yetu kuwa na amani, usalama na utulivu tuliokuwa nao sasa. Ndiyo inayowafanya Watanzania kuwa na umoja, mshikamano na ushirikiano pamoja na tofauti zao za rangi, kabila, dini, maeneo watokako au hata kwa sasa tofauti ya ufuasi wa vyama vya siasa. Ni misingi mizuri na maadili mema ambayo katika kusherehekea miaka 45 ya uhuru wetu hatuna budi kuazimia kuidumisha.