05022019 YOTE.Pmd
Total Page:16
File Type:pdf, Size:1020Kb
NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA KUMI NA NNE Kikao cha Saba – Tarehe 5 Februari, 2019 (Bunge lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Najma Murtaza Giga) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. MOSSY LUKUVI – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI MWENYEKITI: Hati za Kuwasilisha Mezani, tunaanza na Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, karibu. NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO:- Taarifa ya Serikali kuhusu Tathmini ya Hali ya Uchumi na Utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2018 na Mwelekeo hadi Juni, 2019. MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII:- Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI:- Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018. MWENYEKITI: Ahsante sana, Katibu, tunaendelea. NDG. MOSSY LUKUVI – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tunaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu na swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum. Na. 69 Miradi ya MIVARF Kuwawezesha Wananchi Kimtaji MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:- Miradi ya MIVARF ina malengo mapana ya kuwaendeleza wakulima wa vijiji kibiashara na kimtaji; na hatua za awali kama vile ujenzi wa barabara za vijijini umekamilika lakini pia masoko ya kuongeza thamani yapo katika hatua za kukamilika:- Je, ni lini hatua za mwisho za kuwawezesha wananchi kimtaji zitaanza rasmi kwa upande wa Zanzibar? MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha inaunga mkono juhudi za wananchi kushiriki katika uchumi wa kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa mitaji na kuwapatia mafunzo stahiki. Mpango wa Kuwawezesha Wananchi Kimtaji umezingatia hatua zifuatazo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF, imevijengea uwezo wa kiutawala na kiutendaji Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uzalishaji Tanzania Bara na Visiwani ili viweze kuratibu na kusimamia kwa ufanisi matumizi ya mitaji yatakayopatikana kupitia mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha. Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 3 Novemba, 2017, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Benki ya Maendelea ya Kilimo Tanzania (TADB) walisaini makubaliano ya uendeshaji wa Mfuko wa Dhamana. Kwa kupitia makubaliano hayo, Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 22 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kuanza utekelezaji kwa kushirikisha benki za biashara kufikisha huduma ya mikopo kwa makundi mbalimbali. Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania walishatangaza utaratibu wa namna benki mbalimbali za biashara zinavyoweza kushiriki katika Mfuko wa Udhamini ambapo Benki za CRDB, NMB, TPB na PBZ zilionesha nia. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilishakutana na benki zote zilizoonesha nia ya kushiriki katika Mfuko wa Dhamana na kufafanua jinsi Mfuko wa Udhamini unavyofanya kazi. Benki za NMB na TPB wameshakubaliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kushiriki katika utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hatua ya mwisho ya kuwawezesha wananchi kimtaji imeshafikiwa baina ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na Benki za NMB na TPB kama ilivyoelezwa hapo juu, napenda kutoa wito kwa Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) vya uwezeshaji Zanzibar kuwasiliana na Benki za NMB na TPB kwa upande wa Zanzibar ili kupata utaratibu wa kukopa fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo. MWENYEKITI: Mheshimiwa Maida. MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, niipongeze Serikali kwa juhudi zake katika kuwaendeleza wananchi kiuchumi na niwapongeze pia kwa kutoa shilingi bilioni 22 kwa ajili ya kuendeleza SACCOS hizi. Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali lakini pia ninayo maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri lakini niseme kwamba pamoja na Serikali kuingia mikataba na benki na kufikia uamuzi wa kusaini kwa ajili ya kuwaendeleza wakulima hawa kwa kuwapatia mikopo lakini bado benki za Zanzibar zimekuwa zikisuasua kuhusiana na suala la mikopo hiyo. Je, Serikali iko tayari kuzisimamia benki hizi ili kuweza kufikia utekelezaji ili wananchi hawa waweze kupata mikopo hiyo? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nataka kusisitiza tu Serikali kwamba SACCOS zetu mara nyingi hazina elimu za kuendeleza biashara zao kimitaji na kimasoko. Kwa hiyo, naiomba Serikali kufika Zanzibar kuwapa elimu wananchi wa Zanzibar. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu ya maswali hayo. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali la kwanza, ni kweli Benki ya Kilimo (TADB) ilikwishaingia makubaliano na benki nilizoziainisha pale awali ikiwemo Benki ya Watu ya Zanzibar. Kwa hiyo, rai yangu ni kuziomba taasisi za fedha kwa upande wa Tanzania Visiwani kwa maana ya Zanzibar kuichangamkia fursa hii ili wakulima wengi zaidi wa Zanzibar waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na benki hii kwa sababu ipo kwa ajili yao. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi tu niseme kwamba kwa upande wa Zanzibar tunaendelea pia na hatua za kuviwezesha vikundi hivi. Hivi sasa tayari vikundi kwa maana ya SACCOS 231 zimeshafikiwa na tayari zaidi ya shilingi bilioni 24 ziko katika mzunguko kwa ajili ya ukopeshaji. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuziomba na kuzitaka benki za Zanzibar kuchangamkia fursa hii ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili kuhusu elimu, katika Programu hii ya MIVARF, kabla ya kuanza utoaji wa fedha na uwezeshaji iko package ambayo inahusisha masuala ya mafunzo hasa nidhamu ya matumizi ya fedha na utunzaji wa fedha. Kwa hiyo, ombi kuhusu suala la elimu ni kwamba ni sehemu ya mradi huu na imekuwa ikifanyika na ninavyozungumza hivi sasa tayari vikundi 57 vya uzalishaji mali kule Zanzibar wameshapewa elimu ya kutosha juu ya matumizi bora ya fedha na namna ya kukopa. MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Chief Whip. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu niongeze majibu ya ziada kwenye swali zuri sana la Mheshimiwa Maida na hasa faida ambazo wanaweza wakazipata wenzetu wa upande wa pili wa Muungano yaani kule Zanzibar. Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokifanya mpaka sasa ni kuhakikisha kwamba Mradi huu wa MIVARF unakuwa ni 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) kielelezo kizuri cha Muungano wetu katika nchi yetu. Kwa sababu inaonekana upande wa pili wa wenzetu bado mikopo hii hawajaifahamu vizuri na bado hawajanufaika nayo, naomba niliahidi Bunge lako Tukufu, tutafanya ushirikiano na mawasiliano ya karibu na Waziri mwenye dhamana ya Vijana na Uwezeshaji kule Zanzibar ajue uwepo wa mikopo hii ili aweze kutusaidia kusimamia na kuhakikisha kwamba wenzetu wa upande wa pili wa Zanzibar na wao wanafaidika na wanajua uwepo wa mikopo hii kupitia benki yao ambayo itawahudumia kupitia Mpango wa MIVARF. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu. Mheshimiwa Khadija Nassir swali la nyongeza. MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Kumekuwa na masharti magumu sana katika kupata mikopo ukizingatia vikundi vya vijana wengi wanakuwa bado hawana zile dhamana ambazo zinahitajika. Serikali inatuambia nini ili na sisi vijana ambao hatukidhi vigezo hivyo tuweze kufaidika na mikopo hiyo? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu ya swali hilo. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anashughulikia masuala ya vijana na kuwa mstari wa mbele kuwatetea vijana wa Taifa hili la Tanzania. (Makofi) 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kwamba ipo changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa mikopo katika kundi hili kubwa la vijana, Serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, imedhamiria kidhati kabisa kuwasaidia vijana wa Taifa letu kwa kuwakopesha fedha pasipo masharti magumu kama ambavyo wanayapata kupitia taasisi za kifedha. Tunao Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao mpaka hivi sasa umeshakopesha zaidi ya shilingi bilioni 4.5 katika vikundi 237 vya vijana nchi nzima. Kwa hiyo, ni fursa ambayo vijana wanayo kupitia mfuko huu ambapo wanaweza kukopa bila masharti mengi ambayo yapo katika taasisi nyingine