NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA _____________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA ISHIRINI Kikao cha Ishirini na Nne – Tarehe 8 Juni, 2015 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) DUA Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. ESTER A. BULAYA (K.n.y. MHE. JAMES D. LEMBELI - MWENYEKITI WA KAMATI YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA): Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015, pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. MHE. MCH. PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) SPIKA: Ahsante Mchungaji Msigwa. Katibu! MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Maswali tunaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu; atakayeuliza swali la kwanza, Mheshimiwa Mchungaji Luckson Mwanjale. Na. 160 Ujenzi wa Stendi na Barabara za Mji wa Mbalizi MHE. MCH. LUCKSON N. MWANJALE aliuliza:- Ujenzi wa stendi na barabara zake katika Mji Mdogo wa Mbalizi ulikuwa ni sehemu ya ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni za mwaka 2010:- Je, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo? SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu! Watu wote wamekwenda kutangaza nia hawapo humu. (Kicheko) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mchungaji Luckson Ndaga Mwanjale, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, stendi ya mabasi iliyopo katika Mji Mdogo wa Mbalizi na inayotumika ina ukubwa wa mita za mraba 9,209 na inamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Kwa sasa inatumika kwa ajili ya mabasi madogo, daladala na mabasi yaendayo Mikoani. Aidha, Halmashauri ina barabara yenye urefu wa kilometa 1.3 iliyojengwa kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Spika, tayari Halmashauri imekamilisha michoro kwa ajili ya kujenga stendi pamoja na barabara. Tathmini iliyofanyika mwaka wa fedha 2010/2011, ili kuboresha miundombinu ya barabara na stendi hiyo ilionesha kuwa, ili stendi hiyo pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami viweze kukamilika, jumla ya shilingi bilioni 1.3 zilihitajika. Kutokana na gharama za ujenzi kupanda, tathmini iliyofanyika katika mwaka wa fedha 2015/2016, inaonesha kuwa, jumla ya shilingi bilioni 1.6 zitatumika kukamilisha ujenzi huo. 2 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Halmashauri katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, ilipokea jumla ya sh. 150,843,468/= kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya uboreshaji wa stendi hiyo, ambapo jumla ya mita za mraba 2,161.25 zilijengwa kwa kuzijengea tofali kati ya mita za mraba 6,117 za stendi hiyo. Aidha, ili ujenzi wa stendi hiyo uweze kukamilika kwa kuweka tofali jumla ya sh. 338,954,000/= zinahitajika. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Halmashauri ilitenga fedha jumla ya shilingi milioni 525.7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ambapo jumla ya kilometa 1.3 zinaendelea kujengwa. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2015/2016, jumla ya shilingi milioni 150 zimetengwa katika vyanzo vya mapato ya ndani, ili kujenga jumla ya mita za mraba 2,000 katika stendi hiyo na shilingi milioni 566.7 zimetengwa ili kukamilisha ujenzi wa barabara katika mji huo. MHE. MCH. LUCKSON N. MWANJALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, mapato ya Halmashauri ya Mbeya Vijijini hayazidi bilioni mbili kwa mwaka na barabara hiyo, inakisiwa kwamba, itachukua shilingi bilioni 1.6; hamuoni kwamba, kama hela za ndani za Halmashauri zitatumika kujenga, basi ina maana maeneo mengine yote na barabara zingine zote hazitajengwa? Naomba Serikali iniambie kwamba, je, itakuwa tayari sasa kuisaidia Halmashauri kutenga hela kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa stendi pamoja na barabara zake? Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mbeya Vijijini ina vijiji 150 ambavyo vijiji hivi hutegemea misaada yote kutoka katika Halmashauri ambayo kama nilivyosema, fedha inayopatikana ni kidogo sana. Je, Serikali kwa sababu, ilianza kutoa hela shilingi milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa stendi na barabara, je, haiko tayari sasa kutoa fedha hiyo kumalizia ile stendi na barabara? Ahsante. SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu! NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU): Mheshimiwa Spika, Serikali kwa utaratibu ambao tunao huwa tunatenga fedha kwa ajili ya kuendesha miradi ambayo inabuniwa kwenye Halmashauri, lakini Halmashauri zenyewe zinaweka kipaumbele kwa jambo ambalo halihitaji pamoja na kutenga fedha kupitia kwenye bajeti yake na bajeti ya mapato ya ndani hukadiriwa kutokana na makusanyo ya kila mwaka ambayo wanajua wanavyokusanya kiwango hicho na mipango yao ya kazi inaendana na makusanyo waliyonayo. 3 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, ukusanyaji sasa tumeendelea kuuwekea mkazo na Halmashauri nyingi zimeonesha zinakusanya kwa zaidi ya 80%, tunayo matarajio kwamba, mchango ule wa Halmashauri wanaweza kufikia hatua, lakini watakaposhindwa tunao utaratibu wa barua maalum, maombi maalum kwa Wizara na kama Wizara tunakuwa na uwezo tunasaidia. Mheshimiwa Spika, sasa hii ni pamoja na swali la pili ambalo linasema wingi wa vijiji na barabara zake; bado barabara hizi zilizoko kwenye Halmashauri zinazounganisha vijiji na vijiji zinakuwa ziko ndani ya Halmashauri yenyewe. Hata hivyo, tuna ule Mfuko wa Barabara ambao pia, kama Halmashauri imekidhi vigezo kwanza kuwa na Engineer ambaye amepata taaluma ya kutosha, lakini mbili, barabara hizo kuwa na mahitaji ya kujenga barabara mpya kwa maana ya kwa kiwango cha changarawe, tunaweza pia, kuona uwezekano wa kuangalia mapato ya ndani waliyotenga, Mfuko wa Barabara na mahitaji ambayo yanatakiwa yakamilishwe, ili kuweza kukamilisha barabara hizo zinazounganisha vijiji kwenye maeneo yote. SPIKA: Ahsante. Tunaendelea na swali linalofuata, litaulizwa na Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, kwa niaba yake Mheshimiwa Ester Bulaya! Na. 161 Uhaba wa Walimu Shule za Sekondari Mpanda Vijijini MHE. ESTER A. BULAYA (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:- Jimbo la Mpanda Vijijini lina shule za sekondari saba ambazo ziko katika Kata ya Karema, Ikola, Kabungu, Katuma, Mishamo na Mpanda Ndogo, lakini shule hizo zina upungufu mkubwa wa Walimu:- (a) Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha katika shule hizo za Mpanda Vijijini? (b) Je, Serikali haioni kuwa kutokuwa na Walimu kumesababisha kushuka kwa elimu na hivyo kuwafanya wanafunzi kufeli mitihani? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:- 4 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) (a) Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeongeza idadi ya Vyuo vya Ualimu, Vyuo Vikuu na udahili katika kozi za ualimu pamoja na kuajiri Walimu kadiri wanavyofaulu. Mkakati huu umewezesha Serikali kwa mwaka huu wa 2015, kuajiri na kuwapanga katika shule za Sekondari Walimu 19,261. Kati ya hao Walimu 65 wamepangiwa Mpanda Vijijini na imewapanga katika shule za Kabungu Walimu watano, Mpanda Ndogo Walimu tisa, Katuma Ikoa Walimu 10, Mishamo Walimu 12, Mwese Walimu sita na Karema Walimu 10. (b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya sekondari nchini kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari, maarufu unajulikana kama MMES, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa Walimu, vitabu, miundombinu na kuimarisha usimamizi. Mikakati hii imewezesha kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka 43% mwaka 2012 hadi 69.7% mwaka 2014. Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Walimu, hususan wa masomo ya sayansi, wanapatikana wa kutosha katika shule zote na ifikapo mwaka 2016, Serikali itakuwa imekamilisha mradi wa ujenzi wa miundombinu kwa shule 528 zikiwemo shule za Ikola, Ilela, Utembe na Mamba. SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Ester Bulaya, maswali ya nyongeza! MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kupeleka Walimu ni jambo lingine, lakini kuhakikisha Walimu wanafika mashuleni na lenyewe ni jambo lingine. Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa tuliyonayo ni miundombinu yani mazingira mabovu ya Walimu, kwa mfano kumekuwa na tatizo kubwa sana la nyumba za Walimu, usafiri na kiasi kwamba, mbali ya kwamba, tumewapeleka Walimu bado hawako tayari kwenda maeneo ya vijijini. Mwisho wa siku inabakia figure kwamba, Walimu wamekwenda, lakini tatizo la uhaba wa Walimu halimaliziki. Je, ni lini sasa Serikali mtahakikisha mnajenga nyumba za Walimu na kuboresha mazingira yao, ili wabaki kule mnakowapeleka, ili tatizo la Walimu liondoke katika Jimbo la Mheshimiwa Kakoso? Hilo la kwanza. Mheshimiwa Spika, swali la pili, pia shule nyingi zimekuwa na uhaba wa Walimu wa kike ikiwepo shule ya msingi Kunzugu, Jimbo la Bunda. Ni lini sasa tatizo
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages245 Page
-
File Size-